Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu akilaani vikali mauaji ya Sheikh Nimr:

Mkono wa adhabu ya Mwenyezi Mungu utawakumba wanasiasa wa Aal Saud

 

 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei asubuhi ya leo (Jumapili) katika darsa yake ya masomo ya juu ya fiqhi amelaani vikali jinai kubwa iliyofanywa na Saudi Arabia ya kumuua shahidi mwanazuoni muumini na madhlumu, Sheikh Nimr Baqir al Nimr na kusisitiza kwamba, dunia inapaswa kubeba majukumu yake mbele ya jinai hiyo na jinai nyingine mfano wake zinazofanywa na Saudi Arabia huko Yemen na Bahrain. Amesema hapana shaka kuwa, athari ya damu iliyomwagwa kidhulma ya shahidi huyu madhulumu itaenea kwa kasi na ulipizaji kisasi wa Mwenyezi Mungu utawakumba wanasiasa wa utawala wa Aal Saud.
Ayatullah Khamenei amesema: Mwanazuoni huyo aliyedhulumiwa hakuwa akiwahamasisha wananchi kufanya harakati za kutumia silaha wala hakufanya njama yoyote kwa siri, bali kazi yake pekee ilikuwa kukosoa waziwazi (utawala wa Saudia) na kuamrisha mema na kukataza maovu kutokana na ghera yake ya kidini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, Sheikh Nimr na  kumwagwa damu yake kidhulma ni kosa la kisiasa la serikali ya Saudi Arabia na kuongeza kuwa: Mwenyezi Mungu Mtukufu hafumbii macho damu ya watu wanaouawa bila ya dhambi yoyote na athari mbaya ya damu hiyo iliyomwagwa bila ya haki itawakumba haraka sana wanasiasa na viongozi wa utawala huo.
Amekosoa vikali kimya cha wale wanaodai kutetea uhuru, demokrasia na haki za binadamu na uungaji mkono wao kwa utawala wa Saudia unaomwaga damu za watu wasio na hatia kwa sababu tu ya kulalamika na kuukosoa na kusisitiza kuwa, ulimwengu wa Kiislamu na dunia nzima inapaswa kuhisi kuwa na majukumu kuhusu kadhia hii.
Ayatullah Khamenei amesema, mateso na manyanyaso yanayofanywa na askari wa Saudia dhidi ya watu wa Bahrain na kuharibiwa kwa misikiti na nyumba zao na vilevile miezi kumi ya kushambuliwa kwa mabomu wananchi wa Yemen ni mifano mingine ya jinai za utawala wa Saudi Arabia na kuongeza kuwa: Watu wanaoshughulishwa kwelikweli na hatima ya walimwengu na masuala ya haki za binadamu na uadilifu wanapaswa kufuatilia mambo haya na wasiyapuuze na kunyamaza kimya.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Nina yakini kwamba, shahidi Sheikh Nimr atapata rehma za Mwenyezi Mungu na hapana shaka kuwa, kisasi cha Mola Muweza kitawapata madhalimu waliotoa roho yake, na jambo hili linatoa faraja.       
 

 

 

700 /