Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Barua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa Rais Rouhani kuhusu utekelezaji wa JCPOA

Matamshi yoyote kuhusu kubakishwa muundo wa vikwazo ni kinyume na makubaliano ya nyuklia

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amemtumia barua Rais Hassan Rouhani na ambaye pia ni Mkuu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa akiashiria uchunguzi wa kina uliofanyika bungeni na katika Baraza Kuu la Usalama wa Taifa kuhusu makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 (JCPOA) na jinsi yalivyopita katika hatua zote za kisheria. Vilevile ametoa maagizo muhimu juu ya kulindwa maslahi ya kitaifa.  
Matini kamili ya barua ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kama ifuatavyo:   

Bismillahir Rahmanir Rahim.
Janabi Bwana Rouhani
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mkuu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, Mwenyezi Mungu akuzidishie taufiki.
Assalaamu Alaykum.
Baada ya kufanyika mjadala wa kina na wenye uwajibikaji ndani ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na kupasishwa makubaliano yanayojulikana kwa jina la JCPOA; na kupitishwa pia na kamisheni maalumu na kamisheni nyenginezo na pia Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, hatimaye mwafaka huo umekamilisha hatua zake  kisheria na hivi sasa kunasubiriwa maoni yangu kuhusu makubaliano hayo. Ni wajibu wangu hapa kukumbushia nukta kadhaa ili kutoa fursa ya kutosha kwako na kwa wote wanaohusika na suala hilo kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja ya kuweza kulinda na kuchunga manufaa ya taifa na maslahi makuu ya nchi.
1 – Kabla ya jambo lolote, ni wajibu kwangu kuwashukuru kwa dhati wahusika wote wa mchakato huu wenye changamoto nyingi katika vipindi na duru zote ikiwa ni pamoja na: Timu ya mazungumzo ya hivi karibuni ambayo imefanya juhudi zake zote za kuyatetea na kuyatia nguvu makubaliano hayo na kutolea ufafanuzi nukta chanya za mwafaka huo. Vilevile ninawashukuru wakosoaji wote walioyachunguza kwa kina makubaliano hayo na kuonyesha nukta zake dhaifu na kutukumbusha sote kuhusu nukta hizo hasi hususan mkuu na wajumbe wa kamisheni maalumu ya Bunge na pia wajumbe waandamizi wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa ambao kwa kutoa maangalizo yao muhimu, wameweza kujaza mapengo yaliyokuwepo; na hatimaye ninamshukuru pia Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na wabunge kwa kupasisha kwa tahadhari kubwa muswada wa makubaliano hayo na kuionyesha serikali njia sahihi ya kuyatekeleza. Aidha ninalishukuru shirika la taifa la utangazaji (IRIB) na waandishi wa magazeti nchini ambao licha ya kuwa na mitazamo mingi tofauti kuhusu mwafaka huo, lakini wameweza kuwaonesha wananchi sura sahihi ya mwafaka huo. Kuweko majimui ya watu wote hao waliofanya kazi kwa bidii na kwa mazingatio makubwa kuhusiana na suala hili ambalo linaaminika kuwa ni moja ya masuala ambayo yatakumbukwa milele na yenye ibra kwa Jamhuri ya Kiislamu, kwenyewe kunafurahisha na kunapaswa kushukuriwa. Ni kwa sababu hiyo ndio maana mtu unaweza kusema kwa kujiamini kwamba, kuna malipo mema ya Mwenyezi Mungu kwa kila aliyetoa mchango wake wa kiuwajibikaji kwenye suala hilo na watapata pia nusra, rehema na uongofu kutoka kwa Mwenyezi Mungu Inshaallah kwani ahadi ya Mwenyezi Mungu ya kuwanusuru wanaoinusuru dini Yake haivunjiki.
2 – Mheshimiwa Rais! Umekuwemo kwenye masuala ya Jamhuri ya Kiislamu kwa miongo kadhaa sasa, bila ya shaka yoyote unajua vyema kwamba, serikali ya Marekani si katika kadhia ya nyuklia tu bali katika masuala mengine yote, haijawahi kuwa na msimamo wowote mzuri kuhusiana na Iran ghairi ya msimamo wa kiuadui na kujaribu kulikwamisha taifa la Iran katika mambo yake. Si jambo lililo mbali, katika siku za usoni pia, kuona Marekani ikiendeleza siasa hizo hizo kuhusiana na taifa letu. Matamshi ya Rais wa Marekani katika barua mbili alizoniandikia na kusema kuwa hana nia ya kuipindua Jamhuri ya Kiislamu, hayakudumu muda mrefu ila alikengeuka haraka ahadi zake hizo kwa kuunga mkono fitna ndani ya Iran na kuwasaidia kifedha wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu na kutoa vitisho vya wazi kuhusiana na kuishambulia kijeshi Iran - bali hata vitisho vya kutumia silaha za nyuklia; vitisho ambavyo vinaweza kutumika kufungua kesi kubwa dhidi yake katika mahakama za kimataifa – ni sehemu ndogo tu ya nia ya hasa ya viongozi wa Marekani dhidi ya taifa letu. Wataalamu wa kisiasa duniani na idadi kubwa ya wananchi wa mataifa ya dunia wanaelewa kwa uwazi kuwa jambo kuu linalopelekea kuwepo uadui huo usioisha wa Marekani dhidi ya taifa letu ni muundo na utambulisho wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran uliotokana na Mapinduzi ya Kiislamu. Kusimama kidete katika kutetea misimamo ya haki ya Kiislamu ya kupambana na mifumo ya kiistikbari na kibeberu, kusimama kidete mbele ya tamaa na kutotosheka madola ya kibeberu na kuyanyonya mataifa dhaifu, kufichua uungaji mkono wa Marekani kwa madikteta wa karne za kati na siasa zake za kuyakandamiza mataifa huru, kulihami bila ya kusita taifa la Palestina na mkundi ya mapambano ya kitaifa na vilevile kutoa sauti kubwa ya kimantiki na inayokubalika duniani dhidi ya utawala ghasibu wa Kizayuni, ni katika mambo makuu ambayo yanalifanya suala la kuweko uadui wa utawala wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu lisiepukike. Uadui huo utaendelea kuwepo hadi pale Jamhuri ya Kiislamu itakapowakatisha tamaa maadui kwa kutegemea nguvu zake za ndani na kuendelea mbele na misimamo yake bila ya kutetereka.
Mienendo na matamshi ya serikali ya Marekani katika kadhia ya nyuklia na mazungumzo yake marefu na ya kuchosha vimeonesha kuwa suala hilo pia ni miongoni mwa vizingo vya mnyororo wa uadui wao wa kikaidi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Udanganyifu wao katika misimamo yao ya kindumakuwili kati ya matamshi yao ya awali ambayo yalitolewa kwa nia ya kuifanya Iran ikubali mazungumzo ya moja kwa moja na ukiukaji wao wa mara kwa mara wa ahadi zao katika kipindi chote cha mazungumzo ya miaka miwili, na vilevile kufuata kwao matakwa ya utawala wa Kizayuni (Israel) na udiplomasia wao wa kutumia mabavu kuhusuiana na serikali na taasisi za Ulaya zilizohusika kwa njia moja au nyingine katika mazungumzo, yote hayo yanaonesha kuwa, kuingia kijanja Marekani kwenye mazungumzo ya nyuklia hakukufanyika kwa nia ya kutafuta ufumbuzi wa kiadilifu wa suala hilo bali kwa lengo ya kupeleka mbele malengo yake ya kiadui dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Hapana shaka kwamba, kuwa macho daima kuhusu nia za kihasama za serikali ya Marekani na kusimama kidete kwa maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu kumeweza kuzuia hasara kubwa katika mambo mengi.
Pamoja na hayo matokeo ya mazungumzo yaliyopatikana katika kalibu ya makubaliano ya nyuklia (JCPOA), yana nukta zisizoeleweka, udhaifu wa kimuundo na mambo mengine kadhaa ambayo iwapo hakutakuwepo uangalizi makini na wa wakati wote, yanaweza kusababisha hasara kubwa kwa kipindi cha sasa na kwa mustakbali wa nchi hii.
3- Vifungu 9 vya sheria iliyopasishwa hivi karibuni na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) na vipengee kumi vya maelezo yaliyotolewa kwenye maamuzi ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, vina mambo yenye faida na yenye taathira ambayo yanapaswa kuchungwa. Pamoja na hayo kuna nukta nyingine muhimu ambazo ninazibainisha hapa sambamba na kutilia mkazo mambo yaliyoelezwa katika hati hizo mbili.
Kwanza: Kutokana na kuwa kukubali Iran mazungumzo, kimsingi kulitimia kwa lengo la kuondolewa vikwazo vya kiuchumi na kifedha na kwa kuzingatia kuwa kutekelezwa kwa mazungumzo hayo chini ya mpango wa JCPOA kumeakhirishwa hadi Iran itakapotekeleza hatua inazopasa kutekeleza, ni dharura kuwepo dhamana madhubuti na za kutosha ili kuzuia upande wa pili kukiuka mapatano hayo. Miongoni mwa dhamana hizo ni kwa Rais wa Marekani na Umoja wa Ulaya kutangaza kimaandishi kwamba wataondoa vikwazo. Katika tangazo hilo la Umoja wa Ulaya na Rais wa Marekani inapaswa kubainishwa wazi kuwa vikwazo vyote vya Iran vimeondolewa. Kila aina ya matamshi yanayoashiria kuwa muundo wa vikwazo hivyo utaendelea kuwepo, ni sawa na kukiukwa makubaliano ya JCPOA.
Pili: Katika kipindi chote cha miaka minane, kuwekwa aina yoyote ya vikwazo na katika ngazi yoyote na kwa kisingizio chochote kile (vikiwemo visingizio vya kukaririwa-kaririwa na vya kujibunia vya ugaidi na haki za binadamu) na nchi yoyote ya upande wa mazungumzo, kutahesabiwa kuwa ni ukiukaji wa JCPOA na hivyo serikali inawajibika kuchukua hatua za lazima kusimamisha shughuli za JCPOA kwa msingi wa kipengee cha tatu cha sheria ya Bunge.
Tatu: Hatua zinazohusiana na mambo yaliyoashiriwa katika vipengee viwili vinavyofuata, zitaanza kutekelezwa tu baada ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia kutoa tangazo la kufungwa faili la maudhui ya hivi sasa na ya zamani (pmd).
Nne: Hatua ya kujengwa upya kiwanda cha Arak pamoja na kulindwa muundo wake wa maji mazito itaanza kutekelezwa tu baada ya kutiwa saini mkataba wa mwisho na wa kuaminika kuhusu mpango mbadala na kutolewa dhamana za kutosha za utekelezaji wake.
Tano: Mabadilishano ya urani iliyopo iliyorutubishwa na keki ya njano na serikali ya kigeni yataanza kufanyika tu baada ya kusainiwa mkataba wa kuaminika katika uwanja huo sambamba na kutolewa dhamana za kutosha. Muamala na mabadilishano yaliyotajwa yanapasa kutekelezwa taratibu na katika hatua kadhaa.
Sita: Kwa mujibu wa sheria ya Majlisi (Bunge), mpango na utangulizi wa dharura kwa ajili ya ustawi wa kipindi cha kati wa sekta ya nishati ya atomiki ambao unajumuisha njia za kisasa katika hatua tofauti kuanzia sasa hadi miaka 15 na kumalizikia kwenye SWU 190,000, unapaswa kutayarishwa na kuchunguzwa kwa makini katika Baraza Kuu la Usalama wa Taifa. Mpango huo unapasa kuondoa wasiwasi wowote unaotokana na baadhi ya masuala katika viambatisho vya JCPOA.
Saba: Shirika la Nishati ya Atomiki liratibu utekelezaji wa masuala ya utafiti na ustawi katika nyanja mbalimbali kwa namna ambayo, ifikapo mwishoni mwa kipindi cha miaka minane, kusiwepo na uhaba wowote kiteknolojia katika urutubishaji urani kwa kiwango kilichokubaliwa katika JCPOA.
Nane: Izingatiwe kwamba katika masuala ya JCPOA yenye utata, tafsiri ya upande wa pili (kundi la 5+1) haitakubalika, bali marejeo yatakuwa ni hati ya mazungumzo.
Tisa: Kutokana na kuwepo utata na shubha katika matini ya JCPOA, na vilevile, kutokana na kuwa na shaka kwamba upande wa pili hasa Marekani unaweza kukiuka ahadi, kwenda kinyume na makubaliano na kufanya hila na udanganyifu, kuna haja ya kuundwa jopo madhubuti, lenye uelewa na urazini kwa ajili ya kusimamia maendeleo ya kazi, kutekelezwa ahadi na makubaliano na upande wa pili na kuhakikisha yale yaliyobainishwa juu yanafikiwa. Muundo na majukumu ya jopo hili yanapasa yaainishwe na kupitishwa katika Baraza Kuu la Usalama wa Taifa.
Kwa kuzingatia mambo yaliyotajwa, masuala yaliyopitishwa kwenye kikao cha 634 cha Baraza Kuu la Usalama wa Taifa kilichofanyika tarehe 19/5/94 (10 Agosti 2015) yanaidhinishwa kwa kuchunga nukta zilizotajwa.
Kwa kumalizia, kama nilivyokukumbusha Janabi pamoja na viongozi wengine wa serikali kwenye vikao kadhaa, na kama nilivyowatanabahisha wananchi wetu azizi kwenye mikutano ya hadhara, japokuwa ni jambo la lazima kuondolewa vikwazo kwa maana ya kuondoka dhulma na kupatikana haki za taifa la Iran, lakini ustawi wa uchumi, hali bora ya maisha na kumalizwa matatizo yaliyopo hivi sasa hakutawezekana kirahisi isipokuwa kwa kuupa uzito unaotakiwa na kuufuatilia kwa pande zote uchumi ngangari. Ni matumaini yangu kwamba tahadhari zitachukuliwa kuhakikisha malengo haya yanafuatiliwa kwa uzito kamili na hasa kuupa umuhimu maalumu uimarishaji wa uzalishaji wa kitaifa. Aidha uwe na hadhari kuhakikisha hali ya baada ya kuondolewa vikwazo haiishii kwenye uingizaji bidhaa kiholela; na hasa hasa ihakikishwe kuwa hakuna bidhaa yoyote ya matumizi kutoka Marekani inayoingizwa nchini.
Ninamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu akupe taufiki wewe Janabi pamoja na viongozi wengine husika.
Sayyid Ali Khamenei
29 Mehr, 1394
(21 Oktoba, 2015)

 


700 /