Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Mapambano dhidi ya ubeberu yanaungwa mkono na akili na tajiriba

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo (Jumanne) amehutubia hadhara ya maelfu ya wanachuo na wanafunzi wa wengine hapa nchini akisema kuwa mapambano ya taifa la Iran dhidi ya ubeberu ni mapambano ya kimantiki, kiakili na yanayotegemea tajiriba na uzoefu wa kihistoria. Ameashiria matatizo na madhara yaliyotokana na kuiamini Marekani na upeo mfupi wa kifikra wa baadhi ya wanasiasa katika historia ya sasa ya nchi hii na kusema: Marekani ndiyo ileile Marekani ya zamani lakini baadhi ya watu waovu au wapumbavu wanafanya jitihada za kulisahaulisha na kulighafilisha taifa na adui huyo anayefanya njama ili Marekani iweze kupiga hanjari mgongoni katika kipindi mwafaka.
Katika mkutano huo uliofanyika kwa mnasaba wa kumbukumbu ya siku ya tarehe 13 Aban (4 Novemba ) ambayo ni Siku ya Kitaifa ya Kupambana na Ubeberu wa Kimataifa nchini Iran, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekitaja kipindi cha sasa kuwa ni zama za kuthabitisha izza na heshima ya taifa na kuchora ramani ya njia ya maendeleo ya Wairani. Amesema ni jambo muhimu sana kuwa macho, werevu na kuona mbali umma hususan vijana katika kipindi hiki.
Amesema kuwa nukta muhimu katika kufahamu na kuchambua hali ya sasa na kuanzisha harakati ya mustakbali wa nchi ni kuelewa vyema uhakika kwamba mapambano ya Jamhuri ya Kiislamu na wananchi wa Iran dhidi ya ubeberu, -kinyume na maneno yanayosemwa na badhi ya watu,- si harakati isiyo na mantiki na ya jazba, bali ni mapambano yanayotokana na akili na tajiriba na yanayoegamia kwenye msingi wa elimu.
Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa, kutilia maanani uzoefu unaotoa darsa na somo wa mataifa mbalimbali kunazuia macho kufanya makosa na kukosea katika mahesabu. Ameongeza kuwa: Lau tutafumbua macho aya za Qur’ani tukufu zinazohusu kusimama kidete na kupambana na dhulma na ubeberu, basi hapana shaka kuwa tukio kubwa la mapinduzi ya tarehe 28 Mordad mwaka 1332 (19 Agosti 1953) linaonesha jinsi ya kuamiliana na Marekani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza matukio ya kipindi muhimu cha kutaifishwa sekta ya mafuta hapa nchini na kusema, kuiamini na kuwa na matumaini na Marekani ni kosa la kihistoria la Dakta Muhammad Mosaddeq (waziri mkuu wa Iran wa kipindi hicho). Ameongeza kuwa, Musaddiq aliitegemea Marekani kwa ajili ya kukabiliana na Uingereza na matarajio hayo, fikra finyu na mghafala huo vilitayarisha mazingira ya kufanikiwa mapinduzi ya Kimarekani hapa nchini, mapinduzi ambayo yaliharibu kazi zote zilizokuwa zimefanywa na taifa katika kutaifisha sekta ya mafuta, yakahuisha utawala wa kidikteta na tegemezi wa Pahlavi na kuiweka Iran azizi katika matatizo makubwa sana ya kitaifa na mapigo ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni kwa kipindi cha miaka 25.
Ayatullah Khamenei ameashiria satua na ushawishi mkubwa wa Wamarekani nchini Iran baada ya mapinduzi ya tarehe 19 Agosti 1953 na kusema: Mkabala wa mashaka kama hayo, mataifa ambayo hayana viongozi wanaofaa huathirika na kusalimu amri, lakini taifa la Iran kwa kutumia hiba ya Mwenyezi Mungu ya uongozi wa Imam Khomeini, lilipevuka na kupevuka zaidi hatua kwa hatua na likalenga serikali tegemezi ya kipahlavi na muungaji mkono wake mkubwa yaani Mrekani kwa kutumia harakati na mwamko wa Kiislamu. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ushahidi wa hotuba ya Imam Khomeini hapo mwaka 1342 (1963) kuhusu chuki kubwa ya taifa la Iran dhidi ya rais wa Marekani na kusema: Kiongozi huyo imara na mwenye azma thabiti ambaye alikuwa na imani kubwa kwa ahadi za Mwenyezi Mungu, tangu hapo mwanzoni mwa harakati aliwaeleza wananchi wa Iran kwamba njama na shari zote zinatokana na Marekani.
Amekumbusha uadui wa Marekani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu tangu kipindi cha miezi ya mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi na kusema: Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini, Wamarekani kwa kipindi fulani walikuwa na ubalozi mjini Tehran na vilevile walikuwa na uhusiano na serikali ya Iran lakini hawakuacha kufanya njama hata siku moja, na uzoefu huu wa kihistoria unapaswa kuwafahamisha baadhi ya watu kwamba, kuwa na uhusiano na urafiki (na Marekani) hakukomeshi uhasa na njama za nchi hiyo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kutekwa ubalozi wa Marekani mjini Tehran kulikofanywa na wanafunzi wa vyuo vikuu lilikuwa jibu dhidi ya njama zilizokuwa zikifanywa na Washington hapa nchini na kumpa hifadhi adui mkubwa wa taifa la Iran yaani Muhammad Reza Pahlavi. Ameongeza kuwa: Nyaraka zilizopatikana ndani ya ubalozi wa Marekani zilionesha kuwa, ubalozi huo kwa hakika ulikuwa pango la ujasusi na kituo cha kupanga njama daima dhidi ya taifa la Iran na Mapinduzi machanga ya Kiislamu hapa nchini.
Amesema kutafakari kwa kina ndani ya nyaraka zilizopatikana kwenye pango la ujasusi la Marekani mjini Tehran (ubalozi wa Marekani) ni jambo lenye umuhimu na linalotoa somo na kusema: Nyaraka hizo zinaonesha waziwazi kwamba, katika kipindi chote cha kuanza harakati ya wananchi, katika makabiliano ya utawala muovu wa kifalme na wananchi na vilevile baada ya Mapinduzi, Wamarekani daima walikuwa wakifanya jitihada za kutoa pigo dhidi ya taifa la Iran.
Ayatullah Khamenei ameashiria kumbukumbu zilizoandikwa na Robert E. Huyser, jenerali wa Kimarekani ambaye katika msimu wa baridi kali wa mwaka 1357 (1979) alikuja Iran kwa ajili ya kuuokoa utawala wa kidhalimu wa Shah na akasema: Kumbukumbu hizo zinaonesha vyema kwamba, kivitendo, Marekani ilikuwa ikiwaongoza na kuwahamasisha majenerali wa utawala wa Kipahlavi kuwaua wananchi wa Iran.  
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kutoa misaada kwa harakati zilizotaka kujitenga na dhidi ya Mapinduzi, mapinduzi yanayojulikana kwa jina na Nojeh, kumhamasisha Saddam Hussein aishambulie Iran na misaada ya mara kwa mara ya Washington kwa dikteta aliyechukiwa wa Baghdad katika kipindi chote cha miaka 8 ya vita vya kulazimishwa ni sehemu ya vizingo vya mnyororo wa njama za Marekani dhidi ya Iran.
Amesisitiza kuwa katika kipindi cha miaka 37 iliyopita Wamarekani ambao wameelewa vibaya na wameshindwa kuchambua uhakika wa mambo nchini Iran, wamefanya jitihada za kufanya mapinduzi hapa nchini lakini kwa baraka zake Mwenyezi Mungu wameshindwa na wataendelea kushindwa.
Ayatullah Khamenei amesema lengo la kukumbusha mlolongo wa njama za Shetani Mkubwa ni kutaka kuujua vyema zaidi Marekani. Ameongeza kuwa: Katika miaka ya hivi karibuni kuna watu waovu na wanaoongozwa na Marekani au wajinga wanaofanya jitihada za kupuuza uzoefu wa mara kwa mara wa taifa na kutaka kuchora taswira iliyopambwa na kurembwa kuhusu Marekani na kuonesha kuwa, kama Wamarekani awali walikuwa adui wa Iran, hii leo wametupilia mbali uadui huo!
Amesema kuwa, lengo la jitihada hizo ni kutaka kuficha sura halisi ya adui katika fikra za watu ili Wamarekani wadumishe uadui wako chini kwa chini na kwa siri na wapige hanjari mgongoni mwetu wakati mwafaka.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Ukweli ni kuwa malengo ya Marekani kuhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hayajabadilika hata kidogo na kama wataweza kuiangamiza Jamhuri ya Kiislamu basi hawatasita kufanya hivyo hata dakika moja, lakini hawawezi; na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu, hima ya vijana, upeo mkubwa na kuona mbali kwa taifa na maendeleo ya Iran, watashindwa kufikia malengo yao pia katika siku za usoni.
Amegusia baadhi ya mienendo ya kulegeza kamba Marekani kimaonesho tu katika mazungumzo na kusema: Batini na undani wa mwenendo wa Marekani ni kufuatilia malengo yaleyale ya kihasama ya huko nyuma na taifa la Iran haliweza kusahau ukweli huo.   
Katika uwanja huo huo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Mmoja kati ya maafisa wa Marekani katika mazungumzo alizungumzia jinsi anavyochukizwa na vita na hata akalia; badhi ya watu wapumbavu yumkini wakaamini jambo hilo lakini himaya kubwa na misaada isiyosita ya Marekani kwa utawala wa Israel unaotenda jinai, chinjachinja na unaoua watu na himaya ya Wamarekani kwa jinai zinazofanywa dhidi ya watu wa Yemen vinaanika waziwazi utambulisho halisi wa madai na kulia huko.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria uhusiano wa kawaida wa Iran na nchi mbalimbali duniani na hata nchi ambazo hazina moyo safi kwa taifa la Iran na akasema: Kwa mwenedo huu, wananchi wa Iran hawawezi kuiangalia kwa hicho la rafiki Marekani ambayo inatumia kila kitu kwa ajili ya kutoa pigo dhidi ya taifa la Iran na kuiangamiza Jamhuri ya Kiislamu, wala hawatainyooshea mkono wa urafiki kwa sababu dini, akili, dhamira na ubinadamu haulipi taifa la Iran haki ya kufanya hivyo.  
Ayatullah Khamenei amezungumzia pia harakati za pande zote zinazoendelea kufanywa na Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na kusema: Wamarekani wamejua kwamba sababu ya kusimama kidete taifa la Iran ni imani na itikadi za kidini, kwa msingi huo wanashambulia itikadi na thamani hizo kwa kutumia nyenzo za kisasa, lakini wanafunzi, wanachuo na vijana wetu watabatilisha njama na hila hilo.
Amesema kuwa adui anafanya jitihada kubwa ili vyuo vikuu viwe daraja ya kuelekea Magharibi kama hali ilivyokuwa katika kipindi cha fedheha cha utawala wa kifalme hapa nchini, lakini kutokana na kuwa macho kwa vijana wetu azizi, vyuo vikuu vumekuwa ngazi ya kuelekea kwenye malengo ya muda mrefu, na vijana wetu watalinda nafasi hii yenye taathira kubwa.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa maendeleo na uwezo mkubwa wa taifa la Iran ndiyo sababu iliyowaleta maadui katika meza ya mazungumzo ya nyuklia na kuongeza kuwa: Katika mazungumzo hayo pia maadui hao walichukua hatua za kiadui ili asaa wakakwamisha harakati za taifa la Iran.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, sisitizo juu ya uadui mkubwa wa Marekani dhidi ya taifa la Iran halina maana ya kufumbua jicho baadhi ya udhaifu wa ndani ya nchi. Ameongeza kuwa katika upangaji wa sera, utekelezaji wake, juhudi na harakati, kupanga vipaumbele vya mambo mbalimbali na masuala mengine tuna udhaifu ambao adui ameutumia.
Amesema kuwa kughafilika na adui halisi na kushughulishwa na malumbano ya ndani ni makosa makubwa. Ameongeza kuwa: Baadhi ya watu wanasahau adui wa nje kwa kisingizio cha udhaifu na masuala ya ndani.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, hatupasi kumfananisha adui na wale tunaohitilafiana nao katika mitazamo; adui ni yule anayetumia uwezo wake wote kwa ajili ya kutoa dharba na pigo dhidi ya taifa na anataka kuweka madarakani serikali kibaraka, isiyo na maana, iliyosalimu amri na kutishwa na Magharibi, na hatupasi kumsahau adui huyu mwenye kinyongo katika hali zote.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Kukosoa ni ishara ya maendeleo, na jamii iko huru na ina haki ya kukosoa; hata hivyo hatupasi kusahau maneno ya kihistoria ya Imam Khomeini ambaye alikuwa akisema mara kwa mara kwamba, ‘pazeni sauti zenu zote dhidi ya Marekani’.
Ayatullah Khamenei amewausia vijana kutilia maanani masomo na kutafuta elimu, kutanguliza mbele malengo ya umma badala ya matakwa binafsi na kuzidisha uelewa na uwezo wa kuchambua mambo. Ameongeza kuwa: Sauti ya taifa la Iran ndiyo sauti pekee inayofikisha ujumbe ipasavyo na imepazwa dhidi ya dhulma, unyonyaji na ukoloni katika kipindi hiki chenye misukosuko mingi duniani na imefanikiwa kuzivutia nyoyo za mataifa mengine na wasomi, hivyo hatupaswi kupoteza sauti hiyo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambaye maneno yake hayo yalilakiwa kwa nara za “mauti kwa Marekani” za wanafunzi na wanavyuo ameongeza kuwa, nara ya mauti kwa Marekani ya taifa la Iran ina hoja zenye nguvu za kiakili na kimantiki na inatokana na fikra za kimsingi ambazo haziwezi kustahamili dhulma na uonevu.
Amesema nara hiyo ina maana ya mauti kwa siasa za Marekani na ubeberu, na mantiki hii inakubaliwa na taifa lolote litakalopewa ufafanuzi kuhusu jambo hii.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, taifa la Iran linadumisha njia yake kwa azma kubwa na matumaini mengi, na kwa kuzidisha imani, uelewa na kushikamana na vigezo halisi, hapana shaka kuwa vijana wa leo watashuhudia kipindi ambapo mataifa yatajikomboa kutoka chini ya kivuli cha mazimwi ya hofu, na Iran azizi na yenye maendeleo itakuwa kigezo kinachotoa ilhamu kwa mataifa yote.               

700 /