Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Maandamano makubwa ya wananchi tarehe 22 Bahman yatawavunja moyo maadui

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, leo asubuhi ameonana na makamanda na majimui ya maafisa wa Jeshi la Anga na wa kikosi maalumu cha ulinzi wa anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu na kuyataja maadhimisho ya Bahman 22 (ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu) na uchaguzi kuwa ni sikukuu mbili zenye maana pana kwa taifa la Iran. Amesisitiza wajibu wa kujitokeza kwa wingi wananchi na kwa njia ya kutoa pigo kwa adui katika maandamano ya kuadhimisha Bahman 22 (Februari 11) mwaka huu na kusema: Kujitokeza wananchi wote katika uchaguzi wa Machi 7 nako kuna maana ya kutia damu mpya, heshima na nguvu za kuipa kinga Iran na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na wakati huo huo kuvunja na kubatilisha malengo ya adui beberu mwenye hila nyingi.
Vilevile amewapongeza na kuwaenzi wananchi kwa kushiriki kwa wingi katika maadhimisho ya Bahman 22 kila mwaka na kuongeza kuwa: Kujitokeza kwa wingi wananchi katika maadhimisho ya Bahman 22 katika kipindi cha miaka 37 iliyopita, ni kujitokeza kwa udhati wa nyoyo zao kimwili na kiirada na kwa nia ya kweli na mapenzi makubwa kwa Mapinduzi ya Kiislamu na kwamba mwaka huu pia kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu wananchi watajitokeza kwa wingi katika maandamano ya kuadhimisha mapinduzi hayo matukufu; kujitokeza ambako kutatoa pigo kwa adui na kuwavunja moyo wale wote wanaolitakia mabaya taifa la Iran.
Ayatullah Khamenei amekutaja kufanyika maadhimisho ya Bahman 22 kuwa ni kurejea kwenye furaha za sikukuu ya Mapinduzi ya Kiislamu. Amesisitiza kuwa maadhimisho kama hayo ya wananchi hayana mfano wake duniani na kuongeza kuwa: Tangu awali ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hadi leo hii, wananchi wamekuwa wakijitokeza kwenye maadhimisho ya sikukuu hiyo katika hali zote, iwe ni kwa kuvumilia mazingira magumu ya hali ya hewa au wakiwa ndani ya matatizo, miaka yote wamekuwa wakishiriki kwa wingi kwenye sikukuu ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Bahman 22 (Februari 11).
Ameongeza kuwa: Sehemu kubwa ya watu ambao katika miaka ya hivi karibuni wanashiriki katika maandamano ya kuadhimisha Mapinduzi ya Kiislamu ukiangalia umri wao utaona kuwa hawakuwepo wakati wa ushindi wa mapinduzi hayo ya Bahman 22, 1357 (Februari 11, 1979) na kwamba silisila na mlolongo huu usio na kikomo unaonesha nguvu zinazoyafanya Mapinduzi haya kuwa hai daima.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, haipaswi kuruhusu kumbukumbu za tukio hili adhimu zisahauliwe na kuongeza kuwa: Ni lazima uhakika wa Mapinduzi ya Kiislamu ubakie hai muda wote katika akili za watu kwani Mapinnduzi ya Kiislamu ndio kwanza yako katikati ya njia na ili yaweze kuimarisha misingi yake na kufikia kwenye malengo yake matukufu yanahitajia kubakishwa hai katika malengo yake ya asili.
Ayatullah Khamenei amelitaja suala la kuunda jamii ya Kiislamu iliyo imara katika masuala ya elimu, uadilifu, maadili, heshima na maendeleo kuwa ndiyo malengo makuu ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kusisitiza kuwa: Lengo kuu la kambi ya adui ni kusahaulisha malengo hayo aali na matukufu na hatimaye iweze kubadilisha misimamo na mienendo ya watu ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Amesisitiza kuwa, lengo kuu la adui ni kubadilisha muundo na utambulisho wa Mapinduzi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Njama zote za kambi kubwa ya watu wanaoutakia mabaya mfumo wa Kiislamu zinalenga kwenye kuizuia Jamhuri ya Kiislamu isiendelee na harakati yake kuelekea kwenye malengo ambayo yatailetea Iran heshima na nguvu kubwa ili baada ya hapo kambi hiyo irejeshe ubeberu wa waistikbari nchini.
"Njama zote za kambi kubwa ya watu wanaoutakia mabaya mfumo wa Kiislamu zinalenga kwenye kuizuia Jamhuri ya Kiislamu isiendelee na harakati yake kuelekea kwenye malengo ambayo yatailetea Iran heshima na nguvu kubwa ili baada ya hapo kambi hiyo irejeshe ubeberu wa waistikbari nchini."
Ayatullah Khamenei amesema pia kuwa, ni jambo lililoko mbali kutokea vita vya kijeshi dhidi ya Iran kwa hivi sasa lakini hilo halina maana ya kwamba kutokea vita kama hivyo ni jambo lisilowezekana kabisa. Amesisitiza kuwa: Leo hii mpango mkubwa zaidi wa maadui katika kukabiliana na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ni kuendesha vita laini ili kuutoa mfumo wa Kiislamu na wananchi wa Iran kwenye mambo yote yanayolitia nguvu taifa hili.
Amesema, kushindwa taifa fulani kushikamana na masuala yanayolipa nguvu taifa hilo kuna maana ya kusalimu amri mbele ya adui na kuongeza kuwa: Kama taifa litakuwa dhaifu, basi kukabiliana na taifa hilo huwa hata hakuhitajii tena vita vya kijeshi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Njia pekee ya kuzuia hali hiyo ya kutisha, ni kuihifadhi na kuilinda fikra ya kimapinduzi kivitendo, kitabia na katika uchukuaji wa misimamo na kutunga kanuni na sheria.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kuzungumzia suala la uchaguzi na kusema kuwa, uchaguzi ni sawa na kupuliza roho, kutia damu mpya na kulipa taifa na nchi nafsi mpya na kuongeza kuwa: Kwa kutumia vizuri haki yao hiyo ya kimaumbile, wananchi hujitokeza kwenye medani katika nyakati maalumu ili kujiamulia wenyewe ni viongozi gani ambao waliwachagua huko nyuma ambao wamefanya kazi zao vizuri, hivyo waendelee kuwapa tena nafasi ya kuwatumikia.
Ameutaja uchaguzi kuwa ni kuhuisha nguvu za taifa na kutangaza upya utiifu kwa malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Wakati ninaposhikilia sana kwamba watu wote wajitokeze kwenye uchaguzi huwa nina maana ya kwamba, wakati watu wote wanaposhiriki kwenye uchaguzi, nchi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unapata heshima na kinga, hivyo kushiriki katika zoezi hili adhimu, ni faradhi kwa wananchi wote.
Ayatullah Khamenei amesema, miongoni mwa shabaha za daima za kambi ya adui inazoongozwa na Marekani ni kuzusha mpasuko na kuzua kambi mbili kidhabu, bandia na hatari sana kati ya wananchi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu. Amesisitiza kuwa: Kujitokeza vilivyo wananchi katika uchaguzi na kwa mara nyingine kudhihirisha wazi uhusiana na mfungamano wenye nguvu baina ya wananchi na mfumo wa Kiislamu kuna maana ya ushindi kwa Jamhuri ya Kiislamu na kushindwa malengo na shabaha hizo za adui na kwamba kushiriki namna hiyo wananchi katika uchaguzi bila ya shaka yoyote kutaambatana na kupata nusra na msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu - kwa mujibu wa ahadi ya kweli ya Mwenyezi Mungu.
Aidha amekumbushia silisila ya harakati na njama za kila aina za maadui tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ikiwa ni pamoja na mpango wa kuigawa vipande vipande Iran, kufanya mapinduzi ya kijeshi, vita vya miaka minane ilivyolazimishwa Iran kupigana na utawala wa wakati huo wa Iraq na vikwazo vya kila aina na vya kila leo na kusisitiza kuwa: Katika kukabiliana na njama zote hizo, wananchi wa Iran wamesimama imara kuusaidia mfumo wa Kiislamu na Mwenyezi Mungu Naye ameleta nusra Yake kiasi kwamba hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni nguvu ya kieneo na katika baadhi ya masuala nguvu za Jamhuri ya Kiislamu zimepenya na kuwa na taathira katika masuala ya kimataifa.
Akitoa muhtasari wa matamshi yake hadi kufikia hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewasisitizia wananchi akiwaambia: Heshima na fakhari na nguvu za nchi na taifa zimo kwenye kutekeleza vizuri majukumu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambapo kushiriki katika uchaguzi ni katika majukumu muhimu na makubwa zaidi.
Ayatullah Khamenei ameendelea na hotuba yake kuhusiana na uchaguzi kwa kugusia baadhi ya matamshi yasiyofaa yanayosikika siku hizi hapa na pale kwa lengo la kutia tashiwishi na wasiwasi katika nyoyo za watu na kuongeza kuwa: Matamshi hayo yanatolewa kwa malengo ya kisiasa tu na yako mbali na malengo ya kutafuta radhi za Mwenyezi Mungu ingawa hata hivyo hivi sasa sitaki nizungumzie matamshi hayo.
Vilevile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewakumbusha viongozi nchini Iran nukta kadhaa na miongoni mwa nukta muhimu zaidi ni kuacha kujishughulisha na masuala ya kipropaganda na ya kimagazeti. Ameongeza kuwa: Viongozi nchini Iran wanafanya kazi zao kwa msaada wa Mwenyezi Mungu lakini pia wanapaswa kuwa macho wasije wakashughulishwa na makelele ya kila leo ya kiuchaguzi na hivyo kughafilika na majukumu yao muhimu hususan masuala ya uchumi.
"Viongozi nchini Iran wanafanya kazi zao kwa msaada wa Mwenyezi Mungu lakini pia wanapaswa kuwa macho wasije wakashughulishwa na makelele ya kila leo ya kiuchaguzi na hivyo kughafilika na majukumu yao muhimu hususan masuala ya uchumi."
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, uchaguzi ni jambo muhimu mno lakini wakati huo huo amekumbusha kuwa: Pamoja na suala hilo kuwa na umuhimu mkubwa kiasi chote hicho, lakini ni jambo la kupita na kitu ambacho hubakia baada ya wiki chache za kufanyika uchaguzi, ni masuala ya kimsingi ya nchi kama vile kuimarisha misingi ya kiuchumi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia uwezo mkubwa wa nguvukazi iliyoelimika na yenye msukumo mkubwa ya Iran pamoja na sifa za kipekee za kijiografia na akiba na maliasili nyingi muhimu za Iran na kuwasisitizia viongozi nchini kwa kuwambia: Imarisheni uchumi wa nchi kwa kutegemea rasilimali hizo zisizo na mfano kwa namna ambayo itamfanya adui asifikirie kabisa kufanikisha malengo yake humu nchini kupitia kuliwekea taifa letu vikwazo vya kiuchumi.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Viongozi nchini wanapaswa kuuelekeza uwekezaji wa kiuchumi upande wa uzalishaji wa kilimo na wa viwandani, kuimarisha uzalishaji wa bidhaa za ndani na kuondoa tatizo la uzorotaji wa kiuchumi ili kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kwa njia hiyo kumfanya adui akiri kuwa vikwazo vya kiuchumi havina faida.
Ayatullah Khamenei amekumbushia matamshi yake aliyowambia viongozi nchini miaka kumi au 12 iliyopita kuhusiana na udharura wa kuuimarisha kwa ndani uchumi wa nchi na kuongeza kuwa: Kama lengo hilo litafikiwa, basi matatizo yote ya kiuchumi kama vile ukosefu wa kazi, ajira kwa vijana nakadhalika yatapata ufumbuzi mzuri unaotakiwa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema katika kuelezea nukta nyingine muhimu kwamba ni jambo la dharura kuzingatia kikamilifu na kwa wakati wote njama na malengo ya daima ya kambi kubwa na pana ya maadui na kusisitiza kwa kusema: Watu ambao wanaghafilika na kuwasahau maadui wao na kuwa na nyoyo na mtazamo mzuri kuhusiana na maadui hao, kamwe hawawezi kukubaliwa na kushukuriwa na wananchi.
Ameongeza kuwa: Utamuona adui anakuchekea, na wewe unamchekea lakini unapaswa kuwa macho na utambue vyema kuwa nyuma ya kicheko na tabasamu hilo kuna hila na njama zilizojificha.
Ayatullah Khamenei amesisitiza pia kuwa: Inabidi njama za adui katika masuala ya usalama, maisha ya watu, utamaduni, vijana na udhaifu uliomo katika masuala ya kijamii na mengineyo zitambuliwe vyema na kuwekwe sera na sheria madhubuti za kuweza kukabiliana na njama hizo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia matamshi ya mshairi bingwa na malenga wa Iran yaani Saadi Shirazi na kusema: Wakati adui anapoonesha silisila ya urafiki, basi husababisha uadui mkubwa katika nguo ya rafiki, uadui ambao hakuna adui yeyote anayeweza kuufanya.
Amekumbushia pia ujuba na uovu mkubwa wa adui na kuwataka viongozi nchini wawe waangalifu maradufu akisema kuwa: Wamarekani wanakwepa kujibu swali jepesi sana la fikra za walio wengi duniani kuhusiana na kwa nini wanaunga mkono jinai za kinyama zinazofanyika hivi sasa nchini Yemen na kwamba Wamarekani wanaendelea kijeuri na kijuba kuwaunga mkono watu ambao wanaendeleza ugaidi wa kikatili kabisa wa kiserikali wa kuua watu wasio na hatia huko Yemen.
Ayatullah Khamenei ameyataja madai ya Wamarekani ya kwamba wanatetea haki za binadamu na demokrasia kuwa ni istihzai na kichekesho kikubwa na kusisitiza kuwa: Wamarekani wanausaidia na kuuanga mkono kikamilifu utawala wa Kizayuni (wa Israel) ambao unaua kinyama watoto wadogo kama ambavyo wanawasaidia na kuwaunga mkono waitifaki wao katika eneo hili ambao hawatambui hata chembe kitu kinachoitwa uchaguzi, bali hawaelewi chochochote kuhusu uchaguzi!
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Timu inayotawala Marekani imejaa ujuba na jeuri kiasi kwamba inafanya mambo ya kinyama kabisa na baadaye inakuchekea, je hakuna wajibu wa kuwa macho na kuchukua tahadhari kubwa sana mbele ya adui kama huyu?
Ayatullah Khamenei ametoa muhtasari wa maneno yake hadi kufikia hapo kwa kusisitiza kwamba: Wananchi wa Iran wamekuwa macho wakati wote mbele ya adui kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na hadi hivi sasa wako macho na kwamba hadi leo hii harakati adhimu ya taifa la Iran imefanikiwa kufelisha na kuzishinda njama zote za adui huyo beberu na mwenye hila nyingi, na katika siku za usoni pia litaendelea kumshinda adui huyo.
"Wananchi wa Iran wamekuwa macho wakati wote mbele ya adui kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na hadi hivi sasa wako macho na kwamba hadi leo hii harakati adhimu ya taifa la Iran imefanikiwa kufelisha na kuzishinda njama zote za adui huyo beberu na mwenye hila nyingi, na katika siku za usoni pia litaendelea kumshinda adui huyo."
Mwanzoni mwa hotuba yake Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameitaja hatua ya Jeshi la Anga ya kutangaza utiifu wake kwa Imam Khomeini (quddisa sirruh) tarehe 19 Bahman 1357 (mwaka wa Kiirani wa Hijria Shamsia inayosadifiana na Februari 8, 1979) kuwa ni tukio muhimu na lililokuwa na taathira kubwa na ilikuwa ni nyota yenye kuangaza njia katika historia ya Mapinduzi ya Kiislamu. Ameongeza kuwa: Hatua iliyochukuliwa na Jeshi la Anga tarehe 19 Bahman ya kujiunga na wananchi ilibadilisha milingano iliyokuwepo nchini na harakati hiyo ilipata haraka majibu mazuri kutoka kwa wananchi na hili linathibitisha kwamba unapokuwa pamoja (na wananchi), wananchi nao wanakuwa pamoja na wewe.
Vilevile Ayatullah Khamenei amezitaja kazi zilizofanywa na Kikosi cha Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi chote hiki cha miaka 37 iliyopita, kuwa kwa hakika ni kazi nzuri sana na kuongeza kwamba: Leo hii Kikosi cha Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ni majimui imara, yenye nguvu, bunifu na iliyo pamoja na wananchi na kuna wajibu wa kuimarishwa zaidi nguvu na uwezo na uhusiano baina ya kikosi hicho na wananchi kadiri siku zinavyosonga mbele.
Mwanzoni mwa mkutano huo, Brigedia Jenerali, rubani Shah Safi, kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kuienzi tarehe 19 Bahman (Februari 8) ambayo ni Siku ya Jeshi la Anga nchini Iran, amegusia kazi za jeshi hilo katika masuala mbali mbali ya kiulinzi, kielimu na kiutamaduni na kusisitiza kuwa: Kikosi cha Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kinaelewa vizuri mabadiliko mapya yanayotokea katika eneo hili na kinafuatilia kwa karibu, kwa nguvu na kwa msukukumo mkubwa sana matukio yote yanayojiri katika eneo hili na kufanya juhudi za kufanikisha vilivyo malengo yanayowasilishwa kwake ndani ya fremu ya mikakati na stratijia za kiulinzi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

 

700 /