Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu katika mazungumzo yake na Rais wa Azerbaijan:

Kueneza maarifa ya Kiislamu kutaimarisha msaada wa wananchi kwa serikali ya Azerbaijan

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alasiri ya leo amefanya mazungumzo na Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan ofisi kwake hapa mjini Tehran. Ayatullah Khamenei ameashiria uhusiano mzuri wa kisiasa na masuala mengi yanayozikutanisha pamoja Iran na Azerbaijan hususan masuala ya kidini na kimadhehebu ya mataifa hayo mawili na kusema: Kueneza maarifa ya Kiislamu na kuheshimu madhihirisho na nembo za kidini ni sababu ya msaada wa wananchi dhidi ya vitisho vya adui.
Katika mazungumzo hayo Ayatullah Khamenei amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inawaona watu wa Azerbaijan kuwa ni ndugu, jambo ambalo ni juu zaidi ya urafiki na ujirani na kuongeza kuwa: Ni muhimu sana kwa Iran kuona watu wa Azerbaijan wakiwa na uthabiti wa kisiasa, usalama, amani na hali bora, na licha ya kuwepo maelewano ya kiroho kati ya mataifa hayo mawili, lakini pia kuna udharura wa kuzidishwa mabadilishano ya kiuchumi na ushirikiano katika nyanja mbalimbli.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu: “Licha ya kuwepo maelewano ya kiroho kati ya mataifa haya mawili, lakini pia kuna udharura wa kuzidishwa mabadilishano ya kiuchumi na ushirikiano katika nyanja mbalimbli”.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria masuala ya kidini yanayowakutanisha pamoja wananchi wa Iran na wale wa Azerbaijan na kusisitiza kuwa: Itikadi za Kiislamu na Kishia za watu wa Azerbaijan ni rasilimali yenye thamani kubwa na kadiri serikali itakavyoheshimu na kukaribisha zaidi dhihirisho na itikadi za kidini za wananchi ndivyo uungaji mkono wa wananchi kwa serikali na mapambano yao dhidi ya uadui wa baadhi ya madola ya kibeberu utakavyoongezeka.  
Amesema kuwa, sharti la kuweza kukabiliana na fitina za makundi ya kitakfiri kati ya mataifa mbalimbali ni kuimarisha shughuli za Kiislamu. Ameongeza kuwa: Eneo al Azerbaijan lina historia ya miaka mingi ya kidini na ni chimbuko la baadhi ya maulama wakubwa wa Kiislamu, na wananchi wa Azerbaijan ni watu wenye uelewa na makini; hivyo vihamasishi na misaada ya serikali katika shughuli za kidini itakuwa na taathira katika kuvutia upendo na hisia zao.  
Ayatullah Khamenei ameunga mkono matamshi ya Rais wa Azerbaijan aliyesema kuwa, chanzo cha aghlabu ya vitisho vinavyozikabili nchi mbili hizi ni kimoja na kuongeza kuwa: Kueneza maarifa ya Kiislamu na ya Kishia kutakuwa sababu ya msaada wa Mwenyezi Mungu na vilevile dua za Maimamu watoharifu (as) katika kukabiliana na matatizo na vitisho vya aina mbalimbali.
Katika mazungumzo hayo ambayo pia yamehudhuriwa na Rais Hassan Rouhani, Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan ameashiria uhusiano wa karibu uliopo kati ya Tehran na Baku na kusema kuwa, mazungumzo yake nchini Iran yana umuhimu sana. Ameongeza kuwa, utamaduni, dini na historia ya pamoja vimejenga mfungamano mkubwa sana kati ya Iran na Azerbaijan.
Vilevile ameashiria suala la kutiwa saini hati 10 za ushirikiano kati ya Tehran na Baku na kusisitiza kuwa, uhusiano wa pande mbili ni wa kirafiki na mzuri sana. Ameongeza kuwa, kumepigwa hatua nzuri katika nyanja za ushirikiano wa kibiashara, usafirishaji, nishati na viwanda na kunafanyika jitihada zaidi za kuzidisha umoja na uhusiano wa nchi mbili hizo.
Rais wa Azerbaijan amesema kuwa, Tehran na Baku zina mitazamo inayofanana kuhusu masuala ya kimataifa na kuongeza kuwa: Iran ina nafasi muhimu sana katika uwanja wa kuimarisha amani na usalama duniani na kwamba anautambua usalama wa Iran kuwa ni usalama wa Azerbaijan.
Bwana Ilham Aliyev amesema kuwa, vitisho vinavyozikabili nchi hizo mbili vinatokana na chanzo kimoja na kuongeza kuwa, katika safari hii ya Tehran kumefikiwa mapatano ya kushirikiana na Iran katika mapambano dhidi ya ugaidi kwa shabaha ya kurejesha amani na utulivu kwenye eneo hili.
Amesisitiza udharura wa kuheshimiwa thamani na matukufu ya kidini na kugusia huduma za kidini zinazotolewa na serikali ya Azerbaijan. Amesema kuwa, katika kipindi cha baada ya kujitawala Azerbaijan kumejengwa misikiti elfu mbili nchini humo na kwamba nusu ya misikiti hiyo imejengwa katika kipindi cha uongozi wake.
Rais wa Azerbaijan melaani harakati zilizodhidi ya Uislamu na kusema kuwa sababu ya uadui unaofanywa dhidi ya nchi hiyo ni itikadi za kidini za watu wake. Ameongeza kuwa: Uislamu na Ushia vinapendwa na watu wa Azerbaijan na kwamba kuwepo kwa shakhsia mkubwa kama Ayatullah Khamenei katika eneo hili kunawapatia nguvu na nishati kubwa.
Rais wa Azerbaijan: “Kuwepo kwa shakhsia mkubwa kama Ayatullah Khamenei katika eneo hili kunatupatia nguvu na nishati kubwa.”
 

700 /