Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenii:

Dawa ya matatizo ya Afghanistan ni umoja na mshikamano wa kaumu zote

 

 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei,leo asubuhi (Jumanne) ameonana na Bw. Abdullah Abdullah Afisa Mtendaji Mkuu wa serikali ya Afghanistan na kulitaja suala la umoja baina ya makabila na kaumu zote za Afghanistan kuwa ndio utatuzi wa matatizo ya nchi hiyo na huku akiashiria historia na mambo mengi yanayosahilisha kuweko ushirikiano baina ya Iran na Afghanistan amesisitiza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inauhesabu usalama, utulivu na maendeleo ya Afghanistan kuwa ni usalama na maendeleo yake.
Ayatullah Udhma Khamenei amepongeza ubunifu wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na matamshi ya kutia matumaini kuhusiana na kutatuliwa matatizo ya Afghanistan na kuongeza kuwa: Inshaallah serikali ya umoja wa kitaifa ya Afghanistan itaweza kupata muundo wake wa kweli na wa uhakika kwani njia ya kuweza kutatua matatizo ya Afghanistan ni kuleta umoja wa kweli kati ya viongozi na wananchi wa kaumu na makabila tofauti.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia historia ya kuishi kwa salama na amani Waislamu wa Kishia na Kisuni na watu wa kaumu na makabila tofauti nchini Afghanistan na kusema kuwa: Sisi tangu kale tunawajua wananchi wa Afghanistan kuwa ni watu wenye subira, wakinaifu, wachapa kazi, wanaoshikamana na dini na wenye vipaji vya kila namna vya fasihi, lakini hitilafu na mizozo baina ya kaumu mbali mbali na kuzuka mazingira ya kujitokeza undumakuwili, hulidhoofisha taifa lolote lile.
Amekumbushia uungaji mkono wa Iran kwa taifa la Afghanistan ikiwa ni pamoja upinzani wa kipekee wa Jamhuri ya Kiislamu kwa suala la kukaliwa kwa mabavu Afghanistan na Urusi ya zamani na uungaji mkono wa Iran kwa wapiganaji jihadi wa Afghanistan na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu hadi sasa pia iko pamoja Afghanistan na hivi sasa imewapa hifadhi wakimbizi milioni tatu wa nchi hiyo humu nchini.
Ayatullah Udhma Khamenei amelitaja suala la kuweko wanafunzi 16 elfu wa vyuo vikuu raia wa Afghanistan wanaosoma na waliomaliza masomo yao nchini Iran kuwa ni fursa nzuri kwa Afghanistan na kusisitiza kwamba: Serikali ya Afghanistan inabidi iweke vivutio mbali mbali vya kuwafanya raia hao waliomaliza masomo nchini Iran wapende kurejea nchini kwao na kulitumikia taifa lao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia uwezo na suhula nyingi za Iran katika sekta mbali mbali za kielimu, kiufundi na kiuchumi pamoja na kuweko maliasili nyingi na nguvu kazi tajiri nchini Afghanistan na kusisitiza kuwa: Kuongezwa kiwango cha ushirikiano ni kwa manufaa ya pande zote mbili na inabidi ushirikiano na kushibana baina ya mataifa haya mawili kutumiwe vizuri katika kutatua tofauti za mitazamo baina ya nchi mbili kama vile suala la maji na mpaka.
Aidha amekosoa siasa za kuwatenga na kuwaweka pembeni wapiganaji jihadi wa Afghanistan katika miaka ya huko nyuma na kusisitiza kwamba: Kuwaweka pembeni mujahidina kwa visingizio kama vile kuwaita wababe wa kivita, ni siasa ghalati na mbovu na kwamba katika nchi ambayo imekumbwa na mashambulizi ya kijeshi na fitna nyingi, inabidi wananchi wenyewe wawe na moyo wa kupigana jihadi ili kuilinda nchi yao.
Ayatullah Udhma Khamenei amesema kuwa, kutokuwa na uwezo wa kujilinda na kujihami, kwenyewe huandaa uwanja wa kujipenyeza na kujiingiza mabeberu katika masuala ya ndani ya nchi na kuongeza kuwa: Tumeona ni kiasi gani Wamarekani walivyoua watu nchini Afghanistan na kuisababishia madhara makubwa nchi hiyo na hadi leo hii wanaendelea kufanya mauaji na uharibifu nchini humo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesifu moyo wa muqawama wa wananchi wa Afghanistan katika kukabiliana na uvamizi wa Uingereza, Urusi ya zamani na wa Marekani katika miaka ya hivi karibuni na kuongeza kuwa: Moyo wa muqawama na kushikamana ni jambo lililokita mizizi mno kati ya wananchi wa Afghanistan na kwamba katika historia pia ni jambo lililo maarufu kwamba hakuna mvamizi yeyote aliyeweza kubakia muda mrefu nchini Afghanistan.
Katika mazungumzo hayo ambayo yamehudhuriwa pia na Bw. Jahangir, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Bw. Abdullah Abdullah, Afisa Mtendaji Mkuu wa serikali ya Afghanistan ameishukuru Iran kwa misaada na uungaji mkono wake kwa taifa na serikali ya Afghanistan na kuongeza kuwa: Kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini Afghanistan ni hatua nzuri ambayo imeweza kuzuia kutokea matatizo mengi.
Afisa Mtendaji Mkuu wa serikali ya Afghanistan ameongeza kuwa, tatizo kubwa la nchi hiyo ni ukosefu wa usalama na kuweko makundi ya kigaidi na ameongeza kuwa, hivi sasa tunafanya juhudi ili kwa kutawakali kwa Mwenyezi Mungu, na kwa kutumia vizuri mshikamano na uungaji mkono wa wananchi pamoja na ushirikiano na uungaji mkono wa ndugu na marafiki zetu Iran ambao tangu katika kipindi cha jihadi na muqawama hadi hivi sasa wako pamoja nasi, tuweze kutatua matatizo yaliyopo na kuleta uadilifu katika sekta zote nchini Afghanistan.
Bw. Abdullah amemshukuru pia Kiongozi Muadhamu kwa uungaji mkono wake kwa taifa la Afghanistan na vile vile kwa amri yake ya hivi karibuni ya kupewa nafasi za masomo watoto wa Afghanistan nchini Iran na kuongeza kuwa, uungaji mkono huo wenye thamani unaifanya Iran kuwa na nafasi kubwa na muhimu sana katika nyoyo za wananchi wa Afghanistan na kwa serikaki ya nchi hiyo.
Ameongeza kuwa hivi sasa kuna mazingira mazuri ya ushirikiano baina ya Iran na Afghanistan na kwamba katika mazungumzo yetu na viongozi wa Iran tunajitahidi kutafuta njia za kuhakikisha kuwa mazingira hayo yanatumiwa vizuri kadiri inavyowezekana.

 

 

700 /