Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

KiongoziKiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aonana na watu wa Azerbaijan Mashariki

Watu kwenye uchaguzi, wafanye kinyume na matakwa ya adui

Leo Asubuhi Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ameonana na umati mkubwa wa maelfu ya watu wa matabaka mbalimbali kutoka Azarbaijan Mashariki, na huku akitoa shukrani zake za dhati kwa taifa la Iran kutokana na ushiriki wao mkubwa katika maandamano ya tarehe 22 Bahman, sawa na tarehe 11 Februari, amesema kuwa ushiriki huo mkubwa unathibitisha wazi azma thabiti, msimamo imara na mwamko wa wananchi. Amesisitiza kwamba uchaguzi ujao wa tarehe 26 Februari nchini pia utakuwa ni dhihirisho la mwamko wa taifa na uteteaji wake wa mfumo wa Kiislamu, kujitawala na heshima ya taifa. Amewataka wananchi kujitokeza na kushiriki kwa wingi kwenye uchaguzi huo wakiwa na mwamko na ufahamu wa kutosha na hivyo kufanya kinyume na anavyotaka adui wa Mapinduzi ya Kiislamu. Akizungumza mbele ya umati huo mkubwa katika kuwadia maadhimisho ya mapambano ya watu wa Tabriz tarehe 18 Februari mwaka 1978, Ayatullah Khamenei amesifu imani thabiti, mwamko, msisimuko na msimamo imara wa watu wa mkoa wa Azarbaijan katika vipindi muhimu na nyeti katika historia ya Iran na hasa katika kipindi cha Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza juu ya udharura wa kuhuishwa siku muhimu za historia ya Mapinduzi ya Kiislamu. Ameashiria tarehe 22 Bahman ikiwa ni moja ya siku muhimu mno nchini na kuongeza kuwa kwa mujibu wa takwimu za taasisi za kuaminika, ushiriki wa wananchi katika maandamano ya hamasa ya Bahman 22 mwaka huu kote nchini ulikuwa mkubwa zaidi ukilinganishwa na wa miaka iliyopita. Ayatullah Khamenei ametoa shukrani zake za dhati kwa wananchi kutokana na kushiriki kwao kwa wingi katika maandamano hayo na kusisitiza kwamba mahudhurio makubwa ya wananchi katika maandamano hayo yanabainisha wazi kwamba licha ya kuwepo juhudi kubwa zinazofanywa na kambi ya uistikbari duaniani kwa ajili ya kusahaulisha au kuyadhoofisha Mapinduzi kwenye fikra za watu, lakini juhudi hizo hazijadhoofisha kwa namna yoyote ile azma thabiti ya wanachi kuhusiana na suala hilo. Kisha ameashiria uchaguzi unaotazamiwa kufanywa tarehe 26 ya mwezi huu wa Februari hapa nchini na kusisitiza kwamba adui amepanga mpango maalumu kwa ajili ya kutekeleza njama zake kuhusu uchaguzi huo. Amesema kwa kutilia maanani njama hizo, wananchi wa Iran ambao ndio wamiliki halisi wa nchi hii wanapasa kujua baadhi ya mambo ili kuvunja njama hizo chafu na hatari.

Wageni wanataka kuwa na ushawishi kwenye uchaguzi, lengo likiwa ni kutaka kuharibu jina la Baraza la Kulinda Katiba na maamuzi yake

Huku akitangulia kusema kuwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kukatwa mikono miovu ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel nchini Iran kuliwadhalilisha sana maadui hao wa Mapinduzi ya Kiislamu, maadui ambao katika kipindi chote cha miaka 37 hawajawacha kufanya juhudi za kusimamisha kasi kubwa ya taifa la Iran, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amesema kuwa tokea mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu wageni hao walifanya njama za kutaka kuzuia kufanyika uchaguzi nchini Iran lakini kwa sababu wamekata tamaa kuhusiana na suala hilo, katika miaka ya hivi karibuni wameelekeza nguvu zao zote katika kutilia shaka jinsi uchaguzi huo unavyofanyika kwa lengo la kupenya na kubadili mkondo wake. Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa njama zao za uchaguzi wa Februari 26 zimeanza kwa kujaribu kuliharibia jina Baraza la Kulinda Katiba na kutilia shaka maamuzi yake. Amesema baraza hilo ni moja ya taasisi muhimu za mfumo wa Kiislamu wa Iran ambazo tokea mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, zimekuwa zikipingwa vikali na Marekani. Amesema natija ya kutiliwa shaka maamuzi ya baraza hilo ni kujaribu kuonyesha kuwa uchaguzi sio halali. Ameendelea kusema maadui wanajaribu kuonyesha kuwa wakati uchaguzi unapokuwa si halali basi bunge lililochaguliwa kupitia uchaguzi kama huo pamoja na maamuzi yake pia si halali. Kiongozi wa Mapinduzi ameongeza kuwa lengo la njama hizo za hadaa ni kujaribu kuiweka nchi katika hali isiyokuwa na sheria wala bunge katika miaka minne ijayo jambo ambalo amesema wananchi wanapasa kulizingatia kwa makini. Ayatullah Khamenei ameashiria watu wanaoshirikiana na adui ndani ya nchi katika kukuharibu jina la Baraza la Kulinda Katiba na kusema kuwa wengi wao hawazingatii athari za maneno yao na kwamba hawawezi kutuhumiwa kuwa ni wahaini, lakini akaongeza kuwa watu hao wanapasa kuelewa kuwa ushirikiano wao huo unakamilisha njama na mipango hatari ya adui.

Huku akisisitiza kwamba moja ya malengo ya mrengo wa uistikbari ni kutilia shaka uchaguzi na kuyaepusha mataifa ya dunia na dhihirisho la aina yake, halisi na la kuvutia la demokrasia ya kidini, Ayatullah Khamenei ameashiria nafasi muhimu ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, yaani bunge na kuongeza kuwa kwa kubuni na kupitisha sheria, majlisi hutengeneza njia ya reli kwa ajili ya kuiwezesha serikali kutekeleza majukumu yake na kwa hivyo uchaguzi wa wabunge unaofanyika kwa msingi wa mwamko na uelewa una athari kubwa katika kutengeneza njia ya reli na kuainisha muelekeo wa nchi. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi amesisitiza kwamba iwapo Majlisi itakuwa inafuatilia malengo ya kuimarisha maisha ya wananchi, uadilifu wa kijamii, kuboresha uchumi, kuendeleza elimu na teknolojia, kulinda kujitawala kwa nchi na utukufu wa kitaifa, ni wazi kuwa itatengeneza reli inayofaa kuelekea malengo hayo lakini kwamba iwapo itavutiwa na umagharibi na Marekani pamoja na utawala wa mabepari, ni wazi kuwa reli ya Majlisi hiyo itaelekea kwenye malengo hayo na hivyo kuielekeza nchi pabaya. Ayatullah Khamenei ameashiria maneno ya Imam Khomeini (MA) ambaye alikuwa akiamini kuwa Majlisi iko kwenye kilele cha masuala yote nchini, na kusema kuwa huko kuwa kwenye kilele cha mambo hakuna maana ya hatua za utendaji bali ni kusisitiza juu ya umuhimu wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu katika mtazamo wa kuainisha muelekeo wa nchi. Kiongozi Muadhamu pia amezungumzia umuhimu mkubwa wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu katika mfumo wa Kiislamu na kusema kuwa umuhimu huo unatokana na ukweli kwamba baraza hilo ndilo linalomchagua kiongozi wa Mfumo wa Kiislamu, na hivyo kuwa muamuzi na mtungaji mkuu wa sera za nchi na kwa msingi huo uchaguzi wa wawakilishi wa baraza hilo ni suala muhimu mno. Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa iwapo wawakilishi wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomteua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi watakuwa wanafungamana na Mapinduzi, kuwa waaminifu kwa taifa, kufahamu njama za adui na kusimama imara mbele ya njama hizo bila shaka watachukua uamuzi  wa pamoja na kwa wakati unaofaa dhidi ya njama hizo, lakini kwamba kama hawatakuwa hivyo basi maamuzi yao yatakuwa vingine. Ayatullah Khamenei ameashiria hujuma na uzingatiaji wa vyombo vya propaganda vya mrengo wa uistikbari dhidi ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu na kusisitiza kuwa lengo la kusisitiza mara kwa mara udharura wa kuwa na mwamko na uelewa wa kutosha wa wananchi katika uchaguzi linatokana na maudhui hiyohiyo ili wapate kuchukua maamuzi yanayokwenda kinyume na matakwa ya adui. Kwa mara nyingine tena Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ametaka wananchi kushiriki kwa wingi katika uchaguzi na kulinda Mfumo wa Kiislamu, kujitawala na heshima ya kitaifa na kusisitiza juu ya kuwa na mwamko katika kukabiliana na mrengo usiotumia akili na hatari, uliosimama mbele ya taifa la Iran na unaodhibitiwa na kuongozwa na mtandao wa Kizazayuni. Ameongeza kuwa siasa za Marekani na nchi nyingi za Ulaya zinadhibitiwa na mtandao huo na kwamba utendaji wa Wamarekani kuhusiana na kadhia ya nyuklia pia unapasa kutathminiwa kwa mtazamo huo.

Moja ya malengo ya mazungumzo ya nyuklia lilikuwa ni kuimarisha uchumi kupitia uwekezaji wa kigeni lakini Wamarekani wanataka kulizuia jambo hilo pia

Ayatullah Khamenei amesema kuwa baada ya mazungumzo ya muda mrefu ya nyuklia na kufikiwa mapatano katika uwanja huo, kwa mara nyingine tena mmoja wa viongozi wa Marekani alisema hivi karibuni kwamba watachukua hatua ambayo itawapelekea wawekezaji wasithubutu kuwekeza nchini Iran! Huku akisisitiza kwamba matamshi kama hayo yanaonyesha wazi jinsi Marekani ilivyo na uadui mkubwa dhidi ya taifa la Iran, Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa moja ya malengo ya watu ambao katika kipindi hiki cha miaka miwili wamekuwa wakifanya mazungumzo ya nyuklia, na kwa hakika wamefanya juhudi kubwa, lilikuwa ni kuimarisha uchumi wa Iran kupitia uwekezaji wa kigeni lakini kwamba Wamarekani hivi sasa wanataka kulizuia jambo hilo pia. Kiongozi wa Mapinduzi amesema kuwa hiyo ndio maana ikawa inasemekana mara kwa mara kwamba Wamarekani sio watu wa kuaminika. Huku akiashiria upinzani wa wanasiasa wa Marekani dhidi ya kutumiwa nara ya 'Mauti kwa Marekani' katika maandamano,  Ayatullah Khamenei amehoji, 'wakati ambao nyinyi mnafanya hivi, na matendo yenu ya huko nyuma na ya sasa kuonyesha wazi kuwa mna uadui wa moja kwa moja, mnatarajia taifa la Iran likujibuni nini?' Ameongeza kwamba wao bila shaka katika mikutano ya faragha hutabasamu, kupeana mkono na kuongea vizuri ambapo tabia kama hizo zinahusiana na mikutano na mazungumzo ya kidiplomasia na ya faragha ambayo hayaathiri kwa vyovyote vile ukweli wa mambo. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa ukweli wa mambo ni kuwa baada ya mazungumzo ya muda mrefu, kutiwa saini mikataba na kumalizika mambo, hivi sasa wanasema hawataruhusu na kutishia waziwazi kuweka vikwazo vipya. Ayatullah Khamenei amesema: 'Huu ndio ukweli wa mambo kuhusu Marekani na haiwezekani kumfumbia macho adui huyu na kumdhania vizuri.' Amewahutubu wananchi kwa kusema: 'Taifa tukufu la Iran! Mnakabiliana na adui kama huyu. Kwa hivyo mnapasa kuwa macho na waangalifu.' Amesisitiza kuwa njia ya kutatua matatizo ya nchi ni wananchi kuwa na mwamko, kulindwa moyo wa imani katika jamii, kunufaika na vijana walio na azma ya juu na waumini, kuimarisha nchi kiimani, kiuchumi, kielimu na kupitia vyombo vya uongozi. Huku akisisitiza juu ya kulindwa umoja na mshikamano wa wananchi katika kulinda Mapinduzi misingi na malengo yake, Kiongozi wa Mapinduzi amesema: 'Viongozi ambao wanajali hatima ya nchi pia wanapasa kutekeleza majukumu yao kwa ajili ya kupata ridhaa ya Mwenyezi Mungu na kwa maslahi ya wananchi na kutegemea nguvu kazi na uwezo wa ndani ya nchi.'

Ikiwa uchumi wa taifa hautategemea vyanzo vya ndani, hatutafika popote

Huku akisisitiza kwamba uchumi ngangari hauna maana ya kuizingira nchi kwa uzio, Ayatullah Khamenei amesema kuwa uchumi ngangari unatokana na vyanzo vya ndani kuelekea nje kwa maana kwamba kama uchumi wa taifa hautategemea misingi ya ndani ya nchi basi hautafika popote. Amesema ushirikiano wa kiuchumi wa Iran na nchi za nje ni mzuri na kuongeza kuwa bila shaka ushirikiano huo unapasa kuwa mwerevu na ulio na lengo la kuimarisha uchumi wa ndani na kwamba bila shaka lengo hilo haliwezi kufikiwa bila kuwepo ukakamavu wa wananchi na harakati makini za viongozi.

Mwishoni Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: 'Kwa uwezo wake Mweyezi Mungu, vijana wa Iran watashuhudia siku ambayo Marekani na hata nchi kubwa kuliko Marekani pia hazitakuwa na uwezo wa kufanya lolote dhidi ya taifa la Iran.'

Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Mujtahid Shibstari, Mwakilishi wa Fakihi Mtawala katika Mkoa wa Azerbaijan Mashariki ambaye pia ni Imam wa Swala ya Ijumaa wa mjini Tabriz amezungumzia fahari ya kidini ya watu wa Azerbaijan katika vipindi nyeti tofauti vya historia ya Iran na kusisitiza kuwa mapambano ya tarehe 18 Februari, 1978 ya wananchi wa Tabriz ni nukta muhimu katika historia ya Mapinduzi makubwa ya Kiislamu na kwamba yanaoonyesha wazi mwamko wa watu wa Azerbaijan wanaotii utawala wa fakihi.

Imam wa Swala ya Ijumaa wa Tabriz amesema kuwa ushiriki mkubwa wa wananchi katika uchaguzi unathibitisha wazi nguvu ya kimaanawi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa watu walio na mwamko na uelewa wa Azerbaijan kama walivyo wananchi wenzao wa Iran, watashiriki kwa wingi na kwa kuwa macho katika uchaguzi huo uliopangwa kufanyika tarehe 26 ya mwezi huu wa Februari, na hivyo kwa mara nyingine tena kudhihirisha hamasa kubwa na ya kudumu ya taifa la Iran.

700 /