Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu:

Uongozi na nguvu kazi nzuri vinafanya muujiza

Ayatullah Khamenei ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran adhuhuri ya leo (Jumapili) amehutubia hadhara ya makamanda na maafisa wa Jeshi la Majini la Jamhuri ya Kiislamu. Ameashiria umuhimu wa bahari na maendeleo makubwa ya Jeshi la Majini katika kutumia fursa za baharini na kusisitiza udharura wa kudumishwa maendeleo na ujenzi wa Jeshi hilo. Amesema: Nguvu kazi njema, yenye utanashati, fikra na uongozi sahihi sambamba na kusimama kidete, azma kubwa, kutawakali kwa Mwenyezi Mungu na matumaini ya mustakbali mwema ndiyo mambo yanayoweza kuisaidia zaidi Iran ya Kiislamu kufikia nafasi kubwa, ya kihistoria na inayonasibiana na hadhi yake.  
Katika mkutano huo uliofanyika kwa mnasaba wa Siku ya Jeshi la Majini hapa nchini, Amiri Jeshi Mkuu amesema, maendeleo ya jeshi hilo katika miaka ya hivi karibuni yanahisika na kuonekana na kuongeza kuwa: Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu umuhimu, adhama na nafasi nyeti ya bahari vilipuuzwa, lakini hii leo Jeshi la Majini limepiga hatua kubwa za maendeleo japokuwa bado kuna safari ndefu hadi kufikia nafasi inayotakikana.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, bahari ni medani ya mapambano makali na maadui na wakati huo huo uwanja wa shughuli na ushirikiano madhubuti na marafiki. Amesema uwezo wa kufika kwenye maji huru, kuwa na mawasiliano na pande nne za dunia kupitia baharini na uwezekano wa kulinda nchi baharini ni miongoni mwa baraka za bahari na kwa msingi huo wananchi na maafisa wa serikali wanapaswa kuzingatia suala hilo.
Amesema kwamba kufika kwenye nafasi inayooana na hadhi ya kihistoria ya taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu baharini ni wadhifa na jukumu kubwa la Jeshi la Majini. Ameongeza kuwa: Bado tuko mwanzoni mwa njia hiyo na nyinyi ndiyo wanaume wa njia mnaopaswa kuifungua na kutimiza matumaini na mustakbali unaotakikana.
Amiri Jeshi Mkuu amegusia umuhimu wa Bahari ya Oman na pwani ya Makran na kusema: Eneo hilo ni nukta muhimu katika utekelezaji wa majukumu ya Jeshi la Majini na nimetoa na nitatoa maagizo ya dharura kwa viongozi wa serikali kuhusu uhuishaji wa eneo hilo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa sharti la kutimizwa majukumu ya Jeshi la Majini ni ujenzi wa ndani wa jeshi hilo hususan ujenzi wa nguvu kazi inayostahiki, njema, mudiri na nyepesi katika utendaji. Ameongeza kuwa, uongozi na nguvu kazi nzuri vinafanya muujiza, kama ambavyo katika miaka ya hivi karibuni ambapo nchi ilikabiliwa na ingali inakabiliwa na matatizo ya kifedha na bajeti, uzoefu umeonesha kuwa inawezekana kuvuka salama mapungufu na vizuizi mbalimbali hata bila ya kuwa na chochote lakini kwa kuwa na uongozi mzuri.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu chini ya uongozi wa Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) ni dhihirisho la miujiza ya nguvu kazi ya binadamu. Amesema: Kwa kutegemea nguvu ya Mwenyezi Mungu na uwezo na ushawishi wake wa aina yake, Imam Khomeini aliweza kuzusha wimbi kubwa katika bahari ya taifa na akafanikiwa kuuondoa madarakani mfumo tegemezi wa kisiasa uliokuwa na suhula nyingi.
Amesema ushindi wa kustaajabisha wa taifa la Iran katika vita vya kujihami kutakatifu na kumshinda adui aliyekuwa na suhula, zana na aliyekuwa akipewa misaada ya kijeshi na kisiasa ni mfano mwingine wa muujiza wa nguvu kazi ya binadamu. Ameongeza kuwa, hii leo uwezo na maendeleo ya taifa la Iran na majeshi ya nchi umeongezeka zaidi na zaidi na inawezekana kupata mustakbali bora zaidi unaooana na hadhi ya taifa la Iran kwa kusimama kidete, kuwa na azma thabiti, matumaini ya mustakbali mwema na kutawakali kwa Mwenyezi Mungu.  
Kabla ya hotuba ya Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yote ya Iran, Admeri Habibullah Sayyar ambaye ni Kamanda wa Jeshi la Majini ametoa ripoti kuhusu shughuli za jeshi hilo na kusema: Jeshi hili linapiga hatua kubwa kwa utanashati na hima ili kujenga jeshi lenye hadhi na nafasi ya taifa la Iran.             

700 /