Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Wananchi wametimiza wajibu wao ipasavyo katika uchaguzi, sasa ni zamu ya viongozi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo asubuhi (Alkhamisi) alikuwa na kikao cha mwisho na mkuu na wajumbe wa Baraza la Nne la Wanavyuoni Wataalamu linalomchagua na kusimamia kazi za Kiongozi Mku wa Iran.  Katika mkutano huo Ayatullah Khameni ametoa hotuba muhimu sana akiwashukuru wananchi wa Iran kwa kujitokeza kwa wingi na kwa sura yenye maana maalumu katika uchaguzi wa Februari 26 na kutangaza utiifu na mapenzi yao kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, na amebainisha sifa kadhaa maalumu za uchaguzi huo na majukumu muhimu zaidi pamoja na vipaumbele vya Baraza la Wanavyuoni Wataalamu na wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) katika duru hii mpya. Ametaja vipaumbele vitatu vikuu vya hivi sasa na kusema kuwa suala la kujipenyeza maadui linapaswa kuangaliwa kwa uzito mkubwa zaidi na kusisitiza kuwa: Njia pekee ya kufikia kwenye maendeleo ya kweli ni “kuimarisha muundo wa ndani ya nchi katika nyuga za kiuchumi, kiutamaduni na kisiasa”, “kulindwa sifa maalumu za Mapinduzi ya Kiislamu”, “kufanya harakati kijihadi”, “kulinda heshima na utambulisho wa kitaifa na Kiislamu” na “kutoruhusu kumezwa na kumeng'enywa katika mmeng'enyo hatari wa duniani sasa”.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja uchaguzi wa Februari 26 kuwa ulikuwa na maana pana kutokana na kushiriki watu milioni 34 katika uchaguzi huo na kutumbukizwa karibu kura milioni sabini katika mashanduku ya kupigia kura na kuongeza kuwa: Kwa hakika wananchi wa Iran waling'ara sana kwenye uchaguzi huo na kwamba kushiriki asilimia 62 ya watu waliotimiza masharti ya kupiga kura, ni kiwango cha juu sana ikilinganishwa na nchi nyingi duniani hata Marekani. 
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Kwa kushiriki kwao kwa kiwango kikubwa kiasi hicho, kwa hakika wananchi wa Iran wamethibitisha kivitendo imani yao kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Amesema kuchaguliwa au kutochaguliwa baadhi ya wagombea katika chaguzi tofauti ni jambo la kawaida.  Amewashukuru wajumbe wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu ambao hawakufanikiwa kuingia katika duru ya hivi sasa ya baraza hilo  na kusema: Tab'an wako baadhi ya watu wakubwa ambao kupigiwa kura au kutopigiwa kura kwao katika uchaguzi huo hakupunguzi chochote kwenye hadhi  na shakhsia yao na mabwana Yazdi na Misbah ni miongoni mwa watu hao ambao kuwepo kwao kwenye baraza hilo kunaongeza uzito wake na kutokuwemo kwao katika baraza hilo ni hasara.
“kuwepo kwao kwenye baraza hilo kunaongeza uzito wake na kutokuwemo kwao katika baraza hilo ni hasara”
Baada ya hapo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameanza kutaja sifa maalumu za uchaguzi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu hususan uchaguzi wa Februari 26 na kusema kuwa: Uhuru kamili wa wananchi kwa ajili ya kushiriki katika uchaguzi ni miongoni mwa sifa za kipekee za uchaguzi katika mfumo wa Kiislamu, kwa sababu kushiriki katika uchaguzi kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Kiislamu si jambo la kulazimishwa na kwamba wananchi wanashiriki kwenye chaguzi zote kwa mapenzi yao na kwa ari na fikra zao.
Ayatullah Khamenei amelitaja suala la mchuano mkali unaokuwemo kwenye uchaguzi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni sifa nyingine maalumu ya uchaguzi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kuwa: Uchaguzi wa Februari 26 ulikuwa na ushindani mkali kwani mirengo na watu tofauti walishiriki wakiwa na kaulimbiu na anwani tofauti katika uchaguzi huo huku Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB) nalo likitoa nafasi sawa kwa wagombea wote na kila mmoja alifanya juhudi zake kubwa kujitangaza kwa wananchi kwa maana halisi ya neno.
Vilevile amelitaja suala la kufanyika kwa utulivu na usalama kamili uchaguzi huo kuwa ni sifa nyingine kubwa ya uchaguzi wa Februari 26 wa nchini Iran na kuongeza kuwa: “Katika hali ambayo kwenye nchi zinazopakana nasi watu wanaishi katika mazingira ya ukosefu wa amani na vitendo vingi vya kigaidi, uchaguzi huo adhimu na ulioshirikisha idadi kubwa ya watu umefanyika hama nchini bila ya kuweko tukio lolote chungu kwa kadiri kwamba katika mji wa Tehran kuanzia saa mbili asubuhi hadi katikati ya usiku watu waliendelea kupiga kura kwenye vituo vya kupigia kura kwa usalama na utulivu kamili. 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameshukuru juhudi na hatua zilizochukuliwa na jeshi la polisi pamoja na Wizara ya Usalama wa Taifa, Wizara ya Mambo ya Ndani, Jeshi la Sepah na Basiji kwa ajili ya kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unafanyika kwa ufanisi na kwa hatua zao nzuri za kulinda usalama na kuandaa mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi huo na kusema kuwa, moja kati ya sifa maalumu za uchaguzi huo ni kufanyika kwake kwa amani na uaminifu. Ameongeza kuwa: Tofauti na propaganda za maadui na pia madai ya baadhi ya watu ndani ya nchi, uchaguzi katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima ni salama na haijawahi kutokea hata mara moja kufanyika harakati ya kitaasisi ya kuathiri na kutia mkono matokeo ya chaguzi hizo. 
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: Uchaguzi wa Februari 26 umethibitisha tena uongo na kutokuwa sahihi mameno ya watu ambao mwaka 1388 Hijria Shamsia (mwaka 2009) walidai kuwa uchaguzi haukuwa salama kusababisha fitina yenye madhara kwa nchi. 
Ameongeza kuwa: Kama ambavyo uchaguzi uliopita ulikuwa salama kikamilifu, chaguzi za vipindi vya huko nyuma zikiwemo chaguzi za miaka ya 2009 na 2006 nazo zote zilikuwa salama na za haki.
“Uchaguzi wa Februari 26 umethibitisha tena uongo na kutokuwa sahihi mameno ya watu ambao mwaka 1388 Hijria Shamsia (mwaka 2009) walidai kuwa uchaguzi haukuwa salama kusababisha fitina yenye madhara kwa nchi”. 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, hatua ya kiungwana kabisa ya wagombea ambao hawakupata ushindi kwenye uchaguzi wa mara hii, ni sifa nyingine ya kipekee ya uchaguzi wa Februari 26 na kuongeza kuwa: Tofauti na vitendo visivyo vya kiungwana vya watu walioshindwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2009 ambao walikataa kukukubali kushindwa na wakazusha fitina iliyoisababishia hasara kubwa nchi na kumtia tamaa adui, watu ambao hawakupata ushindi katika uchaguzi wa mara hii wameonesha uungwana mkubwa kiasi kwamba wamewapongeza wenzao waliochaguliwa na wananchi na jambo hilo kwa kweli ni adhimu na ni lenye thamani kubwa.
Ayatullah Khamenei ametoa muhtasari wa maelezo yake kufikia hapo akisema: Kitendo cha wananchi cha kutangaza imani yao kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kimefanyika kupitia uchaguzi huo wa Februari 26 katika hali ambayo katika upande wa pili adui alikuwa anafanya njama za kuzusha kambi mbili baina ya wananchi na mfumo wao wa utawala na pia kujaribu kuupotezea itibari uchaguzi huo ni jambo muhimu na lenye thamani kubwa.
Amezungumzia pia mashambulizi ya miezi ya hivi karibu dhidi ya Baraza la Kulinda Katiba la Iran na kuelezea masikitiko yake makubwa kuhusiana na watu ambao wanamfuata kibubusa adui bila kujua ambao wanalishambulia baraza hilo bila ya sababu yoyote na kuongeza kuwa: Baraza la Kulinda Katiba lilifanya kazi yake vizuri na kwa uzito wa hali ya juu na hata kama kulitokea tatizo fulani, tatizo hilo ni la kisheria ambalo inabidi sheria yenyewe ilirekebishe.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kazi ya kuchunguza ustahiki wa kugombea wa watu 12 elfu tena katika muda wa siku 20 tu ni tatizo la kisheria ambalo inabidi lirekebishwe na sheria yenyewe, na si sahihi kutumia tatizo hizo la kisheria kulishambulia Baraza la Kulinda Katiba.
Ayatullah Khamenei ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu umuhimu wa kazi ya kuainisha watu wenye sifa za kugombea kwa kuuliza swali akisema: Je, inawezekana kweli kumjua mtu anayestahiki kugombea bila ya kuchunguza na kuainisha sifa zake? Na je, kama hilo halikufanyika, kutakuwa na majibu ya kumjibu Mwenyezi Mungu?
Aidha amekumbusha kuwa: Kama Baraza la Kulinda Katiba litashindwa kuainisha sifa za watu waliojitokeza kugombea, haiwezekani kuwa na uhakika wa ustahiki wa kugombea watu hao, hivyo kazi ya baraza hilo si kosa, bali huko ni kutekeleza sheria.
Vilevile Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa Baraza la Kulinda Katiba ni moja ya taasisi za asili za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ambayo imekuwa ikishambuliwa na kuhujumiwa na mabeberu tangu mwanzoni kabisa mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuongeza kuwa: Jaribio lolote la kutaka kuvuruga itibari ya Baraza la Kulinda Katiba ni kitendo kisicho cha Kiislamu, ni kinyume cha kanuni, ni kinyume cha sheria na ni kinyume na manufaa ya Mapinduzi ya Kiislamu.
“Baraza la Kulinda Katiba ni moja ya taasisi za asili za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ambayo imekuwa ikishambuliwa na kuhujumiwa na mabeberu tangu mwanzoni kabisa mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu”.
Amesisitiza kuwa: Ni jambo la kawaida kuhuzunika kwa watu ambao inathibitika kuwa hawana sifa za kugombea, lakini hilo halimpi haki mtu ya kuharibu hadhi ya Baraza la Kulinda Katiba, bali kama ana malalamiko anapaswa kuyafuatilia kwa njia za kisheria.
Baada ya kubainisha sifa hizo maalumu na ujumbe wa kila aina uliomo kwenye uchaguzi wa Februari 26, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, wananchi wametekeleza vizuri jukumu lao kwa kujitokeza vilivyo na kwa wingi mkubwa kwenye medani hiyo ya uchaguzi na sasa ni zamu ya viongozi nchini kutekeleza vizuri majukumu yao baada ya kupata ridhaa hiyo ya wananchi.
Awali Ayatullah Khamenei amebainisha majukumu ya wajumbe wa baraza hili jipya la Wanavyuoni Wataalamu likiwa ni moja ya nguzo muhimu sana za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema kuwa: Jukumu la Baraza la Wanavyuoni Wataalamu ni kubakia kuwa la kimapinduzi, kufikiria kimapinduzi na kufanya mambo yake yote kimapinduzi.
Amesema, kuchungwa kwa sifa hizo tatu kuu ni miongoni mwa majukumu muhimu sana Wanavyuoni Wataalamu katika kuchagua Kiongozi Mkuu wa nchi na kusisitiza kuwa: Katika kuchagua Kiongozi Mkuu ajaye, kula ulazima wa kuweka kando masuala ya kuona haya, kuangalia maslahi binafsi na vitu kama hivyo na badala yake azingatiwe Mwenyezi Mungu, mahitaji ya nchi na uhakika wa mambo katika uhalisia wake.
“Jukumu la Baraza la Wanavyuoni Wataalamu ni kubakia kuwa la kimapinduzi, kufikiria kimapinduzi na kufanya mambo yake yote kimapinduzi”.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Kama kutafanyika uzembe wowote ule katika utekelezaji wa jukumu hilo kubwa, basi bila ya shaka yoyote kutazuka matatizo katika msingi wa kazi za mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na za nchi.
Ayatullah Khamenei vilevile ameashiria suala la kuweko maulamaa, watu wakubwa na shakhsia muhimu sana katika Baraza la Wanavyuoni Wataalamu na kuongeza kuwa, jukumu jingine muhimu sana la wajumbe wa baraza hilo ni kubainisha matakwa na matatizo ya wananchi kwa viongozi na vilevile kuwaelewesha na kuwabainishia wananchi uhakika wa mambo. 
Vilevile amezungumzia majukumu ya wajumbe wa duru mpya ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) kwa kuashiria nasaha zake za kila siku za kuhakikisha kuwa Bunge linaisaidia serikali katika kazi zake. Ameongeza kuwa: Kushirikiana na kuisaidia serikali hakuna maana ya kwamba Bunge lifumbie macho majukumu yake ya kisheria.
Baada ya hapo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia majukumu ya viongozi wa serikali na kusema: Katika mazingira ya sasa ya nchi yetu, kuna majukumu na vipaumbele vitatu vikuu ambavyo inabidi viongozi serikalini wavizingatie: 1- Ni uchumi ngangari na wa kusimama kidete, 2- ni kuendelea kwa kasi kubwa harakati ya kielimu nchini na 3- ni kulinda utamaduni wa nchi, taifa na vijana.
Ayatullah Khamenei kwa mara nyingine amesisitiza kipaumbele cha kwanza akisema, matatizo ya kiuchumi nchini hayataweza kutatuliwa kama hazitatekelezwa inavyopasa siasa za uchumi ngangari na kamwe hayatapatikana maendeleo ya kiuchumi nchini kama siasa hizo hazitatekelezwa ipasavyo. Ameongeza kwamba: Ilikuwa imeamuliwa kuwa serikali ianzishe kambi maalumu kwa ajili ya kuendeshea siasa za uchumi ngangari na aainishwe kamanda wa kuendesha kambi hiyo; ingawa hilo limeshafanywa lakini inabidi athari za hatua hizo zionekane.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusema: Viongozi serikalini wanapaswa kuainisha wazi uhusiano uliopo baina ya kazi na juhudi zao za kiuchumi kwa upande mmoja na uchumi ngangari na wa kusimama kidete kwa upande wa pili na inabidi kigezo cha ushirikiano na mpango wowote wa kiuchumi nchini, kiwe ni siasa za uchumi ngangari ambazo zimekusanywa na wataalamu wengi na zinakubaliwa kwa kauli moja na sehemu kubwa ya weledi na watambuzi wa masuala ya uchumi.
Ayatullah Khamenei ameashiria pia kipaumbele cha pili yaani kuendelea na harakati yenye kasi kubwa ya kielimu na kusema kuwa: Kama tunataka tuwe na nguvu, heshima na tuwe marejeo ya wengine duniani, hatuna budi kujiimarisha kielimu na tuhakikishe kuwa kasi ya harakati ya kielimu haikwami mahala popote pale. 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Inabidi suala la maendeleo ya kielimu lipewe uzito wa hali ya juu sana kwani moja ya matunda mazuri ya jambo hilo ni kuwa na uchumi unaotokana na kuuza elimu.
Ayatullah Ali Khamenei amegusia pia kipaumbele cha tatu kinachopaswa kupewa uzito mkubwa na viongozi serikalini yaani kuyawekea kinga mambo ya kiutamaduni nchini na kusisitiza kuwa: Kabla ya jambo lolote ni lazima tuwe na imani kamili kuhusu manufaa, lengo na shabaha ya kuweka kinga za kiutamaduni na baada ya hapo tuweke mipangilio mizuri na tuhakikishe inatekelezwa kivitendo.
Vilevile amesema: Iwapo vipaumbele hivyo vitatu vitapewa uzito unaotakiwa katika ajenda za kazi za viongozi wa serikali, basi matokeo yake yatakuwa ni nchi kupata maendeleo ya kweli inayoyahitajia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kuwa maendeleo ya kijuu juu yanayopatikana kupitia njia ya kuwa na ustawi wa kidhahiri tu na wa kuingiza bidhaa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuwafurahisha kwa muda mfupi watu katika jamii yana madhara makubwa kwa wananchi hao na kusisitiza kuwa: Maendeleo yanapaswa kuwa ya kimsingi na yenye mizizi uliyokita chini ya ardhi, na inabidi maendeleo hayo yawe imara na yategemee misingi ya ndani na si ya nje ya nchi.
Amelitaja suala la kulindwa sifa ya kimapinduzi, harakati ya kijihadi, kulindwa heshima na utambulisho wa kitaifa na Kiislamu na kutoruhusu kumeng'enywa ndani ya mmeng'enyo hatari wa kiutamaduni, kiuchumi na kisiasa wa dunia, kuwa ni jambo jengine la lazima kwa ajili ya maendeleo ya nchi. Vilevile amegusia njama za adui za kutaka kujipenyeza ndani ya jamii ya Iran na kusema: Kwa mujibu wa taarifa za kina, mabeberu wakiongozwa na Marekani wanaendesha mpango kabambe wa kujipenyeza nchini Iran. Kujipenyeza huko si kwa sura ya kufanya mapinduzi, kwani wanajua vyema kuwa jambo hilo haliyumkiniki kabisa katika muundo wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hivyo wanafuatilia njama zao hizo kupitia njia nyingine mbili tofauti. 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekutaja mikakati ya maadui ya kuelekeza mawimbi ya njama zao upande wa viongozi na upande wa wananchi kuwa ndizo njia mbili kuu zinazotumiwa na adui kwa ajili ya kujipenyeza nchini na kuongeza kuwa: Lengo la adui la kufanya njama za kujipenyeza katika safu za viongozi nchini, ni kuvuruga mahesabu ya viongozi hao ambapo matokeo yake yatakuwa ni kuingia fikra na irada ya viongozi hao kwenye makucha ya adui na kama hilo litatendeka, basi adui hatakuwa tena na haja ya kuingia moja kwa moja katika masuala ya nchi, bali kiongozi fulani ndani ya nchi tena bila ya yeye mwenyewe kujua; atakuwa anachukua maamuzi yale yale yanayotakiwa na adui.
“Lengo la adui la kufanya njama za kujipenyeza katika safu za viongozi nchini, ni kuvuruga mahesabu ya viongozi hao ambapo matokeo yake yatakuwa ni kuingia fikra na irada ya viongozi hao kwenye makucha ya adui”.
Amesema, shabaha nyingine ya mashambulio ya adui kwa ajili ya kujipenyeza katika masuala ya Iran ni imani na itikadi za wananchi kuhusiana na dini tukufu ya Kiislamu, Mapinduzi ya Kiislamu, Uislamu wa kisiasa na majukumu yote ya mambo hayo yaani kujenga jamii na ustaarabu wa Kiislamu. Ameongeza kuwa: Kuondoa uhuru wa nchi ni nukta nyingine inayolengwa na adui anayetaka kujipenyeza katika masuala ya Iran na inasikitisha kuona kuwa kuna baadhi ya watu ndani ya nchi wanaofanya mambo kiuanagenzi na ambao wanaunga mkono jambo hilo kiasi kwamba wanathubutu hata kusema kuwa uhuru na kujitegemea nchi ni maudhui kongwe iliyopitwa na wakati na leo hii haina maana tena. 
Ayatullah Khamenei ameitaja njama nyingine inayofanywa na adui kuwa ni kujaribu kubadilisha imani na mitazamo wa wananchi na kujaribu kuwasahaulisha usaliti uliofanywa na Wamagharibi dhidi yao na kukumbusha kuwa: Katika propaganda zao duniani utaona wanapenda sana kuuliza swali hili kwamba kwa nini Jamhuri ya Kiislamu na viongozi wake wanaipinga Magharibi na Marekani kwa kiasi chote hiki?
Amesema: “Sisi tumepata pigo kubwa kutoka kwa Wamagharibi na hatupaswi kabisa kusahau maovu tuliyofanyiwa na Wamagharibi. Mimi si kwamba naunga mkono kukata uhusiano na nchi za Magharibi, hapana, bali tunapaswa kuwa na tahadhari na tujue ni watu wa namna gani tunaoamiliana nao”.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha ametaja mambo kadhaa ya waziwazi yanayoonesha uadui wa Magharibi dhidi ya taifa la Iran kutoka katika kipindi cha katikati mwa utawala wa wafalme wa Qajar nchini Iran hadi leo hii na kusema: Udhaifu waliokuwa nao wafalme wa Qajar ulitoa fursa kwa Wamagharibi kuweka mashinikizo na kujinufaisha binafsi jambo ambalo liliishia kwenye kukwama maendeleo ya taifa letu. Baada ya hapo akaja Reza Khan na baadaye Wamagharibi wakamuweka madarakani mwanawe, na baada ya hapo pia wakaikandamiza harakati ya mwamko wa kitaifa ya tarehe 19 Agosti 1953 na wakaanzisha taasisi ya kikatili ya Savak dhidi ya wananchi wa Iran.
Ayatullah Khamenei ameendelea kutoa mifano ya mambo maovu yaliyofanywa na Wamagharibi dhidi ya taifa la Iran kwa kusema: Kuangamiza sekta ya kilimo, kusimamisha maendeleo ya kielimu, kuwateka nyara wanafikra amilifu na kuwasukuma vijana wa Iran kwenye masuala ya ufuska na uraibu wa mihadarati kuwa ni sehemu nyingine ya mipango ya kiuadui iliyoendeshwa na Wamagharibi katika kipindi cha watawala wa kifalme wa Pahlavi nchini Iran. Ameongeza kuwa: Tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Wamagharibi walianza upinzani wao dhidi ya mapinduzi hayo, waliwaunga mkono watu wanaopinga Mapinduzi ya Kiislamu katika mipaka ya Iran na wakawapa fedha, silaha na misaada ya kisiasa, wakaeneza uvumi wa uongo na kufanya uadui dhidi ya Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) na dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu na viongozi wanamapinduzi na hata katika vita pia walimsaidia kwa hali na mali Saddam kwa kadiri walivyoweza. Walimpa misaada ya kijeshi, kijasusi na kisiasa (ili kupambana na utawala mchanga wakati huo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran). 
Vilevile amekitaja kitendo cha maadui cha kuiwekea vikwazo Iran kuwa ni mfano mwingine wa uadui wa Wamagharibi dhidi ya taifa hili na kuongeza kuwa: Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu haukuwa na nia kabisa ya kuwa na uadui na Magharibi, bali uliweka misingi ya kuwa huru na kujitegemea Iran, na hii ndio maana Wamagharibi waliamua kuufanyia uadui mfumo huu wa Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia namna Ulaya inavyofuata kibubusa siasa za Marekani katika masuala tofauti kama vile vikwazo na propaganda za kiuadui dhidi ya Iran na kukumbusha kuwa: Sisi ni viongozi wa nchi na taifa na tuna majukumu ya kihistoria, na kama hatutasimama kidete, imara na kishujaa kukabiliana na uadui wa maadui, basi maadui hao wataimeza nchi na taifa na haipasi hata chembe kuruhusu jambo hilo kutokea.
“Kama hatutasimama kidete, imara na kishujaa kukabiliana na uadui wa maadui, basi maadui hao wataimeza nchi na taifa”.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia matamshi ya baadhi ya viongozi nchini wanaosema kuwa, inabidi tuwe na maelewano na dunia nzima na kusema: “Ni kweli inabidi tuwe na maelewano mazuri na dunia nzima, lakini si kuwa na uhusiano na Marekani na utawala wa Kizayuni. Aidha tunapaswa kutambue kuwa, dunia haimalizikii Magharibi na Ulaya tu”.
Vilevile ameashiria jinsi nchi zaidi ya 130 zilivyoshiriki kwenye kikao cha Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) cha hapa mjini Tehran na kusema: Leo hii madola yenye nguvu duniani yameenea sehemu zote na eneo la Mashariki mwa dunia na eneo la Asia nalo ni eneo pana na kubwa sana.
Ayatullah Khamenei amesisitiza pia kuwa, awali Wamagharibi walijiwekea msingi wa kulifanyia uadui moja kwa moja taifa la Iran, lakini hivi sasa wameamua kutumia mbinu ya kujipenyeza ndani ya taifa hili. Ameendelea kusema: Adui ameandaa mpango wenye njia kama kumi hivi za kuwa na ushawishi wa kielimu, kiutamaduni na kiuchumi nchini Iran kama vile kujipenyeza kupitia vyuo vikuu, wasomi na wataalamu, kushiriki katika mikutano ambayo kijuu juu inaonekana ni ya kielimu lakini asili na lengo lake kuu ni kujipenyeza nchini pamoja na kutuma maafisa wao wa masuala ya usalama kwa jina la kufanya kazi za kiutamaduni.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amesema, njia bora na ya kimsingi ya kukabiliana na njama hizo za kujipenyeza adui ni kujiimarisha ndani ya nchi na kukumbusha kuwa: Iwapo Iran ya Kiislamu itakuwa imara na tajiri ndani kwa ndani, basi watu hao hao ambao leo hii wanatoa vitisho hivi na vile, watafika mahali walazimike kupanga safu kwa ajili ya kuwa na uhusiano mzuri na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Amesisitiza kuwa: Hivi sasa Wamagharibi wanakuja na kurudi humu nchini lakini hadi hivi sasa hakujaonekana athari yoyote nzuri ya safari zao hizo; inabidi ionekane kivitendo kwamba safari hizi zina taathira gani la sivyo maeleweno ya kwenye karatasi hayana faida yoyote. 
“Hivi sasa Wamagharibi wanakuja na kurudi humu nchini lakini hadi hivi sasa hakujaonekana athari yoyote nzuri ya safari zao hizo”.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amewashukuru viongozi nchini kwa juhudi mbalimbali wanazofanya kulihudumia taifa na kusema kuwa: Uzoefu wa miaka 37 ya Jamhuri ya Kiislamu umeonesha kuwa, tunapaswa kuwe imara kifikra, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kielimu na wakati tutakapofikia daraja hiyo, ndipo hapo tutakapoweza kusema kuwa tuna hadhi na heshima inayotakiwa.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Ayatullah Ali Khamenei amewaenzi na kuwataja kwa wema wajumbe wa duru ya nne ya Baraza la Uongozi la Wanavyuoni Wataalamu waliotangulia mbele ya Haki hususan Ayatullah Vaez Tabasi na Ayatullah Khazali na kusema: Ndugu zetu hawa wawili kwa hakika walikuwa na daraja kweli ya utaalamu katika Baraza la Wanavyuoni Wataalamu na walipasi vizuri kwenye mitihani ya kutekeleza majukumu yao kupitia baraza hilo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia historia nzuri ya mapambano ya Ayatullah Vaez Tabasi na utumishi wake katika kipindi cha Mapinduzi ya Kiislamu kwenye Haram tukufu ya Imam Ridha AS huko Mash'had, kaskazini mashariki mwa Iran na kusema kuwa: Mwanachuoni huyo alikuwa mtu muwazi, muumini na mwenye misimamo isiyotetereka na alibainisha misimamo yake hiyo kwa uwazi kabisa katika vipindi nyeti sana na hata katika fitna za mwaka 2009, aliweka pembeni haya na urafiki na kusimama imara katika medani ya kuilinda Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mapinduzi ya Kiislamu. 
Vilevile amekutaja kujitokeza kwa wingi na kwa adhama na shauku kubwa wananchi katika shughuli ya maziko ya Ayatullah Vaez Tabasi kuwa kunaonesha namna wananchi wa Mash'had wanavyothamini wema wanaotendewa na kuongeza kuwa: Maisha ya mtu huyu mkubwa katika kipindi chake cha kutekeleza majukumu yake hayakubadilika na yaliendelea kuwa yale yale ya chini na ya kawaida kabisa na kamwe hakuruhusu maisha ya anasa yaharibu maisha yake bali aliendelea kuishi katika nyumba hiyo hiyo aliyokuwa akiishi kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu na amefariki dunia akiwa katika nyumba hiyo hiyo.
Vilevile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuhusu Ayatullah Khazali kwamba: Marehemu huyo amepasi vizuri sana pia kwenye mtihani mwingine mgumu sana na wakati yalipozuka masuala ya watu wake wa karibu na watu wanaonasibishwa naye, yeye alisimama kwa ushujaa kamili kuyahami Mapinduzi ya Kiislamu ambapo ni sifa za namna hii na harakati kama hizo za kimapinduzi ndizo zinazowapa heshima na thamani watu wakubwa kama hawa.
Ayatullah Khamenei ametoa mkono wa pole kwa mnasaba wa siku za kukumbuka kufa shahidi Bibi Fatimatu Zahra (Salamullahi Alayha) na kusema: Inabidi katika kutaja sifa za mtukufu huyo izingatiwe kwamba hakutamkwi maneno yatakayozusha hitilafu na chuki kati ya Waislamu kwani leo hii siasa kuu za kibeberu za kambi ya kiistikbari ni kuzusha mizozo na mifarakano baina ya Waislamu wa Kishia na Kisunni.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Hakuna tatizo kuzungumzia historia kwa kuchunga mipaka, kwa heshima na kwa kuzingatia maslahi ya Umma lakini kutaja mambo hayo ya kihistoria hakupaswi kuwe sababu ya kuzusha mizozo na chuki baina ya Waislamu.
Amesema, vita na mapigano yaliyopo kwenye eneo la Mashariki ya Kati hivi sasa yanatokana na malengo ya kisiasa kikamilifu na ametoa nasaha akisema: Maadui wa Uislamu wanafanya njama za kufanya tofauti hizo kuwa mizozo ya kimadhehebu ili isiwe rahisi kumaliza vita na mapigano hayo baina ya Waislamu; hivyo sisi hatupaswi kusaidia kufikiwa lengo hilo hatari sana.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia namna Waislamu wa Kisuni wanavyouawa shahidi katika kulinda haram za Ahlul Bait AS na jinsi familia za mashahidi hao zinavyojivunia na kuona fakhari kwa jambo hilo na kusema kuwa: Mwanachuoni mwenye busara hatumii ulimi wake kuwachochea na kuwachokoza Waislamu wenzake na hivyo ikawa sababu ya kutekelezwa njama za Wamarekani na Wazayuni za kueneza mizozo na chuki kati ya Waislamu.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Yazdi, Mkuu wa Baraza la Uongozi la Wanavyuoni Wataalamu amepata fursa ya kuzungumza na sambamba na kutoa mkono wa pole kwa mnasaba wa siku za kukumbuka kufa shahidi Bibi Fatimatu Zahra pamoja na kuwakumbuka Ayatullah Vaez Tabasi na Ayatullah Khazali. Vilevile ametoa ripoti fupi kuhusiana na kikao cha 19 cha Baraza la Wanavyuoni Wataalamu. 
Naye Ayatullah Hashemi Shahroudi, Naibu wa Mkuu wa Baraza la Wanavyuoni Wataalamu ametoa ripoti fupi kuhusiana na mambo muhimu zaidi pamoja na matamshi na mazungumzo yaliyofanyika baina ya wajumbe wa baraza hilo na wageni walioalikwa kwenye kikao cha hivi karibuni cha baraza hilo la Wanavyuoni Wataalamu. 

700 /