Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Tutatetea harakati ya Wapalestina kwa nguvu zetu zote

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu asubuhi ya leo (Jumatano) amehutubia hadhara kubwa ya makamanda 2500 wa vikosi vya wapiganaji wa kujitolea wa Basiji  waliokwenda kuonana naye akiitaja taasisi hiyo kuwa ni mwakilishi mwenye baraka nyingi na anayestawi wa taifa. Amebainisha mbinu za kiadui zinazotumiwa na ubeberu dhidi ya taifa la Iran na kusisitiza kuwa: Katika mpambano na vita halisi vya kambi ya ubeberu na kambi ya kupigania utambulisho na uhuru, taifa la Iran litatekeleza wajibu wake wa kuwatetea watu wanaodhulumiwa hususan taifa shujaa la Palestina katika Intifadha ya Ukingo wa Magharibi.
Ayatullah Khamenei amelipongeza taifa kwa mnasaba wa tarehe 5 Azar (mwaka wa Kiirani) ambayo ni siku ya kutolewa amri ya kuundwa kikosi cha jeshi la kujitolea la Basiji hapa nchini na kusema amri hiyo ilikuwa ubunifu wenye baraka wa Imam Khomeini. Amesema kuwa kuundwa kwa makundi ya mapambano kuna historia katika baadhi ya nchi na vipindi vya mapambano dhidi ya ukandamizaji, lakini suala la kubakia hai makundi hayo ya mapambano baada ya kupata ushindi, kustawi zaidi na kupanuka na kuboreka zaidi ni makhsusi kwa jeshi la Basij.
Akiarifisha maana ya kina ya Basiji, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Basiji wanatokana na wananchi na ni mwakilishi wa taifa zima, na mabasiji ni wananchi wanaoshiriki katika medani zote wanakohitajika kwa malengo aali ya kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na kwa ari na moyo usiochoka na kudhihirisha vipawa vyao bila ya kuogopa hatari yoyote katika njia hiyo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, moja kati ya hakika za kustaajabisha za Basiji ni kudhihirisha na kustawisha vipawa vya wananchi katika sura na kalibu ya Basiji. Ameongeza kuwa, mbali na makamanda mashuhuri na wakubwa wa kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu (vita vya Iraq dhidi ya Iran), watu wakubwa ambao wamefanya na wanafanya kazi adhimu na kubwa katika nyanja za sayansi na teknolojia kama mashahidi wa nyuklia, pia walikuwa na ni mabasiji.
Amesema kuwa miongoni mwa sifa makhsusi za Basiji ni kushiriki katika nyanja mbalimbali za kijeshi, kielimu, kiteknolojia kisanaa, kiutamaduni na katika uchumi ngangari. Ameongeza kuwa: Nimewaagiza viongozi wa serikali watumie uwezo wa Basiji katika uchumi ngangari; hata hivyo makamanda wa Basiji wanapaswa kuwa macho sana kwa sababu masuala ya fedha na uchumi ni miongoni mwa mambo yanayotelezesha sana na miongoni mwa mitego ya adui.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, lengo la kushiriki Basiji katika medani mbalimbali ni kulinda maadili, thamani na utambulisho wa kimapinduzi na wa kitaifa mbele ya adui msaliti, laghai, anayeghushi na mwenye sifa za shetani. Ameongeza kuwa hii leo serikali ya Marekani ndiyo dhihirisho la uadui wa ubeberu dhidi ya taifa la Iran.
Amesisitiza kuwa, kwa sasa mapigano makubwa zaidi katika upeo wa kimataifa ni kati ya kambi ya harakati ya ubeberu ikiongozwa na Marekani na kambi ya harakati ya maadili na kujitawala kitaifa na kiutambulisho chini ya mhimili wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Amesema kuwa, mbali na taasisi na vyombo vya kisiasa, ubeberu unapata himaya ya nguvu ya kifedha na misaada ya makampuni na mashirika makubwa ya Kizayuni, bali kwa hakika kambi ya ubeberu inapanga mambo yake kwa kutumia mihimili mitatu ya fedha, mabavu na udanganyifu.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema udanganyifu katika utendaji wa vyombo vya kisiasa na kidiplomasia vya ubeberu una maana ya mabeberu kukudunga jambia moyoni wakati wanapokuwa wakionesha tabasamu mbele yako na kukukumbatia.
Ametilia mkazo udharura wa kuwa macho daima mbele ya mbinu mbalimbali za uadui laini na mgumu wa mabeberu na kusema: Miongoni mwa maudhui muhimu sana katika uadui laini ni kutumia mradi wa kupenya hapa nchini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema baadhi ya watu walilalamika ilipozungumziwa maudhui ya mradi wa adui wa kutaka kupenya hapa nchini na wakasema kuwa suala hilo linatumiwa kwa ajili ya maslahi ya kimirengo. Ameongeza kuwa, ni makosa iwapo kuna watu wanaotumia suala hilo kimirengo lakini maneno hayo hayapasi kutughafilisha na kutusahaulisha asili ya suala la mradi wa adui wa kutaka kupenya ma kuingia nchini.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa jambo muhimu ni kutambua kwamba adui anafanya mikakati na mipango katika uwanja huo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kupenya kwa watu na kupenya kwa mitandao na makundi ni mbinu mbili kuu zinazotumiwa na wapangaji wa njama hiyo.
Akieleza kupenya kwa watu ambako kuna mifano mingi katika kipindi kilichopita na cha sasa, amesema kuwa: Katika mbinu hii ambayo ina historia ya muda mrefu katika taasisi za kisiasa, serikalini na hata katika taasisi za kidini, watu wanaopenya wanaingia katika nyumba za wanaokusudiwa au katika taasisi na jumuiya za watu wenye majukumu kwa kutumia barakoa la mwenendo au maneno na katika sura ya rafiki.  
Ayatullah Khamenei amesema kuwa miongoni mwa malengo ya kupenya kwa watu ni kukusanya habari za kipelelezi na kufanya ujasusi na kuongeza kuwa, lengo muhimu zaidi la kupenya kwa watu ni kuongoza na kuathiri maamuzi yanayochukuliwa nchini. Amesema, katika mbinu hii ya kuathiri maamuzi, mtu anayejipenyeza hufanya juhudi za kubadili mtazamo wa afisa au mtu mwenye taathira katika harakati za jamii na nchini kuhusu masuala mbalimbali ili achukue maamuzi au kufanya harakati kwa mujibu wa matakwa ya mabeberu.  
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema upenyaji wa mtandao na makundi ndiyo mbinu hatari zaidi nyingine na kuongeza kuwa, katika mbinu hiyo adui kwa kawaida anatumia nyenzo mbili za fedha na vishawishi vya ngono na kujenga mitandao ndani ya taifa na nchi kwa shabaha ya kubadili maadili na itikadi na hatimaye mtindo wa maisha.
Ayatullah Khamenei amesema, katika upenyaji hatari sana wa kimtandao, majmui ya watu huunganishwa pamoja kwa lengo bandia na la uongo kwa kutumia mbinu tofauti kwa shabaha ya kubadili mtazamo wao kuhusu masuala mbalimbali na kuufanya mtazamo wao uwe sawa na ule wa adui.
Amesema kubadilishwa kwa mtazamo hutayarisha mazingira ya kubadilika kwa maadili, itikadi na thamani na kwa utaratibu huo maadui wa kigeni hutimiza malengo yao bila ya kujulikana wala kukabiliwa na hatari.
Ayatullah Khamenei amesema, maafisa wa serikali, wakurugenzi, wasomi na watu wenye taathira katika maamuzi muhimu ya nchi ndio walengwa wa mradi wa adui wa kupenya hapa nchini. Amesisitiza tena kwamba haipasi kupuuza suala hili la njama za kutaka kupenya maadui hapa nchini na umuhimu wake kwa kutumia dhana kwamba, baadhi ya watu wanalitumia vibaya na kimirengo suala hilo.
Amesema kuwa mijadala ya pambizoni inakamilisha mradi wa njama za adui za kutaka kujipenyeza hapa nchini na kuongeza kuwa: Katika kadhia hii watu wanaoshikamana barabara na maadili, thamani na mambo ya msingi hutuhumiwa kuwa wana misimamo mikali na fikra za kuchupa mipaka ili chini ya kivuli cha kunyamaza kwao kimya na kudhoofishwa taratibu maadili na matukufu, kutayarishwe mazingira mazuri ya kufanikisha mradi wa njama za kupenyeza hapa nchini.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amekosoa vikali watu na mirengo inayowahujumu Basiji kwa tuhuma ya kuwa na misimamo ya kufurutu mipaka na kusema: Sisemi kwamba watu na mirengo hiyo inafanya hayo kwa kujua, lakini kwa tuhuma hizo, inadhoofisha ngome imara ya Basiji kwa kujua au bila ya kujua, na kukamilisha mradi hatari wa njama za adui za kutaka kupenya nchini.
Amewanasihi watu wanaotumia nafasi na majukwaa mbalimbali kudhoofisha na kuwaweka makosani wale wanaounga mkono nguzo na misingi ya Mapinduzi na kuongeza kuwa, watu wanaozungumzia maadili, misingi ya Mapinduzi na Imam Khomeini hawapasi kutuhumiwa kuwa ni watu wa kimirengo na waliofurutu mipaka.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake Ayatullah Khamenei ameashiria suala la ustawi, kukua, taathira na baraka endelevu za Basiji na kusisitiza kuwa, mustakbali wa Basiji unang’ara; hata hivyo kuna ulazima wa kuwa na tahadhari na maradhi na matatizo yanayotishia mti imara wa Basiji hususan kutoka kwa ndani.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema ghururi, mghafala unaotokana na ghururi na kuingia katika mashindano ya mali za dunia ni miongoni mwa maradhi ya ndani ambayo Basiji na wanabasiji wanapaswa kujihadhari nayo kikamilifu.
Akieleza vipaumbele vya Basiji, Ayatullah Khamenei ametilia mkazo uchamungu na kuwa na uoni sahihi na kuongeza kuwa: Tunapaswa kutambua vyema uwanja wa ndani hapa nchini, nyayo za miguu ya maadui na nguvu za ndani ya nchi na kuelewa ipasavyo nafasi ya juu na yenye fahari ya taifa la Iran katika eneo hili na duniani.
Amekosoa watu wanaokana uwezo mkubwa wa taifa la Iran kwa kujiona duni na hakiri mbele ya Magharibi na kusema: Tuna baadhi ya udhaifu ndani ya nchi lakini hatupasi kupuuza nafasi muhimu ya Iran katika eneo hili na ulimwenguni na mafanikio na nguvu za taifa hili kubwa, azizi na sharifu kwa kughurika na wageni na kulidunisha taifa.
Ayatullah Khamenei amesema, kuwa tayari siku zote ni miongoni mwa vupaumbele vya Basiji. Amesema hatuwezi kukaa kimya katika mzozo wa kambi ya ubeberu dhidi ya kambi ya maadili na kupigania kujitawala na kwa msingi huo misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko wazi kikamilifu na ni ya kimantiki katika masuala mbalimbali ya kieneo hususan maudhui ya Palestina na masuala ya Bahrain, Yemen, Syria na Iraq.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, lengo kuu la kambi ya ubeberu ni kuwasahaulisha watu thamani na malengo ya Palestina. Ameongeza kuwa, Intifadha ya wananchi wa Palestina imeanza katika Ukingo wa Magharibi licha ya njama zote zinazofanywa na kambi ya ubeberu na madola ya Kiarabu yanayoandamana na mabeberu hao.
Ayatullah Khamenei amegusia pia utendaji wa kidhalimu wa vyombo vya habari vya mabeberu kuhusu maudhui ya Palestina na kusema: Vyombo vya habari vinawaita wananchi wanaorusha mawe kupinga kitendo cha kukaliwa kwa mabavu ardhi zao na kuharibiwa nyumba zao kuwa ni magaidi! Amesema vyombo hivyo vya habari vinaliunga mkono kundi lililoharibu maisha na heshima ya Wapalestina kwa kudai kuwa linajihami na kujilinda. Amehoji kuwa je, mwenendo kama huo kuhusu maudhui ya Palestina ni kosa na dhulma ndogo inayopaswa kufumbiwa macho na kunyamaziwa kimya?
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, Iran itatetea harakati ya wananchi wa Palestina kwa nguvu zote, kwa njia zote na wakati wowote itakapoweza.
Ayatullah Ali Khamenei amezungumzia pia kadhia ya Bahrain na kusema: Kosa la watu wa Bahrain ni lipi? Je, wanadai kitu kingine zaidi ya kura ya kila mmoja kati ya wananchi? Je, hii si demokrasia? Na je, wamagharibi si wanadai kuwa wanatetea demokrasia?
Ameashiria mashinikizo na madhila yanayofanywa na kundi dogo la madhalimu linaloshikilia madaraka ya nchi dhidi ya wananchi wa Bahrain na kusema: Dhulma za kundi hilo dogo zimefikia kiwango cha kuyavunjia heshima matukufu na maombolezo ya Muharram ya watu wa Bahrain.
Ayatullah Khamenei amezungumzia pia miezi kadhaa ya mashambulizi yasiyosita yanayofanywa dhidi ya watu wanaodhulumiwa wa Yemen na kusema: Katika hali hiyo taasisi zinazodai kutetea demokrasia na haki za binadamu zinawaunga mkono wale wanaoendelea kuwashambulia watu wa Yemen.
Kuhusu masuala ya Syria na Iraq, Ayatullah Khamenei amesema: Kambi ya ubeberu inawaunga mkono magaidi habithi na waovu zaidi katika nchi hizo mbili na inataka kuwaainishia Wasyria jinsi ya kuunda serikali ya nchi yao wenyewe.
Amesema: Nyinyi ni kina nani na mna haki gani ya kuwaainishia majukumu Wasyria kutokea upande ule wa dunia?
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Basiji anaweza kubainisha kuwa, misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu masuala ya Palestina, Syria, Iraq, Yemen na Bahrain ndiyo misimamo ya kimantiki zaidi inayoweza kuchukuliwa na mwanadamu mwenye insafu na akili.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei amekitaja kikosi cha  kujitolea cha Basiji kuwa ni dafina isiyoisha na kusisitiza kuwa, kwa taufiki Yake Mwenyezi Mungu, taifa la Iran litalinda dafina hiyo yenye thamani kubwa na kuichimba zaidi na kufikia kilele cha juu cha maendeleo kwa msaada wa hima, azma kubwa na kuona mbali; na maadui hawataweza kufanya lolote.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Meja Jenerali Muhamamd Ali Jafari ambaye ni Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Basiji ni mtoto wa kiroho wa mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Ameongeza kuwa, Basiji wanajitayarisha kubeba majukumu ya kimataifa kwa ajili ya kutimiza malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na kubadili mlingano wa nguvu kwa maslahi ya wanaodhulumiwa na Waislamu.
Vilevile Brigedia Jenerali Muhammad Reza Naqdi, mkuu wa Jumuiya ya Basiji amehutubia hadhara hiyo akiashiria suala la kutimia matakwa ya hayati Imam Khomeini ya kupanuliwa zaidi kikosi cha Basiji katika matabaka yote ya wananchi na kusema: Wanabasiji watashikamana na ahadi yao kwa mashahidi hadi tone la mwisho la damu zao na hawataketi ila baada ya kuangamiza kabisa dhulma.                    
                    
 
          
      
     

700 /