Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei akihutubia wakurugenzi wa IRIB:

Lengo kuu la vita laini vya adui ni kubadili hakika ya Jamhuri ya Kiislamu na itikadi za wananchi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo (Jumatatu) amehutubia hadhara ya viongozi na wakurugenzi wa Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) na wajumbe wa baraza linalosimamia utendji wa shirika hilo akieleza malengo ya vita laini iliyoratibiwa, kubwa na ya pande zote ya mfumo wa ubeberu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu. Amesema kubadilisha itikadi za wananchi ndiyo lengo muhimu zaidi la vita hivyo tata. Ametilia mkazo nafasi ya kipekee ya IRIB katika mpambano huo mkubwa, na kusisitiza udharura wa kuwepo mipango mizuri na ya kitaalamu kwa ajili ya kutimiza majukumu ya Shirika la Utangazaji la Taifa.    
Mwanzoni mwa hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei amezungumzia umuhimu wa Shirika la Utangazaji la Taifa katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuashiria harakati adhimu ya upashaji habari na msaada wa vyombo vipya vya habari vilivyochomoza hivi karibu.  Amesema kuwa: Shirika la Utangazaji la Taifa (IRIB) liko katika medani ya mpambano huo wa ajabu na mkubwa, ambao ni medani tata na nzito mno ya vita laini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa wito kwa wanafikra, wasomi, watu wenye uchungu na taifa lao na wenye ari wasome na kuchunguza kwa kina vipenge mbalimbali vya vita laini na kuongeza kuwa: Malengo ya vita laini ni yale yale ya vita vya kutumia silaha, na tofauti yake ni kuwa katika vita laini, malengo yake yanafuatiliwa kwa kina na kwa upana zaidi.
Vilevile amegusia baadhi ya utata na hatari nyingi zaidi za vita laini ikilinganishwa na vita vya kutumia zana za kivita na kuongeza kuwa: Vita laini - tofauti na vita vya kutumia silaha na zana za wazi za kivita – si vya waziwazi, havieleweki na kuhusika na hata wakati mwingine, upande wa pili hutoa pigo, lakini jamii inayolengwa na mashambulizi hayo hupatwa na usingizi na haihisi wala kushughulishwa na mashambulizi hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Vita vya kutumia silaha kwa kawaida huzusha hasira za wananchi na kuzusha umoja na mshikamano wa kitaifa kati ya watu wa taifa linaloshambuliwa ilhali  vita laini huondoa msukumo wa kupambana na badala yake hutayarisha uwanja wa kuzuka hitilafu na mizozo ndani ya taifa linaloshambuliwa.
Baada ya kubainisha hatari kubwa na zenye kutia wasiwasi za vita laini, ikilinganishwa na vita vya kutumia silaha, Ayatullah Ali Khamenei ameongeza kuwa: Vita laini haviihusu Iran peke yake lakini kuhusiana na Iran, lengo kuu la vita hivyo vilivyopangiliwa vyema ni kubadili hakika na dhati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kubakisha sura na dhahiri yake tu.
Amesisitiza kuwa, kubadili batini na sira kuna maana ya kubadili azma, kaulimbiu, maarifa ya kimapinduzi pamoja na malengo yake makuu. Ameongeza kuwa: Katika fremu ya malengo ya vita laini vya adui, suala la kuendelea kuwepo jina la Jamhuri ya Kiislamu na hata kuwepo mtu mwenye kuvaa kilemba (mwanazuoni wa dini) katika nafasi ya juu kabisa ya utawala nchini, si jambo muhimu kwa adui, bali lililo muhimu kwake ni kuifanya Iran itumikie malengo ya Marekani, ya Uzayuni na ya kanali ya madola ya kibeberu duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, viongozi na wananchi ndio walengwa wakuu wa vita hivyo laini na kusisitiza kuwa: Kuhusu mipango ya vita laini vinavyowalenga viongozi nchini Iran ni kwamba nimeshazungumza na viongozi na nitaendelea kuzungumza nao juu ya jambo hilo, lakini walengwa wakuu wa vita laini ni wananchi hususan watu wenye vipaji, wasomi wa vyuo vikuu, wanachuo, vijana na wanaharakati walio mstari wa mbele katika jamii ya Iran.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Maadui wanataka kuwaathiri wananchi wa Iran na kubadilisha sehemu kubwa ya itikadi zao hususan vijana na watu wenye vipaji na ushawishi katika jamii. Amesema: Miongoni mwa mambo yanayolengwa na maadui hao ni itikadi za kidini, kisiasa na kiutamaduni za wananchi.
Ameongeza kuwa: Wananchi wetu wana itikadi zao maalumu kuhusu dini, familia, suala la wanawake na wanaume, uhuru, kupambana na mabeberu, demokrasia ya Kiislamu na masuala mbalimbali ya kiutamaduni na upande wa pili unafanya njama za kuvuruga au kubadili itikadi hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema miongoni mwa malengo ya vita laini ni kubadilisha itikadi na kurejesha za zamani. Amesisitiza kuwa: Wananchi wa Iran wana itikadi zao maalumu kuhusiana na utawala mbovu na wa kidikteta uliopita hapa nchini na kinachofanyika kwenye vita laini ni kujaribu kuyafanya mambo maovu, machafu na meusi ya kipindi hicho yaonekane mazuri na yenye kung’ara.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Kwa kubadili itikadi za sasa za wananchi na kurejesha za zamani, maadui wanataka wananchi wa Iran waamini kuwa, hakukuwepo haja wala ulazima wa kutokea Mapinduzi ya Kiislamu yaliyokuja kuangamiza maovu ya huko nyuma.
Amesema, kubadilisha itikadi za wananchi wa Iran kuhusu mustakbali na hali ya hivi sasa ni shabaha nyingine ya vita laini na kuongeza kuwa: Maadui wanafanya njama za kuwaonesha vijana wa leo nchini Iran kuwa, hali ya nchi yao hivi sasa inatia aibu na haiwezekani kabisa kupata maendeleo katika siku za usoni kupitia mfumo uliopo wa utawala, ili kwa njia hiyo wawakatishe tamaa vijana na kuwapokonya nguvu za kufanya harakati, kujielimisha na kufanya kazi kwa bidii.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaja njama za kujaribu kuleta itikadi zisizo za kweli ndani ya vijana wa Iran kuhusu masuala ya dunia hususan Marekani na Ulaya na kujaribu kuzidhihirisha nchi hizo kuwa zilizoendelea, zenye maisha bora na amani na bila ya matatizo yoyote, kuwa ni lengo jingine la vita laini. Ametoa muhtasari wa matamshi yake kuhusu maudhui hiyo akisema: Lengo kuu na la juu kabisa la vita laini ni kuisambaratisha ndani kwa ndani Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kubadili hakika na dhati yake kupitia njia ya kuharibu itikadi za watu na kudhoofisha imani zao hususan vijana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia uwezo wa vifaa na zana za kuendeshea vita laini za adui na kuongeza kuwa: Maendeleo na ustawi wa kila uchao katika mitandao ya Intaneti ni kwa ajili ya kufanikisha malengo ya vita laini, lakini muhimu zaidi ya zana na maendeleo hayo ni jeshi kubwa la watu wenye vipawa vikubwa katika masuala ya kifikra, siasa, fasihi, jamii na wanaharakati wakubwa wa vyombo vya mawasiliano na medani mbalimbali za sanaa, vitu ambavyo vina taathira na nguvu kubwa sana za kuweza kufanikisha malengo ya vita laini.
Vilevile ameitaja mipango na kufanya kazi kwa bidii na kwa uratibu kuwa ni katika sifa maalumu za wapangaji na waendeshaji wa vita laini na kuongeza kuwa: Katika kazi zote za uzalishaji wa vitu mbalimbali zikiwemo bidhaa za sauti, taswira na maandishi za upande unaolikabili taifa la Iran, kunafuatiliwa malengo ya kufanikisha vita baridi, lakini  mambo hayo aghlabu yanafanyika kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kueneza tabia ya kutekeleza mafundisho ya dini kwa kiwango cha chini sana na dini ya kisekula ambayo inaoana na mienendo ya kila aina ya watu binafsi na ya kijamii kuwa ni miongoni mwa malengo ya siri ya mipango mikuu ya kijamii yanayopiganiwa kufanikishwa na vyombo vya habari vya madola ya kibeberu na kuongeza kuwa: Maadui wana mipango kabambe na madhubuti ya kufuatilia malengo yao hayo tata mno, lakini sisi tuko nyuma katika uwanja huo.
Ayatullah Khamenei vilevile amepongeza juhudi zinazofanywa na chombo cha umma cha utangazaji, IRIB, na wakati huo huo ameongeza kuwa: Bidii na jitihada hizo zinapaswa kuimarishwa zaidi malengo yake yaenezwe kitaalamu bila ya ria wala kutia chumvi kwa kuzingatia uwezo wa vipindi na ratiba zote za shirika hilo la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili viweze kuwavutia walengwa na kuwafanya wavikubali.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, kazi muhimu zaidi ya kufanya kwa ajili ya kufanikisha malengo ya chombo hicho cha utangazaji cha taifa katika kupambana na vita laini vya maadui, ni kuwa na utafiti na tathmini ya kina, sahihi na kutilia maanani hali ya sasa ya ndani, ya kieneo na ya kimataifa ya Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Tathmini na utafiti huo utaziunganisha akili na misimamo ya viongozi na wakuu wa daraja mbalimbali ndani ya shirika hilo na ndio msingi wa harakati zote za shirika hilo.
Ayatullah Khamenei amesema kujiepusha na suala la kuongeza chumvi kuhusu uwezo uliopo, kuzingatia matatizo yaliyopo, kutokubali kuathiriwa na propaganda potofu za madola ya kigeni, kujiepusha na suala la kuangalia mambo kwa mtazamo finyu na wa kijuujuu na kutilia maanani uwezo wa hivi sasa na wa dhati vina taathira katika utafiti na tathmini ya kimsingi ndani ya Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ameongeza kuwa: Ulinganisho sahihi wa hali ya hivi sasa ya Iran na hali yaliyokuwa nayo mapinduzi makubwa duniani katika kipindi cha miaka kama ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, unaweza kutoa picha halisi ya hali ya hivi sasa ya Iran.
Ayatullah Khamenei amegusia matatizo mengi, vita vya ndani vya umwagaji damu na hata kurejea baadhi ya mapinduzi ya zama hizi kwenye tawala zilizopinduliwa na kuongeza kwamba: Hali ya hivi sasa ya Iran inapaswa kupimanishwa na hali iliyokuwa nayo Marekani miaka karibu arubaini baada ya kutolewa tangazo muhimu la uhuru wa nchi hiyo, na ilinganishe na hali iliyokuwa nayo Ufaransa baada ya miongo minne ya Mapinduzi Makubwa ya Ufaransa, ili hali ya sasa ya Iran na maendeleo makubwa yaliyopatikana hapa nchini baada ya ushindi Mapinduzi ya Kiislamu ieleweke vyema.
Akiendelea kueleza udharura wa kuwepo tathmini ya kimsingi na ya pande zote katika Shirika la Utangazaji la Iran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Kuna udharura wa kutiliwa maanani propaganda chafu za vyombo vya habari vya madola ya kibeberu ambavyo, ili kuweza kutimiza malengo yao ya vita laini, vinapindua kikamilifu ukweli wa mambo kuhusu Iran mbele ya walimwengu na hata kati ya Wairani wenyewe. Amesema, taswira inayooneshwa na vyombo hivyo vya madola ya kibeberu kuhusiana na dunia pia imepotoshwa kikamilifu.
Ayatullah Khamenei amependekeza kwa wakuu na wakurugenzi wa shirika hilo la utangazaji la taifa kwamba, ili kuweza kuwa na tathmini ya kina na ya kuzingatia ukweli wa mambo, wanapaswa kupimanisha baina ya nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu na hali ya baadhi ya nchi za eneo la Mashariki ya Kati ambazo zimekuwa zikiishi chini ya kivuli cha Marekani katika kipindi cha miongo minne iliyopita.
Vilevile amesema: Ulinganishaji huo utaonesha madhara makubwa ya kusalimu amri na kheri na maendeleo ya kusimama kidete.
Baada ya kutoa ufafanuzi kuhusu udharura wa Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa na tathmini ya kimsingi na ya kina kama msingi wa vipindi na ratiba zote za shirika hilo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha kazi ya pili ya chombo hicho cha utangazaji cha taifa kwa ajili ya kufuatilia malengo yake ipasavyo na kitaalamu akisema kuwa, kuna dharura kwa chombo hicho kuarifisha na kubuni fikra ya kimsingi.
Ayatullah Khamenei ameashiria stratijia na mikakati aliyoiwasilisha kwa Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) tangu baada ya kuteuliwa Bw. Sarafraz kuongoza taasisi hiyo na kusisitiza kuwa: Mikakati hiyo yote inapaswa kupewa umuhimu mkubwa na kuwekewa ratiba na mipangilio mizuri na ya kitaalamu. Hata hivyo amesema  kumefanyika kazi nzuri katika baadhi ya mambo kuhusu mikakati hiyo.
Ayatullah Khamenei amesisitiza udharura wa kuwepo ratiba na mipango mizuri ya kufanikisha stratijia iliyowasilishwa kwa Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB kwa ajili ya kufanikisha harakati za chombo hicho cha utangazaji cha taifa.
Amesema, taasisi hiyo ni chombo cha utangazaji cha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, nchi na Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Shirika la IRIB ni kambi iliyo mstari wa mbele na amilifu katika medani ya kupambana na vita laini na kwamba wakurugenzi na wafanyakazi wa chombo hicho cha utangazaji cha taifa, ni makamanda na wanajeshi kwenye vita hivyo.
Vilevile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa shukrani zake kutokana na jitihada na bidii kubwa zinazofanywa na wafanyakazi wa shirika hilo la utangazaji la taifa hususan Bw. Sarafraz, mkuu wa Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) na kusema kuwa, Bw. Sarafraz ni mtu mchapa kazi, mwenye bidii kubwa, mwenye hima, anayefanya kazi kwa utaratibu na mpangilio mzuri, asiyependa makuu na aliyejiweka mbali na masuala ya anasa, msafi na mwenye uchungu na mali ya umma, shujaa, jasiri wa kuchukua maamuzi mazito, mbunifu, mwenye mawazo mapana na anayekwenda na wakati.
Ameongeza kuwa: Sifa hizo zenye thamani kubwa zinastahiki kupongezwa na zinapaswa kudumishwa. Amesema sifa hizo ni jambo la dharura kwa shirika kama IRIB ambalo ni shirika lenye nafasi na umuhimu mkubwa sana ikilinganishwa na taasisi nyinginezo hapa nchini.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Bw. Muhammad Sarafraz, Mkuu wa Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) ametoa ripoti fupi kuhusu mipango na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na shirika hilo.
Amegusia changamoto na matatizo mbalimbali linayokumbana nayo shirika hilo la utangazaji la taifa na kusema: Kufanyia marekebisho muundo wa kiidara na vilevile marekebisho ya ajenda na sheria za shirika hilo, kuandaa utangulizi wa kuanzishwa mfumo unaokubalika wa upashaji habari, kuweka mipango kwa ajili ya kuimarisha nafasi ya IRIB katika mitandao ya Intaneti na mitandao ya kijamii ya simu za mkononi na kuongeza ubora wa vipindi vya chombo hicho cha utangazaji ni miongoni mwa harakati na mikakati muhimu zaidi ya Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ameongeza kuwa: Kufuatilia masuala muhimu na ya kimsing kama vile kueneza fikra za Mapinduzi ya Kiislamu, uchumi ngangari, mtindo wa maisha ya Kiirani - Kiislamu na ustawi wa kielimu, kuasisiwa kituo maalumu cha kupanua uandikaji wa miswada ya filamu, kupangiliwa upya na kuanzishwa kanali ya televisheni ya watoto, kuanzishwa kundi la elimu ya ujumi (aesthetics) na sayansi za utambuzi (cognitive Sciences),  kutumiwa nguvu kazi kijana na za waumini katika uongozi wa vitengo mbalimbali vya shirika hilo, kuongeza idadi ya walengwa na vipindi vya shirika hilo la utangazaji la taifa na kuongeza taathira na ushawishi wa kanali za televisheni za al Alam na Press TV, kuanzisha Shirika la Habari la IRIB, kufanywa ya kisasa na ya kiutaalamu zaidi Kanali ya Habari, kusisitizia mno suala la kufayiwa uchambuzi na kutolewa ufafanuzi matukio mbalimbali, kuanzishwa kanali za televisheni za lugha za Azari, Kikurdi na Kiurdu ndani ya Kitengo cha Matangazo ya Ng'ambo cha Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB), kuzalishwa upya vyanzo mbalimbali vilivyohifadhiwa katika kitengo cha kuhifadhi vitu tofauti, kuupa umuhimu mkubwa muziki wa kidini na wa kimapinduzi, kuzingatia umuhimu wa imani ya wananchi na kuwafanya wahisi kwamba wanaishi katika usalama, ni mipango na hatua nyingine za shirika hilo la utangazaji la taifa.

700 /