Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Ni marufuku kuzungumza na Marekani kwa sababu ya madhara yake mengi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo (Jumatano) amehutubia hadhara ya makamanda na wafanyakazi wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah), familia zao na familia za mashahidi wa jeshi hilo. Ameashiria nafasi na mchango wa vijana wanamapinduzi wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Sepah na vijana shupavu wa kusini katika kulinda usalama wa baharini na kumtia woga adui na akasema: Maadui wanataka kubadilisha mahesabu ya maafisa wa Iran na kubadili fikra za wananchi hususan vijana hivyo wananchi wote wanapaswa kuwa macho na makini.
Ayatullah Khamenei ameashiria umuhimu wa suala la usalama na kusema: Utayarifu daima unapaswa kumtia woga na hofu adui kama inavyosisitiza Qur'ani Tukufu ili asiwe na ujasiri wa kufanya mashambulizi, kwani kama kutakuwepo upenyo basi adui atatumia njia hiyo.
Amesema, kwa baraka za kuundwa kambi ya kimapinduzi ya kusini inayoundwa na kikosi cha majini cha jeshi la Sepah na vijana shujaa wa kusini, maagizo ya Qur'ani ya kumtia woga adui yamefanyiwa kazi.
Amiri Jeshi Mkuu amesema, Iran kamwe haitakuwa ya kwanza kuanzisha vita na kuongeza kuwa: Uvamizi na kutaka kuwa na satua ni ada na tabia ya adui, kwa msingi huo kuna ulazima wa kuzidisha uwezo wa kielimu na zana kupitia uvumbuzi na ubunifu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza udharura wa kuwepo ushirikiano kati ya vikosi vya majini vya jeshi la Sepah na vile vya Jeshi la Taifa na ulazima wa kuwaenzi vijana waliokuwa na imani kama Shahidi Nader Mahdavi na wenzake ambao walipambana kishujaa mbele ya manowari za Wamarekani na kuwapa somo kubwa ambalo halitasahaulika na kusema: Kutokana na kusimama imara na ushujaa huo, maadui wa utawala wa Kiislamu walielewa kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran si mfumo wa kuamiliana nao vyovyote vile watakavyo wao.
Ayatullh Khamenei pia amepongeza suala la kuandamana na familia na wake wa makamanda na wafanyakai wa kikosi cha majini katika kutembelea maeneo ya kusini hapa nchini.
Ameendelea na hotuba yake kwa kuashiria mipango hatari ya madola ya kibeberu kwa ajili ya eneo la Mashariki ya Kati na kusema: Madola hayo hayasiti kutumia silaha hatari sana na mbinu za kinyama kwa ajili ya kuua wanadamu wasio na hatia. Ameongeza kuwa madai yao ya kutetea haki za binadamu na haki za raia ni kinyume na ukweli na hayana ukweli kabisa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa mashambulizi yaliyofanywa dhidi ya hospitali nchini Afghanistan na mauaji ya wananchi katika nchi za Syria, Iraq, Yemen, Palestina na Bahrain ni mfano wa jinai zinazofanywa na madola ya kibeberu duniani, ukatili na unyama wao. Ameongeza kuwa, hii leo hatari kubwa zaidi kwa dunia ni unafiki, ria na urongo wa wale wanaodai kutetea haki za binadamu.
Ayatullah Khamenei amezungumzia pia mchango na nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha sasa katika eneo la Mashariki ya Kati na akasema: Katika hali kama hiyo na kwa taufiki yake Mwenyezi Mungu, Iran mbali na kuzuia kupenya kwa adui ndani ya nchi, imefanikiwa pia kuzuia utekelezwaji wa njama na mipango yake mingi katika kanda hii.
Amesema kufeli kwa adui ndani ya nchi na nje ya kanda hii kumetokana na baraka za kuwa macho, utayarifu, azma ya vijana wanamapinduzi na nguvu za Jamhuri ya Kiislamu katika eneo hili; kwa msingi huo uadui mkubwa zaidi wa madola ya kibeberu unaelekezwa kwa Iran na madai ya Marekani ya kutaka kufanyika mazungumzo na Iran pia yameibuliwa katika fremu hiyo kwa ajili ya kupenya na kuingia Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakosoa baadhi ya watu kwa kutozingatia na kutafakari mambo ipasavyo hapa ndani ya nchi na ambao hawatilii maanani uzito wa maudhui hii na kusema: Sambamba na watu hawa wenye fikra finyu, kuna watu wasiojali katika jamii ambao hawayapi umuhimu wala kujali maslahi ya kitaifa ya nchi.
Ayatullah Khamenei ameashiria baadhi ya masuala yanayojadiliwa na watu wenye wenye fikra finyu na wasiojali  kuhusu suala la kufanya mazungumzo na Marekani na akasema: Watu hawa wanasena: Inakuwaje watu kama Imam Ali (as) na Imam Hussein (as) walifanya mazungumzo na maadui wao lakini sasa inakuwa marufuku kufanya mazungumzo na Marekani?
Akijibu suala hilo, Ayatullah Khamenei amesema: Uchambuzi kama huo kuhusu masuala ya historia ya Uislamu na masuala ya nchi unaonesha upeo wa juu wa ufinyu wa fikra kwa sababu Imam Ali na Imam Hussein (as) hawakufanya mazungumzo na Zubair na Amr bin Sa'd kwa maana inayotambulika kwa sasa, yaani kuamiliana na adui, bali watukufu hao wawili waliutia hofu upande wa pili na kuwanasihi wamuogope Mwenyezi Mungu.
Ayatullah Khamenei amesema: Inasikitisha kwamba ili kuhalalisha suala la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kufanya mazungumzo na Shetani Mkubwa (Marekani), badhi ya watu wenye mitazamo duni wamekuwa wakizungumzia suala hilo kwa njia hii katika magazeti, hotuba na mitandao ya kijamii, suala ambalo ni makosa kabisa.
 Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa Iran haipingi asili ya kufanya mazungumzo na nchi mbalimbali zikiwemo za Ulaya na zisizo za Ulaya na kuongeza kuwa, lakini suala hilo ni tofauti kuhusu Wamarekani kwa sababu kufanya mazungumzo na Iran katika mtazamo wao kuna maana ya kufungua njia kwa ajili ya kupenya na kuingilia mambo mbalimbali hapa nchini.
Ameashiria ushirikiano wa Marekani na mirengo ya Kizayuni dhidi ya binadamu na kusisitiza kuwa: Kufanya mazungumzo na Marekani kuna maana ya kufungua njia kwa ajili ya kupenya katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa na kiusalama hapa nchini.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameshiria pia mazungumzo ya hivi karibuni ya nyuklia (kati ya Iran na kundi la 5+1) na kusema: Katika mazungumzo hayo upande wa pili ulifanya jitihada kubwa za kutumia fursa zote kwa ajili ya kuwa na ushawishi na kupenya Iran na kufanya harakati dhidi ya maslahi ya taifa, lakini timu ya Iran ilikuwa macho japokuwa Wamarekani walipata fursa katika baadhi mambo.
Ayatullah Khameeni amesema: Ni marufuku kufanya mazungumzo na Marekani kwa sababu suala hilo si tu kwamba halina faida yoyote, bali pia lina madhara mengi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Kipindi cha sasa ni muhimu sana katika upande wa harakati na juhudi zinazofanywa na maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ambazo tunazielewa vyema, kwa sababu maadui wanataka kubadilisha mahesabu ya maafisa wa Iran na kubadili fikra za wananchi kuhusiana na masuala ya kimapinduzi, kidini na maslahi ya taifa ya nchi hii.
Ametilia mkazo kuwa vijana ndio walengwa wakuu katika suala la kubadili fikra za wananchi na amewataka vijana wawe macho zaidi. Ameongeza kuwa: Kwa baraka zake Mwenyezi Mungu, vijana wetu katika vyuo vikuu na katika vikosi vya jeshi wako macho na wanachapa kazi, na mimi sina wasiwasi wote katika upande huo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia tukio la Mubahala (mdahalo wa Mtume na Manasara wa Najran) na kusimama kidete Mtume (saw) na Ahlul Bait mkabala wa kambi ya ukafiri na amewaambia vijana wanamapinduzi hapa nchini kwamba: Kama ambavyo katika tukio la Mubahala katika zama za mwanzoni mwa Uislamu, imani yote ilisimama kupambana na ukafiri, leo hii pia katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imani yote imesimama kupambana na ukafiri; vilevile kama ambavyo katika zama hizo usafi wa kimaanawi na kiroho wa Mtume (saw) na Watu wa Nyumba yake ulimshinda na kumuondoa adui katika medani, hii leo pia taifa la Iran litamshinda na kumuondoa adui wake katika medani kwa kutumia nguvu yake ya kimaanawi.
Mwishoni mwa hotuba yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: Kama tutakuwa tayari kuinusuru dini ya Mwenyezi Mungu, hapana shaka kuwa Mwenyezi Mungu atatimiza ahadi yake ya kuwanusuru na kuwasaidia wanaoinusuru dini yake na wale wanaoutakia mabaya mfumo wa Kiislamu watashindwa katika njama na mipango yao ya kiusalama, kijeshi, kiuchumi na kiutamaduni.         
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Admeri Fadavi ambaye ni Kamanda Mkuu wa kikosi cha majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) alitoa hotuba fupi akipongeza ushujaa wa jeshi hilo katika kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu. Amesema: Askari wako tunasubiri amri ili tutoe somo na ibra ya kihistoria kwa Shetani Mkubwa na vibaraka wake wanaokera na wanaoua wageni na watoto katika eneo hili.
Kamanda Fadavi amesema jeshi la Sepah liko tayari kikamilifu na kuongeza kuwa, kudhihirishwa sehemu ndogo tu ya uwezo wa kivita na utayarifu wa kikosi cha majini cha Sepah kumewalazimisha maadui wajadili suala la kubadili stratijia yao ya baharini, wakati yale wanayojua kuhusu jeshi la Iran ni machache sana na hayawezi kulinganishwa na yale wasiyoyajua.  

700 /