Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Katika majibu yake kwa barua ya Rais Rouhani:

Matunda haya yamepatikana kutokana na kusimama imara

 

 

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amejibu barua ya Rais Hassan Rouhani kuhusiana na kumalizika mazungumzo ya nyuklia ambapo ameelezea kufurahishwa kwake na matunda ya kusimama imara taifa la Iran mbele ya vikwazo vya kidhalimu na kurudi nyuma pande zilizokuwa zinakabiliana na Iran kutokana na jitihada za wasomi na wanasayansi wa nyuklia wa Iran na jitihada za watu wote waliohusika kwenye mazungumzo hayo. Ayatullah Khamenei amesisitiza na kutilia mkazo nukta tano muhimu katika barua hiyo iliyotumwa kwa Rais Hassan Rouhani.
Matini kamili ya majibu hayo ni hii ifuatayo:
 Bismillahir Rahmanir Rahim
Janab Dk. Rouhani,
Mheshimiwa Rais (wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran(
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh
Ninaitumia fursa hii kuelezea furaha yangu kwa kuona kuwa muqawama wa taifa kubwa la Iran mbele ya vikwazo vya kidhulma na jitihada za wataalamu wetu wa nyuklia katika kuendeleza teknolojia hiyo muhimu na juhudi zisizochoka za timu za mazungumzo, hatimaye zimepelekea pande za upande wa pili ambazo baadhi yake ni maarufu kwa kulifanyia uadui taifa la Iran, zimelazimika kurudi nyuma na kuondoa baadhi ya vikwazo hivyo vya kibeberu; na ninakushukuru wewe na timu nzima ya mazungumzo na mheshimiwa waziri mwenyewe (wa mambo ya nje wa Iran) na wahusika wote. Ninapenda kuitumia fursa hii kukumbusha masuala yafuatayo:
Mosi: Ihakikishwe kuwa upande wa pili unatekeleza kikamilifu ahadi zake. Hata hivyo matamshi ya siku mbili tatu zilizopita yaliyotolewa na baadhi ya wanasiasa wa Marekani yanatufanya tuwe na mtazamo mbaya kikamilifu.
Pili: Maafisa wote wa serikali watahadharishwe kwamba, utatuzi wa matatizo ya kiuchumi nchini yamo katika jitihada zisizosita na za hekima za sekta zote nchini kupitia uchumi wa kimuqawama na kwamba kuondolewa vikwazo tu hakutoshi katika kuleta ustawi wa kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.
Tatu: Katika kulitangaza suala hilo inabidi lipewe umuhimu suala la kuwatangazia wananchi kuwa, taifa limegharamika mno katika kufikia kilichofikiwa kwenye jambo hili. Maandishi na matamshi yanayotolewa kwa lengo la kujaribu kufifiliza na kupunguza umuhimu wa uhakika huo na kuona kuwa jambo hili limewezekana kutokana na kufadhiliwa na upande wa Magharibi, kwa hakika hayawatendei haki wananchi.
Nne: Haya matunda yaliyopatikana mbele ya kambi ya kiistkbari na kibeberu katika suala hili, yamepatikana kutokana na muqawama na kusimama kidete taifa. Jambo hili linapaswa liwe funzo kubwa kwetu sote katika masuala na mambo yote yanayohusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Tano: Kwa mara nyingine ninasisitiza kwamba isije ikasahauliwa tabia ya tawala za kibeberu hususan Marekani ya hadaa na kuvunja ahadi katika suala hili na masuala mengineyo.
Ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu akupe taufiki wewe na viongozi wengine nchini.
Sayyid Ali Khamenei
29 Dei 94
(Januari 19, 2016(

 

 

700 /