Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu katika ujumbe wake wa Nairuzi na mwaka mpya wa 1395:

Mwaka mpya ni mwaka wa Uchumi Ngangari, Hatua na Vitendo

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa ujumbe wa kuanza mwaka mpya wa 1395 Hijria Shamsia akiwapa mkono wa kheri ya mwaka mpya na Nairuzi wananchi wote na Wairani hususan familia tukufu za mashahidi na majeruhi wa vita. Vilevile amewakumbuka na kuwaenzi mashahidi na Imam Khomeini na kusema: “Mwaka mpya ninaupa jina la Mwaka wa Uchumi Ngangari, Hatua na Vitendo”.
Ayatullah Khamenei ameashiria suala la kusadifiana siku ya kuzaliwa Bibi Fatima Zahra (as) na mwanzo na mwisho mwaka mpya 1395 na kusema anatarajia kuwa mwaka huu utakuwa mwaka wenye baraka kwa taifa la Iran na katika mwaka huu tutaweza kupata darsa na somo kutokana na miongozo na maisha ya Bibi huyo adhimu kwa kufaidika na masuala ya kiroho ya mtukufu huyo.
Katika tathmini yake kuhusu mwaka uliopita, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, mwaka 1394 ulichanganya pamoja matukio matamu na machungu, panda shuka, na ulikuwa na fursa na vitisho na kuongeza kuwa: Kuanzia machungu ya tukio la Mina (Saudi Arabia) hadi tamu ya maandamano ya tarehe 22 Bahman (11 Februari) na uchaguzi wa tarehe 7 Esfand (26 Februari) vilevile tajiriba ya mapatano ya nyuklia (kati ya Iran na kundi la 5+1) ambayo yamehuisha matumaini na yanayoambatana na wasiwasi, yote hayo ni sehemu ya matukio ya mwaka uliopita wa 1394.
Ameashiria matarajio, fursa na vitisho vinavyotazamiwa katika mwaka huu mpya na kusema: Sanaa na kazi kubwa ni kutumia fursa ipasavyo na kuvibadili vitisho kuwa fursa kwa kadiri kwamba, mwishoni mwa mwaka kuwepo tofauti inayohisika hapa nchini; hata hivyo ili kufikia matarajio hayo kuna ulazima wa kufanya juhudi na kazi za usiku na mchana na vilevile kufanya harakati na jitihada bila ya kusita”.
Akibainisha nukta muhimu na ya kimsingi katika harakati kuu ya taifa la Iran, Ayatullah Khamenei amesema: Taifa la Iran linapaswa kufanya kazi ya kujiondoa katika nafasi ya kupatwa na madhara ya vitisho vya adui na kufikisha vitisho hivyo kiwango cha sifuri.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, kipaumbele cha kwanza na cha haraka katika harakati hiyo muhimu ni suala la uchumi na kuongeza kuwa: Iwapo taifa, serikali na viongozi wote wataweza kufanya kazi sahihi, zinazofaa na madhubuti katika kadhia hii ya uchumi kuna matarajio kuwa kazi hizo zitakuwa na taathira katika mambo mengine kama masuala na matatizo ya kijamii na masuala ya kimaadili na kiutamaduni.
Amesema kuwa, uzalishaji wa ndani, kutayarisha nafasi za kazi, kuondoa tatizo la ukosefu wa ajira na harakati na ustawi wa kiuchumi na kukabiliana na mdororo katika sekta hiyo ndiyo masuala muhimu ya uchumi. Ameongeza kuwa: Masuala hayo ni miongoni mwa mambo yanayowasumbua wananchi na wananchi wanayahisi na wanataka utatuzi wake; vilevile takwimu na matamshi ya viongozi yanaonesha kuwa, matakwa hayo ya wananchi ni sahihi na ya mahala pake.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, uchumi ngangari ndiyo dawa ya matatizo ya kiuchumi na jibu la matakwa ya wananchi. Ameongeza kuwa, kwa kutumia uchumi ngangari tunaweza kupambana na ukosefu wa ajira na mdororo wa uchumi, kudhibiti ughali wa bidhaa, kusimama kidete mbele ya maadui na kutengeneza fursa nyingi kwa ajili ya nchi na kuzitumia.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa sharti la kupata mafanikio hayo ni kuchapakazi na kufanya juhudi kwa mujibu wa sera za uchumi ngangari. Ameongeza kuwa, ripoti za serikali zinaonesha kuwa, kumefanyika kazi kubwa katika uwanja huo lakini kazi hizo ni utangulizi na zinahusu hukumu na amri zilizotolewa kwa taasisi mbalimbali.
Amesema wadhifa wa viongozi ni kuchukua hatua za kivitendo katika uwanja wa uchumi ngangari na kusisitiza kuwa, kuna udharura wa kudumishwa harakati na kazi za mipango ya uchumi ngangari na matokeo yake yaonekane na kuoneshwa kwa wananchi.
Ayatullah Khamenei amesema uchumi ngangari, hatua na vitendo ni mithili ya njia iliyonyooka na ya wazi kuelekea upande wa kukidhi mahitaji ya nchi. Vilevile amewashukuru watu wote wanaofanya jitihada katika uwanja huo na kusema kuwa: Haitazamiwi kwamba hatua na kazi hiyo itaondoa matatizo yote katika kipindi cha mwaka mmoja lakini iwapo hatua na utendaji vitafanyika kwa mipango sahihi, hapana shaka kuwa, athari zake zitaonekana mwishoni mwaka huu.          
  

700 /