Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Wamarekani wanakodolea jacho la tamaa uchaguzi wa Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, leo asubuhi (Jumatatu) ameonana na maimamu wa Swala za Ijumaa kutoka pembe zote za Iran na huku akiashiria utukufu na nafasi ya juu mno ya Swala ya Ijumaa amesema kuwa, sala hiyo ni kitovu cha imani, busuri na maadili mema na kwamba jukumu kuu la maimamu wa Swala za Ijumaa ni kubainisha uhakika wa mambo na kuwa viongozi wa kiutamaduni na kisiasa katika jamii. Vilevile amesema kuwa, uchaguzi ni jambo muhimu mno na kwa hakika ni neema kubwa sana na huku akisisitizia haja ya wananchi kujitokeza kwa wingi kadiri inavyowezekana katika chaguzi za mwezi Isfand (mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia) amebainisha maana ya kina ya "haki ya watu" katika nyuga za "utekelezaji, usimamiaji na haki za wagombea, orodha za wagombea katika uchaguzi, kulindwa kura za wananchi na kukubali matokeo" na kusisitiza kuwa hivyo ni vitu vyenye maana pana vinavyoufanya uchaguzi kuwa kamili na kwamba wananchi wanapaswa kulizingatia kikamilifu suala la kujipenyeza Wamarekani katika masuala ya ndani ya Iran hasa kwa vile (Wamarekani) wameonesha tamaa kubwa ya kujipenyeza kwenye chaguzi hizo.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa: Sababu iliyomfanya aiite Sala ya Ijumaa kuwa ni kitovu cha imani, busuri na na maadili mema ni kwamba hivi sasa tumo katika kupambana na maadui kimaanawi, kiitikadi, kiimani na kisiasa; vita ambavyo tumelazimishwa kuingia ndani yake kama tulivyolazimishwa katika kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu, hivyo kujihami ni jambo la lazima na la dharura kabisa.
Aidha amegusia uwezo wa taifa la Iran wa kujihami kikamilifu na kuongeza kuwa: Katika jihadi hii, (tunapaswa tutambue kuwa) imani, muono wa mbali, taqwa na maadili mema ya watu ndivyo vitu vinavyolengwa na maadui na kuenezwa virusi hatari sana katika jamii.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, jukumu kubwa zaidi la maimamu wa Sala za Ijumaa ni kubainisha ukweli na uhakika wa mambo na kuongeza kuwa: Maimamu wa Sala za Ijumaa ambao ni maulamaa wa miji na warithi wa Mitume wanapaswa waitumie vizuri nafasi ya kijamii ya Sala ya Ijumaa kubainisha na kuweka wazi ukweli na uhakika wa mambo.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema, kuzungumza na watu ana kwa ana na uso kwa uso kupitia Sala ya Ijumaa ni jambo lenye taathira kubwa na ni jambo muhimu zaidi kuliko mawasiliano yasiyo ya moja kwa moja na ya kutumia njia mpya za mawasiliano. Amesisitiza kuwa, Maimamu wa Sala za Ijumaa wanapaswa kuitumia vizuri fursa hiyo muhimu, na kuitumia Sala ya Ijumaa ambayo ni moyo wa utamaduni wa kila mji, kutoa miongozo ya kisiasa na kiutamaduni kwa watu.
Vile vile amesisitiza kwamba, kutoa miongozo ya kiutamaduni ni jambo la kimsingi zaidi kuliko kutoa miongozo ya kisiasa na kuongeza kuwa: Moja ya ya malengo makuu ya maadui wa Uislamu na wa taifa la Iran, ni kuharibu utamaduni na maadili ya wananchi wa Iran hususan mtindo wao wa maisha.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia vielelezo na nukta tofauti za mtindo wa maisha ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Adabu na kujiepusha kikamilifu na kutumia maneno ya matusi hata wakati mtu anapowazungumzia wapinzani ni katika masuala muhimu kwenye mtindo wa maisha ya Kiislamu na kwamba maadui wanafanya njama kubwa za kuwaweka mbali wananchi wa Iran na tabia hiyo njema na inasikitisha kusema kuwa wamefanikiwa katika baadhi ya mambo.
Vile vile amelitaja suala la hulka na kuwa na mazoea mazuri katika maisha kama vile kuwa na tabia ya kusoma vitabu, kuwa ni kielelezo kingine muhimu mno cha mtindo wa maisha ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Inabidi wananchi na hasa vijana wahamasishwe kupenda kusoma vitabu; na wasomi na watu wenye vipawa nao washajiishwe kuandika na kuzalisha vitabu vya kila aina na huwenda ikawezekana kulifanya kila eneo la Sala ya Ijumaa katika mji kuwa kituo kikuu cha kutoa na kuonesha vitabu vya kila namna, vinavyotakiwa na jamii na vinavyokwenda na wakati.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa, moja ya masuala muhimu katika suala la Sala ya Ijumaa, ni kuivutia zaidi jamii ya vijana nchini na kuongeza kuwa: Kuwavutia vijana (kujitokeza kwa wingi kwenye Sala za Ijumaa) hakuwezekani kwa kuwahamasisha kwa maneno tu, bali inabidi vijana wavutiwe kushiriki katika Sala za Ijumaa kwa ufahamu na moyo wa dhati.
Amelitaja suala la kutamka maneno makini na yenye ushahidi katika masuala ya kisiasa na kiutamaduni pamoja na maneno yenye mambo mapya kuwa kunaandaa uwanja wa kuvutiwa vijana kushiriki kwa wingi kwenye Sala ya Ijumaa na kusisitiza kuwa: Kuja na maneno yenye mambo mapya hakuna maana ya kuja na mambo ya bidaa na uzushi, bali maneno yenye mambo mapya yanapaswa yapatikane kupitia kupiga mbizi katika mambo hayo na kuzingatia kwa kina na kutaamali ndani yake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema ni jambo la dharura kwa maimamu wa Sala za Ijumaa kuwa na uhusiano wa karibu na wa kiudugu na watu na kujiweka mbali na ghururi, riya na majivuno, kuwa na mwenendo wa wanafunzi wa kidini, kuwa kama baba na kujiepusha na miamala ya kiidara na ya kujifanya wakubwa ili kwa njia hiyo waweze kuwavutia vijana zaidi kwenye Sala za Ijumaa. Ameongeza kuwa: Katika khutba za Sala za Ijumaa, inabidi ukweli usemwe hata kama utakuwa mchungu kwa walengwa, lakini kwa kutumia dalili na mantiki na msisitizo mkubwa.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitizia wajibu wa maimamu wa Sala za Ijumaa, Kamati Kuu ya Sala nchini Ira na vile vile wananchi ya kulinda nafasi na heshima ya Maimamu wa Sala za Ijumaa na kuongeza kuwa: Kusimamishwa Sala za Ijumaa ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni taufiki kubwa ambayo inabidi thamani yake ijulikane na ni kwa msingi huo ndio maana inabidi khutba za Sala ya Ijumaa zizingatie mahitaji ya kila leo ya jamii.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa uchaguzi ni suala muhimu sana na kwa hakika ni neema kubwa na kuongeza kuwa: Baraka hii ya kweli, inatokana na muono wa kina na wa mbali wa mbinu ya Imam Khomeini (quddisa sirruh) ambaye tofauti na mtazamo wa baadhi ya watu, yeye aliamini kuwa uchaguzi ni kitu cha lazima katika utawala wa Kiislamu na wananchi ndio wenye nchi na aliamini kuwa maamuzi na chaguo la wananchi lazima yapewe nafasi kuu.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Ni chini ya kivuli cha mtazamo huo na uamuzi wa kiistratijia wa Imam, ndio maana hadi leo hii wananchi wa Iran daima wako pamoja na Mapinduzi (ya Kiislamu) kwani wanaona kuwa maamuzi yao yanaheshimiwa na yana athari nchini.
Aidha Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, katika upande wa ndani ya nchi, uchaguzi hulifanya taifa kujihisi kuwa huru, kuwa na utambulisho na kuwa na maamuzi ndani ya nchi yao na kwa upande wa kieneo na kimataifa, uchaguzi unailetea Iran na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu heshima na itibari.
Ayatullah Udhma Khamenei amesisitizia haja ya wananchi kujitokeza kwa wingi kadiri inavyowezekana katika chaguzi mbili zijazo na kuongeza kuwa: Kadiri wananchi watakavyojitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi, ndivyo uimara na itibari ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na nchi ya Iran unavyozidi kuwa mkubwa na ni kwa sababu hiyo ndio maana mara zote tumekuwa tukisisitiza kuwa watu wajitokeze kwa wingi katika uchaguzi na mara hii pia tunalisisitizia tena suala hilo kwani mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unategemea hisia, matakwa na chaguo la wananchi.
Vile vile amewalaumu watu wanaodai kuwa wana wasiwasi na usahihi wa uchaguzi na kuongeza kuwa: Inaonekana kuna baadhi ya watu wamezoea na wamekumbwa na maradhi mabaya ambayo yanawafanya mara zote unapokaribia uchaguzi waanze kupiga ngoma ya kudai wana wasiwasi na uchaguzi ili kuiharibu neema kubwa ya uchaguzi kwa madai yao hayo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Tab'an inawezekana kukatokea dosari za hapa na pale katika uchaguzi, lakini kamwe haijawahi kutokea dosari za kimsingi za kuweza kuharibu uchaguzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja msingi uliowekwa na sheria ya uchaguzi, kulindwa na kusimamiwa uchaguzi na taasisi zote husika na kuchungwa usalama wa uchaguzi na viongozi wa serikali na wasio wa serikali katika hatua zake zote kuwa ni katika masuala ambayo yanaufanya kila uchaguzi nchini Iran kuwa salama na kuongeza kwamba: Baadhi ya serikali zinazoingia madarakani huwa zinatofautiana na serikali nyingine kwa daraja 180, lakini miamala yao yote katika uchaguzi huwa sawa sawa na kwamba chaguzi zote nchini Iran zimekuwa zikifanyika kwa usalama kamili na Inshaallah chaguzi za hivi sasa pia zinatakuwa vivyo hivyo.
Baada ya hapo, Ayatullah Udhma Khamenei amebainisha vipengee tofauti vya ‘mafhumu' yenye maana pana ya "Haki za Watu" katika uchaguzi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ufafanuzi kuhusu Haki za Watu kwa kuanza na haki ya mgombea akisema: Miongoni wa maeneo yanayotumiwa kuchunga haki za wananchi katika uchaguzi ni kuwa, kama mtu ametimiza masharti, huyo hatolewi katika kugombea, bali lazima ihakikishwe kuwa anafunguliwa uwanja wa kujinadi kwa watu na kinyume chake ni vivyo hivyo, kama mtu hakutimiza masharti ya kugombea, iwe ni katika uchaguzi wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu au Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, hapaswi kuingizwa kwa namna yoyote ile katika orodha ya wagombea na iwapo mambo hayo mawili hayakuzingatiwa, itakuwa haki za watu zimekanyagwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kura za wananchi ni amana na kuongeza kuwa: Kulindwa amana hiyo ni kipengee kingine cha Haki za Watu.
Ameongeza kuwa: Watu wote ambao wanahusika katika uendeshaji, usimamiaji, kuhesabu kura na kutoa majumuisho ya kura na kutangaza matokeo, kila mmoja anapaswa kulinda kikamilifu amana hiyo ya kura za wananchi na kwenda kinyume kidogo tu na jambo hilo ni kusaliti amana hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kukubali matokeo ya kisheria ya uchaguzi kuwa ni kipengee kingine cha kuchunga Haki za Watu na kuongeza kuwa: Wakati vituo cha kisheria vinapotangaza matokeo ya uchaguzi na kuthibitishwa matokeo hayo, kupinga matokeo yaliyotolewa na taasisi husika huwa ni kukanyaga na kwenda kinyume na Haki za Watu.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia namna wapiga kura nchini Iran walivyojitokeza kwa wingi mkubwa wa watu milioni 40 katika uchaguzi wa mwaka 2009 na kuongeza kuwa: Mwaka huo, kuna baadhi ya watu walitoa matamshi yasiyofaa na ya kuchukiza walipodai kuweko udanganyifu katika uchaguzi huo na kutaka kuvuruga matokeo yake. Ameongeza kuwa, sisi tuliwalegezea kamba sana watu hao na maelezo yake kwa kweli ni marefu, na tuliwaambia njooni muchague wenyewe masanduku yoyote ya kura mnayotaka, ili yahesabiwe upya, lakini walipuuza nasaha zetu kwani hawakuwa na lengo la kukubaliana na ukweli.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbusha kuwa, mambo yaliyofanywa na watu hao pamoja na madai yao, yalilisababishia hasara nyingi taifa na nchi na hadi hivi sasa hasara hizo hazijafidiwa na sijui lini zitaweza kufidiwa.
Ameendelea kuzungumzia Haki za Watu kwa kuzungumzia suala la kutoa orodha ya uchaguzi.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema: Kuchunga Haki za Watu katika mapendekezo ya wagombea wa mirengo tofauti kuna maana kwamba suala la urafiki na kuvutia mrengo fulani lisiruhusiwe kuathiri orodha zinazotolewa, bali jambo la kuzingatia katika kuteua wagombea liwe ni ustahiki wa kweli wa mgombea.
Vile vile ametoa nasaha maalumu kwa wananchi kuhusu kuchagua wagombea akiwataka wawape kura zao na wawaamini watu na mirengo ambayo wana yakini kuwa ni wapenzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wasichague wagombea kwa malengo maalumu ambayo baadhi ya wakati yanakuwa mabaya.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake mbele ya majimui ya Maimamu wa Sala za Ijumaa kutoka kona zote za Iran kwa kuzungumzia maudhui muhimu mno na tata ya kujipenyeza adui.
Amesema: Watu wenye mfungamano wa Usalama wa Taifa wanajua vyema kuwa, kuna mitego mingi mno iliyotegeshewa Iran au mitengo ambayo inaendelea kupanuliwa hivi sasa ili maadui waweze kujipenyeza kwenye irada na maamuzi ya taifa la Iran.
Ayatullah Udhma Khamenei amegusia udharura wa kuwa macho wananchi na kusisitiza kuwa: Kama tutajaalia kuwa, kuna mtu fulani asiyefaa amejipenyeza katika Baraza la Wanavyuoni Wataalamu au katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu au katika taasisi nyingine za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, basi tujute kuwa mtu huyo atakuwa mithili ya nchwa anayeibebenya ndani kwa ndani na misingi ya utawala.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Katika upande wa kujipenyeza maadui, inabidi kuwaelewesha wananchi madhara ya jambo hilo bila ya kutoa tuhuma kwa wengine na kutoa mifano ya wazi kuhusiana na kujipenyeza huko.
Ayatullah Udhma Khamenei amekumbushia kipindi kilichopo hivi sasa ambacho ni nyeti mno na kuongeza kuwa: Kambi kubwa ya maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu na wa taifa la Iran - kwa kutumia njama za kila namna - muda wote wanafanya njama zao kwani wanahisi kuwa wamekabiliwa na hatari kubwa ya kuenea aidiolojia na fikra za Uislamu sahihi katika maeneo tofauti duniani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Fikra ya Uislamu sahihi ni mithili ya upepo mwanana wa maua yenye harufu nzuri unaonea kila mahala na kulea watu madhubuti na makini katika maeneo tofauti duniani, na ndio maana wapinzani wa Uislamu wanaishambulia Jamhuri ya Kiislamu kwa mashambulizi ya kila aina ya kisiasa na kipropaganda ili kukabiliana na uhakika huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria namna mabeberu wanavyotumia mbinu ya kuchochea watu ndani ya nchi na kufanya mashambulizi ya kipropaganda na kisiasa na kutumia fedha nyingi kutega mitego ya kimaadili na aina kwa aina ya hila nyinginezo na kuongeza kuwa: Watu wote wana wajibu wa kuwa macho katika kukabiliana na hatari ya kujipenyeza adui.
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Ayatullah Udhma Khamenei amegusia namna Wamarekani wanavyoziangalia kwa jicho la tamaa chaguzi mbili zinazotarajiwa kufanyika hivi karibuni nchini Iran na kuongeza kuwa: Wamarekani wanataka mabadiliko kama sisi, lakini mabadiliko tunayoyataka sisi ni kupunguza mwanya uliopo baina ya nchi na jamii yetu na malengo maatakatifu ya Uislamu na ya Maipnduzi ya Kiislamu lakini Wamarekani wao wanataka kinyume kabisa na mabadiliko yanayokusudiwa na taifa la Iran. Mabadiliko wanayoyataka Wamarekani ni kuiweka mbali jamii ya Iran na malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuivuta Iran karibu na malengo yao ya kibeberu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kwa ajili ya kufanikisha lengo lao hilo, Wamarekani wanaukodolea macho ya tamaa uchaguzi wa Iran, lakini taifa kubwa na lililo macho la Iran, - iwe ni katika uchaguzi au katika masuala mengine yote - wamekuwa wakifanya kinyume kabisa na wanavyotaka maadui na kutoa pigo kubwa kwa maadui hao kama walivyofanya zamani.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Taqwai, mkuu wa Baraza la Kutunga Sera za Maimamu wa Sala za Ijumaa nchini Iran amegusia suala la kufanyika kongamano la Maimamu wa Sala za Ijumaa na kuongeza kuwa: Hivi sasa kwa ushirikiano na wananchi kunasaliwa Sala za Ijumaa katika maeneo 845 tofauti ya nchini Iran.
Amelitaja suala la kulinda njia ya Imam Khomeini na ya Mapinduzi ya Kiislamu kuwa ni miongoni mwa majukumu makubwa zaidi ya maimamu wa Sala za Ijumaa nchini na kuongeza kuwa: Kuiunga mkono mihimili mitatu mikuu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama), kuwaelimisha wananchi na kuziweka mbali mimbari za Sala za Ijumaa na mirengo ya kisiasa ni kazi muhimu zaidi na mikakati mikuu ya Baraza la Kutunga Sera za maimamu wa Sala za Ijumaa nchini.
Mwishoni mwa mkutano huo, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewasalisha hadhirina Sala za Adhuhuri na Alasiri.

 

700 /