Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu katika mazungumzo yake na Rais Putin:

Marekani ina mpango wa muda mrefu wa kulidhibiti eneo la magharibi mwa Asia

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alasiri ya leo (Jumatatu) amemkaribisha na kufanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin wa Russia ofisini kwake hapa mjini Tehran.  Ayatullahil Ali Khamenei amekaribisha suala la kuimarishwa zaidi ushirikiano wa pande mbili, kieneo na kimataifa na kuipongeza Moscow kwa mchango wake wenye taathira katika masuala ya kieneo hususan katika kadhia ya Syria. Amesema kuwa njama za muda mrefu za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati zina madhara kwa mataifa na nchi zote hususan Iran na Russia na kwamba njama hizo zinapaswa kuzimwa kwa kuwa macho na kushirikiana kwa karibu.  
Katika mazungumzo hayo yaliyoendelea kwa kipindi cha karibu masaa mawili, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amemtaja Rais Putin kuwa ni shakhsia mkubwa katika dunia ya leo na kushukuru juhudi zilizofanywa na Russia kuhusu kadhia ya nyuklia ya Iran. Amesema suala hili limefikia tamati lakini Iran haiwaamini kabisa Wamarekani na kwamba inafuatilia kwa makini sana mienendo na utendaji wa serikali ya Marekani katika uwanja huo.
Amegusia pia jitihada kubwa za Bwana Putin na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu kwa ajili ya kupanua zaidi uhusiano wa pande mbili na akasema: Kiwango cha ushirikiano ukiwemo wa masuala ya kiuchumi kinaweza kustawishwa zaidi kuliko hiki cha sasa.
Ayatullah Khamenei amezungumzia pia ushirikiano mzuri wa Tehran na Moscow katika nyanja za kisiasa na kiusalama na ameitaja misimamo ya Rais wa Russia kuhusu masuala mbalimbali hususan katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu uliopita kuwa ni mizuri sana na yenye uvumbuzi. Ameongeza kuwa: "Marekani daima inajaribu kuwaweka mahasimu wake katika hali ya kutoa majibu, hata hivyo wewe Rais Putin, umeweza kuzima siasa hizo".
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, maamuzi na hatua za Moscow katika kadhia ya Syria zimezidisha hadhi na heshima ya kieneo na kimataifa ya Russia na ya Putin mwenyewe na kuongeza kuwa, Wamarekani katika njama zao za muda mrefu wameazimia kufidia mapungufu yao ya kihistoria ya kutokuwa na udhibiti katika eneo la magharibi mwa Asia kwa kuikalia kwa mabavu Syria na kisha kueneza udhibiti wao katika eneo hilo; njama ambazo ni tishio kwa mataifa na nchi zote hususan Russia na Iran.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, katika suala la Syria Wamarekani na wafuasi wao wanataka kutimiza malengo yao waliyoshindwa kuyafikia kupitia njia ya kijeshi kwa kutumia uwanja wa siasa na kwenye meza ya mazungumzo, hivyo kuna udharura wa kuwa macho na kuzuia jambo hilo kwa misimamo imara.  
Ayatullah Khamenei amesema, sisitizo la Wamarekani kwamba Bashar Assad aondoke madarakani, yaani Rais halali na aliyechaguliwa na wananchi wa Syria, ni miongoni mwa nukta dhaifu za siasa za waziwazi za Washington na kuongeza kuwa, Rais wa Syria alichaguliwa kwa kura za wananchi wengi wenye mitazamo mbalimbali ya kisiasa, kidini na kikaumu katika uchaguzi uliofanyika kote nchini humo, na Marekani haina haki ya kupuuza kura hizo na chaguo hilo la wananchi wa Syria.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Kuhusu masuala ya Syria, njia yoyote ya utatuzi wa mgogoro wa nchi hiyo inapaswa kuendelezwa baada ya kuwasilishwa kwa wananchi na kwa uungaji mkono wao na wa viongozi wa nchi hiyo.
Ayatullah Khamenei ameitaja misaada ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja ya Marekani kwa makundi ya kigaidi likiwemo kundi la Daesh kuwa ni miongoni mwa nukta za udhaifu wa wazi wa siasa za Marekani na kuongeza kuwa, kushirikiana na nchi ambazo hazina hadhi katika fikra za waliowengi kieneo na kimataifa kutokana na uungaji mkono wao kwa magaidi kunaonesha kuwa viongozi wa Marekani hawana udiplomasia wa kiungwana.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa kwa sababu hiyo Jamhuri ya Kiislamu haifanyi na wala haitafanya mazungumzo na Marekani katika maudhui yoyote ile isipokuwa katika suala la nyuklia tu nalo kwa sababu makhsusi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Utatuzi sahihi wa maudhui ya Syria ni jambo muhimu na lenye taathira kubwa katika mustakbali na eneo hili. Ameongeza kuwa, iwapo magaidi wanaofanya jinai kubwa nchini Syria hawataangamizwa, basi harakati zao zenye uharibifu zitapanuka na kufika Asia ya Kati na maeneo mengine.  
Katika mazungumzo hayo, Rais Vladimir Putin wa Russia ameashiria uzoefu wenye thamani wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kueleza kufurahishwa kwake na mazungumzo kati yake na Kiongozi Muadhamu. Rais Putin amesema, kuimarisha uhusiano wa nchi mbili ikiwemo katika uwanja wa teknolojia, anga za mbali na teknoloji za kisasa kumeshika kasi zaidi na kwamba Moscow ina furaha kubwa kushirikiana ipasavyo na Tehran katika masuala ya usalama na kutatua migogoro ya kieneo na ya kimataifa.
Putin amesema Jamhuri ya Kiislamu ni nchi inayojitawala, imara na yenye mtazamo mzuri sana na kusisitiza kuwa Iran ni mshirika wa kuaminika na wa kutegemewa katika masuala ya kieneo na kimataifa.
Rais wa Russia amesema: Sisi, tofauti na baadhi ya nchi, hatuwezi kuwasaliti washirika na waitifaki wetu na kamwe hatutachukua hatua yoyote ya nyuma ya pazia dhidi ya marafiki zetu; na kama tutakuwa na hitilafu basi tutaelewana kupitia mazungumzo.
 Bwana Putin amesema kuwa misimamo ya Iran na Russia kuhusu kadhia ya Syria inakaribiana sana. Ameashiria umuhimu mkubwa wa kuwepo kushirikiano katika uwanja huo na kusema: Sisi pia tunasisitiza kwamba mgogoro wa Syria unaweza kutatuliwa kupatia njia ya kisiasa tu na kukubali kura za wananchi na matakwa ya makundi na kaumu zote za Wasyria. Amesema hakuna mtu mwenye haki ya kuwatwisha Wasyria matakwa yake na kuchukua maamuzi badala yao kuhusu muundo wa serikali na hatima ya Rais wa Syria.
Rais wa Russia amesema, kama ulivyosema wewe mheshimiwa, Wamarekani wanataka kufikia malengo yao ambayo hayakutimia katika medani ya vita huko Syria, kwenye meza ya mazungumzo na sisi tunafuatilia suala hilo kwa makini.
Vladimir Putin amesisitiza udharura wa kudumishwa mashambulizi ya Russia dhidi ya makundi ya kigaidi nchini Syria na akasema, kuna udharura wa kushirikiana na kubadilishana mawazo kati ya Tehran na Moscow kuhusu mchakato wa utatuzi wa kisiasa wa kadhia ya Syria. Amesema kuwa, watu wanaodai kuwa vinara wa demokrasia duniani hawapasi kupinga kufanyika uchaguzi nchini Syria.  
Mwishoni mwa mzungumzo hayo Rais wa Russia amemtunuku Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu zawadi yenye thamani kubwa ya mojawapo na nakala za kale zaidi za Qur’ani Tukufu. Ayatullah Khamenei amemshukuru Rais Putin kwa zawadi hiyo.    

700 /