Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu:

Chuo kikuu cha kidini cha Qum kinapaswa kuendelea kuwa cha kimapinduzi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo asubuhi (Jumanne) ameonana na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa Wanafunzi wa Hawza (Chuo Kikuu cha kidini) ya Qum na sambamba na kubainisha hadhi na nafasi muhimu isiyo na mbadala na yenye taathira kubwa ya Hawza za kidini katika ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini ameashiria baadhi ya njama zinazofanywa kwa ajili ya kuondoa mapinduzi katika Hawza na chuo kikuu cha kidini. Amesisitiza kuwa: Hawza ya Qum inapaswa iendelee kuwa chuo cha kimapinduzi na kitovu cha Mapinduzi na kwamba ili kuweza kulifikia lengo hilo kunahitajika fikra, tadbiri na mipangilio mizuri.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameanza hotuba yake kwa utangulizi kuhusu taathira kubwa ya Hawza ya Qum katika ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na  kudumisha mapinduzi hayo na kusema kuwa: Kuna mambo mawili yalikuwa na taathira kubwa na ya wazi katika ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, moja ni vyuo vikuu na pili ni Hawza.
Ayatullah Khamenei amegusia suala kuwepo daima harakati za mapambano katika vyuo vikuu kwenye nukta na maeneo mbalimbali ya dunia kutokana na mazingira ya vyuo vikuu na welewa wanaokuwa nao wanafunzi wa vyuo hivyo kuhusu masuala ya zama na kuongeza kuwa: Mapambano na wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Iran yamekuwepo muda wote, iwe ni katika kipindi cha mapambano ya Kiislamu au hata kabla yake; hata hivyo mapambano hayo ya wanachuo hayakuweza kuwa na taathira kubwa kutokana na kuwa taathira zake hazikuenea kwenye maeneo mengi hivyo yalishindwa kuleta mabadiliko na mapinduzi yoyote nchini.
Amesema, mapambano ya wanafunzi wa vyuo vikuu katika ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yalikuwa na taathira kubwa kutokana na kuwemo ndani yake kitu cha asili na muhimu, nayo ni mapambano yaliyoambatana na fikra ya kidini. Ameongeza kuwa: Tunawashukuru wanafunzi wa vyuo vikuu kwa mapambano hayo, lakini kama watu wa dini wasingeliingia kwenye mapambano hayo, basi bila ya shaka yoyote mapambano hayo yangeliishia tu kwenye maeneo ya vyuo vikuu hivyo.
Kiongozi Muadhamu wa Maipnduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa, suala la kuenea sehemu zote na kuathiri ni sifa mbili kuu za harakati ya watu wa dini katika Mapinduzi ya Kiislamu. Pia amesema, Hawza ya Qum iko katika sehemu mbili, sehemu moja ni ya marja'a (kiongozi mkuu wa kidini) na sehemu ya pili ni ya wanafunzi na ndio maana Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) alikuwa akitoa matamko, taarifa na hotuba zake akiwa marja'a wa kidini, lakini watu ambao walizifikisha hotuba na mitazamo ya Imam hadi ndani kabisa ya jamii na kuwafikia hata watu wa maeneo ya mbali sana, ni mashekhe na wanafunzi wa kidini.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: Lau isingelikuwepo Hawza ya Qum, labda harakati ya Imam Khomeini isingelifanikiwa na hili linathibitisha nafasi muhimu sana ya Hawza ya Qum katika kuundika na kuimarika Mapinduzi ya Kiislamu.
Ameongeza kuwa: Zile nguvu ambazo ziliwafanya wananchi wamiminike mabarabarani na kufanya maandamano ya mamilioni ya watu, ni taathira za wanafunzi wa kidini ambao walizifikisha fikra na nia ya Imam Khomeini hadi katika maeneo ya mbali kabisa ya Iran.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kitu kilichounganisha mzingo na duara baina ya Imam Khomeini na kuundika Mapinduzi ya Kiislamu ni Hawza ya Qum. Ameongeza kuwa: Ni kwa kuzingatia nafasi hiyo bora na isiyo na mbadala ya Hawza ya Qum katika ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, ndio maana hivi sasa maadui wamepata msukumo mkubwa zaidi wa kukabiliana na fikra za kimapinduzi kwenye kituo hicho cha kidini.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Kama tunataka mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu uendelee kuwa wa Kiislamu na kimapinduzi, basi hatuna budi kuhakikisha kuwa Hawza inaendelea kuwa ya kimapinduzi kwani kama Hawza haitakuwa ya kimapinduzi, basi mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu utatumbukia katika hatari ya kukumbwa na upotoshaji kuhusu Mapinduzi ya Kiislamu.
Amesisitiza pia kuwa, kuna wajibu wa kuhisi hatari kwa jambo lolote lile linaloelekea kupiga vita fikra za kimapinduzi katika vituo vya kidini na kuongeza kuwa: Kuna ulazima wa kukabiliana na hatari hiyo kwa fikra, tadbiri na mipangilio iliyojaa hekima ili kuhakikisha kuwa Hawza ya kidini ya Qum inaendelea muda wote kuwa Hawza ya kimapinduzi na kitovu cha Mapinduzi sambamba na kuhakikisha kuwa fikra na harakati za kimapinduzi ndani ya Hawza hiyo zinapanuka na kupata nguvu zaidi.
Ayatullah Khamenei amegusia pia mbinu zinazotumiwa na maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema kuwa: Baadhi ya wakati utaona wanayapinga waziwazi Mapinduzi ya Kiislamu lakini wakati mwingine wanatumia njia zisizo za moja kwa moja kupinga misingi na nguzo za kiitikadi za Mapinduzi ya Kiislamu, hivyo inabidi kuwa na hisia kali kuhusu mambo hayo na hii ndiyo sababu ya kusisitizia mara kwa mara udharura wa kuwa macho katika kukabiliana na ubeberu wa Marekani.
Amesema, sababu kuu inayowafanya mabeberu kuipinga Jamhuri ya Kiislamu ni kusimama imara Iran katika kukabiliana na mfumo wa kidhalimu uliopo duniani hii leo. Ameongeza kuwa: Kama kusimama huko kidete kwa Iran hakungekuwepo basi juweni wazi kuwa madola ya kibeberu yasingelikuwa na upinzani wowote dhidi yenu, hata ukijiita kwa jina lolote lile.
“Kama kusimama huko kidete kwa Iran hakungekuwepo basi juweni wazi kuwa madola ya kibeberu yasingelikuwa na upinzani wowote dhidi yenu, hata ukijiita kwa jina lolote lile”.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekitaja kitendo cha maadui na mabeberu wa dunia cha kupinga misingi na masuala yaliyosisitizwa na Imam Khomeini, mwanachuoni mwenye hekima, mwenye muono wa mbali na mwenye mwamko, kuwa ni mbinu nyingine inayotumiwa na mabeberu hao ili kukabiliana na Mapinduzi ya Kiislamu na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Ameongeza kuwa: Maana halisi ya kuwepo vita hivi vya kisiasa na kipropaganda dhidi ya misingi na mambo yaliyosisitizwa na Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu) ni kupinga Uislamu wa kisiasa na Uislamu wa kweli ambao kwa mara ya kwanza tangu kudhihiri Uislamu nchini Iran umeweza kuunda utawala na kuongoza nchi.
Vilevile amebainisha njia ya kukabiliana na njama za kudhoofisha fikra na moyo wa kimapinduzi katika Hawza na vyuo vya kidini akisema: Majimui husika katika Hawza hususan Baraza la Wawakilishi wa Wanafunzi wa Hawza ya Kidini ya Qum zinaweza kupanua wigo wa ratiba na mipango yao ya kuwa na mawasiliano yasiyokatika na ya maana katika Hawza nzima na pia kuunda vikundi vya kifikra kwa ajili ya kutafuta njia sahihi za kueneza fikra za kimapinduzi na vilevile kutafuta na kutatua matatizo na shubha zinazosumbua akili za wanafunzi wa kidini na kwamba hayo ni mambo ambayo yana nafasi muhimu katika uwanja huo.
Ayatullah Khamenei amelitaja Baraza la Wawakilishi wa Wanafunzi wa Dini wa Hawza ya Qum kuwa ni ubunifu mzuri sana na ni kitu ambacho inabidi kilindwe na kiimarishwe katika upande wa kisheria, nafasi yake na pia katika upande wa ndani ya baraza hilo na vitu vyake.
Ameongeza kuwa: Ni kwa kuwa na mtazamo kama huo na pia ni kwa kuwa na mipango inayotakiwa pamoja na taufiki ya Mwenyezi Mungu ndipo itakapowezekana kulea mamia ya walimu wenye ufanisi na wanamapinduzi. Aidha amesema, itawezekana pia kueneza moyo wa kimapinduzi kadiri inavyowezekana kupitia uhusiano wa ndani ya nyoyo na wa kimaanawi baina na wanafunzi wa dini na walimu wao katika Hawza za kidini.
Mwishoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Licha ya kuwepo baadhi ya mambo yasiyokubalika ya hapa na pale, lakini mwelekeo jumla wa harakati ya nchi (ya Iran) ni mzuri na harakati hiyo inazidi kupiga hatua za kimaendeleo na kwamba upeo wa mustakbali bora wa taifa hili uko wazi katika nyuga zote kwa uwezo na baraka za Mwenyezi Mungu.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimin Husseininejad, Mkuu wa Baraza la Wawakilishi wa Wanafunzi wa Kidini wa Hawza ya Qum ametoa ripoti fupi kuhusu ratiba na kazi za baraza hilo pamoja na mipango yake ya baadaye.
  

700 /