Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Ulaya inapaswa kurekebisha udhaifu wake wa kutokuwa huru mbele ya Marekani

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei  jioni ya leo (Jumatatu) amemkaribisha ofisini kwake Bw. Alexis Tsipras, Waziri Mkuu wa Ugiriki. Katika mazungumzo yake na mgeni huyo Ayatullah Khamenei ameshiria historia inayong'ara ya uhusiano wa kiutamaduni na kiustaarabu baina ya Iran na Ugiriki na kusisitiza kuwa, ziara ya Waziri Mkuu huyo wa Ugiriki nchini Iran inaweza kuwa mwanzo mzuri wa kuzidisha kiwango cha mabadilishano ya kibiashara na kuweka mikakati ya ushirikiano wa muda mrefu baina ya nchi mbili.
Ayatullah Khamenei amegusia pia matamshi ya Waziri Mkuu wa Ugiriki kuhusiana na kuweko mitazamo na manufaa yanayokinzana baina ya nchi za Ulaya na kuongeza kuwa, bara la Ulaya lina haki ya kukosolewa kwani tofauti na huko nyuma, hivi sasa nchi hizo hazina misimamo huru mbele ya Marekani na inabidi watu wa Ulaya warekebishe udhaifu wao huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusu matamshi ya Waziri Mkuu wa Ugiriki kuhusiana na Syria kwamba: Ugaidi ni ugonjwa hatari sana na ambukizi ambao kama watu wote watalipa uzito mkubwa suala la kupambana nao, basi unaweza kudhibitiwa; hata hivyo jambo la kusikitisha ni kuona kuwa kuna baadhi ya watu- kwa njia ya moja kwa moja au isiyo ya moja kwa moja- wanayasaidia magenge ya kigaidi.
Vilevile amegusia nukta za pamoja na zinazofanana katika siasa za Iran na Ugiriki na kumwambia Waziri Mkuu wa Ugiriki kwamba: “Serikali yako na wewe mwenye mna siasa na misimamo huru na ni matumaini yetu mtaweza kuyashinda matatizo yenu ya kiuchumi kama ambavyo ni matumaini yetu kuwa, ziara yako hii itaandaa uwanja wa kulindwa zaidi manufaa ya nchi zote mbili.”
Katika mazungumzo hayo ambayo yamehudhuriwa pia na Bw. Is’haq Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran, Waziri Mkuu wa Ugiriki, Bw. Alexis Tsipras, amemhutubu Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa kumwambia: “Wewe ni kiongozi wa taifa kubwa lenye mambo mengi ya kujivunia la Iran ambaye una nafasi muhimu mno katika historia ya kulinda malengo matukufu na uhuru wa watu wa nchi hii.”
Bw. Alexis Tsipras ameongeza kuwa, safari yake nchini Iran inaonesha kuweko nia ya kweli ya pamoja ya kisiasa kwa ajili ya kupanua wigo wa ushirikiano wa nchi mbili hizi katika daraja zote na kuongeza kuwa, safari yake hiyo nchini Iran ni nukta muhimu sana katika uhusiano wa pande mbili na ni kwa manufaa ya nchi zote hizi mbili.
Waziri Mkuu wa Ugiririki amegusia pia kuweko mitazamo na manufaa yanayokinzana pamoja na utata na matatizo ya nchi za Ulaya na kuongeza kuwa: Uchumi wa nchi za Ulaya unategemeana na ni jambo zito sana kufanya mabadiliko kwenye uchumi huo na kwamba ili hali hiyo irekebishwe, kuna udharura wa kubadilishwa kabisa mlingano wa nguvu ndani ya Umoja wa Ulaya.
Bw. Alexis Tsipras, Waziri Mkuu wa Ugiriki aidha amesema kuhusiana na kadhia ya Syria kuwa: Ni matumaini yetu tutashuhudia mabadiliko chanya katika kadhia ya Syria kwani mgogoro wa nchi hiyo una madhara mengi ya kibinadamu ambapo mamia ya maelfu ya watu wamelazimika kukimbia makazi yao na kuelekea kwenye nchi nyingine kama vile Ugiriki kutokana na mashambulizi ya makundi ya kigaidi nchini mwao.

 

700 /