Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Madai ya kuwepo bunge la serikali na bunge dhidi ya serikali ni urongo mtupu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo (Jumatano) ametoa hotuba muhimu katika hadhara kubwa ya wananchi wa Najafabad akitoa maelezo ya kina kuhusu msamiati wa "misimamo ya kati na misimamo mikali" na kuwataka wananchi wote hususan viongozi na wanasiasa kuwa macho mbele ya njama za adui za kutaka kuzusha kambi mbili bandia na za kutwisha katika nga ya sasa ya uchaguzi. Amesema kuwa uchaguzi ni medani ya kutunisha kifua kitaifa, kuonesha uaminifu, kusimama kidete kwa taifa na kulinda heshima na kujitawala. Amesisitiza kuwa, watu wote wanaoitakia izza na heshima Iran ya Kiislamu wanapaswa kushiriki katika uchaguzi wa Ijumaa ijayo hapa nchini na kwamba tarehe 7 Esfand (26 Februari) dunia itaona jinsi wananchi wa Iran watakavyohudhuria kwa wingi na kwa hamu kubwa kwenye masanduku ya kupigia kura.
“Watu wote wanaoitakia izza na heshima Iran ya Kiislamu wanapaswa kushiriki katika uchaguzi wa Ijumaa ijayo”.
Sambamba na kutoa mkono wa pole kwa mnasaba wa kukumbuka siku ya kufa shahidi Bibi Fatima al Zahra (as), Ayatullah Ali Khamenei ameashiria chaguzi mbili muhimu sana za Bunge na Baraza la Watalamu zitakazofanyika siku ya Ijumaa na kusema: Umuhimu wa uchaguzi nchini si kupiga kura pekee bali uchaguzi una maana ya kutunisha kifua na misuli kwa taifa la Iran mbele ya adui baada ya aina mbalimbali za mashinikizo, vikwazo vya kidhalimu na propaganda chafu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Amesema kuwa mahudhurio makubwa ya wananchi katika zoezi la uchaguzi yatazidisha haiba na adhama ya Mapinduzi ya Kiislamu kote duniani na kuongeza kuwa, mbali na kuonesha nguvu, azma na kusimama kidete, uchaguzi pia unadhihirisha uaminifu, ushujaa na ukakamavu wa taifa kubwa katika medani ya kupambana na malengo mabaya.
Baada ya kuzungumzia umuhimu wa mahudhurio makubwa ya wananchi waliokamilisha masharti ya kupiga kura katika uchaguzi, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria njama mbalimbali zilizofanywa na maadui wakati wa chaguzi mbalimbali hapa nchini kwa kipindi cha miaka 37 iliyopita na kusema: Kutuhumu chaguzi zinazofanyika nchini Iran kuwa ni za uongo, njama za kufifiza na kutaka kupunguza idadi ya wananchi wanaoshiriki katika chaguzi hizo na kuwaambia watu kuwa kushiriki kwao katika chaguzi hizo hakuna faida kwa madai kwamba matokeo yake yanajulika tangu hapo awali ni miongoni mwa propaganda chafu za watu waovu kwa ajili ya kuwazuia wananchi kushiriki katika chaguzi mbalimbali katika miaka iliyopita, na hata katika baadhi ya vipindi maafisa wa serikali ya Marekani walieleza waziwazi misimamo yao ya kupinga chaguzi za Iran.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kutokana na tajiriba yao, Wamarekani wameelewa kwamba, misimamo yao ya wazi itakuwa na matokeo yanayokwenda kinyume na malengo yao, kwa msingi huo katika uchaguzi wa sasa wameamua kunyamaza kimya lakini vibaraka na mamluki wao wanatekeleza njama mpya kwa kutumia mbinu za aina mbalimbali.
Akitoa ufafanuzi kuhusu njama hizo mpya, Ayatullah Khamenei amesema kuwa, wanaolitakia mabaya taifa la Iran wameelekeza juhudi zao katika kuzusha kambi mbili bandia katika uchaguzi wa sasa ili kueneza uvumi wa kuwepo mgawanyiko baina ya wananchi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kuwa hakika ya uchaguzi, kama yalivyo mashindano mengine, ni vuguvugu, kushinda na kushindwa na kuongeza kuwa, kushinda au kushindwa huko katika uchaguzi hakuna maana ya kugawanyika taifa katika kambi mbili, kuwepo mgawanyiko katika jamii na kuwepo uadui kati ya wananchi. Amesisitiza kuwa madai ya kuwepo kambi mbili nchini Iran ni uongo mtupu.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, kambi mbili halisi nchini Iran ni kambi ya watu waaminifu kwa Mapinduzi ya Kiislamu na misingi ya Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) na kambi ya ubeberu na waitifaki wake. Ameongeza kuwa katika suala hilo taifa zima la Iran ni wanamapinduzi, waungaji mkono wa Mapinduzi na waaminifu kwa Imam Khomeini, fikra na misingi yake. Amesema chanzo kikuu cha madai hayo ya kutengeneza kambi mbili bandia hapa nchini kiko nje ya nchi lakini inasikitisha kuona kwamba, wakati mwingine madai hayo yanakaririwa ndani ya nchi.  
“Kambi mbili halisi nchini Iran ni kambi ya watu waaminifu kwa Mapinduzi ya Kiislamu na misingi ya Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) na kambi ya ubeberu na waitifaki wake”.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema madai ya kuwepo kambi mbili za "bunge la serikali" na "bunge dhidi ya serikali" ni miongoni mwa kambi mbili bandia na za uongo zinazopigiwa debe katika anga ya sasa ya uchaguzi hapa nchini. Amesema kuwa waliobuni madai hayo wanafanya jitihada za kueneza propaganda kwamba, sehemu moja ya wananchi wa Iran inaunga mkono bunge la serikali na sehemu nyingine inapinga bunge la serikali, ilhali taifa la Iran halitaki bunge la serikali wala bunge lililo dhidi ya serikali.
Ayatullah Khamenei amesema taifa la Iran linataka bunge linaloshikamana na dini, lenye kuwajibika, shujaa, lisilohadaika, ngangari katika kukabiliana na tamaa na tabia ya kutaka kujitanua ya ubeberu, linalolinda heshima na kujitawala kwa taifa, linalotaka maendeleo halisi ya nchi, lenye imani na harakati ya kielimu ya vipawa vya vijana, lenye imani na uchumi unaotegemea uzalishaji wa ndani ya nchi, linalojua vyema mashaka na matatizo ya wananchi, lenye azma ya kutatua matatizo hayo, lisilotishika mbele ya Marekani na linalotekeleza vyema majukumu yake ya kisheria.
Ameongeza kuwa wananchi wote wa Iran wanataka bunge kama hilo na wala si bunge linalomuunga mkono fulani au fulani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia mipango ya Marekani kwa ajili ya kipindi cha baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia (kati ya Iran na kundi la 5+1) na kusema: Baada ya makubaliano hayo Wamarekani walikuwa na mpango kwa ajili ya Iran na mpango mwingine kwa ajili ya eneo la Mashariki ya Kati na wangali wanafuatilia mipango hiyo kwa sababu wanajua vyema ni nchi gani inayosimama imara kukabiliana na malengo yao machafu katika eneo hili.
Ayatullah Khamenei amesema, Wamarekani wanatumia vibaraka katika kutekeleza mipango yao nchini Iran na kuongeza kuwa: Tangu kulipozungumziwa suala la vibaraka na udharura wa kuwa makini mkabala wa vibaraka hao, baadhi ya watu ndani ya nchi walipatwa na fadhaa wakisema kwa nini daima kunazungumziwa suala la vibaraka; hata hivyo fadhaa hiyo haikuwa mahala pale. Amesisitiza kuwa, suala la kuwapo watu vibaraka ni hakika na kweli lakini wakati mwingine kibaraka mwenyewe huwa hajui na kuelewa njia aliyongia ndani yake.   
 Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria matamshi ya Imam mwenye mwamko na tajiriba na kusema kuwa, baadhi ya wakati maneno ya adui husikika kupitia watu wenye nafasi za juu katika jamii na kuongeza kuwa, watu kama hao huenda wasiwe wamechukua pesa au kutoa ahadi kwa adui lakini bila kutambua, huenda wakawa wanakariri maneno ya adui na hivyo kuanda uwanja wa kupenya adui kwa njia moja au nyingine. Ayatullah Khamenei ameashiria aina tofauti ya wapenyaji ambao hata baadhi yao mara nyingine huwa hawajitambui na kusema, katika miaka ya hivi karibuni, mbunge mmoja alikariri maneno ya adui na kuutuhumu mfumo wa Kiislamu kuwa unasema uongo.
Kiongozi wa Mapiduzi ya Kiislamu ameashiria mfano mwingine na kuongeza: 'Katika kipindi ambacho ujumbe wa mazungumzo ya nyuklia wa nchi yetu ulikuwa unajishughulisha na mazungumzo magumu  na kwa hakika kupambana na upande wa pili, na rais wa hivi sasa wakati huo ndiye aliyekuwa mkuu wa ujumbe huo, baadhi ya wabunge waliwasilisha muswada wa dharura bungeni, ambao ulikuwa ukiunga mkono madai ya upande wa pili katika mazungumzo, na rais wa hivi sasa wa nchi alilalamikia muswada huo kwa hoja kuwa ulikuwa ukihudumia maslahi ya adui. Kiongozi wa Mapinduzi amewataka viongozi na wanasiasa wote kuwa macho mbele ya upenyaji wa maadui na kuongeza kuwa, sharti la kuwa macho huko ni kuwa, pale adui anapotaka kuwagawanya watu katika makundi kupitia njia ya kusifu kundi au watu fulani, wananchi wanapasa kuchukua msimamo na kuonyesha kuchikizwa kwao na adui huyo bila kusita.
"Chukueni msimamo na kudhihirisha kuchukizwa kwenu na kusifiwa na adui."
Ayatullah Khamenei amekumbusha maneno ya Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) aliyesema kwamba: 'Adui anapokusifuni, mnapasa kutilia shaka mienendo na kazi zenu' na kuongeza kuwa, maneno hayo ya Imam ni 'desturi na mwongozo wa utendaji kazi wa Mapinduzi.' Kwa msingi huo msimamo wa haraka unapasa kuchukuliwa dhidi ya kusifiwa na wageni na kutoghafilika na suala hilo. Amesisitiza kwamba sharti la kuendeshwa vyema nchi kubwa kama hii na kushughulikia masuala ya wananchi watukufu na shupavu kama hawa, ni kuwa na mwamko, kuwa macho na kuwa na azma thabiti mkabala wa adui.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewanasihi viongozi na wanasiasa kujiepusha na fasihi ya kisiasa ya adui kama vile kutumia maneno ya 'misimamo mikali,' na 'misimamo ya wastani' na kuongeza kuwa, tokea mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu watu walio na nia mbaya dhidi ya Mfumo wa Kiislamu wamekuwa wakitumia maneno hayo na makusudio yao ya 'misimamo mikali' ni watu wanaofungamana na kushikama zaidi na Mapinduizi ya Kiislamu, fikra na misingi ya Imam Khomeini (MA), na wanatumia neno 'misimamo ya wastani' wakikusudia watu wanaosalimu amri na kupatana na wageni.
Ayatullah Khamenei amesema: 'Watu wanaotumia maneno hayo ndani ya nchi wanapasa kutalii kwa kina maarifa ya Kiislamu kwa sababu hakuna mgao kama huo katika Uislamu na 'wastani' na 'kati kwa kati' ni maneno yaliyo na maana ya 'njia nyoofu.' Kwa msingi huo hakuna 'msimamo mkali' mkabala na 'njia ya wastani' isipokuwa waliopotoka na kuacha njia iliyonyooka. Ameongeza kuwa, kwenye njia nyoofu kuna uwezekano wa baadhi ya watu kwenda kwa kasi na wengine kwenda taratibu, jambo ambalo halina kasoro yoyote.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa katika fasihi ya kisiasa ya wageni, Daesh pia wanaitwa kuwa watu walio na misimamo mikali, katika hali ambayo Daesh wametoka kwenye njia ya Uislamu, Qur'ani na njia nyoofu.
Katika kufupisha maneno yake kuhusiana na maudhui hii, Ayatullah Khamenei amesema kuwa, watu wanaotumia maneno ya msimamo mkali nje ya mipaka ya nchi hii makusudio yao ni watu waaminifu kwa Mapinduzi na ambao ni Hizbullah. Kwa msingi huo ndani ya nchi tahadhari inapasa kuchukuliwa ili kusitimizwe malengo ya adui kwa kukariri maneno hayo.
“Makusudio yao wanapotumia neno 'misimamo mikali' ni watu wanaofungamana na kushikama zaidi na Mapinduizi ya Kiislamu, fikra na misingi ya Imam Khomeini (MA)”.
Huku akiashiria kukiri Marekani kwamba nchini Iran hakuna watu wenye misimamo ya wastani, Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa taifa zima la Iran linaunga mkono Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza juu ya kudumishwa mapinduzi hayo. Amesema, baadhi ya wakati makosa na mtelezo hutokea lakini hakuna Muirani yoyote anayetaka kuwaunga mkono au kuwa tegemezi kwa wageni hao.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria umuhimu wa jinsi ya kuchagua na kuwahutubu wananchi kwa kusema: 'Matokeo ya aina yoyote ya kuchagua kwenu sawa yawe mazuri au mabaya yatawarejea nyinyi wenyewe; hivyo juhudi zifanyike ili kupata chaguo zuri.'
Ayatullah Khamenei amesema kuridhia au kutoridhia Mwenyezi Mungu Mtukufu ni matokeo mengine ya jinsi ya kufanya uchaguzi na kuongeza kuwa, juhudi zifanyike ili uchaguzi ufanyika kwa makini, muono wa mbali na kwa utambuzi mzuri.
Amesisitiza kwamba katika kuwachagua wabunge na wanachama wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi wa Mfumo wa Kiislamu, juhudi zinapasa kufanyika ili kuwachagua watu walio na imani ya dini, waaminifu na watiifu kwa Mapinduzi ya Kiislamu, wenye misimamo imara katika njia ya Mapinduzi, wasioogopa adui, walio na azma thabiti na mashujaa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Kama hamuwajui vyema baadhi ya watu (wagombea) msiseme kuwa hamtapiga kura, bali mnapasa kushauriana na watu mnaojua vyema viwango vya kushikamana kwao na dini, uaminifu na mwamko wao ili kufanya uchaguzi sahihi.
“Ili kufanya uchaguzi sahihi, shaurianeni na watu mnaojua vyema viwango vya kushikamana kwao na dini, uaminifu wao na mwako wao”.  
Huku akisisitiza kuwa kwenye njia hii malengo, wajibu na majukumu vinaeleweka vyema, Ayatullah Khamenei ameseme: "Iwapo kazi hii muhimu itatekelezwa kwa njia inayofaa, bila shaka Mwenyezi Mungu atasaidia na bila kujali matokeo ya uchaguzi, matokeo hayo yatakuwa na manufaa kwa taifa. Amesema: "Tuna imani kubwa kwamba licha ya kuwepo juhudi za watu walio na nia mbaya, lakini Mwenyezi Mungu amelikadaria taifa la Iran ushindi wa mwisho na kwa uwezo wake adui hatafanikiwa kutoa pigo dhidi ya Mapinduzi na Mfumo wa Kiislamu.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesifu imani, ukweli, utiifu na msimamo imara wa watu wa Najafabad katika njia ya Mapinduzi ya Kiislamu na kusema: "Katika kipindi cha mapambano ya Kiislamu watu wa Najafabad walionyesha msisimuko, hamasa na uelewa wa hali ya juu katika kuunga mkono mapambano na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia, na katika vipindi tofauti hasa katika kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu, kwa mara nyingine tena, walionyesha kupevuka, ushujaa, msimamo thabiti na ustahiki wao.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Hasanati, Imam wa Swala ya Ijumaa ya Najafabad aliashiria ushujaa na hamasa ya watu wanaolea mashahidi wa mji huo katika kipindi cha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na vita vya kujitetea kutakatifu ambapo walitoa zaidi ya mashahidi 2,500 na kusema: "Watu waaminifu wa Najafabad wanasisitiza juu ya kuheshimu ahadi na agano waliloahidiana na Uislamu, Qur'ani Tukufu, Imam Khomeini (MA) na Kiongozi mwenye busara wa Mapinduzi na wataendelea kuheshimu ahadi hiyo hadi tone la mwisho la damu yao."

 

700 /