Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mazungumzo yake na Rais wa Ghana:

Taifa la Syria ndilo linalopaswa kuchukua uamuzi kuhusu mustakbali wa Syria si Marekani

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alasiri ya leo amemkaribisha ofisi kwake na kufanya mazungumzo na Rais John Dramani Mahama wa Ghana. Katika mazungumzo hayo Ayatullah Khamenei ameashiria mtazamo chanya na wa upendeleo wa Iran katika suala la kuzidisha ushirikiano na nchi za Kiafrika tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini na kusema: Madola makubwa ya kibeberu yanapinga kuwapo uhusiano mzuri kati ya Iran na nchi za Afrika na ndiyo sababu ya vita, mapigano na wafadhili wa makundi ya kigaidi; hata hivyo tiba ya matatizo yote hayo imo katika kukurubiana zaidi nchi zinazojitawala na kuzidisha ushirikiano wao.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, maslahi ya madola ya kibeberu yamo katika kuvuruga usalama na kuanzisha vita mbalimbali katika maeneo tofauti ya dunia na kuongeza kuwa: Makundi ya Kigaidi katika eneo hili na barani Afrika yalianzishwa na mashirika ya ujasusi ya Marekani, Uingereza na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kuhusu matamshi ya Rais wa Ghana aliyezungumzia mashaka ya Syria yanayosababishwa na ugaidi, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amehoji kwamba, vipi makundi ya kigaidi yanapewa silaha za kisasa na fedha, na kuongeza kuwa: Chanzo cha matatizo yote ni madola ya kibeberu ambayo Marekani ndio kinara wao, na utawala wa Kizayuni wa Israel ni dhihirisho la shari.
Amesema kuwa, siasa za Jamhuri ya Kiislamu katika kadhia ya Syria ni kuunga mkono amani na kuongeza kuwa, daima Iran imefanya jitihada kuhakikisha kwamba kadhia hiyo inahitimishwa kwa maslahi ya taifa la Syria na inaamini kwamba, haiwezekani kuainisha tiba ya matatizo ya taifa fulani kutoka nje ya nchi husika.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, Wamarekani na watu wa Ulaya hawawezi kuliainishia majukumu taifa la Syria na kwamba ni taifa la Syria pekee ndilo linalopaswa kuchukua uamuzi kuhusu mustakbali wake.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa njia ya utatuzi wa suala la Syria na kukabiliana na matatizo kama ugaidi na mashaka yanayowapata watu wa Palestina ni kushirikiana na kukaribiana zaidi nchi huru na zinazojitawala. Amesema kuwa, Iran na Ghana zina uwezo mkubwa na tuna matumaini kwamba safari hii itapelekea kuzidishwa ushirikiano.
Vilevile amepongeza mapambano ya kupigania uhuru ya baadhi ya shakhsia wa Kiafrika dhidi ya wakoloni na kusema: Shakhsia hao wakubwa wamepandisha juu utambulisho wa Kiafrika duniani.
Katika mazungumzo hayo ambayo pia yamehudhuriwa na Rais Hassan Rouhani, Rais wa Ghana, John Dramani Mahama ameashiria ustaarabu tajiri wa Iran na maendeleo yake makubwa katika nyanja za elimu na sayansi na kusema kuwa matamshi ya Kiongozi Muadhamu yanahamasisha ujenzi wa dunia yenye amani na usalama.
Kuhusu suala la Palestina, Rais wa Ghana amesema kuwa, mashaka na matatizo ya taifa la Palestina yanayatia wasiwasi mataifa yote na kuna ulazima wa kushirikiana kwa ajili ya kutetea haki za Wapalestina.
Vilevile amegusia harakati za makundi ya kigaidi barani Afrika na magharibi mwa Asia na amepongeza mapaambano halisi ya Iran dhidi ya ugaidi. Rais John Dramani Mahama wa Ghana amesema kuhusu hali tata ya Syria kwamba: “Siasa za nje za Iran zinasimama kweli juu ya msingi wa kuheshimu haki ya mataifa mengine ya kujiainishia mustakbali wao na tuna matumaini kwamba, suala la Syria litatatuliwa kwa mchango na nafasi muhimu wa Iran katika mapambano dhidi ya ugaidi.
Rais wa Ghana ameipongeza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na misaada yake ya kibinadamu kwa watu wa Ghana na kusema: “Kwa niaba ya mataifa ya bara la Afrika, ninachukua fursa hii kuishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na nafasi yake ya kuzihami harakati za kupigania uhuru barani humo hususan harakati ya kupambana na utawala wa ubaguzi wa rangi huko Afrika Kusini.
Rais wa Ghana ameashiria pia mazungumzo yake hapa mjini Tehran na kutiwa saini hati kadhaa za maelewano na kusema kwamba, nchi yake iko tayari kuzidisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali.
          

 

700 /