Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu akizugumza mbele ya Waziri wa Mambo ya Nje na mabalozi wa Jamhuri ya Kiislamu:

Suala la nchi nyingine kuchukua maamuzi juu ya nfumo wa serikali ya Syria ni uzushi hatari sana

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran leo asubuhi (Jumapili) amekutana na kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Nje, mabalozi pamoja na manaibu balozi wa Jamhuri ya Kiislamu (na kubainisha misingi na stratijia thabiti na imara za siasa za nje katika katiba na mambo ya lazima yanayofungamana na misingi na siasa hizo) na kubainishia njia za kimantiki na madhubuti za Iran katika utatuzi wa masuala muhimu ya kieneo, yakiwemo ya Syria, Yemen na Bahrain. Amesisitiza kuwa malengo ya Marekani na ya Iran yanatofautiana kwa digrii 180. Ayatullah Khamenei amesema kuwa siasa za nje ya nchi ni siasa zilezile za nje za Mfumo katika katiba na kuongeza kuwa siasa hizo za nje zinatokana na Uislamu na malengo ya Mapinduzi na kwamba wakuu wa Wizara ya Mambo ya Nje pamoja na mabalozi na manaibu balozi wa wizara hiyo kwa hakika ni wawakilishi, askari na wahudumu wa misingi hiyo. Ameongeza kuwa siasa za nje kama zilizvyo za nchi zote za dunia, zimesimama juu ya misingi ya maslahi ya muda mrefu, kanuni na thamani, misingi ambayo haibadiliki kwa kuja na kuondoka madarakani serikali tofauti. Amesema kazi za serikali hizo huwa ni kutumia mbinu na uvumbuzi tofauti katika utekelezaji wa stratijia za siasa za nje.
Kiongozi wa Mapinduzi ameongeza: Mbinu zote za kidiplomasia za serikali tofauti zinapasa kuhudumia zaidi misingi ya siasa za nje katika katiba na wawakilishi wa kisiasa wa Iran nje ya nchi wanapasa kujihesabu kuwa ni wawakilishi na watetezi halisi wa mantiki ya siasa za mfumo. Huku akiashiria propaganda kubwa za wageni kuhusu 'mabadiliko ya lazima au ya hiari' katika siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa uchambuzi huo wa ndoto za alinacha wa Wamagharibi kwa hakika unatokana na shinikizo la ukweli huu kwamba siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu, kwa uchache katika upeo wa kieneo, ni kama ngome madhubuti na mwamba imara ambao unayazuia madola ya kibeberu na hasa Marekani kueneza ushawishi wao katika eneo, na hivyo kubakia daima katika ndoto ya kutaka kuzibadili siasa hizi. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amesema kuwa siasa za Wamarekani katika eneo nyeti la Asia Magharibi ndiyo sababu kuu ya kuvurugika kwa hali ya mambo katika eneo na kuongeza kuwa kinyume na maoni ya baadhi ya watu, Marekani ni sehemu muhimu ya matatizo ya eneo na sio sehemu ya utatuzi wa matatizo hayo. Amesisitiza kwa mara nyingine kuwa siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hazijabuniwa na watu binafsi bali zinatokana na misingi imara ya katiba na kuongeza kuwa katika katiba, Uislamu ndicho kipimo cha siasa za nje na kwa hivyo misimamo kuhusiana na nchi na masuala tofauti inapaswa kuzingatia vipimo na sifa za kidini. Ayatullah Khamenei ameashiria misingi mingine ya siasa za nje katika katiba yakiwemo majukumu ya kidugu kuhusiana na Waislamu wote duiani, kuwaunga mkono wanyonge ulimwenguni, kupiga vita ukoloni na kuzuia upenyaji wa wageni katika nyanja zote, kulindwa pande zote za utawala, kulindwa haki za Waislamu wote, kutowajibika mbele ya madola ya kibeberu, uhusiano mzuri wa pande mbili na serikali zisizo adui, kujiepusha na kila aina ya uingiliaji wa masuala ya ndani ya mataifa na kuunga mkono mapambano ya kupigania haki ya mataifa dhaifu katika kukabiliana na madola ya kiistikbari katika pembe zote za dunia na kuongeza kuwa misingi hii ya kuvutia, mipya na ya kiwango cha juu imeyavutia mataifa mengi na hasa wasomi. Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ambazo zina stratijia na sifa hizi ni siasa za nje za kimapinduzi na kwamba iwapo zinataandamana na stratijia erevu katika utekelezaji wake, bila shaka zitakuwa na matokeo makubwa na ya kushangaza na kuwa na uwezo wa kutatua sehemu kubwa ya matatizo ya ulimwengu wa Kiislamu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameshiria baadhi ya athari chanya za utekelezaji wa stratijia za siasa za nje na kuongeza: Utekelezwaji wa siasa za kimapinduzi katika nyanja zote, ukiwemo uwanja wa kidiplomasia, umeimarisha nguvu, athari, nafasi ya nchi, utukufu na itibari ya Wairani miongoni mwa mataifa. Ayatullah Khamenei amesisitiza juu ya kudumishwa bila kusita stratijia thabiti za siasa za nje na kuongeza: Hatudai kwamba tumefikia malengo yetu yote wala hata kuyakaribia kwa sababu utekelezaji wa 'siasa za nje za kimapinduzi' kiutendaji umekabiliwa na baadhi ya mighafala, uzembe, mielekeo isiyo erevu na vizuizi vya nje. Hata hivyo nafasi tukufu ya hivi sasa ya nchi inatokana na siasa hizihizi za busara na kama hatungetekeleza misingi hii, Mwenyezi Mungu ndiye anayejua tungekumbana na matatizo na mapigo yapi ya kushangaza (makubwa) ndani ya mipaka (yetu nchini).
Katika kufupisha sehemu hiyo ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amewahutubu wasimamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje, mabalozi na mabalozi wadogo kwa kusisitiza: Endeleeni kukariri kwa azma thabiti, nguvu na fahari, kudumishwa kwa misingi ya kimapinduzi na stratijia thabiti za siasa za nje ili wageni na vibaraka wao wa ndani wasiwe na matarajio ya kubadilishwa kwa siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika kuendeleza hotuba yake Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia mambo yanayotokana na kufungamana na misingi na stratijia za siasa za nje. Amesema: Zingatieni kwamba mbinu na stratijia za siasa za nje zinapasa kuhudumia misingi ya kistratijia na sio kwenda kinyume na misingi ya Mapinduzi kwa kisingizio cha utumiaji mbinu maalum.
Kiongozi Muadhamu amesema 'kujiamini, uwazi na kusimama imara katika kukabiliana na masuala pinzani na vizuizi' ni mambo mengine ya lazima katika siasa za nje na wakati huohuo kuongeza: Bila shaka usanii katika udiplomasia ni kuweza kubainisha fikra na misimamo kwa njia inayoathiri zaidi. Amesema mantiki ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu masuala ya kieneo inaungwa mkono kimataifa na ni imara, na kubainisha mapendekezo ya Iran katika utatuzi wa masuala hayo kwa kusema: Kuhusiana na suala la Palestina, sisi huku tukipinga uwepo wa utawala ghasibu, bandia na kulaani vikali maafa na jinai zinazotekelezwa kila siku na utawala huo, tumependekeza kufanyika uchaguzi ambao utawashirikisha Wapalestina wote, jambo ambalo pia linaoana kikamilifu na vipimo vya hivi sasa duniani. Ameongeza kuwa: Kila serikali itakayotokana na kura hizi za taifa la Palestina inapasa kuainisha majukumu ya Wapalestina na wakazi wa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, hata hivyo katika kupinga pendekezo letu hili la kimantiki, wamesema hii itakuwa na maana ya kusamabaratika utawala huo ghasibu. Ni wazi kuwa utawala huu bandia unapasa kusambaratika. Kuhusu Syria pia Kiongozi Muadhamu amesisitiza: Maneno (msimamo) yetu kuhusu suala hili ndiyo maneno yenye nguvu zaidi. Tunaamini kuwa hakuna haja ya nchi nyingine kukusanyika na kuchukua uamuzi kuhusiana na serikali fulani na rais wa serikali hiyo. Huo ni uzushi hatari mno ambapo hakuna serikali yoyote duniani inayokubali kuutekeleza dhidi ya nafsi yake. Ayatullah Khamenei ameongeza: Utatuzi wa suala la Syria ni uchaguzi na ili kufikia lengo hilo, misaada yote ya kijeshi na kifedha kwa wapinzani inapasa kukatwa. Kwanza vita na machafuko yanapaswa kusimamishwa ili watu wa Syria wapate fursa ya kumchagua kiongozi wanayemtaka katika mazingira ya amani na utulivu.
Kuhusu suala hilo amepinga vikali kugawanywa kwa nchi na kubadilishwa kuwa maeneo madogomadogo ya kikabila na kuongeza: Kuchukuliwa mojawapo ya makundi ya wabeba silaha kuwa kituo cha maamuzi na uundaji serikali, si jambo la mantiki wala linalokubalika, na bila shaka kanuni na fomyula kama hizi kivitendo zitadumisha tu vita.
Ayatullah Khameni pia amesema kuhusiana na Iraq: Kugawanywa kwa nchi hiyo katika maeneo ya Waarabu wa Kishia, Waarabu wa Kisuni na Wakurdi kunakinzana moja kwa moja na maslahi ya wananchi, hakutekelezeki, hakuna maana na wala hakukubaliki. Amesema: Umoja wa ardhi ya Iraq na kuheshimiwa kura za wananchi kama marejeo, ni misingi ya pendekezo la Iran la kutatuliwa suala la Iraq. Kuhusiana na Yemen Kiongozi Muadhamu amesema: Kusimamishwa mara moja kwa jinai za Saudia na kuanza mazungumzo ya Wayemen kwa Wayemen kunaweza kumaliza mapigano ya nchi hiyo. Amesema: Mwenendo (siasa) wa Wasaudia katika nchi za Yemen na Syria ni wa kindumakuwili. Wanasema kuhusiana na Yemen kwamba wameingilia kijeshi nchini humo kutokana na ombi la rais aliyestaafu na mtoro wa nchi hiyo lakini hawako tayari kutekeleza ombi la rais halali wa Syria la kuwataka wasimamishe uungaji mkono wao kwa makundi ya wapinzani wabeba silaha. Kuhusiana na Bahrain, Kiongozi Muadhamu pia amesema: Watu wa Bahrain hawataki jambo jingine isipokuwa haki yao ya kupiga kura na kumchagua kiongozi wanayemtaka na sisi tunaona kwamba takwa lao hilo ni la kimantiki. Baada ya kubainisha mapendekezo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kutatuliwa masuala ya kieneo, Ayatullah Khamenei amesema: Chanzo kikuu cha ghasia hizi ni uungaji mkono wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni na makundi ya kigaidi na siasa hizi zinatofautiana na siasa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa digrii 180.
Huku akipinga kufanyika mazungumzo na Marekani kuhusiana na masuala ya kieneo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Wamarekani wanataka kutwisha watu maslahi yao na sio kutatua matatizo. Wao wanataa kutwisha asilimia 60 hadi 70 ya matakwa yao katika mazungumzo na kutekeleza pamoja na kutwisha malengo yao mengine kinyume cha sheria, hivyo mazungumzo yana maana gani? Huku akiendelea na hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kuimarisha uhusiano na nchi jirani, za Kiislamu na za Kiafrika ni jambo jingine linalopaswa kuzingatiwa katika siasa za nje.
Ayatullah Khamenei amesema wakuu na wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje wanafaa kuitwa kuwa askari na wapiganaji vita katika mstari wa mbele katika uwanja wa kimataifa na kuongeza: Wizara ya Mambo ya Nje inatekeleza vyema majukumu yake kwa kuzingatia malengo na nyadhifa zake na hasa katika uzoefu wa hivi karibuni wa mazungumzo ya nyuklia, ambapo Bwana Dakta Zarif na wafanyakazi wenzake walifuzu vyema mtihani.
Huku akisifu juhudi na azma ya timu ya mazungumzo, Kiongozi wa Mapinduzi amesema: Kuhisi kuwa na nguvu na kuketi pembeni ya madola sita yenye nguvu duniani, kutetea malengo na kuthibitisha uepo wao kwa upande wa pili, ni miongoni mwa nukta za nguvu zilizoonyeshwa na wazungumzaji wa nchi yetu katika mazungumzo ya nyuklia. Amesema uzingatiaji dini ni nukta yenye nguvu zaidi ya Dakta Zarif na kuongeza: Mimi daima hukuombeeni dua nyinyi wapendwa.
Kiongozi wa Mapinduzi ameendelea kusema: Katika utekelezaji wa Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji  (JCPOA), fuatilieni kwa karibu pia nukta muhimu zilizoainishwa na hili pia ni jambo linalowezekana, kama alivyoniambia Mheshimiwa Rais, kufikiwa kwa baadhi ya natija mwanazoni lilikuwa ni jambo lisiloweza kufikirika lakini nyinyi mlisimama imara na sisi pia tukasimama imara na yote yakawezekana.
Sehemu ya tatu na ya mwisho ya hotuba ya Ayatullah Khamenei ilihusu nasaha na tahadhari kwa kwa mabalozi na wawakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nje ya nchi.
'Kuegemea na kutegemea nukta za nguvu na uwezo wa taifa' ikiwemo 'nafasi nyeti na muhimu ya wananchi nchini', 'nguvu kazi inayofaa, yenye ujuzi, kijana na nyingi', 'maendeleo makubwa ya kushangaza ya kielimu na kiteknolojia, 'mfungamano wa kina wa mabalozi na wawakilishi wa nje na misingi ya dini na moyo wa kimapinduzi' na 'kunufaika na uwezo wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) na kuwa na nafasi katika upatikanaji wa uchumi ngangari' ni miongoni mwa nahasa hizo.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Dakta Zarif, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliashiria mazingira nyeti ya eneo na kusisitiza: Maagizo na mistari myekundu iliyoainishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu imekuwa msingi wa shughuli za Wizara ya Mambo ya Nje na katika kipindi cha baada ya JCPOA pia barua ya hivi karibuni aliyomuandikia Rais kuhusiana na namna ya kutekelezwa JCPOA utakuwa msingi wa shughuli hizo.
Huku akiashiria uzingatiaji wa Wizara ya Mambo ya Nje kuhusu suala la kukabiliana na upenyaji na vilevile utekelezwaji wa uchumi ngangari Dakta Zarif amesema: Katika kongamano la mwaka huu la mabalozi na manaibu balozi, tutafanya juhudi za kunufaika na hali iliyopo kwa ajili ya kuendeleza malengo ya uchumi ngangari na vilevile kuimarisha mrengo wa mapambano katika eneo na kutatua matatizo ya Asia Magharibi kwa msingi wa vipimo vinavyokusudiwa na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

700 /