Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Kubakia hai malengo na nara za Mapinduzi kunamkasirisha adui

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo asubuhi (Jumatano) amehutubia hadhara ya wanafunzi wa vyuo vikuu na vijana wenye vipaji bora vya kielimu nchini akitoa nasaha na tahadhari muhimu kwa watu wenye vipawa na viongozi nchini. Pia amesisitizia ulazima wa kuipa uzito wa hali ya juu taasisi ya watu wenye vipawa ikiwa ni taasisi ya kitaifa na ya kiistratijia na vilevile kuandaa uwanja wa kuchanua na kutoa msaada wa kielimu vijana hao wenye vipaji katika jamii. Amesema, mashirika ya elimu za kimsingi ni miongoni mwa nguzo kuu za uchumi ngangari na wa kusimama kidete. Ameongeza kuwa: Kutokana na baraka za malengo, kaulimbiu na harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu katika jamii, na kushiriki kwa wingi vijana wenye vipawa katika medani mbalimbali na harakati adhimu na yenye kasi kubwa ya maendeleo ya kielimu na kitekonolojia ambayo imeanza nchini Iran, mustakbali wa nchi hii ni mustakbali bora ulio wazi, unaong'ara na utakaokuwa na maendeleo, nguvu na ushawishi mkubwa zaidi wa kimaanawi katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kwa ujumla na kwamba watu ambao wanajaribu kudhoofisha moyo wa vijana wa Iran na kuwakatisha tamaa kuhusu hali yao ya hivi sasa na mustakbali wao, wanafanya usaliti kwa nchi na kwa heshima na matukufu ya taifa.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kuonana na vijana wenye vipawa, wenye misimamo na wenye nishati ni faraja sana kwake na kunazidisha matumaini moyoni. Ameashiria namna vijana wa Iran walivyo werevu na walivyo na akili nyingi ikilinganishwa na wastani wa vijana wa mataifa mengine duniani na kuongeza kuwa, kutokana na kwamba nguvu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nguvu za dhati, vijana weledi wa mambo, wenye imani thabiti, wawajibikaji na wenye vipawa, ni moja ya fursa bora na utajiri mkubwa kwa taifa.
Baada ya kutoa utangulizi huo, Ayatullah Khamenei ametoa nasaha kadhaa kama baba kwa vijana hao wenye vipaji. Amesema, kuwa kipawa ni neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu na nasaha yake ya kwanza kabisa kwa vijana hao ni kuwataka wamshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hiyo. Amewaambia vijana hao walioshika nafasi za juu kielimu nchini kwamba: Vipaji hivyo ni katika baraka za Mapinduzi ya Kiislamu kwani mapinduzi hayo matukufu yamewapa vijana wa Iran shakhsia bora, utambulisho na ujasiri na hivyo kupata fursa ya kutumia vizuri uwezo na vipaji vyao.
Ayatullah Khamenei amemeyataja mafanikio ya vijana wa Iran ya kutwaa nafasi na daraja bora za kielimu kati ya nchi mia mbili duniani kuwa ni matunda mengine ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kwamba: Iran leo hii imefika kwenye daraja ya juu ya kielimu katika hali ambayo katika kipindi chote cha zaidi ya miongo mitatu iliyopita, imekumbwa na vizuizi mbalimbali kama vile vita vya kulazimishwa (vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya utawala mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran), na muda wote huo imekuwa chini ya mashinikizo ya kila namna ya kisiasa na vikwazo vya kiuchumi.
Vilevile amewambia vijana hao wa Iran wenye vipawa kwamba: Nafasi hiyo bora ya kielimu mumeipata kutokana na kuweko usalama na amani nchini, hivyo mnapaswa kujua thamani ya watu wanaosabilia kila kitu kwa ajili ya kulinda usalama wa nchi na wa taifa lenu kama vile shahidi Hamedani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja maziko ya shahidi Hamedani yaliyofanyika kwa kufana na kwa kushiriki wimbi kubwa la watu hususan katika mji wa Hamedan kuwa yanaonesha namna taifa la Iran linavyowathamini na kuwajali watu wanaojitolea katika njia ya kudhamini usalama wa nchi yao na kuongeza kuwa: Kama usalama utakosekana, utafiti na kazi zote za vyuo vikuu na maendeleo ya kielimu ya nchi nayo hayatakuwepo.
Kutanguliza mbele moyo wa jihadi na kujitolea kuliko moyo wa kujiona juu na bora zaidi, ni nasaha ya pili iliyotolewa na Ayatullah Khamenei kwa vijana hao wenye vipawa.
Amesema, miongoni mwa magonjwa makubwa wa watu wenye nafasi za juu katika jamii ni kujiona bora mbele ya wengine na kusisitiza kuwa, hayo ni miongoni mwa maradhi mabaya ya kinafsi ambayo inabidi mujiepushe nayo na msiruhusu kabisa yakukumbeni, na kwamba njia pekee ya kukabiliana na maradhi hayo ni kuimarisha moyo wa jihadi katika nafsi zenu na kufanya kazi kwa bidii na juhudi zenu zote kwa nia moja tu ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu na kuitambua kila kazi mnayoifanya kuwa ni wadhifa wenu wa kidini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, kushiriki katika kambi na safari za pamoja za kijihadi ni miongoni mwa njia za kuimarisha moyo wa kijihadi na kuongeza kuwa: Kushiriki kwenye kambi za kijihadi huwa sababu ya kuwaelewa vizuri wananchi na kutambua vyema mashaka na matatizo ya jamii.
Ayatullah Khamenei amegusia pia uzoefu wake wa muda mrefu katika miaka ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na namna baadhi ya maafisa wasivyojuwa uhakika wa mambo na matatizo yaliyopo katika jamii hususan katika maeneo ya vijijini na kwenye miji ya mbali na kusema kuwa, matatizo yanayowatesa watu wa familia maskini ni miongoni mwa mashaka, tabu na shida zilizopo katika jamii nchini. Ameongeza kwamba, kuwa katika kambi za kijihadi ni fursa nzuri kwa vijana kuweza kujua hali halisi ilivyo kwenye maeneo hayo na vilevile ni fursa nzuri ya kuweza kutoa huduma za moja kwa moja kwa wananchi.
Amekosoa safari za pamoja za wanafunzi wa vyuo vikuu kuelekea na kupiga kambi katika baadhi ya nchi za Ulaya licha ya maonyo yaliyotolewa huko nyuma na kusisitiza kuwa: Safari za namna hiyo ni moja ya mambo mabaya na makosa makubwa, na kwamba kambi za kijihadi ni bora mno na za heshima zaidi, kuliko safari hizo za kwenda barani Ulaya.
Katika nasaha zake za tatu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewausia vijana wenye vipaji kubakia nchini na badala ya kwenda katika nchi za kigeni kwa matumaini kupata hali bora aidi. Amesema fanyeni uhandisi sahihi wa nchi na kudhamini bongo, silisila ya mishipa na kiunzi cha mifupa ya jamii badala ya kwenda nje ya nchi na kutumbukia kwenye mfumo wa mmeng'enyo usio na huruma na wenye tamaa wa wageni.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia matatizo na baadhi ya mapungufu yanayoonekana nchini licha ya kuwepo maendeleo na uwezo wa kila namna na kuongeza kuwa: Kubakia nchini na kufanya bidii za kuondoa mapungufu na matatizo yaliyopo na kuwa chanzo cha tathira nzuri kwa wananchi ni jambo la fakhari na heshima.
Kutoduwaa mbele ya Wamagharibi ni nasaha za nne za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa vijana wenye vipawa bora vya kielimu nchini na amelitolea ufafanuzi zaidi suala hilo akisema: Ijapokuwa wamagharibi wamepiga hatua kubwa katika upande wa sayansi na teknolojia, lakini hatupaswi kuduwazwa na jambo hilo kwani nguvu na uwezo wa dhati wa vijana wa Kiirani ni mkubwa zaidi. Amesema, kama mtu ataamua kulinganisha hali ya Iran na maeneo mengine, basi inabidi alinganishe baina ya kipindi cha zaidi ya miongo mitatu iliyopita ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na zaidi ya kipindi cha miongo mitatu ya nchi nyingine, baada ya nchi hizo kupata uhuru.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: Kizazi cha hivi sasa cha vijana kinaweza kujiletea fakhari za maendeleo na kupiga hatua kubwa za ustawi wa kielimu na kuimarisha misingi ya kujitegemea kielimu nchi yao kwa heshima na fakhari kubwa.
Baada ya hapo ameanza kutoa nasaha kuhusiana na uongozi na usimamiaji wa mambo kwa viongozi hapa nchini na pia kwa vijana wenye vipaji, kwa kusisitizia ulazima wa kuipa umuhimu na uzito wa hali ya juu Taasisi ya Watu Wenye Vipaji nchini. Ameongeza kuwa: Taasisi ya Watu wenye Vipawa ni taasisi ya kitaifa na ya kiistratijia, hivyo si sahihi kuviachia vyuo vikuu tu kuendesha taasisi muhimu kama hiyo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu vilevile ameitaka Taasisi ya Watu Wenye Vipaji nchini Iran kuwa na mipangilio mizuri kwa ajili ya kuandaa uwanja na mazingira mazuri ya kudhihiri na kujitokeza kivitendo uwezo na vipaji bora vya vijana nchini. Amesisitiza kuwa: Inabidi vijana wenye vipaji waandaliwe mazingira mazuri ya kazi na kuhisi kuwa wana manufaa na faida kubwa kwa jamii na kuwashawishi wabakie nchini.
Ayatullah Khamenei ametaja baadhi ya hatua muhimu zinazopaswa kuchukuliwa na watu wenye vipaji kwa ajili ya kuendelea na harakati ya kielimu nchini Iran kuwa ni pamoja na kusahilishwa mchakato mzima wa masomo wa watu wenye vipawa, kupanuliwa na kustawisha mwenendo wa kuunda mashirika mbalimbali ya elimu za kimsingi na kuanzishwa vitengo mbalimbali vya kielimu katika vyuo vikuu chini ya usimamizi wa wahadhiri wenye itikadi madhubuti za kidini na wanamapinduzi. Amesisitiza kuwa mchango wa wahadhiri katika vitengo mbalimbali vya kielimu una umuhimu mkubwa  na inabidi watumiwe walimu ambao wana itikadi ya kujenga na kustawisha mustakbali bora wa Iran, wenye uchungu wa nchi na wanaoshikamana na matukufu ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Vilevile ameitaka Taasisi ya Watu Wenye Vipawa nchini Iran kufuatilia daima matunda na matokeo ya kazi mbalimbali zinazofanyika nchini. Ameashiria suala la uchumi ngangari na wa kusimama kidete  na kusema: Moja ya njia za kufanikisha siasa za uchumi ngangari na ambayo ilitangazwa tangu mwanzoni kabisa mwa harakati za uchumi huo na kuungwa mkono na wanafikra nchini, ni kuyasaidia na kuyaunga mkono mashirika ya elimu za kimsingi na kuwa na ratiba na mipango maalumu ya kufanikisha jambo hilo.
Vilevile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kwa haraka haraka nukta nyingine kuhusiana na uchumi ngangari akisema: Kuhusu namna ya kuendesha na kuendeleza sera za uchumi ngangari hivi sasa muda hauruhusu kulizungumzia suala hilo, lakini siridhishwi na kasi ya hivi sasa ya utekelezaji wa sera hizo.
Baada ya kubainisha nukta hiyo, Ayatullah Khamenei amezungumzia ulazima wa kuweko mpango makini wa kutumiwa vizuri uwezo wa mashirika ya elimu za kimsingi kwa ajili ya kufanikisha siasa za uchumi ngangari na kuongeza kwamba: Ninatoa pendekezo kwamba maudhui ya moja ya vikao vya vijana wenye vipaji iwe ni maalumu kwa ajili ya kujadili namna vijana hao wanavyoweza kutoa michango yao katika uchumi ngangari, ili tuweze kuandaa mpango wa kitaifa kwa kutumia fikra na elimu ya vijana.
Amesema kuwa, suala la kutafuta na kulea vipaji bora katika shule za msingi na za elimu ya kati lina umuhimu mkubwa sana. Ameashiria mpango uliopewa jina la "Shehab" katika Wizara ya Elimu na Malezi ya Iran kusema: Waziri wa Elimu na Malezi anapaswa kusimamia yeye mwenyewe utekelezaji wa mpango huo na kuufanyia uchunguzi wa kina na asiruhusu mpango muhimu kama huo kudharauliwa na kutothaminiwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kutoa onyo kuhusu mambo kadhaa. Onyo la kwanza limehusiana na watu ambao wanatumia magazeti, majarida, majukwaa na mimbari kufanya kampeni za kuwakatisha tamaa muda wote wananchi na vijana na kukanusha maendeleo ya kielimu na mafanikio makubwa ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka viongozi nchini kuwa macho na makini kuhusu watu wa namna hiyo na kusisitiza kwamba: Maendeleo ya kustaajabisha ya kielimu ya Iran katika nyuga za nano, seli shina na teknolojia ya nyuklia si ndoto, bali ni uhakika ambao unajulikana wazi dunia nzima; hivyo kitendo cha kuwakatisha tamaa vijana na kukanusha harakati adhimu na yenye kasi kubwa ya kielimu na kiteknolojia ya taifa la Iran, ni usaliti kwa nchi na kwa heshima na kwa matukufu ya taifa.
Ayatullah  Khamenei amegusia pia mrengo wa watu ambao wanawatafuta watu wenye vipaji vya kielimu nchini na kuwaelekeza nje ya nchi na amewataka viongozi kuwa macho mbele ya mrengo huo. Amesema: Tahadhari yangu nyingine inahusiana na baadhi ya viongozi, wakuu na baadhi ya wahadhiri wanaokabiliana na watu waumini, wanamapinduzi na walioshikamana vilivyo na mafundisho ya dini katika vyuo vikuu na mawaziri wanapaswa kuwa macho kikamilifu kuhusu kadhia hiyo na wasiruhusu jambo hilo kutokea.
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa muhtasari wa hotuba yake na kusema: Mimi nina ushahidi wa matumaini mazuri kuhusu mustakbali bora wa Iran.
Vilevile ameashiria namna kundi kubwa la vijana nchini Iran linavyohisi kwamba ni jukumu lao kulitumikia taifa na nchi yao na kusema kuwa, sehemu kubwa ya vijana hao ni wale wenye vipaji. Aidha amegusia kuendelea kuwa hai malengo, kaulimbiu, nara na harakati ya kimapinduzi katika jamii ya Iran na kusema: Hii ndio sababu kuu inayowafanya maadui walikasirikie taifa la Iran, na kwa msingi huo wanasema, itakuwa vigumu sana kukabiliana na Iran madhali kaulimbiu za Mapinduzi ya Kiislamu ziko hai nchini.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Hivi sasa kaulimbiu na malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu yako hai katika jamii ya Iran kiasi kwamba hata baadhi ya watu wasioshikamana na kaulimbiu hizo wanalazimika kujionesha kidhahiri kuwa wako pamoja na kaulimbiu hizo, na Mapinduzi ya Kiislamu yanazidi kusonga mbele kwenye njia yake iliyonyooka. Amesisitiza kuwa jambo hili linayapambanua Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na mapinduzi mengineyo makubwa duniani.
Vilevile amesisitiza kuwa: Madhali harakati na fikra ya Mapinduzi ya Kiislamu itaendelea kuwepo nchini, maendeleo, ustawi na nguvu za Iran zitaendelea kuongezeka siku hadi siku na kuzidi kuwa na nafasi ya juu ya ushawishi wa kiroho na kimaanawi katika eneo la Mashariki ya Kati na nje ya eneo hili.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Dk Sattari, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika masuala ya sayansi na teknolojia ambaye pia ni mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Watu Wenye Vipawa nchini Iran ametoa hotuba fupi na kusema kuwa, kipaumbele kikuu cha leo hii nchini ni kuipa mazingatio makubwa elimu na teknolojia. Ameongeza kuwa: Iran hivi sasa inawahitajia sana watu wenye vipaji vya kila namna ambao kwa kujiamini na kwa kufanya kazi kwa bidii, wanaweza kuiletea nchi mafanikio makubwa katika nyuga zote kama walivyofanya katika nyuga za teknolojia ya "Nano na Bio" (Nanobioteknolojia).
Makamu wa Rais wa Iran katika masuala ya sayansi na teknolojia amebainisha pia kuwa, watu wenye vipaji wana deni kubwa kwa nchi yao na kuongeza kuwa: Hatupaswi baada ya kuondolewa vikwazo, kuifanya nchi yetu kuwa soko tu la matumizi ya bidhaa zinazotoka nje ya nchi, bali tunapaswa kuhakikisha kuwa, tunazalisha wenyewe teknolojia za kila namna ili kwa njia hiyo tuweze kuongeza utajiri wa nchi yetu kupitia uzalishaji wa elimu.
Dk Sattari amesisitiza pia kwamba kuna wajibu wa kuingia sekta binafsi katika uwanja wa utafiti kama ambavyo kuna udharura kwa kuweko uwekezaji katika fikra na ubunifu wa watu wenye vipawa na kuongeza kuwa: Kuongezeka nishani za ubora wa kimasomo wanazopata wasomi wa Iran, kuupa kipaumbele utafiti wa masuala ya kimsingi, kutekeleza mpango wa Shehab, kuviunga mkono na kuvisaidia vitengo vya utafiti vya wanafunzi wa shule za msingi, kupanua wigo wa kazi za watu wenye vipawa na kulipa umuhimu mkubwa suala la udiplomasia wa kiteknolojia, ni miongoni mwa hatua muhimu zilizochukuliwa na Idara ya Sayansi na Teknolojia ya Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Taasisi ya Taifa ya Watu Wenye Vipaji nchini.

700 /