Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Maafa ya kusikitisha ya Mina hayapasi kusahauliwa

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei adhuhuri ya leo (Jumatatu) ameonana na maafisa wa kusimamia ibada ya Hija wa Iran na kuyataja maafa machungu mno na ya kusikitisha sana ya Mina kuwa ni miongoni mwa mitihani ya Mwenyezi Mungu. Amezilaumu tawala za nchi mbalimbali na hususan tawala za nchi za Magharibi na mashirika yanayodai kutetea haki za binadamu kwa kunyamazia kimya msiba huo mkubwa kusisitiza kuwa: Tukio hilo halipaswi kabisa kusahauliwa na kwamba chombo cha diplomasia na Taasisi ya Hija ya Iran vina wajibu wa kulifuatilia ipasavyo suala hilo.
Ayatullah Khamenei ameashiria jukumu la utawala unaopokea mahujaji kuhusiana na mahujaji elfu saba waliopoteza maisha kwenye maafa ya Mina na kuongeza kuwa: Ilitegemewa kuwa ulimwengu wa Kiislamu ungelisimama kwa sauti moja kutangaza hasira na malalamiko yao baada ya kutokea maafa hayo, lakini jambo la kusikitisha ni kuona kuwa, ukitoa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hakuna sauti nyingine yoyote ya kulalamikia maafa hayo iliyotolewa kiasi kwamba hata tawala za nchi ambazo raia wao wamepoteza maisha kwenye maafa hayo, hazikuonesha malalamiko makubwa kuhusu suala hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kufuatilia na kufanyika mazungumzo na tawala za nchi mbalimbali kuhusiana na uzito wa maafa hayo na kutafutwa njia za kuzuia kujitokeza tena jambo hilo kuwa ni jukumu muhimu la viongozi wa Iran hususan chombo cha udiplomasia nchini na kuongeza kuwa: Dhahiri ya tukio hilo inaonesha kuwa, maafa hayo yametokana na uzembe wa utawala unaopokea mahujaji lakini vyovyote iwavyo, kadhia hiyo si suala la kisiasa bali mjadala hapa ni kwamba maelfu ya Waislamu wamepoteza maisha yao wakati wa kutekeleza ibada na amali za Hija wakiwa katika vazi la Ihram; hivyo suala la kuifuatilia kadhia hiyo inabidi lipewe uzito wa hali ya juu.
Vilevile amesema kuwa, upande mwengine unaopaswa kufuatiliwa ni kimya mutlaki cha mashirika na taasisi zinazodai kutetea haki za binadamu za barani Ulaya na Marekani na kuongeza kuwa: Mashirika yanayosema uongo na ya kinafiki yanayodai kutetea haki za binadamu na vilevile tawala za nchi za Ulaya ambazo baadhi ya wakati utaziona zinazusha makelele mengi mno duniani kwa kuuawa mtu mmoja, zimenyamazia kimya kabisa uzembe uliopelekea kupoteza maisha maelfu ya watu huko Mina.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Watu hao wanaojinadi kuwa ni watetezi wa haki za binadamu, kama ni wakweli katika madai yao hayo, basi wanapaswa wawatake waliosababisha maafa ya Mina wabebe dhima ya maafa hayo, wawatake wafidie hasara zake na watoe dhamana kuwa maafa kama hayo hayatatokea tena.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kuendelea kulifuatilia na kulibakisha hai suala hilo muhimu kuwa ni jukumu la Taasisi ya Hija na Ziara ya Iran na kusisitiza kuwa: Suala hili halipaswi kunyamaziwa kimya na wala kusahauliwa na linapaswa liendelee kuzungumziwa kwa miaka mingi ijayo katika duru za kimataifa na mawimbi ya harakati hiyo yaelekewe kwa tawala za nchi za Magharibi na kwa taasisi na mashirika yanayodai kutetea haki za binadamu duniani.
Vilevile amewashukuru sana maafisa na wasiamiaji wote wa ibada ya Hija nchini Iran hasa Hujjatul Islam Qadhi Asgar kutokana na ufuatiliaji wake wa karibu na kwa moyo na misimamo yake isiyotetereka na pia Mkuu wa Taasisi ya Hija na Ziara ya Iran, Bw. Saeed Ouhadi kutokana na harakati za kila upande na kuwa tayari kujibu maswali wakati wote na kutekeleza vizuri jukumu lake na ameongeza kuwa: Ujira na malipo mema ya wahusika wote wa masuala ya Hija yako kwa Mwenyezi Mungu kutokana na jitihada zao kubwa na subira yao ya kupigiwa mfano na kwamba subira na jitihada hizo kubwa katika njia ya Mwenyezi Mungu ndizo ambazo Bibi Zainab (as) aliziita kuwa jamali na uzuri baada ya kukumbwa na masaibu yote yale yaliyotokea kwenye jangwa la Karbala.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Qadhi Asgar, mwakilishi wa Faqihi Mtawala (Waliyyul Faqih) na msimamiaji wa mahujaji wa Iran ametoa ripoti fupi kuhusu kazi zilizofanyika katika Hija ya mwaka huu na vilevile ametoa ufafanuzi kuhusu hatua zilizochukuliwa kuhusiana na tukio la kuporomoka winchi ndani ya Masjidul Haram na maafa machungu ya Mina na kuongeza kuwa: Maafa ya Mina yametokea kutokana na usimamiaji mbovu na ukosefu wa tadbiri wa viongozi wa Saudi Arabia na kwamba suala hilo litaendelea kufuatiliwa kwa karibu na vyombo husika. Amesema kutawekwa kumbukumbu nzuri kuhusiana na matukio na maafa hayo.
Kwa upande wake, Bw. Saeed Ouhadi, Mkuu wa Taasisi ya Hija na Ziara ya Iran amesema kuhusiana na kurejeshwa nchini Iran mahujaji waliofariki dunia kidhulma katika maafa ya Mina na kuwahudumia watu waliojeruhiwa kwenye maafa hayo kwamba, ufuatiliaji wa kina wa kujua hali ya mahujaji wengine wa Kiirani waliopotoeza maisha huko Mina zinaendelezwa kwa nguvu kubwa na vyombo vyote husika.
Mkuu wa huyo wa Taasisi ya Hija na Ziara ya Iran ametoa ripoti pia kuhusu kazi zilizofanyika kwenye ibada ya Hija mwaka huu.

700 /