Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu katika mazungumzo na Rais wa Iraq:

Wamarekani hawapaswi kuruhusiwa kuzungumzia suala la kuigawa Iraq

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran leo asubuhi (Jumanne) ameonana na kuzungumza ofisini kwake na Rais Fuad Masum wa Iraq pamoja na ujumbe alioandamana nao.
Katika Mazungumzo hayo Kiongozi Muadhamu amesema kuwa uhusiano mkubwa iliopo kati ya nchi na mataifa mawili ya Iran na Iraq ni wa kina, kihistoria na ulio juu ya uhusiano wa kawaida wa nchi jirani na zilizo katika eneo moja.
Akisisitiza udharura wa kulindwa umoja wa taifa la Iraq, Ayatullah Khamenei amesema: Taifa la Iraq ni taifa kubwa na lililo na historia kongwe na lenye vijana shupavu na wenye mwamko ambapo uwezo huo unapaswa kutumiwa vyema kwa ajili ya kuifikisha Iraq katika nafasi yake inayostahiki. Huku akiashiria uhusiano wa kidugu, kirafiki na kiupendo uliopo kati ya mataifa mawili ya Iran na Iraq licha ya kuwepo kwa historia ya miaka minane ya vita vya kulazimishwa vya Saddam Hussein dhidi ya Iran kwa uchochezi wa wageni, Kiongizi Muadhamu amesema, jambo hilo ni la kustaajabisha na kuongeza: Maandamano ya Arubaini ya Imam Hussein (as) ni mfano wa uhusiano huo wa kirafiki kwa kadiri kwamba watu wa Iraq hufanya kila wanaloweza katika kuwapokea, kuwakirimu na kuwaonyesha upendo wafanyaziara wa Kiirani. Kiongozi Muadhamu ameongeza: Viongozi wa nchi mbili za Iran na Iraq wanapasa kufanya kila wanaloweza ili kunufaika na mazingira pamoja na fursa hii kwa maslahi ya nchi mbili.
Huku akielezea kufurahishwa kwake na mafanikio ya Iraq katika siku za hivi karibuni na kushindwa kwa kiwango fulani fitina ya Daesh, Ayatullah Khamenei amesisitiza kulindwa kwa umoja wa hivi sasa wa Iraq na kuogeza: Katika muundo wa serikali ya Iraq, rais wa nchi ana nafasi maalumu na hivyo anaweza kuwa na nafasi muhimu katika kupunguza hitilafu na kuimarisha umoja nchini.
Ameashiria njama zinazofanywa na baadhi ya pande za kigeni kwa ajili ya kuzua hitilafu huko Iraq na kusema: Watu wa Iraq, wawe ni Mashia, Masuni au Wakurdi wamekuwa wakiishi pamoja kwa karne nyingi bila matatizo yoyote lakini kwa masikitiko baadhi ya nchi za eneo hili na vilevile wageni wanataka kuzifanya tofauti zilizopo kuwa kubwa kuliko kiasi, ambapo jambo hilo linapaswa kuzuiwa na kujiepusha na kila aina ya visingizio vinavyoweza kuleta hitilafu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba kudhihirishwa hitilafu na kuenezwa kwenye uwanja wa umma wa Iraq bila shaka kunaandaa uwanja wa kudhihirishwa matamshi ya uingiliaji ya wageni na kusema: Mazingira hayapasi kuwa kwa namna ambayo yanawafanya Wamarekani wathubutu kuzungumzia waziwazi suala la kuigawa Iraq katika maeneo tofauti.
Ayatullah Khamenei amehoji: Je, ni kwa nini nchi kama Iraq ambayo ni nchi kubwa, tajiri na iliyo na historia ya maelfu ya miaka igawanywe kwenye maeneo madogomadogo ili daima iwe ni uwanja wa hitilafu na ugomvi? Ameongeza: Bila shaka viongozi wa Iraq watapanga na uhusiano wa nchi hiyo na nchi za kigeni ikiwemo Marekani kwa msingi wa maslahi na manufaa ya watu wa nchi hiyo lakini Wamarekani hawapaswi kupewa fursa ya kuichukulia Iraq kuwa milki na mali yao, ambapo huizungumzia na kuichukulia uamuzi wanavyotaka.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, Iraq ya leo ambayo ni taifa kubwa na iliyo na vijana shupavu na walio na mwamko inatofautiana kikamilifu na Iraq ya zamani, na kuongeza: Vijana wa Iraq sasa wameamka na kutambua nguvu na uwezo wao na bila shaka vijana kama hao hawatakubali kuwa chini ya ubeberu wa Marekani.
Amesema wapiganaji wa kujitolea wa Iraq katika vita na Daesh ni dhihirisho halisi la mwamko na nguvu hiyo ya vijana wa Iraq na kusisitiza: Fursa na uwezo huu wa vijana wa Iraq unapaswa kutumiwa vyema kuliko wakati mwingine wowote kwa ajili ya kuifikisha nchi hii katika nafasi yake inayofaa. Ayatullah Khamenei amesisitiza utayarifu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya kuhamishia Iraq uzoefu na uwezo wake wa kielimu, kiteknolojia, kiulinzi na kihuduma na kuongeza: Juhudi zinapasa kufanywa kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi wa nchi mbili.
Katika mazunumzo hayo ambapo pia Bwana Es'haq Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alihudhuria, Rais Fuad Masum wa Iraq ameelezea kufurahishwa kwake na kukutana na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuashiria nafasi na athari kubwa ya maneno ya Ayatullah Khamenei kwa watu na viongozi wa Iraq, akiwa ni mujtahidi na marja' taklidi mkubwa na kusema: Nasaha zako kuhusiana na kulindwa umoja na kujiepusha na hitilafu nchini Iraq bila shaka zitakuwa na athari kubwa.
Rais wa Iraq ameshukuru na kuipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa misaada yake kwa taifa la Iraq hasa katika mazingira magumu ya mashambulio ya Daesh dhidi ya nchi hiyo. Ameashiria masuala ya pamoja ya kihistoria, kidini na kiutamaduni ya mataifa mawili ya Iran na Iraq na kusema: Sisi tunataka kuimarishwa zaidi kwa uhusiano wa nchi mbili hizi na kunufaika na uzoefu na uwezo wa Iran katika nyanja mbalimbali.
Rais Fuad Masum ametathmini hali jumla ya Iraq na mshikamano wa ndani ya nchi hiyo kuwa umeboreka ikilinganishwa na huko nyuma na kuongeza: Mafanikio mengi yamepatikana pia katika kupambana na Daesh, na kuwepo taratibu jeshini, wapiganaji wa kujitolea na Pishmarg wa Kikurdi kumeandaa uwanja wa kutolewa mapigo makali dhidi ya Daesh.

700 /