Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu:

Uislamu ni dini ya udugu, upendo na kheri

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alasiri ya leo (Jumapili) amezungumza na Rais Gurbanguly Berdimuhamedow wa Turkmenistan aliyemtembelea ofisi kwake hapa mjini Tehran. Ayatullah Ali Khamenei ameashiria uhusiano wa kirafiki wa Iran na Turkmenistan na nyanja nyingi zilizopo kwa ajili ya kustawisha zaidi ushirikiano wa pande mbili na kukabiliana na sera za kuzusha vita na mapigano katika eneo hili na kusema: Njia ya kukabiliana na mirengo ya kigaidi na kuzima ushawishi wao ni kuwashirikisha wananchi katika shughuli sahihi za Kiislamu na kuimarisha harakati za kifikra za Kiislamu zenye misimamo ya wastani na ya kimantiki.
Ayatullah Khamenei ameyataja mataifa mawili ya Iran na Turkmenistan kuwa ni majirani ambao ni kama ndugu. Amesisitiza udharura wa kutumiwa uwezo mkubwa uliopo kwa ajili ya kustawisha ushirikiano na kuongeza kuwa, kuna ulazima wa kuchukuliwa hatua zenye taathira na za kivitendo kwa shabaha ya kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa usalama, hali bora na maendeleo ya majirani na nchi za Kiislamu vina manufaa kwa Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Mipaka ya Iran na Turkmenistan ni mipaka ya amani na utulivu na inapelekea kupatikana utulivu kwa pande mbili. Vilevile amesisitiza kuwa uwezekano wa kutumia njia ya Iran kwa ajili ya kuelekea Ghuba ya Uajemi na bahari huru ni fursa yenye thamani kwa Tukmenistan.
Vilevile ameashiria usalama wa Iran na Turkmenistan katika mazingira yenye mivutano na machafuko mengi kwenye eneo hili na kusema kuwa, kuna udharura wa kuzidishwa ushirikiano kwa ajili ya kudumisha hali hiyo.
Amesema kuwa ili kuweza kukabiliana na ukatili na ugaidi muovu wa kundi la Daesh na makundi mengine ya kitakfiri ambayo yanafanya jinai kwa kutumia jina la Uislamu, kuna udharura wa kushirikishwa wananchi katika shughuli sahihi za Kiislamu, na njia bora zaidi ya kuzima ushawishi wa makundi hayo ni kuimarisha harakati za kifikra za Kiislamu zenye misimamo ya wastani na ya kimantiki.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, jinai za kutisha zinazofanywa na makundi ya kigaidi kama kukata vichwa na kuwachoma moto watu ni ushahidi kwamba makundi hayo yako mbali kabisa na Uislamu. Amesisitiza kuwa, Uislamu ni dini ya udugu, upendo na kuwatakia mema watu wengine na jinai hizo hazina mfungamano wowote na Uislamu.
Kwa upande wake Rais wa Turkmenistan Gurbanguly Berdimuhamedow amesema katika mazungumzo hayo ambayo pia yamehudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais, Bwana Is’haq Jahangiri, kwamba amefurahishwa na safari yake mjini Tehran na kwamba anaona fahari kukutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ameongeza kuwa Iran na Turkmenistan daima zimekuwa na uhusiano mzuri na wa kihistoria na zinashirikiana katika machungu na mafanikio ya kila mmoja wao. Ameongeza kuwa: Matamshi yako uliposema kwamba Iran na Turkmenistan si nchi jirani tu bali ni ndugu wawili yanaihamasisha na kuifurahisha serikali na taifa la Turkmenistan.
Rais wa Turkmenistan amekumbusha nasaha za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika safari zake za huko nyuma hapa nchini na kusema: Maneno yako kama kiongozi mweledi na mwanafikra yana thamani kubwa kwetu sisi na utekelezaji wake umekuwa na matokeo mazuri.
Vilevile amegusia uwezo mkubwa wa nchi hizi mbili kwa ajili ya kustawisha uhusiano hususan katika sekta za gesi, usafirishaji na ujenzi wa barabara na akasema: Utekelezaji wa miradi ya ujenzi na ya kiuchumi ya pamoja ya Iran na Turkmenistan utakuwa na faida kwa nchi zote za eneo hili.
Rais Gurbanguly Berdimuhamedow wa Turkmenistan amekumbusha historia na umuhimu wa Njia ya Hariri na kusema baadhi ya nchi zina hamu ya kufika kwenye bahari huru kupitia njia ya Iran na Turkmenistan.
Vilevile amesema kuwa hali ya sasa ya kisiasa ya eneo hili hairidhishi. Ameashiria jinai zinazofanywa na kundi la kigaidi la Daesh na kusema: Daesh na mfano wake hawajui kabisa Uislamu na inasikitisha kwamba makundi hayo yanafadhiliwa na kuungwa mkono na baadhi ya nchi.             

700 /