Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Vijana wenye imani na wanamapinduzi katika vyuo vikuu wapewe uwanja

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mapema leo amehutubia hadhara ya wakuu wa vyuo vikuu, vituo, taasisi za elimu ya juu na bustani za sayansi na teknolojia na vituo vya utafiti hapa nchini. Ameeleza kwa urefu historia, turathi na tajiriba ya kielimu hapa nchini hususan katika kipindi cha kabla na baada ya kudhihiri Uislamu na nafasi na mchango wa vyuo vikuu katika historia ya sasa hususan katika harakati ya Kiislamu na baada ya Mapinduzi ya Kiislamu. Vilevile amesisitiza udharura wa vyuo vikuu na vituo vya kielimu kuweka mipango kwa ajili ya kutumia turathi na tajiriba kubwa ya kielimu kwa shabaha ya kujenga ustaarabu wa kisasa wa Kiislamu. Amesema kuwa miongoni mwa masharti ya vyuo vikuu kuweza kuwa na mchango katika kujenga ustaarabu mpya wa Kiislamu ni kuchunguza mahitaji ya kielimu kwa ajili ya kipindi cha sasa na mustakbali, kuchukua hatua za kuzuia kupungua kasi ya maendeleo ya kielimu hapa nchini, utekelezaji makini wa ramani kamili ya elimu, kutiliwa maanani ubora katika taasisi za elimu ya juu, kufuatulia ipasavyo uhusiano baina ya vyuo vikuu na sekta ya viwanda, kushiriki ipasavyo vyuo vikuu katika uchumi ngangari, kueneza anga ya utamaduni wa kiimani na Kiislamu, kupanua zaidi uelewa na muono wa mbali wa kidini na kisiasa na kuwapa uwanja wanachuoni na wahadhiri wanaojali masuala ya kidini, kimapinduzi na wanaoshikamana barabara na dini.
Katika kikao hicho Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, vikao na watu wa vyuo vikuu ndiyo vikao bora zaidi kwake. Ameashiria nafasi ya elimu kama wenzo wa maendeleo na uwezo wa nchi na kusema: Chuo kikuu ndiyo kituo muhimu zaidi cha kulea na kutayarisha viongozi wa baadaye wa nchi kwa kadiri kwamba, utendaji mzuri au mbaya wa vyuo vikuu katika uwanja huo utakuwa na taathira katika mustakbali wa nchi.
Ayatullah Khamenei amezungumzia historia ya kulea na kutayarisha shakhsia na wasomi wakubwa nchini Iran mithili ya Ibn Sina (Avicenna), Farabi, Zakaria Razi, Kharazmi na wasomi wengine wengi katika nyanja mbalimbali na kusema: Katika kipindi chote cha historia, Iran imekuwa kilele cha kuzalisha fikra na elimu na mwenendo huo ulikuwepo hadi kabla ya kipindi cha tawala za Qajar na Pahlavi.
Amesema kuwa, inasikitisha kwamba katika kipindi cha Qajar na Pahlavi harakati ya elimu hapa nchini ilisimama kutokana na sababu makhsusi, na wakati wa kuchanua elimu barani Ulaya sisi hatukuweza kutumia vyema vipawa vyetu katika nyanja mbalimbali za kielimu na maadili ya kielimu; kwa msingi huo tuliachwa nyuma na harakati ya elimu na sayansi ya dunia.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria ratiba na mipango ya Wamagharibi kwa ajili ya nchi eti za ulimwengu wa tatu kwa shabaha ya kulea viongozi kwa mujibu wa fikra na mtindo wa maisha wa Kimagharibi kupitia vyuo vikuu na akasema: Wamagharibi walikabiliwa na matatizo katika kutekeleza mipango yao nchini Iran kutokana na utambulisho wa Kiirani na vilevile kuenea na kuimarika fikra za Kiislamu na kidini kati ya wanafunzi wa vyuo vikuu na wadau wa sekta hiyo, na baada ya harakati ya Kiislamu hapo mwaka 1341 (Hijria Shamsia) pia kulianza harakati kubwa iliyokuwa ikistawi kila siku ya kidini katika vyuo vikuu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambao ulikuwa mithili ya zilzala na mtetemeko kwa ulimwengu wa Magharibi na Mashariki wa wakati huo ulikuwa na taathira kubwa katika vyuo vikuu, na wasaidizi wa kweli na waliojitolea zaidi wa Mapinduzi ya Kiislamu walikuwa katika vyuo vikuu.
Ameashiria hali ya vyuo vikuu vya Iran katika kipindi cha miaka 37 iliyopita, panda shuka na mielekeo mbalimbali ya iliyokuwepo ndani ya mfumo na mirengo tofauti ya kifikra ndani ya vyuo vikuu na kusema: Kwa sasa swali muhimu zaidi ni kwamba, kwa kutumia turathi hii ya kihistoria na kielimu na tajiriba yenye thamani kubwa ya Mapinduzi ya Kiislamu, vyuo vikuu vinaweza vipi kuwa nafasi muhimu katika kuunda ustaarabu mpya wa Kiislamu ambao ndiyo jamii kamilifu ya Uislamu?
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewataka maafisa wa taasisi za elimu ya juu na wakuu wa vyuo vikuu na vituo vya elimu kutafakari kwa kina katika uwanja huo. Amesema kuwa mipango na ratiba zote na vilevile njia ya harakati ya vyuo vikuu inapaswa kuelekea upande wa kuwa na mchango katika kuunda ustaarabu mpya wa Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, sharti la kufanya harakati katika njia hiyo ni kuwa na habari za kina na ufuatiliaji wa karibu sana wa maafisa wa Wizara ya Sayansi na Wizara ya Afya kuhusu hali halisi ya vyuo vikuu. Amesisitiza kuwa, si sahihi kutosheka na ripoti tu bali kuna ulazima wa kufanyika uchunguzi kwa kuhudhuria katika medani ili ijulikane malengo yaliyokusudiwa yamefikiwa kwa kiasi gani.
Amesema kuwa, kuwepo kwa nguvu kazi yenye uwezo na vipawa kwa ajili ya harakati ya kielimu ni jambo lenye umuhimu, lakini muhimu zaidi ni mwelekeo na dira ya elimu, kwani iwapo dira ya kielimu haitakuwa sahihi wala haikuwa katika fremu na kalibu ya maadili na masuala ya kiroho, basi itakuwa na taathira nyingi mbaya.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja ukoloni na bomu la nyuklia kuwa ni mifano miwili ya kihistoria ya matokeo ya elimu kuwa katika njia isiyo sahihi na kuongeza kuwa: Daima tunapaswa kuwa macho ili elimu na sayansi viandamane na maadili na masuala ya kiroho.
Ayatullah Khamenei amesema ni jambo la dharura kupima mahitaji ya kielimu ya sasa na ya mustakbali ya nchi. Ameongeza kuwa, katika harakati ya kielimu lazima mahitaji ya kipindi cha sasa na mahitaji ya siku za usoni ya nchi yatiliwe maanani na kuwekeza katika taaluma na nyanja ambazo zinahitajiwa nchini.
Amesema kuwa, kuelekezwa makala za kielimu na tasnifu za shahada ya uzamivu upande wa mahitahi ya sasa na ya siku za usoni ya nchi ni maudhui yenye umuhimu na kuongea kuwa, elimu ya nyuklia ni miongoni mwa mambo yanayohitajiwa hapa nchini na kwa miaka mingi iliyopita tumewekeza katika suala hilo, kwani iwapo hatutaweza kutumia mafuta au akiba ya mafuta ikiisha, hapana shaka kuwa tutahitaji nishati mbadala.
Kwa mara nyingine tena Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kazi iliyofanywa na wasomi vijana wa Iran ya kuzalisha urani iliyorutubishwa kwa daraja ishirini na kusema: Katika kipindi ambacho nishati ya kituo cha nyuklia cha Tehran ambacho kinazalisha dawa za nyuklia (radiopharmaceutical) ilikuwa inakaribia kumalizika na Wamagharibi wakaweka masharti yenye madhila kwa ajili ya kutoa nishati hiyo, vijana wetu wenye vipawa na imani walifanya jutihada za usiku na mchana na kuzalisha nishati iliyorutubishwa kwa daraja 20 na hivyo wakakidhi mahitaji ya nchi katika uwanja huo.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa awamu ngumu zaidi ya kurutubisha urani ni ile ya kurutubisha madini hayo hadi daraja 20 na kwamba urutubishaji wa urani wa juu zaidi hadi daraja 99 unawezekana kirahisi na kusema: Hii ndiyo sababu ya kiwewe cha Wamagharibi katika kadhia ya nyuklia ya Iran. Amesema kama Wamagharibi wangekabidhi nishati ya kituo cha nyuklia cha Tehran kwa wakati mwafaka Tehran isingerutubisha madini ya urani kufikia daraja 20.
Akikamilisha sehemu hii ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amesema: Ni muhimu sana kupima na kutathmini mahitaji ya kielimu na kuwekeza katika elimu inayohitajika hapa nchini na suala hilo linapaswa kupewa mazingatio siku zote. 
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ni jambo la dharura kuzidisha kasi ya maendeleo ya kielimu kwa ajili ya kufidia kubakia nyuma katika sekta hiyo na vilevile ni muhimu kudumishwa harakati ya kielimu. Amesema kuwa inasikitisha kuona kwamba, baadhi ya watu ambao wamo ndani ya vyuo vikuu wanawaambia wanafunzi katika vyuo hivyo kwamba maendeleo ya kielimu yanayosemwa nchini Iran ni uongo! Kama maendeleo hayo si ya kweli basi mbona Kituo cha Utafiti cha Utawala wa Kizayuni wa Israel kinaeleza wasiwasi wake kuhusu maendeleo ya kisayansi na kielimu ya Iran?
Ameashiria kubakia nyuma kihistoria kwa Iran katika sekta ya elimu na kusema: Iwapo kasi ya sasa ya maendeleo ya kisayansi itapungua hapa nchini ufa na mwanya baina yetu na harakati ya kielimu ya dunia utakuwa kubwa zaidi; kwa msingi huo tunapaswa kulinda kasi yetu ya maendeleo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia ulazima wa vyuo vikuu kuwa vituo vikuu vya utafiti, kutekelezwa ipasavyo ramani kuu ya elimu nchini, kuzingatia ubora wa elimu ya juu na kuainisha vielelezo kwa kina, kwa kutumia mantiki na kwa kuzingatia uhalisia wa mambo na kuweko mfungamano na uhusiano wa karibu baina ya vyuo vikuu na sekta ya viwanda na kuongeza kuwa: Moja kati ya njia za kuandaa fursa za kazi kwa ajili ya wanachuo wanaohitimu masomo ni kuweko uhusiano baina ya vyuo vikuu na viwanda na sharti la kufanikisha suala hilo ni kuweko mipangilio mizuri ya wizara husika na kuanzishwa ushirikiano mpana baina ya vyuo vikuu na sekta ya viwanda katika sekta ya serikali na isizo ya serikali.
Ayatullah Khamenei ametilia mkazo ulazima wa kuweko mchango mkubwa wa vyuo vikuu katika kufanikisha uchumi ngangari na kupitia mashirika ya elimu za kimsingi.  Kuhusu suala la utekelezaji wa sera za uchumi ngangari, amesema: Kuhusiana na utekelezaji wa uchumi ngangari, jambo ambalo lilipaswa kutokea bado halijatokea na viongozi serikalini ndio kwanza wamewasilisha kwangu ripoti kuhusiana na mipango iliyokusudiwa kwa ajili ya utekelezaji wa sera za uchumi huo.
Ameendelea kwa kuzungumzia masuala ya utamaduni katika vyuo vikuu na kukosoa baadhi ya hatua zilizochukuliwa kwenye vyuo hivyo.  Amesema: Baadhi ya watu wanafanya makosa kwa kufananisha kazi za utamaduni na matamasha ya muziki na kuweka kambi zenye michanganyiko ya watu wa jinsia zote na wanajaribu kuhalalisha jambo hilo lisilo sahihi kwa kusema kuwa, wanachuo wanapaswa kuwa na furaha!
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Suala la kuwa na furaha ni zuri katika mazingira yoyote yale, lakini cha kujiuliza ni kwamba furaha hiyo ipatikane kwa gharama gani? Kwa gharama ya kufanya sherehe na kuweka kambi zenye mchangayiko wa wanawake na wanaume? Hivi Wamagharibi wamefaidika nini katika utamaduni wao wa kuchanganyika wanaume na wanawake zaidi ya jinai za kijinsia tunazoziona leo? Kwa nini basi tufuate mbinu hiyo?
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa kazi ya kiutamaduni ina utambulisho mwingine na kusema kuwa, maafisa wa masuala ya utamaduni katika vyuo vikuu wanapaswa kuelewa nini wanafanya. Kazi sahihi ya kiutamaduni ni kulea mtu mwenye imani, mwenye maadili, mwanamapinduzi, anayeamini thamani na matukufu, anayeipenda nchi na utawala wa Kiislamu na mwenye maarifa na utambuzi mkubwa wa masuala ya kidini na kisiasa.  
Amelitaja suala la vijana kuwa na mtazamo wa kuona mbali wa kidini na kisiasa na kuwazuia kutumbukia kwenye mitego na kuteleza kwenye itikadi zao kuwa ni muhimu sana na kusisitiza kuwa: Sababu iliyowafanya watu wengi wateleze katika fitna ya mwaka 2009, - na watu hao hawakuwa watu wabaya,- ni kukosa kwao kuwa na muono wa mbali. Wakati upande wa pili unakwambia kuwa uchaguzi ni kisingizio tu bali kinacholengwa hasa ni mfumo wenyewe wa Jamhuri ya Kiislamu, mtu mwenye imani na mfumo huo anapaswa kufanya nini? Kama hatokuwa na muono wa mbali, basi atashindwa kutekeleza jukumu lake inavyopasa na katika wakati mwafaka.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kujenga moyo wa kujiamini na matumaini ya mustakbali bora kati ya vijana kuwa ni kazi nyengine za kiutamaduni iliyo lazima kufanywa kwenye vyuo vikuu na kuongeza kuwa: Nchini Iran kuna mambo mengi sana ya kutia matumaini kama vile uwezo mkubwa wa taifa, nafasi na nguvu za hivi sasa za nchi.
Ayatullah Ali Khamenei amelitaja suala la kujiona duni kuwa ni jambo la hatari sana na kuongeza kwamba: Kujiona duni, kudunisha uwezo na nguvu ya taifa humfanya mtu ndani ya nchi aseme: “Sisi si lolote si chochote na tumetengwa”, ilhali watu wote wanaona na kukiri kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina nguvu na ushawishi katika eneo hili!
Vilevile amelitaja suala la kulea vijana walioimarika kiimani, wenye itikadi thabiti na wenye uhuru wa kifikra, kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi kuwa ni miongoni mwa kazi za dharura za kiutamaduni kwenye vyuo vikuu. Amesema: Habari zilizonifikia kutoka katika baadhi ya vyuo vikuu ambazo natarajia kuwa si za kweli, ni kinyume na haya tuliyosema, kwa kadiri kwamba habari zinasema kuwa katika vyuo vikuu jumuiya za watu waumini, wanamapinduzi na wenye fikra nzuri zinawekewa mashinikizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewaambia maafisa wa Wizara ya Sayansi na Tiba na wakuu wa vyuo vikuu nchini kwamba: Mnapaswa kuwafungulia njia vijana wanamapinduzi, waliojengeka kiimani, wenye moyo na fikra nzuri, walioshikamana na dini na wenye heshima na izza ya nafsi kwa kadiri ya kuhakikisha kwamba anga inamilikiwa na vijana wa namna hiyo.
Ayatullah Khamenei amemalizia hotuba yake kwa kugusia mapenzi yake makubwa na ya muda mrefu ya chuo kikuu na jamii ya watu wa vyuo vikuu na kusisitiza kuwa: Leo hii vyuo vikuu na wanachuo wanakumbwa na mawimbi ya njama kubwa zaidi na kwamba maadui wa Iran wana woga mkubwa wa kuweko wasomi wa vyuo vikuu wenye moyo wa kimapinduzi na jasiri wa kuingia vilivyo kwenye medani mbalimbali na kuharibu mistari myekundu ya maadui hao sambamba na kupeperusha juu bendera ya elimu na kunawirisha kaulimbiu za Mapinduzi ya Kiislamu. Amesema ili kukabiliana na harakati hii ya kielimu ya Iran maadui wanafanya mikakati na kutumia fedha nyingi.
Vilevile amegusia namna wakoloni walivyobadilisha mbinu zao na kuongeza kuwa: Wanachofanya mabeberu hivi sasa ni kuhakikisha wanabadilisha fikra za wanaharakati, watu werevu na wenye vipaji wa nchi fulani na kuwafanya watu hao wawatumikie malengo ya mabeberu badala ya kutumikia nchi zao.
Ayatullah Khamenei pia amesisitiza udharura wa kuenezwa thamani za taifa katika maeneo ya vyuo vikuu na kusema kuwa: Inabidi kuzizingatia na kuzipa umuhimu dukuduku za wanachuo wanaothamini matukufu na masuala ya Mapinduzi ya Kiislamu na vilevile maelfu ya wahadhiri wa vyuo vikuu ambao ni waumini wa kweli na ni wanamapinduzi na inabidi kuwaenzi vilivyo wahadhiri hao na kujua thamani yao.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Dk Mohammad Farhadi, Waziri wa Sayansi, Utafiti na Teknolojia wa Iran ametoa hotuba fupi na kulitaja suala la kuupa umuhimu uchumi unaotegema elimu za kimsingi na kuzalisha utajiri kupitia elimu na teknolojia kuwa ni katika ajenda kuu za wizara yake katika upande wa kufanikisha sera za uchumi ngangari na wa kusimama kidete. Amesema: Kuandaa na kupasisha hati ya uchumi ngangari, kuangalia upya na kufanyia marekebisho mipango na ratiba za masomo, kushirikiana na sekta mbalimbali za viwanda na za kutoa huduma nchini, kulitilia maanani suala la utekelezaji wa hati ya Chuo Kikuu cha Kiislamu, kuanzisha kozi na masomo ya kuwajenga wanachuo na kuwafanya wawe na uhuru wa kufikiri na kutilia nguvu anga ya kidini na kimapinduzi katika vyuo vikuu, ni miongoni mwa hatua na mikakati muhimu sana ya wizara yake.
Naye Dk Ghazizadeh Hashemi, Waziri wa Afya, Matibabu na Elimu ya Tiba amesema Iran hivi sasa inashika nafasi ya kwanza katika eneo la Mashariki ya Kati katika upande wa uandikaji makala na ni ya 24 duniani katika suala hilo na kuongeza kuwa: Kupata daraja ya juu ya kuwa marejeo ya kielimu katika eneo hili, kuwa amilifu na mwenye taathira katika nyuga za kimataifa, kuipa umuhimu tiba ya jadi, ya kitaifa na maadili ya udaktari, kuanzisha chuo cha tiba na dini, kuchunga haki za wagonjwa na kuanzisha hospitali maalumu kwa ajili ya wanawake, ni miongoni mwa ajenda za wizara yake .
       
        
                   

700 /