Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu katika mazungumzo yake na Rais wa China:

Uhusiano wa kistratijia wa Iran na China ni sahihi na wenye hikima

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei, leo jioni (Jumamosi) alimkaribisha ofisini kwake Rais Xi Jinping wa Jamhuri ya Watu wa China na ujumbe alioandamana nao. Amegusia historia kongwe ya uhusiano wa kibiashara na kiutamaduni baina ya mataifa mawili ya Iran na China na kusisitiza kuwa: Serikali na taifa la Iran muda wote lilikuwa na linaendelea kufuatilia suala la kustawisha uhusiano wake na nchi huru na zinazoaminika kama vile China na ni kwa sababu hiyo ndio maana makubaliano baina ya marais wa Iran na China ya kuwa na uhusiano wa kiistratijia wa miaka 25 yakawa ni makubaliano sahihi kabisa na ya hekima sana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameyataja matamshi ya Rais wa China kuhusiana na ulazima wa kufufuliwa na kuhuishwa "Njia ya Hariri" na kustawishwa ushirikiano kati ya nchi zilizoko kwenye njia hiyo kuwa ni fikra nzuri kikamilifu na ni fikra inayokubalika na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haitoweza kusahau ushirikiano mzuri wa China katika kipindi cha vikwazo.
Ayatullah Ali Khamenei amelitaja suala la nishati kuwa moja ya masuala muhimu katika dunia ya leo na kusisitiza kuwa: Iran ndiyo nchi pekee huru katika eneo hili ambayo inaweza kuaminiwa katika upande wa nishati kwani tofauti na baadhi ya nchi za eneo hili, siasa za Iran kuhusiana na nishati haziathiriwi na kitu chochote kile kisichokuwa cha Kiirani.
Vilevile ameashiria siasa za kibeberu za baadhi ya nchi hususan Marekani na ushirikiano wao usio na mwamana na nchi nyingine na kuongeza kuwa: Jambo hilo limezifanya nchi huru kupanua zaidi ushirikiano baina yao na kwamba makubaliano ya Iran na China ya kuwa na uhusiano wa kiistratijia wa miaka 25 yamefikiwa katika fremu hiyo hiyo na kwa hakika inabidi pande mbili zilipe uzito mkubwa suala la kufuatilia makubaliano hayo na kuyaingiza kwenye hatua za utekelezaji.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia namna utamaduni wa Iran unavyopenda na unavyovutika upande wa Mashariki na kuongeza kuwa: Wamagharibi hawajahi kufanikiwa kuvutia imani ya taifa la Iran.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, siasa za Marekani kuhusu Iran ni mbaya zaidi na ni za kiuadui zaidi ikilinganishwa na za nchi nyingine za Magharibi na kuongeza kwamba: Ni siasa hizo za kiuadui za Marekani ndizo zilizolifanya taifa la Iran na viongozi wa nchi hii kulipa umuhimu suala la kustawisha uhusiano wake na nchi huru duniani.
Vilevile amesisitiza kuwa: Kuunga mkono suala la "China Moja" ni katika siasa za kimsingi na zisizobadilika za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na amegusia matamshi ya Rais wa China kuhusu kustawishwa na kuimarishwa uhusiano wa kiusalama baina ya nchi mbili hizi na kuongeza kuwa: Ni jambo la kusikitisha kuona kuwa eneo letu hili limekumbwa na ukosefu wa amani kutokana na siasa ghalati za Wamagharibi na vile vile welewa mbaya, potofu na ghalati kuhusu mafundisho ya dini tukufu ya Kiislamu. Amesema: Kuna hatari hali hiyo ikawa mbaya zaidi hivyo inabidi kuwe na ushirikiano wa kweli na wa busara ili kuzuia kutokea jambo kama hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, baadhi ya nchi za eneo hili ndizo chanzo kikuu cha fikra hizo potofu na kuongeza kuwa: Wamagharibi nao, badala ya kupambana na chanzo cha fikra na makundi hayo ya kigaidi, wanawashambulia na kuwashinikiza Waislamu barani Ulaya na Marekani wakati makundi hayo ya kigaidi yanatofautiana kikamilifu na fikra sahihi ya Uislamu.
Ayatullah Khamenei amegusia namna Wamarekani na Wamagharibi wanavyong'ang'ania kutumia jina la "dola la Kiislamu" kuyaita baadhi ya makundi ya kigaidi na kusema: Kung'ang'ania msimamo huo ni kuwavunjia heshima Waislamu na badala ya kutatua tatizo lililopo, msimamo huo - kwa njia isiyo ya moja kwa moja - unaandaa uwanja wa kuimarika na kuzidi kupata nguvu makundi hayo.
Aidha ameyataja madai ya Wamarekani ya kudai kuunda muungano wa kupambana na ugaidi kuwa ni hila tu za dola hilo la kibeberu na kusisitiza kuwa: Huo ndio msimamo wa Wamarekani katika masuala yote na kamwe hawana mwamana katika vitendo vyao vyote.
Mwishoni mwa matamshi yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameelezea matumaini yake kwa kusema: Matokeo ya mazungumzo na makubaliano ya Tehran yatakuwa na manufaa kwa pande zote mbili kwa maana halisi ya neno.
Katika mazungumzo hayo ambayo yamehudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiisamu ya Iran, Rais Xi Jinping wa Jamhuri ya Watu wa China ameelezea kufurahishwa kwake na kupata fursa ya kuitembelea Iran kama ambavyo ameshuruku kwa mapokezi mazuri, ya kiudugu na kiikhlasi aliyoyapata kutoka kwa serikali na taifa la Iran. Amesema mapenzi hayo yanatokana na kuweko ushirikiano na mabadilishano ya kirafiki na ya muda mrefu baina ya nchi mbili hizi na kuongeza kuwa: Ushirikiano wa pande mbili kati ya Iran na China umesimama juu ya msingi wa kulinda manufaa ya pande hizo na inabidi ushirikiano huo upanuliwe na kustawishwa zaidi kadiri siku zinavyosonga mbele.
Rais wa China ameashiria historia ndefu ya mawasiliano baina ya Iran na China kupitia njia ya kale ya kibiashara maarufu kwa jina la "Njia ya Hariri" na kusema kuwa, njia hiyo ni nembo ya amani, maendeleo na mabadilishano ya kiurafiki ya kibiashara. Ameongeza kuwa: Nchi zilizoko kwenye njia hiyo, zinaweza kushirikiana zaidi na kufikia malengo yao ya ustawi kupitia ushirikiano huo na kujiwekea kinga nzuri mbele ya kigezo cha kiuchumi cha Wamarekani kinacholenga kuvuruga milingano ya kiuchumi katika eneo hili.
Bw. Xi Jinping amesema: Baadhi ya madola makubwa ya kibeberu yanataka kuhodhi kila kitu na yanaendesha siasa za msituni za "imma uwe na sisi au uwe adui yetu" lakini maendeleo ya uchumi unaochipukia hivi sasa yameyapokonya madola hayo udhibiti wa uchumi duniani na yameandaa uwanja mzuri kwa ajili ya kuimarika fikra na siasa za tawala huru ulimwenguni.
Rais wa China amelitaja suala la uungaji mkono wa nchi yake kwa "kadhia ya nyuklia ya Iran" na pia uungaji mkono wa Iran kwa suala la "China moja iliyoshikamana" kuwa ni mfano mzuri wa kuweko kuaminiana na pia kuwa na siasa huru nchi hizi mbili na kuongeza kuwa: Sisi tunaendelea kwa uhuru na njia yetu ya ustawi na tuko tayari - kama tulivyokuwa pamoja na Iran katika kipindi chote cha vikwazo - kuendelea kuwa pamoja na Iran na kupanua ushirikiano wetu katika nyuga zote baada ya kuondolewa vikwazo.
Bw. Xi Jinping amegusia faida nyingi za kijiografia, nguvu kazi na nishati za Iran na kusema: Uchumi wa China na Iran unahitajiana na unakamilishana na katika ziara yangu hii tumefikia makubaliano kuhusu mipango ya ushirikiano wa kiistratijia wa miaka 25 na tuko tayari kupanua na kuimarisha ushirikiano katika sekta nyingine zote za kiutamaduni, kielimu, kiteknolojia, kijeshi, na kiusalama katika kiwango cha washirika wa kiistratijia.
Rais wa China amesema, ni jambo la dharura kuwa na mikakati mizuri ya kuongeza wigo wa ushirikiano wa kiusalama baina ya nchi mbili katika kukabiliana na ugaidi na masuala mengine tata kwenye eneo hili.
Aidha Bw. Xi Jinping amesema kuwa, matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ni ya hekima sana na amemwambia Kiongozi Muadhamu kwamba: Serikali na taifa la China linakuangalia kwa jicho la upendo, udugu na urafiki na ni matumaini yetu utasaidia kustawi zaidi uhusiano wa nchi hizi mbili kama ulivyofanya huko nyuma.
 

700 /