Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Umma wa Kiislamu unapaswa kujenga ustaarabu mpya wa Kiislamu

Sambamba na kuwadia mwezi 17 Mfunguo Sita, siku ya kuadhimisha Maulidi ya Bwana Mtume Muhammad SAW na Imam Jafar Sadiq AS, viongozi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na wageni walioshiriki kwenye mkutano wa Umoja wa wa Kiislamu, mabalozi wa nchi za Kiislamu na majimui ya wananchi wa matabaka tofauti, leo asubuhi wameonana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei mjini Tehran.
Katika mkutano huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu sambamba na kutoa mkono wa baraka na fanaka kwa mnasaba wa maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Bwana Mtume mtukufu SAW na Imam Sadiq AS ameashiria suala la kupulizwa roho ya uhai na umaanawi wa kweli baada ya ujio wa Mtume wa Uislamu na namna neema ya kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad SAW na kudhihiri Uislamu ilivyoweza kuhuisha dunia iliyokuwa imekufa na kuteketezwa na ujahilia na kusema kuwa, jukumu kubwa zaidi la ulimwengu wa Kiislamu leo hii hususan kwa maulamaa na wasomi wanaoangalia mambo kwa njia sahihi, ni kufanya jitihada kubwa za dhati kwa ajili ya kupuliza roho ya kweli ya Uislamu na masuala ya kiroho ulimwenguni dhidi ya dhulma, ubaguzi na machafuko yaliyoenea kila mahali duniani leo. Amesisitiza kuwa, hivi sasa ni zamu ya ulimwengu wa Kiislamu kutumia elimu na suhulka za kisasa duniani na vile vile akili na hekima na tadibiri na mtazamo wa mbali kwa ajili ya kusimamisha ustaarabu mpya wa Kiislamu duniani.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa suala la kuadhimisha siku ya kuzaliwa Mtume wa Uislamu SAW ni muhimu sana, lakini umuhimu wake ni mdogo mno ikilinganishwa na umuhimu wa kutekeleza inavyopasa majukumu yanayotakiwa hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Majukumu ya umma wa Kiislamu hayamalizikii tu kwenye kuadhimisha siku ya kuzaliwa Bwana Mtume Muhammad SAW au siku ya kubaathiwa na kupewa kwake Utume, bali ulimwengu wa Kiislamu unapaswa uelekeze zaidi nguvu zake katika kuunda ustaarabu mpya wa Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Ustaarabu mpya wa Kiislamu hauna maana ya kuvamia ardhi za watu wengine, wala kukanyaga haki za binadamu na wala kuyatwisha mataifa mengine akhlaki na utamaduni hu wa Kiislamu na vitu kama hiyo ambavyo vinafanywa na ustaarabu wa Magharibi, bali ulimwengu wa Kiislamu unapaswa hima yake yote iwe ni kufikia kwenye staarabu wake wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia namna Wamagharibi walivyotumia elimu na falsafa ya ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kujenga ustaarabu wao na kuongeza kuwa: Ijapokuwa ustaarabu huo wa Magharibi umeonesha mambo mazuri ya kiteknolojia, kasi ya maendeleo, urahisi wa kufikia baadhi ya mambo na zana mbali mbali za kisasa za maisha ya mwanadamu, lakini umeshindwa kumletea mwanadamu furaha, ufanisi na uadilifu bali pia kunashuhudiwa migongano na mikinzano hata ndani ya ustaarabu huo wenyewe wa Magharibi.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, katika dhahiri yake, ustaarabu wa Magharibi unaonekana ni ustaarabu wenye mambo mengi mazuri na mvuto mkubwa, lakini hivi sasa imethibitika kuwa katika upande wa maadili, ustaarabu huo ni fasidi na mbovu kabisa na katika upande wa umaanawi pia ni pumba na bua kiasi kwamba hata Wamagharibi wenyewe wanaukiri waziwazi uhakika huo.
Aidha amesisitiza kuwa hivi sasa ni zamu ya ulimwengu wa Kiislamu kuweka misingi madhubuti ya ustaaarabu mpya wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Wanasiasa wa ulimwengu wa Kiislamu si watu wa kutegemewa katika jitihada za kulifikia lengo hilo na kwamba maulamaa wa kidini na wasomi wa kweli ambao kibla chao si Magharibi, wanapaswa wafanye kazi ya kuwaamsha watu katika umma wa Kiislamu na wajue kuwa, ni jambo linalowezekana kabisa kuanzisha ustaarabu wa namna hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia uwezo na nafasi pana ya ulimwengu wa Kiislamu ikiwa ni pamoja na kuwa na ardhi nzuri zilizoko kwenye maeneo bora kabisa ya kijiografia, utajiri mkubwa wa maliasili na nguvu kazi yenye vipaji vya kila namna na kuongeza kuwa: Iwapo uwezo huo ulio nao ulimwengu wa Kiislamu utaoanishwa vizuri na mafundisho ya kweli ya Uislamu, basi umma wa Kiislamu utaweza kuonesha kwa namna nzuri kabisa ubora wa vipaji vyake katika nyuga za kielimu na kisiasa na kiteknolojia na vile vile katika nyanja za kijamii.
Ayatullah Khamenei ameutaja mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni mfano mzuri wa uwezekano wa kuyafikia malengo hayo makubwa na kuongeza kuwa: Kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Iran ilikuwa imebaki nyuma sana katika upande wa kielimu, kisiasa na kijamii na katika upande wa kisiasa ilikuwa imetengwa na katika upande wa masuala ya ndani ya nchi pia ilikuwa ni tegemezi kikamilifu. Lakini leo hii kwa baraka ya Uislamu, taifa la Iran limeonesha utambulisho na shakhsia yake na nchi imepiga hatua kubwa muhimu za kielimu na kiteknolojia na elimu za kisasa kiasi kwamba imekuwa ni moja ya nchi bora katika nyanja hizo duniani.
Ayatullah Khamenei vile vile amesisitiza kuwa, mfano huu unaweza kuenea na kushuhudiwa katika ulimwengu mzima wa Kiislamu na kuongeza kuwa: Hata hivyo kufikia kwenye nafasi hiyo kuna masharti yake na miongoni mwa masharti hayo ni kupunguzwa nguvu za jinamizi la madola ya kibeberu kwa mataifa ya Waislamu suala ambalo tab'an lina gharama zake kwani ni jambo lisiloyumkinika kufikia malengo makubwa kama hayo bila ya kuyagharamikia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, katika ustaarabu wa Kiislamu - tofauti na ustaarabu wa Magharibi - hakuna nchi yoyote itakayokuwa chini ya ubeberu wa nchi nyingine. Ameongeza kuwa, katika kuweka misingi ya ustaarabu mpya wa Kiislamu, hatupaswi kuelekeza macho yetu kwa Wamagharibi na wala kutekwa na tabasamu au kuchukia kwao, bali tunachopaswa kufanywa ni kuendelea na njia yetu sahihi kwa kutegemea uwezo na suhula zetu wenyewe.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, moja ya mbinu zinazotumiwa na maadui kwa ajili ya kuzuia kuundwa ustaarabu mpya wa Kiislamu, ni kuzusha mifarakano na mizozo baina ya Waislamu. Ameongeza kuwa: Tangu suala la Ushia na Usuni lilipoanza kuingizwa kwenye msamiati wa viongozi wa kisiasa wa Marekani, watu wenye ufahamu na wenye muono wa mbali walikumbwa na wasiwasi kwani ilionekana wazi kuwa, viongozi hao wa Marekani wameanzisha njama mpya na hatari zaidi kuliko za huko nyuma dhidi ya ulimwengu wa Kiislamu.
Amesisitiza kuwa, Wamarekani wanapinga asili ya Uislamu na hatupaswi kudanganywa na matamshi yao ya kujifanya wanayaunga mkono baadhi ya makundi ya Waislamu. Ameongeza kuwa: Matamshi ya rais wa zamani wa Marekani baada ya kutokea matukio ya tarehe 11 Septemba ambaye alitangaza wazi kuanza vita vya msalaba, kwa hakika ni uthibitisho usiopingika wa kuweko vita vya ulimwengu wa kibeberu dhidi ya Uislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa matamshi yanayotolewa na viongozi wa hivi sasa wa Marekani ya kudai wanakubaliana na Uislamu, yanakwenda kinyume kabisa na uhalisia wa mambo.
Amesema: Viongozi wa hivi sasa wa Marekani wanapinga asili ya Uislamu wenyewe; na tofauti na madai yao, wanachofanya ni kuzusha mifarakano kati ya Waislamu, na mfano wa wazi wa jambo hilo, ni kuanzisha kwao magenge ya kigaidi kama vile Daesh na magenge mengine ambayo yameundwa na kusaidiwa kisilaha, kisiasa na kimafunzo kwa fedha za vibaraka wa Marekani na ndio maana leo hii tunashuhudia maafa haya makubwa yanayotokea katika ulimwengu wa Kiislamu hivi sasa.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba madai ya viongozi wa Marekani ya kujifanya kuwa wanawaunga mkono Masuni kuliko Mashia ni uongo mkubwa na kuongeza kuwa: Hivi kwani wananchi wa Ghaza ambao wanashambuliwa kwa kila namna si Masuni? Je, wananchi wa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan (huko Palestina) ambao wako chini ya mashinikizo yote haya, si Masuni?
Vilevile amegusia matamshi ya mwanasiasa mmoja Mmarekani aliyesema kuwa, adui wa Marekani ni fikra za Kiislamu na kusisitiza kwamba: Wamarekani hawatofautishi baina ya Waislamu wa Kishia na Waislamu wa Kisuni, bali wanampinga Muislamu yeyote yule anayeamua kuishi kwa mujibu wa sheria na mafundisho ya Kiislamu na kusimama kidete kuupigania Uislamu wake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, tatizo kuu la Wamarekani dhidi ya Waislamu ni kushikamana kwao vilivyo na mafundisho na sheria za Kiislamu na kufanya jitihada za kuanzisha ustaarabu mpya wa Kiislamu.
Amesisitiza kuwa: Ni kwa sababu hiyo ndio maana wakati ulipoanza mwamko wa Kiislamu, Wamarekani walishtushwa mno na mwamko huo na wakafanya njama za kuudhibiti na wamefanikiwa kufanya hivyo katika baadhi ya nchi, lakini mwamko wa Kiislamu si kitu kinachoweza kuzimwa na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu mwamko huo utafikia tu malengo yake bila ya shaka yoyote ile.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja lengo na shabaha kuu ya kambi ya kiistikbari kuwa ni kuzusha vita vya ndani vya baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe na kuangamiza miundombinu ya nchi za Waislamu kama vile Syria, Yemen na Libya na kuongeza kuwa: Hatupaswi kunyamazia kimya na kusalimu amri mbele ya njama hizo, bali tunapaswa kusimama imara kukabiliana na njama hizo tukiwa tumejipamba kwa sifa za muono wa mbali na kulinda istikama na kutotetereka.
Vilevile ameukosoa ulimwengu wa Kiislamu kwa kunyamazia kimya mashinikizo waliyo nayo Waislamu wa Bahrain na mashambulizi ya usiku ya mchana ya karibu mwaka mzima sasa wanayofanyiwa wananchi wa Yemen pamoja na hali za Syria na Iraq, kama ambavyo ameashiria pia matukio ya hivi karibuni ya nchini Nigeria na kusema kuwa: Kwa nini sheikh mpenda amani, mrekebishaji wa umma, muumini na aliye tayari kuishi salama na watu wote anafanyiwa ukatili wa kiasi chote hiki na karibu watu elfu moja wanauliwa kiholela na wanawe wanauliwa shahidi na ulimwengu wa Kiislamu unanyamaza kimya?
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Malengo ya maadui wa Uislamu ni ya hatari sana na ni jukumu letu sote kuwa macho na kuwa na muono wa mbali na kwamba ni jukumu la maulamaa wa Kiislamu na wasomi wa kweli wa Kiislamu kuzungumza na wanasiasa wenye mwamko na wenye uchungu na dini yao ili wayabainishe hadharani masuala hayo.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Katika hali ambayo ulimwengu ulioghiriki katika matumizi ya mali na nguvu unatafuta njama hatari mno za kuufanyia ulimwengu wa Kiislamu, hakuna mtu yeyote mwenye haki ya kulala na kutoona mambo yanayotendeka dhidi ya Waislamu duniani leo.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametoa mkono wa baraka kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kuzaliwa Mtume mtukufu wa Uislamu SAW na Imam Jafar Sadiq AS na kusema kuwa, Mtume wa Uislamu ni ruwaza njema ya kimaadili na ucha Mungu na kuongeza kuwa: Bwana Mtume Muhammad SAW amewaletea walimwengu somo la umoja, mshikamano, udugu na kupendana.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, leo hii tunahitajia mno kufuata mafundisho ya Bwana Mtume Muhammad SAW kuliko wakati mwingine wowote na kusema kuwa: Kwa mshikamano wa taifa na uongozi wa kiongozi wetu mtukufu, tumeweza kupata ushindi mbele ya madola ya kibeberu na njia ya ushindi huo itaendelea.
Vile vile amezungumzia chaguzi mbili zinazokuja za Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) na ule wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu (linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu) na kusema kuwa chaguzi hizo ni mtihani wa kuonesha adhama na haiba ya Iran kwa walimwengu na kuongeza kuwa: Kila mmoja anapaswa kufikiria na kuupa kipaumbele ushindi wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na wa nchi katika chaguzi hizo.
Rais Rouhani ameashiria pia hamasa ya wananchi wa Iran ya tarehe 9 Dey 1388 (mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia sawa na Disemba 30, 2009) na kusisitiza kuwa, tarehe 9 Dey ni siku ya ulinzi wa taifa la Iran kwa Ahlul Bait wa Bwana Mtume Muhammad SAW, kuulinda mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, sheria na kulinda utawala wa fakihi na fakihi mtawala.
Rais Rouhani aidha amesema, usalama wa leo hii wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unatokana na busara, hekima, mipangilio mizuri na tadibiri ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na ili kuweza kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa neema hiyo inabidi tuzidi kushikamana na kuusaidia ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kuzikomboa nchi za ulimwengu huo kutoka kwenye matatizo ya ugaidi na uingiliaji wa madola ya kibeberu kwenye masuala ya ndani ya nchi hizo.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aidha amebainisha kuwa, maadui wameutumbukiza ulimwengu wa Kiislamu katika mizozo ya wenyewe kwa wenyewe na kuongeza kuwa: Kama nchi kubwa za Kiislamu zitakuwa kitu kimoja na kufikiria manufaa makuu ya Waislamu, basi itakuwa ni rahisi sana kutatua matatizo yanayoyakumba mataifa ya Kiislamu.
Aidha amebainisha kuwa, baadhi ya nchi za Kiislamu badala ya kushirikiana kiutamaduni na kiuchumi zenyewe kwa zenyewe, zinakimbilia kwa mataifa ya nje ya eneo hili na kuongeza kuwa: Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa nchi fulani inachukizwa na ushindi wa taifa fulani katika uga wa kisiasa na inapeleka rasilimali ya kisiasa ya ulimwengu wa Kiislamu mikononi mwa madola ya kibeberu kwa thamani ya chini kabisa.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: Nchi ambayo imechangia pakubwa katika kuporomoka bei ya mafuta duniani, hivi sasa imekumbwa na nakisi ya dola bilioni mia moja katika bajeti yake ijayo na hili linaonesha kuwa mtu ambaye anawachimbia kisima watu wengine, yeye mwenyewe huwa wa kwanza kutumbukia kwenye kisima hicho.
Mwishoni mwa mkutano huo, wageni kadhaa walioshiriki kwenye mkutano wa 29 wa Umoja wa Kiislamu wamepata fursa ya kuonana na kuzungumza kwa karibu na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

700 /