Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Katika mazungumzo yake na maafisa wanaosimamia uchaguzi

Kiongozi Muadhamu: Sheria zinapaswa kuheshimiwa ipasavyo

 

 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, leo asubuhi (Jumatano) amehutubia hadhara kubwa ya maafisa wanaosimamia na kuendesha uchaguzi wa awamu ya kumi ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) na uchaguzi wa awamu ya tano wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu (linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu). Ametoa ufafanuzi kuhusiana na adabu na mambo yanayoweza kudhamini ushindani salama katika uchaguzi amesema kuwa, taifa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo washindi watakaopata fakhari kubwa kwa kuweko ushindani wenye nguvu wa kitaifa katika medani ya uchaguzi. Vilevile amewabainishia viongozi nchini nukta kadhaa muhimu kuhusiana na kuanza kutekelezwa makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 (JCPOA) na kuwaasa viongozi nchini akiwaambia: Marekani ni ile ile Marekani ya zamani, tahadharini na hadaa zake hata katika utekelezaji wa haya matokeo ya hivi sasa ya mazungumzo ya nyuklia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, chaguzi hizo mbili zijazo nchini ni muhimu mno na ni kubwa na huku akisisitiza kuwa uchaguzi ni ushindani na ni mchuano wa kitaifa amesema: Kwa hakika katika mchuano huo, suala la mshindi na mshindwa huwa halina maana kwa taifa kwani vyovyote itakavyokuwa, taifa la Iran ndilo hatimaye litakalokuwa mshindi wa kweli kwenye mchuano huo.
Ayatullah Udhma Khamenei ameongeza kuwa: Iwapo taifa la Iran litaingia vizuri, kwa nia ya kweli na kwa nguvu zote kwenye medani ya uchaguzi na kujaza masanduku ya kura kwa kura na kwa nia yao ya kweli, basi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaona fakhari na itajivunia kuwa na wananchi kama hao.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha mambo ya lazima ya kuwa na mchuano salama katika uchaguzi kwa kusema: Sharti muhimu zaidi la kuwa na ushindani salama, ni kushiriki watu wote waliotimiza masharti ya kupiga kura, hata wale watu ambao hawakubaliani na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Inawezekana kuweko watu ambao wana tatizo na hawakubaliani na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, lakini ni jambo lililo wazi kuwa watu hao hawapingi na hawana tatizo na suala la usalama, maendeleo na heshima ya nchi, hivyo kama watu hao wanataka hali hiyo ya usalama katika taifa iendelee kuwepo, na heshima ya taifa lao iongezeke na kudhaminiwe maendeleo na harakati inayozidi kuimarika ya ustawi wa nchi yao, basi wao nao wanapaswa kushiriki kwenye uchaguzi.
Ameongeza kuwa: Watu ambao wanashiriki katika uchaguzi kwa lengo la kutekeleza majukumu yao na kwa nia ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu, bila ya shaka yoyote watajiandalia mazingira ya kupata radhi za Mola wao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa muhtasari wa matamshi yake hadi kufikia hapo kwa kusisitiza kuwa: Sharti la kwanza na muhimu la kuwa na ushindani salama, ni kushiriki watu wote na kwa hamasa na shauku kubwa katika uchaguzi na kwa uwezo na taufiki ya Mwenyezi Mungu, wananchi walio macho na wanaongalia mbali wa Iran watashiriki hivyo katika chaguzi mbili zijazo.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Kuna baadhi wamekaa wanavizia wakisubiri tu wananchi imam wasijitokeze kabisa katika uchaguzi, au wasusie au wasijitokeze kwa wingi katika uchaguzi ili wapate kutekeleza njama zao dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, lakini wananchi wa la Iran mara zote wamekuwa wakionesha uwezo wao mkubwa wa kufelisha uviziaji huo na watafanya hivyo hivyo pia katika uchaguzi wa mara hii.
Amelitaja sharti la pili la kuweko ushindani salama katika uchaguzi kuwa ni kushiriki wananchi kwa mwamko, busuri, fikra sahihi na muono wa mbali katika uchaguzi na kuchagua watu wema na kuongeza kuwa: Inabidi wananchi wawachague watu ambao baada ya kupokea majukumu, wenyewe wawe kinga ya balaa la matatizo ya nchi na kuelekeza nguvu zao zote katika kuwatumikia wananchi na kulinda maslahi na manufaa ya umma, watu ambao hawataiuza nchi kwa adui na ambao hawatakanyaga maslahi na manufaa ya taifa kwa kuwaonea haya watu wengine.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine amegusia matamshi yake kwamba, hata wale watu ambao wana tatizo na hawakubaliani na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu wanapaswa kushiriki katika uchaguzi na kuongeza kuwa, maneno hayo hayana maana kuwa, wananchi wawachague na kuwapeleka bungeni watu ambao hawakubaliani na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: Hakuna sehemu yoyote ile duniani ambapo watu wanaopinga asili ya mfumo unaotawala nchi hiyo, wanaoruhusiwa kuingia katika taasisi za kuchukua maamuzi ya nchi, bali kuna baadhi ya nchi kama vile Marekani ambayo inajinadi kuwa ni nembo ya uhuru duniani - na hata kuna baadhi ya watu wenye mtazamo finyu wanaoamini madai hayo ya Marekani na wanaeneza propaganda ili kuwafanya watu wengine nao waamini hivyo - wakati wa ushindani wa kambi mbili za Mashariki na Magharibi, Marekani ilikuwa ikiwaweka pembeni watu ambao walikuwa wakituhumiwa kuwa na fikra japo kidogo tu za kisoshalisti (na haikuruhusu kuwa nafasi kwenye taasisi za utawala watu wa namna hiyo).
Ameongeza kwamba: Wakati tunaposisitiza kuwa, kuna wajibu wa kuwapeleka bungeni watu ambao wanakubaliana na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na maslahi yake na matukufu ya nchi huwa tunalinda haki ya umma ambayo ina taathira za moja kwa moja katika kufanyika uchaguzi ulio salama.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia mambo mengine ya lazima kwa ajili ya kufanyika uchaguzi salama akisema: Kuhakikisha kuwa taasisi zote zinazohusika na uchaguzi zinaheshimu sheria, kutozidharau na kuzivunjia heshima taasisi za sheria, kutotia tashiwishi katika akili wa wananchi, kuheshimiana wagombea na kutovunjiana heshima bali kujiepusha na hata kusengenyana, kujiepusha na kutoa ahadi zisizotekelezeka na zilizo kinyume cha sheria na kuamiliana kiuaminifu na wananchi, ni katika vielelezo na adabu za ushindani salama katika uchaguzi ambazo inabidi zichungwe kikamilifu.
Ayatullah Ali Khamenei amezungumzia suala la kutia tashiwishi katika fikra na akili watu kwa kugusia baadhi ya matamshi na matendo ya baadhi ya watu na kusema: Kuna baadhi ya watu utawasikia mara zote wanatumia neno "watu wenye misimamo mikali" na lengo la watu hao ni mrengo wa watu waumini wanaoshikamana vizuri na dini wakati ambapo si sahihi hata kidogo kuwatuhumu vijana wanamapinduzi na walioshikamana vizuri na dini kuwa wana misimamo mikali kwani vijana hao wako katika medani kwa ikhalasi kamili na kwa dhati yao yote na kila wakati linapokuja suala la kulinda mipaka na utambulisho wa taifa, utawaona vijana hao wako katikati ya medani ya mapambano.
Amesisitiza kuwa: Si sahihi kuwahusisha vijana waumini, wanamapinduzi na walioshikamana vilivyo na mafundisho ya dini na matukio mabaya mno na ghalati kama vile kuvamiwa ubalozi wa Saudia, mara tu matukio kama hayo yanapotokea (na hata kabla ya kufanyiwa uchunguzi matukio hayo).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Akili na ufahamu wa vijana hawa wanampinduzi na wanaoshikamana vizuri na dini pamoja na utambuzi wao kuhusu baadhi ya masuala ni mkubwa kuliko hata baadhi ya watu wakubwa, hivyo si sahihi kuwashambulia na kujaribu kuwadhoofisha vijana hao wanaojitolea kwa hali na mali kuyalinda Mapinduzi na dini tukufu ya Uislamu kwa sababu ya kushambuliwa ubalozi wa Saudia na kabla ya hapo ubalozi wa Uingereza, matukio mawili ambayo yote mawili hayana faida kwa nchi na wala kwa Uislamu.
Ayatullah Khamenei ametoa muhtasari wa matamshi yake kuhusu uchaguzi kwa kusema: Uchaguzi ni neema na fursa kubwa na ni wajibu wetu kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa neema hiyo, kupitia kufanya uchaguzi mzuri na salama, hivyo haipasi kuharibu na kuleta tashiwishi katika harakati na fakhari hiyo kubwa kwa kutoa matamshi yasiyo sahihi na kufanya mambo yasiyofaa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameihusisha sehemu ya pili ya hotuba yake na kuzungumzia nukta muhimu kuhusiana na utekelezaji wa Mpango Kamili wa Utekelezaji unaohusiana na makubaliano ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 (JCPOA). Amemshukuru Rais Rouhani na Waziri wa Mambo ya Nje na wajumbe wote waliounda timu ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran na kuongeza kuwa: Tab'an, Jamhuri ya Kiislamu haikuweza kupata mambo yote iliyoyataka katika mazungumzo hayo, lakini kwa hakika watu wote waliohusika kwenye suala hilo wamefanya kazi kubwa na Inshaallah Mwenyezi Mungu atawalipa mema kwa kazi yao hiyo.
Ayatullah Khamenei amewalaumu watu ambao wanajaribu kuonesha kuwa hata haya matokeo ya kiwango hichi ya JCPOA eti yanatokana na fadhila za Marekani na kuongeza kuwa, kuna baadhi ya watu wanataka kutumia fursa hii kukuza na kuisafisha sura mbaya na kibeberu ya Marekani! Kwa hakika jambo hilo ni aibu na ni la hatari sana.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, jambo hilo si la busara na si la kimantiki hata kidogo na kuongeza kuwa: Kama beberu na dhalimu atakupora kwa nguvu eneo, nyumba na mali zako na wewe ukafanya juhudi kubwa na kumlazimisha beberu na dhalimu huyo atoke katika sehemu fulani ya nyumba yako, je, itasemwa kuwa matunda hayo umeyapata kwa fadhila za dhalimu huyo au huwa ni matunda ya nguvu na juhudi zako mwenyewe?
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: Mafanikio ya nyuklia ni matunda ya jitihada, akili na vipaji vya wasomi na wataalamu wa Iran wakiwemo wanasayansi wanne wa nyuklia waliouawa shahidi pamoja na uungaji mkono na kusimama kidete taifa la Iran na kwamba uhakika huo pamoja na jitihada za viongozi nchini ndiyo mambo yaliyomlazimisha adui kurudi nyuma, hivyo ni kukosa insafu kikamilifu kitendo cha baadhi ya watu cha kudai na kufanya propaganda za kujaribu kuonesha kuwa matunda haya yamepatikana kwa fadhila za Wamarekani.
Ametoa ushahidi kutoka katika matamshi ya wazi ya hivi karibuni ya Wamarekani na kusema: Lengo la adui la kuiwekea vikwazo Iran, ni kuwafanya wananchi wa Iran wakasirike na watoke mabarabarani kupinga mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, lakini taifa letu limevumilia na kusimama imara na muda wote limekuwa likilinda heshima na nguvu zake kupitia kuwa pamoja na Jamhuri ya Kiislamu na viongozi wa nchi yao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Tab'an mimi ninaamini kuwa, ingeliwezekana kufanya vizuri zaidi ya hivi, lakini kwa hali yoyote ile fursa na uwezekano uliokuwepo umetuletea matunda hayo na kwa kweli ni matunda mazuri yanayopasa kuzingatiwa.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, Marekani ni sanabu kubwa na mabeberu wengine wa Magharibi ni vijisanamu vidogo vidogo vya kiistikbari. Aidha ametoa ufafanuzi kuhusu malengo hasa ya maadui wa Iran katika kadhia ya nyuklia kwa kusema kuwa: Mtu anaweza kuapa kwamba pande zilizokuwa zinafanya mazungumzo na sisi zilikuwa zinajua kuwa Iran haina mpango wa kumiliki bomu la nyuklia lakini pande hizo zilikuwa zinafuatilia mambo mengine kwa kisingizio cha miradi ya nyuklia.
Amesema, kujaribu kukwamisha harakati kuu ya wananchi na inayozidi kupiga hatua ya taifa la Iran na kuondoa ushawishi unaozidi kuongezeka wa Jamhuri ya Kiislamu katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kiujumla, ndilo lengo kuu la kambi ya kiistikbari la kushadidisha mashinikizo kwa jina la miradi ya nyuklia na ameongeza kuwa: Maadui walitaka wafanikishe malengo yao hayo ili kuyaonesha mataifa ya dunia kuwa hata Jamhuri ya Kiislamu imeshindwa kuongoza na kuendeleza mfumo wa utawala uliosimama juu ya misingi ya kidini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kwamba: Watu wote wakiwemo viongozi nchini wanapaswa kutambua vyema malengo makuu ya Wamarekani. Wamarekani wanatumia mabavu na propaganda kusukuma mbele malengo yao, na inabidi kuwa macho na kusimama imara katika kukabiliana nao.
Ayatullah Khamenei amewataka viongozi wa serikali na wajumbe wa timu ya kusimamia utekelezeaji wa JCPOA wajue kuwa wanapaswa kuwa macho mbele ya hadaa na hila za Marekani na kuongeza kuwa: Marekani imebobea katika kufanya hila na hadaa, hivyo msiviamini vicheko na tabasamu zake.
Aidha amesema, malengo ya hivi sasa ya siasa za Marekani ni malengo yake yale yale ya zamani ya zama za Regan na Bush dhidi ya Iran na kuongeza kuwa: Viongozi nchini wanapaswa kuwa macho na wahakikishe kwamba Wamarekani wanatekeleza inavyopasa ahadi zake katika mpango wa JCPOA, na iwapo Wamarekani hawatofanya hivyo, basi na Iran nayo ifanye kama watakavyofanya wao.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa shukrani nyingi kwa watu azizi wanaoendesha harakati ya kulinda Mapinduzi ya Kiislamu katika suala la kuwakamata wanajeshi wa Marekani walioingia kwenye maji ya Iran na kusema kuwa: Walinzi hao wa Mapinduzi ya Kiislamu walikabiliana vilivyo na wanajeshi hao wa Marekani walioingia katika maji ya Iran na kuwaonesha sura halisi ya Iran na nguvu zake, hivyo viongozi nchini nao wanapaswa kufanya kama hivyo katika nyuga zote na popote pale adui atakapovuka mistari ya manufaa ya taifa la Iran wasimame kidete na kwa nguvu zote kumzuia.
Ayatullah Khamenei amegusia kwa namna nyingine pia sura halisi ya Marekani kwa kusema: Matukio yanayotokea hivi sasa katika ukanda huu yanathibitisha malengo ya miaka michache iliyopita ya Wamarekani wakati waliposisitizia kuundwa Mashariki ya Kati mpya. Amesema: Mashariki ya Kati mpya inayokusudiwa nja Wamarekani ni Mashariki ya Kati iliyojaa vita, ugaidi, taasubu na misimamo finyu kupindukia na iliyoghiriki kwenye mapigano ya kidini na ya ndani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametumia pia fursa hiyo kutoa nasaha akisema: Itambueni Marekani ya kweli kupitia matendo yake kama hayo.
Ayatullah Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kupinga madai yanayosema kuwa, kuondolewa vikwazo kuna maana ya kumalizika matatizo ya kimaisha ya wananchi na kutatutiliwa matatizo yao ya kiuchumi na kuongeza kuwa, kuboreka hali ya maisha ya wananchi na kupatikana maendeleo ya kiuchumi kunataka mipango na usimamiaji mzuri ambao nimekuwa nikizielekeza serikali zote zinazoingia madarakani humu nchini.
Vilevile ameutaja uchumi wa kimuqawama na wa kusimama kidete kuwa ndio mkakati mkuu wa kutatua matatizo ya kiuchumi na huku akisisitizia wajibu wa viongozi nchini kulipa uzito wa hali ya juu suala la kufuatilia utekelezaji wa ratiba zilizopo za kufanikisha uchumi huo na kuongeza kuwa: Kuwakodolea macho maadui hakuwezi kutatua tatizo lolote na inabidi uchumi wa Iran uwe imara na wenye nguvu kiasi kwamba utaweza kukabiliana na mitikisiko yote ya nje na kutoathiriwa na mititigo hiyo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amezungumzia nukta nyingine muhimu kwa kusema: Safari za mara kwa mara za ujumbe tofauti wa nchi za kigeni wanaoingia na kutoka humu nchini na kutiwa saini mikataba mbalimbali kusije kukaruhusiwa kutia madhara viwanda, uzalishaji wa bidhaa za ndani na kilimo nchini, hivyo viongozi wanatakiwa kuchukua tahadhari kuhusu suala hilo.
Mwishoni mwa hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei amesisitiza kuwa: Kushikamana na dini, busuri na muono wa mbali, kujipamba kwa sifa za kimapinduzi na kuimarisha nguvu zake taifa la Iran ni mambo ambayo hadi hivi sasa yamefanikiwa kufelisha njama mbaya sana za maadui walioapa kuliletea madhara taifa la Iran na kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu leo hii pia taifa hili litazishinda siasa zote za mabeberu wa dunia na litaweza kufanikisha malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu chini ya kivuli cha jitihada za pamoja za watu wote; zenye ikhlasi na mshikamano na kuhurumiana.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Jannati, Katibu wa Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ametoa hotuba fupi na kusema kuwa, uchaguzi ni neema ya Mwenyezi Mungu na ni ngao ya usalama, heshima na utukufu wa taifa la Iran na Jamhuri ya Kiislamu.Vilevile ameishukuru Wizara ya Mambo ya Ndani kwa kuonesha ushirikiano mzuri katika hatua mbalimbali za uchaguzi na kuongeza kuwa: Juhudi zetu zote tumezielekeza kwenye kufanya uchaguzi salama, ulio huru, unaoheshimu sheria, wenye ushindani na katika mazingira ya salama na ili kufanikisha jambo hilo, Baraza la Kulinda Katiba linasimamia hatua zote za uchaguzi huo ikiwa ni pamoja na hatua ya kuchunguza watu waliotimiza masharti ya kugombea na kamwe halitaathiriwa na mashinikizo na mambo mengine yoyote ya pembeni.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Ndani (wa Iran) ametoa ripoti fupi kuhusiana na kazi zinazofanywa na Tume ya Uchaguzi nchini kwa ajili ya kusimamia uchaguzi uliojaa hamasa na utakaofanyika kwa kuchunga kikamilifu sheria. Bw. Rahmani Fazli amegusia pia hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ikiwa ni pamoja na kutumia uwezo wa kisheria wa Iran, kuwaelewesha kila kitu na kila siku wananchi kuhusu uchaguzi, kuweka uwazi na kufanya juhudi za kudhamini usalama kamili na kutumia uwezo na suhula zote zinazohitajika kwa ajili ya kulifanikisha jambo hilo muhimu na kuongeza kuwa: Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ina ushirikiano mzuri sana na taasisi na vyombo vingine vyote vinavyohusiana na suala la uchaguzi.

 

 

700 /