Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu katika mazungumzo yake na Waziri Mkuu wa Algeria:

Nchi za Kiislamu zinapaswa kutafuta njia ya kivitendo ya kukabiliana na magaidi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kabla ya adhuhuri ya leo amemkaribisha ofisini kwake Waziri Mkuu wa Algeria Abdelmalek Sellal na ujumbe unaoandamana naye.
Katika mazungumzo hayo Ayatullah Ali Khamenei ameashiria misimamo ya kisiasa inayokaribiana ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Algeria na akasema: Mbali na kukaribiana misimamo hiyo ya kisiasa, taifa la Iran lina mtazamo chanya kuhusu nchi na wananchi wa Algeria na suala hilo linatokana na jihadi ya Waalgeria dhidi ya ukoloni katika kipindi cha Mapinduzi ya Algeria.
Amesema uhusiano wa kiroho kati ya mataifa unatayarisha mazingira ya kustawisha zaidi ushirikiano hususan katika nyanja za kiuchumi na kuongeza kuwa, kiwango cha ushirikiano wa Iran na Algeria kiko chini sana, hivyo inatarajiwa kuwa, safari ya sasa ya Waziri Mkuu wa Algeria hapa nchini na kuundwa kwa kamisheni ya pamoja katika siku chache zijazo na vilevile safari ijayo ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran nchini Algeria vitaimarisha zaidi uhusiano wa kiuchumi wa nchi hizi mbili.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria matamshi ya Waziri Mkuu wa Algeria kuhusu kundi la Daesh na udharura wa nchi za Mashariki ya Kati kupambana ipasavyo na magaidi wanaochafua sura ya Uislamu na akasema: Maudhui ya Daesh na makundi ya kigaidi yaliyozagaa katika eneo hili kwa kutumia jina la Uislamu si maudhui ya kawaida bali magaidi hawa wameletwa na wanaungwa mkono (na pande nyingine).
Ayatullah Khamenei ameeleza kusikitishwa na uungaji mkono wa baadhi ya nchi za Waislamu za Mashariki ya Kati kwa magaidi wa Daesh. Vilevile ameashiria misaada na nuungaji mkono wa Marekani na maadui wa Uislamu kwa magaidi hao na kusisitiza kuwa: Kupitia njia ya mazungumzo na ushirikiano, nchi za Kiislamu zinazoumizwa na hali hii na zenye maelewano zaidi zinaweza kufikia njia ya utatuzi wa kivitendo kwa ajili ya kukabiliana na magaidi.
Amekumbusha kambi ya mapambano iliyozishirikisha nchi za Algeria, Iran, Syria na nchi nyingine kadhaa ambayo iliundwa mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kusema: Baadhi ya nchi zinazoifuata Marekani kibubusa zilizuia kuendelea kwa shughuli na harakati za kundi hilo lakini inaonekana kuwa, sasa kuna mazingira yanayofaa kwa ajili ya kuundwa tena majmui kama hiyo itakayozishirikisha nchi za Kiislamu zenye mitazamo inayofanana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, iwapo majmui hiyo itaundwa, nchi hizo za Kiislamu zinaweza kuwa na taathira katika masuala muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu na kuchukua hatua za kivitendo kwa ajili ya kutatua matatizo ya eneo hili na kupambana na magaidi.
Mwishoni mwa mazungumzo hayo Ayatullah Khamenei ameeleza matarajio yake kwamba Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria atapata ahueni na kupoma haraka.  
Katika mazungumzo hayo Waziri Mkuu wa Algeria, Abdelmalek Sellal ameutaja mkutano wa nchi zinazouza gesi kwa wingi duniani uliofanyika mjini Tehran kuwa umekuwa na mafanikio. Amegusia mazungumzo yake na maafisa wa Iran na kusema: Misimamo ya Iran na Algeria katika masuala mengi ya kisiasa hususan kuhusu maudhui ya kupambana na kundi la Daesh inakaribiana sana na kwamba anataraji kuwa, kwa kutilia maanani mazungumzo ya Tehran, kiwango cha uhusiano wa kiuchumi cha nchi hizo mbili kitapanda na kufikia kiwango kinachokubalika.  

700 /