Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Kuna udhaura wa kukabiliana na siasa za Marekani za kutaka kubadili utambulisho wa mataifa

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alasiri ya leo ameonana na kufanya mazungumzo na Rais Evo Morales wa Bolivia aliyeko safarini hapa nchini. Ayatullah Ali Khamenei amepongeza kusimama imara na kishujaa kwa Bolivia na baadhi ya nchi nyingine za Amerika ya Latini dhidi ya sera za kutumia mabavu na dhulma za kambi ya ubeberu na akasema: Siasa hatari za Marekani duniani na katika eneo la Amerika ya Kusini zinalenga kubadili utambulisho wa vijana. Amesisitiza kuwa, kuna udharura wa kukabiliana na siasa hizo za kibeberu kwa kuimarisha azma na kuzidisha uhusiano na ushirikiano.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa kusimama kidete kwa ajili ya kupambana na sera za kutaka makuu na za beberu Marekani ni sifa muhimu bali kuna muhimu zaidi kwa Bolivia na Bwana Morales kuliko hata kutaifishwa sekta ya mafuta ya nchi hiyo. Ameongeza kuwa, Iran ilikuwa nchi ya kwanza duniani iliyojiondoa kikamilifu kwenye udhibiti wa Marekani kutokana na harakati ya wananchi na Imam Khomeini na ikasimama kidete mbele ya upinzani wa kambi mbili za Mashariki na Magharibi na aina mbalimbali za mashinikizo ya kijeshi, kiusalama na kiuchumi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kwa msingi huo Jamhuri ya Kiislamu inamuunga mkono mtu yeyote katika eneo lolote duniani ambaye anasimama kukabiliana na dhulma na ubeberu.
Ameashiria suhula na vipawa vingi vya Bolivia na kusema: Uwezo huo na uhusiano wa nchi mbili hizi na vilevile nyanja nyingi zilizopo za ushirikiano vinaweza kuhudumia maslahi ya mataifa mbalimbali na kusimama kidete kwa ajili ya kukabiliana na madhalimu.
Ayatullah Khamenei amesema, maendeleo ya kiuchumi ya Bolivia ni jambo la dharura na lenye thamani kwa ajili ya kuweza kujitawala kisiasa na kiuchumi na kuongeza kuwa, mbali na maendeleo hayo kuna ulazima pia wa kuwepo maendeleo katika upande wa masuala ya kiroho na kiutamaduni.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa siasa za Marekani duniani na katika eneo la Amerika ya Latini zinalenga kubadili utambulisho wa wenyeji na vijana kwa kutumia mbinu za kisasa za mawasiliano. Ameongeza kuwa: Iwapo Wamarekani watafanikiwa katika siasa zao hizo na kuweza kubadili fikra za vijana na kuzifanya za Kimarekani, wataweza kuzidhibiti nchi hizo bila ya kutumia mapinduzi ya kijeshi na hatua nyingine.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema njia ya kukabiliana na siasa za Marekani za kubadili utambulisho wa wenyeji na vijana ni kuimarishwa utambulisho wa wenyeji na kueneza thamani na matukufu kwa vijana. Amesisitiza kuwa, inawezekana kupata ushindi katika vita hivyo kwa kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuimarisha irada na azma ya wananchi.  
Kwa upande wake, Rais Evo Morales wa Bolivia ameeleza furaha ya kukutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema: Tunakutambua wewe mheshimiwa kuwa ni baba na kiongozi wa mapinduzi yote huru hususan mapinduzi ya eneo la Amerika ya Latini na tumejifunza masomo mengi kutokana na hotuba zako zenye thamani, zinazotoa ilhamu na kutia matumaini.
Amezitaja sera za Marekani za kuingilia mambo ya mataifa mengine kuwa ndiyo kiini cha matatizo na kusema: Mwanzoni nilipopewa jukumu la kuongoza nchi nilijibu tahadhari ya Wamarekani kuhusu suala la kuwa na uhusiano na Iran kwa kusema, sisi ni nchi inayojitawala na hatuhitaji idhini ya yeyote kwa ajili ya kufanya uhusiano na nchi nyingine.
Rais wa Bolivia amesema nchi yake haitalegeza kamba mbele ya Wamarekani na kuongeza: Tumethabitisha zaidi kujitawala na uhuru wetu kwa kutaifisha sekta ya mafuta ya Bolivia na tumekomesha miaka mingi ya uvamizi wa Magharibi.
Bwana Morales amesema kiwango cha maendeleo na huduma katika kipindi cha baada ya kujitawala Bolivia kimeongezeka maradufu ikilinganisha na kipindi cha kuwa tegemezi kwa Magharibi. Amesisitiza udharura wa kupata uhuru na kujitawala kiuchumi sambamba na kujitawala katika masuala ya siasa na kusema: Hii leo pato ghafi la taifa (GDP) la Bolivia limeongezeka kwa zaidi ya dola bilioni 36, kiwango ambacho ni mara nne zaidi ikilinganisha na kipindi cha utegemezi wa nchi yetu.
Rais wa Bolivia ameashiria uzoefu na uwezo mkubwa wa Iran katika nyanja mbalimbali za sayansi na teknolojia na kusema: Iran na Bolivia ni waitifaki wawili wa kihistoria, kiutamaduni na baina ya wananchi na kwamba anatarajia kuwa, uhusiano wa pande mbili utaimarishwa zaidi katika nyanja mbalimbali.
Bwana Morales amesema Bolivia daima inapongeza misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu na ina imani kwamba, Iran itadumisha njia yake kwa azma kubwa zaidi.  
Rais wa Bolivia ameongeza kuwa, Bolivia pia iko imara, ngangari na azma kubwa katika fremu ya ushirikiano na uhusiano wake na nchi za kimapinduzi na ngangari kama Iran.

700 /