Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu:

Hotuba za Imam ndiyo msingi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, leo asubuhi ameonana na Admeli Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa pamoja na manaibu na wataalamu wa sekretarieti ya baraza hilo. Ameashiria namna istilahi na neno "usalama" lilivyo tata na lilivyo na vipengee vingi tofauti katika dunia ya leo na kulitaja jukumu la Baraza Kuu la Usalama wa Taifa kuwa ni kuchukua maamuzi kwa kuangalia upana na vipengee vyote vya neno usalama.

Ameongeza kuwa jukumu kuu la sekretarieti ya baraza hilo ni kuandaa maamuzi ya kuonesha njia sahihi ya uchukuaji maamuzi ndani ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa. Amesisitiza kuwa: Ili sekretarieti hiyo iweze kutekeleza vizuri na kwa njia sahihi wadhifa muhimu sana wa kuandaa maamuzi, anga inayotawala sekretarieti ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na maamuzi yake inapaswa kwenda sambamba na fikra sahihi, halisi za kimapinduzi na za kihizbullah. (za watu wanaoshikalama barabara na mafundisho ya dini)."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, usalama ni haja muhimu sana kwa jamii na kwa msingi huo suala hilo limeashiriwa mara nyingi katika Qur'ani Tukufu. Amesisitiza kuwa, suala la usalama katika dunia ya sasa limevuka mzingo wa masuala ya kijeshi na kugusa pia masuala ya uchumi, maisha, utamaduni, siasa, kijamii, fikra na maadili..

Ayatullah Khamenei amelitaja jukumu kuu la Baraza Kuu la Usalama wa Taifa kwamba ni kuwa na mtazamo mpana kuhusu kadhia ya usalama na kuzingatia vipengee vyake vyote. Ameongeza kuwa: Sekretarieti ya baraza hilo inapaswa kutekeleza vizuri wajibu wake mkuu wa kuandaa maamuzi kwa namna ambavyo misimamo inayochukuliwa na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa iwe inachukuliwa kutokana na kuwa na mtazamo sahihi unaozingatia pande zote za neno usalama.

Vilevile amegusia kazi tofauti za sekretarieti ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na kusema kuwa: Suala la sekretarieti ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa ya kuweza kutekeleza kwa njia sahihi majukumu yake, linategemea kutawala kikamilifu anga ya asilimia mia moja ya kimapinduzi katika chombo hicho kwani kama misimamo inayokinzana na misimamo ya Mapinduzi ya Kiislamu itajipenyeza kwenye suala la uandaaji wa maamuzi katika sekretarieti ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa, basi matunda yanayotakiwa hayataweza kupatikana.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, misimamo na mielekeo ya kimapinduzi si njozi na fikra zisizo na ukweli na kuongeza kuwa: Misimamo na mwelekeo wa kimapinduzi ni jambo la kweli, lililo wazi kikamilifu na ni lenye msingi katika matamshi ya Imam Khomeini.

Ayatullah Khamenei ameashiria njama za baadhi ya watu za kutaka kubadili misingi mikuu na ya wazi ya Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Imam Khomeini ni dhihirisho la Mapinduzi ya Kiislamu na kwa msingi huo hotuba zake zilizoandikwa katika makumi ya vitabu ni misingi ya Mapinduzi. Amesema, mambo yaliyokaririwa na Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) katika matamshi yake hayo ni mipaka na mistari mikuu na ndiyo misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Kwa mujibu wa matamshi ya Imam, suala la "wananchi," "uhuru wa nchi," "kushikamana na dini na misingi ya Uislamu," "kupambana na ubeberu," "kadhia ya Palestina," "suala la maisha ya wananchi," "kuwazingatia wanyonge na kutokomeza umaskini" ndiyo misingi mikuu ya Mapinduzi ya Kiislamu ambayo katika mkusanyiko wake kunapatikana muundo mkuu na halisi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, maamuzi ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa yanapaswa kuwa ndani ya fremu ya misingi mikuu ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Fikra sahihi na halisi ya kimapinduzi na "kihizbullah" inapaswa kutawala kikamilifu ndani ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na sekretarieti ya baraza hilo.

Amesema kuwa tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini baadhi ya watu hawakukubaliana na fikra za kimapinduzi na baadhi yao pia hawakuwa na itikadi ya kupambana dhidi ya ubeberu licha ya kuwa ndani ya mfumo wa Kiislamu; hivyo kuna udharura wa kukabiliana na mrengo huu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa katika kipindi chote cha miaka 37 iliyopita ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini daima kumekuwepo mapambano na kuongeza kuwa, hii leo mpambano huo umekuwa mgumu na tata sana kutokana na mbinu mpya na tata zinazotumiwa na adui kama maudhui ya anga ya intaneti na taathira zake za kiutamaduni, kiitikadi, kijamii na dhidi ya usalama.

Ayatullah Khamenei ameashiria jinsi mbinu mpya zinazotumiwa na maadui zinavyoathiri pole pole na kimya kimya misingi ya ndani kabisa ya usalama katika jamii na kuongeza kuwa: Baraza Kuu la Usalama wa Taifa lina wajibu wa kufuatilia masuala yote hayo katika sekta tofauti na hatimaye kuyachukulia maamuzi na ndio maana sekretarieti ya baraza hilo inapaswa kuwa na fikta sahihi na kufanya juhudi daima na za kiutaalamu kwa kutegemea msingi wa fikra ya kimapinduzi na baadaye kuandaa maamuzi sahihi ya kuweza kukabiliana vilivyo na mbinu tata na mpya za adui wa usalama na amani ya taifa.

Mwishoni mwa hotuba yake, amemtaja Admeri Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa kuwa ni miongoni mwa kumbukumbu nzuri sana za kipindi cha vita vya kujihami kutakatifu (Vita vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa zamani wa Iraq dhidi ya utawala mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran) na ameishukuru sekretarieti ya baraza hilo kutokana na jitihada na kazi zake nzuri za kuandaa ripoti muhimu na za wakati mwafaka kuhusiana na maudhui mbalimbali.

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Bw. Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa ametoa ripoti fupi kuhusu kazi za sekretarieti ya baraza hilo na kusema kuwa, kupanga sera, kuratibu na kusimamia ndiyo majukumu makuu ya Baraza Kuu la Usalama wa Taifa nchini. Ameongeza kuwa, sekretarieti ya baraza hiyo ina jukumu la kuunga mkono na kusaidia kiutaalamu maamuzi wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa na kwamba nafasi hiyo daima inapaswa ioane na iwe katika mkondo wa siasa kuu za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na za Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

 

700 /