Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu mapema leo akipiga kura:

Wananchi wote washiriki kwenye uchaguzi ili kuzidisha hadhi ya taifa na kuwavunja moyo maadui

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei mapema leo na katika dakika za kwanza kabisa za kuanza chaguzi za Bunge la 10 na Baraza la 5 la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi wa Juu wa Iran, amehudhuria katika kituo nambari 110 cha kupigia kura katika Husainiya ya Imam Khomeini mjini Tehran na kutumbukiza kura zake katika masanduku ya kura.

Baada ya kupiga kura, Ayatullah Ali Khamenei ametoa hotuba fupi akiutaja uchaguzi kuwa ni wajibu na wakati huo huo haki ya taifa. Ameongeza kuwa, uchaguzi ni kazi kubwa, ya kheri na yenye umuhimu mkubwa na katika baadhi ya nyakati yenye umuhimu mara dufu. Amesema, katika mafundisho ya Uislamu kumeusiwa kutenda kazi na amali njema mapema na kwa haraka.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza udharura wa kutekeleza wajibu huo haraka na kuongeza kuwa: "Kama tulivyosema hapo awali, kila mtu anayeipenda Iran, Jamhuri ya Kiislamu, izza, heshima na adhama ya taita la Iran anapaswa kushiriki katika uchaguzi huu".

Vilevile amewataka wananchi kushiriki katika uchaguzi wa leo kwa nia ya kheri na kwa lengo la kuzidisha hadhi na kujitawala kikamilifu kwa nchi hii na kusema: "Matunda ya kushiriki kwenye zoezi hili ni heshima na kujitawala kwa taifa, na sisi tuna maadui waliokodoa macho ya tamaa; hivyo uchaguzi huu unapaswa kufanyika kwa njia itakayomkatisha tamaa adui na kumvunja moyo".  

"Uchaguzi huu unapaswa kufanyika kwa njia itakayomkatisha tamaa adui na kumvunja moyo".

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameeleza matumaini kwamba, wananchi wa Iran watapata taufiki ya kushiriki kwa wingi katika uchaguzi wa leo kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita, na kuwa sababu ya maendeleo na heshima ya nchi hii.  

  

700 /