Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Uchumi ngangari utalinda njia ya kimapinduzi ya Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei katika siku ya kwanza ya mwaka mpya (wa Kiirani wa 1395 Hijria Shamsia) ametoa hotuba muhimu mbele ya hadhara kubwa ya wafanya ziara na majirani wa Haram toharifu ya Imam Ridha AS. Katika hotuba hiyo muhimu Ayatullah Khamenei amebainisha maana halisi na malengo ya siri na hatari sana ya fikra za watu za kusalimu amri ambazo Marekani naa baadhi ya watu hapa nchini wanataka kuziingiza katika fikra za taifa la Iran kwa kuonesha njia mbili za uongo na za kujibunia. Vilevile ametoa mapendekezo kumi ya kimsingi ya kufanikisha kaulimbiu ya uchukuaji hatua na utekelezaji wa kivitendo katika uwanja wa uchumi ngangari na kusisitiza kuwa: Njia hii ya kimantiki na wakati huo huo ya kimapinduzi itailinda na kuipa kinga Iran azizi mbele ya vitisho na vikwazo na itaiwezesha serikali kutoa ripoti ya kivitendo na ya kujenga imani ya wananchi mwishoni mwa mwaka huu chini ya kivuli cha kupendana na kushirikiana watu wote pamoja na kusaidiana na kufanya kazi kwa pamoja mihimili mitatu mikuu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa mara nyingine tena ametoa mkono wa baraka na fanaka kwa taifa la Iran kwa mnasaba wa kuanza mwaka mpya wa Hijria Shamsia na kusadifiana mwaka huo wa 1395 mwanzo wake na mwisho wake na siku ya kuzaliwa Bibi Fatimatu Zahra (as) akisema kuwa, kusadifiana huko ni baraka kwa Iran.
Ayatullah Khamenei ameendelea na hotuba yake kwa kutoa ufafanuzi mpana kuhusu kaulimbiu ya mwaka huu na kwa nini imeamuliwa mwaka huu wa 1395 Hijria Shamsia ubebe kaulimbiu hiyo ya "Uchumi wa Ngangari, Hatua na Vitendo."
Amesisitiza kuwa, kuchaguliwa nara na kaulimbiu hiyo kwa ajili ya mwaka huu wa 1395 kumefanyika kwa msingi wa kimantiki na kwa kutegemea hoja zenye nguvu na amewataka wananchi wote  hususan vijana kuzingatia na kuangalia kwa kina na kwa tadibiri msingi huo wenye hoja madhubuti. Amesema: Huenda baadhi ya watu wangependelea kaulimbiu ya mwaka huu ihusu masuala ya kiutamaduni au kimaadili, lakini kwa kuzingatia masuala mbalimbali yaliyopo nchini, imeamuliwa kaulimbiu ya mwaka huu, kama ilivyokuwa kwa miaka kadhaa iliyopita, iwe ya kiuchumi ili suala hilo la kiuchumi lienee na kujikita vizuri katika mazungumzo, vitendo na fikra za watu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Kuchaguliwa kaulimbiu hiyo kwa ajili ya mwaka huu kumekuja baada ya kufanyika utafiti wa kina na kuzingatiwa pande zote za masuala yanayohusiana na nchi.
Ametoa ufafanuzi zaidi kuhusu mtazamo huo mpana kwa kusema: Hivi sasa Wamarekani wanataka kupandikiza fikra maalumu kati ya watu wenye vipawa na wenye ushawishi katika jamii na hatimaye waweze kupenya na kuathiri fikra za watu wote hapa nchini. Fikra hiyo ni kutaka kuonesha kuwa taifa la Iran liko njia panda na halina njia nyingine ila kuchagua moja ya njia hizo mbili!
Ayatullah Khamenei amesema, njia hizo mbili zinazokusudiwa na Wamarekani ni kwamba taifa la Iran ama likubali kuwa pamoja na Marekani au likubali kuwa chini ya mashinikizo ya Marekani wakati wote na likubali kubeba matatizo ya jambo hilo. 
Amegusia pia utajiri, nyenzo za kisiasa na vyombo vikubwa vya kipropaganda pamoja na zana za kijeshi za Marekani na kusema kuwa: Kwa mujibu wa fikra hiyo maalumu, inabidi nchi zote duniani zikubaliane na Marekani na zikubali kuburuzwa na Wamarekani na kuachana na baadhi ya misimamo, misingi na mistari myekundu ya nchi na taifa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Hata katika makubaliano ya hivi karibuni ya nyuklia ambayo pamoja na kuungwa mkono na pia timu yetu ya mazungumzo kukubalika, lakini suala hilo hata huko nako limetendeka na katika baadhi ya masuala, mheshimiwa waziri wetu wa mambo ya nje aliwahi kuniambia: Hatukuweza kulinda baadhi ya mistari myekundu.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Hii ina maana ya kwamba, wakati upande wa pili unapokuwa ni serikali kama ya Marekani, kuwa pamoja na upande huo kuna maana ya kuachana na baadhi ya masuala ambayo ni msingi muhimu wa taifa.
Amesisitiza kuwa, kuna baadhi ya watu ndani ya nchi wanakubaliana na fikra hiyo hatari sana ya kuweko njia mbili za uongo na hata wanafanya juhudi za kufanya fikra hiyo ikubalike nchini. Amesisitiza kuwa: Watu hao wanasema kuwa, uchumi wa Iran una fursa na nafasi nyingi kama ambavyo wanadai pia kwamba, kustafidi na fursa na uwezo wote huo hakuwezekani kupitia mazungumzo ya nyuklia tu, bali kuna masuala mengine yanayoihusu Marekani ambayo inabidi wananchi na viongozi wa Iran wayachukulie maamuzi na hatua. 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, miongoni mwa masuala yanayofuatiliwa na watu wenye fikra hizo baada ya makubaliano ya nyuklia, ni mazungumzo na ushirikiano baina ya Iran na Marekani kuhusiana na msuala ya eneo la magharibi mwa Asia na vilevile mazungumzo kuhusu hitilafu zilizopo baina ya Tehran na Washington kwa maana ya kwamba Iran iachane na misingi na mistari yake myekundu.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, kwa mujibu wa mtazamo huo maalumu, matatizo ya kiuchumi nchini yataweza kutatuliwa pale tu tutakapofanya mazungumzo na Marekani katika masuala mbalimbali na kulegeza kamba kwenye misimamo yetu. Amesema: Watu hao wanasema, kama yalivyopatikana maafikiano ya nyuklia yajulikanayo kwa jina la JCPOA, kufanya mazungumzo na Marekani kuhusu masuala mengine na hata kuhusu katiba ya nchi yetu kunaweza kuzaa makubaliano mengine na JCPOA nambari mbili, tatu na nne ili kwa kupitia mazungumzo na maafikiano hayo, wananchi wetu waweze kuishi kwa raha, na matatizo yao nayo yaweze kutatuliwa.
Ameongeza kuwa: Maana halisi ya fikra hiyo hatari sana ni kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ianze pole pole kuachana na misingi yake yenye nguvu na usalama wake na masuala yake mengine ya kimsingi ambayo inashikamana nayo kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu na katika fremu ya mfumo wa Kiislamu, masuala kama vile kushikamana na mapambano na kuyaunga mkono kisiasa mataifa ya Palestina, Yemen na Bahrain na kuifanya misimamo yake iwe karibu na matakwa ya Marekani!
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusema kuwa: Kulingana na fikra hiyo maalumu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inabidi iwe sawa na baadhi ya tawala za Waarabu ambao kwa jeuri kubwa wameunyooshea mkono wa urafiki utawala wa Kizayuni wa Israel, hivyo wanataka na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nayo hatimaye iwe pamoja na utawala wa Kizayuni.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, katika fremu ya fikra hiyo hatari mno, ulegezaji kamba utaendelea hatua kwa hatua na kusisitiza kuwa, kama tutafanya kwa mujibu wa inavyotaka na inavyopenda Marekani, basi Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lazima isahau zana zake za ulinzi na badala yake muda wote itafute njia za kujibu na kukidhi matakwa ya siasa za kupenda makuu za Marekani.
Vilevile ameashiria makelele mengi ya kipropaganda yaliyopigwa hivi karibuni na vyombo vya habari vya Magharibi kuhusiana na mazoezi ya makombora ya Iran na kusema: Katika hali ambayo Marekani inafanya mara kwa mara mazoezi ya kijeshi katika eneo la Ghuba ya Uajemi ambalo masafa yaliyopo baina yake na Marekani ni maelfu ya kilomita, Wamarekani hao hao wanazusha makelele mengi wakati Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapofanya mazoezi ya kijeshi ndani ya ardhi yake na ndani ya mipaka yake ya usalama.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, kama tutakubaliana na fikra hiyo maalumu, basi tujue kuwa siasa za Marekani za kupenda kujikumbizia kila kitu upande wake na kulegeza kamba Iran katika misimamo yake hakutaishia hapa. Ameongeza kuwa: Iwapo fikra hiyo itakubaliwa basi mwendo wa kulegeza misimamo utaendelea na itafika mahala bila ya shaka Jamhuri ya Kiislamu ya Iran italazimika kujibu maswali ya Wamarekani ya kwa nini imeanzisha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH na kikosi cha Quds kama ambavyo pia italazimika kujibu kwa nini siasa zetu za ndani zimepangiliwa kwa kuzingatia sheria za Kiislamu, kwa nini mihimili mitatu mikuu ya dola nchini inafanya kazi kwa msingi wa sheria za Kiislamu, kwa nini Baraza la Kulinda Katiba haliungi mkono sheria zinazopingana na mafundisho ya Uislamu na mambo kama hayo.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa: Kama tutalegeza kamba mbele ya Marekani, basi tujue kuwa adui atajisogeza mbele hatua kwa hatua na itafika mahala Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itapoteza hadhi na heshima yake na itabakia na gamba la nje tu lisilo na chochote ndani yake.
Ameongeza kuwa: Kwa mujibu wa msingi na uchanganuzi na fikra hiyo ya maadui, kama taifa la Iran linataka kujivua na shari ya Marekani halina njia nyingine isipokuwa kuachane na vielelezo vya Jamhuri ya Kiislamu, mafundisho ya Uislamu na mambo yanayohusiana na masuala yake ya usalama.
Baada ya kutoa ufafanuzi kuhusu vipengee vinavyohusiana na fikra hiyo maalumu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameanza kuzungumzia hatari za fikra hiyo kwa kusema: Masuala ambayo yanasahauliwa katika fikra hii ni pamoja na kwamba, makubaliano yoyote yale na Marekani yana maana ya kulazimika Iran kutekeleza ahadi zake na wakati huo huo kukubaliana na hadaa, udanganyifu na ahadi zisizo na dhamana ya kutekelezwa za Wamarekani, suala ambalo hivi sasa tunaliona kwa macho yetu na hii ni hasara iliyo wazi.
Ayatullah Khamenei ametoa ushahidi wa kuthibitisha maneno hayo kwa kutoa mfano wa makubaliano ya nyuklia. Amesema: Hata katika haya makubaliano ya nyuklia, tunaona kuwa Wamarekani wamekataa kutekeleza ahadi zao na kwa mujibu wa matamshi ya mheshimiwa waziri wetu wa mambo ya nje, Wamarekani wametekeleza ahadi hizi kwenye makaratasi tu, lakini kivitendo hawakutekeleza ahadi hizi bali hata wanatumia njia mbalimbali za kuzuia kutekelezwa ahadi zao hizo.
Ameongeza kuwa: Hivi sasa na licha ya kuwepo makubaliano ya nyuklia, bado miamala yetu ya kibenki inakabiliwa na vizuizi mbalimbali, fedha za Iran nazo hazijarejeshwa kwani nchi za Magharibi na nchi zinazoathiriwa na misimamo ya Wamagharibi zinawaogopa Wamarekani.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, suala jingine linalosahauliwa katika njama za maadui za kuonesha kuweko njia mbili za uongo kwa taifa la Iran ni kujiuliza swali kwamba, ni nini hasa sababu na msingi wa uadui na chuki za Marekani dhidi ya taifa la Iran? Amesema: Kwa kuzingatia nafasi muhimu ya kiistratijia ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati, utajiri mkubwa wa mafuta na gesi, idadi kubwa ya watu, vipaji vingi vya kila namna na utajiri mkubwa wa historia yake kongwe, Iran inahesabiwa kuwa ni waridi la eneo hili, lakini nchi hii ya aina yake, ilikuwa kwenye makucha ya ubeberu wa Wamarekani kwa makumi ya miaka. Hata hivyo, kupitia Mapinduzi ya Kiislamu, wananchi wa Iran yameikomboa nchi yao kutoka katika ubeberu wa kuchupa mipaka wa Wamarekani 
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Mapinduzi ya Kiislamu si tu yameitoa Iran kwenye makucha ya Wamarekani, bali yamefanikiwa kukuza moyo wa muqawama na kusimama kidete mataifa ya eneo hili na hadi nje ya eneo hili dhidi ya ubeberu wa Marekani.
Ameongeza kuwa: Wamarekani wanaiona Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ndiyo sababu kuu ya kushindwa siasa zao za kuunda Mashariki ya Kati Kubwa na njama zao za kuufanya utawala wa Kizayuni wa Israel udhibiti kila kitu katika eneo hili na vile vile kushindwa uadui dhidi ya Yemen, Syria, Iraq na Palestina. Hivyo uadui wa Wamarekani dhidi ya taifa la Iran ni mkubwa mno na ni wenye mizizi mirefu, na uadui huo hautamaliza hadi pale watakapoweza kufufua ubeberu wao nchini Iran.
Ayatullah Khamenei ameendelea kubainisha sababu mbali mbali za kufanyiwa uadui taifa la Iran kwa kuashiria ubeberu wa muda mrefu wa Uingereza na baadaye Marekani dhidi ya Iran na kusema: Waingereza na Wamarekani walikuwa wamepiga kambi na kujiwekea ngome katika nchi hii na kupitia kupiga kambi kwa huko waliweza kufanikisha ubeberu wao nchini Iran, lakini Mapinduzi ya Kiislamu yaliyofanywa na vijana wanamapinduzi, yamefanikiwa kuvunja ngome zote hizo na kujenga ngome nyingine mpya kwa ajili ya kuilinda Jamhuri ya Kiislamu na manufaa ya taifa la Iran.
Ameendelea kusema kuwa: Wamarekani hivi sasa wameweka mipango mbalimbali na wanatumia wenzo wa udiplomasia kujaribu kujenga upya ngome zao hizo zilizoharibiwa na kuangamizwa na ngome za Mapinduzi ya Kiislamu. 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Utawala wa kidikteta na kitaghuti wa Pahlavi, ndiyo iliyokuwa ngome kubwa ya Marekani nchini Iran lakini Mapinduzi ya Kiislamu yameng'oa mizizi ya utawala wa kifalme na wa watu binafsi na mahala pake umejenga ngome madhubuti inayojulikana kwa jina la utawala wa wananchi wote.
Aidha amesema, kujenga hofu ya kuyaogopa madola makubwa hususan Marekani ni ngome nyingine iliyoandaliwa na mfumo wa kibeberu na kuongeza kuwa: Tofauti na kipindi cha utawala wa taghuti, leo hii katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hakuna mtu yeyote ambaye ana utambuzi wa mambo, mweledi na aliyeshikamana na matukufu ya kidini, anayeiogopa Marekani.
Ayatullah Khamenei pia ameashiria kuwa, kuna uwezekano leo hii pia kukawa na watu ambao bado wanaiogopa Marekani na kuongeza kuwa: Taghuti hakuwa na njia nyingine ila kuiogopa Marekani kwani hakuwa na kitu cha kumuunga mkono, lakini katika Jamhuri ya Kiislamu, kuiogopa Marekani ni jambo lisiloingia akilini kwani Jamhuri ya Kiislamu ina uungaji mkono wa taifa kubwa la Iran.
Vilevile amesema, njia nyingine inayotumiwa na dola la kibeberu la Marekani ni kupandikiza tabia ya kutojiamini na kuondoa sifa ya kujiamini kitaifa. Ameongeza kuwa: Kwa kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu, ngome hiyo iliyokuwa inakubali kuburuzwa na mabeberu imebadilishwa kuwa ngome kubwa na madhubuti ya "sisi wenyewe tunaweza."
Ayatullah Khamenei amelitaja suala la kuitenganisha dini na siasa kuwa ni ngome nyingine ya maadui ya kutaka kufanikishia ubeberu wao nchini Iran na kuongeza kuwa: Mapinduzi ya Kiislamu yamefanikiwa pia kuvunja ngome hiyo.
Kiongozi Maudhamu wa Maipnduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kusema kuwa, lengo na makusudio yake yaliyo wazi wakati anaposema adui ni Marekani na kuongeza kuwa: Wanasiasa wa Marekani na Wizara ya Hazina ya nchi hiyo kwa upande mmoja wamehifadhi vikwazo vya nchi hiyo kwa ujanja mkubwa na hawako tayari kuviondoa na wanatumia mbinu tata sana za kuonesha waziwazi uadui wao kwa kuzungumzia mara kwa mara kuendeleza vikwazo dhidi ya Iran na kwa upande wa pili wanatandika kitanga cha Sini Saba (kitanga cha vitu saba vinavyoanzia na sin kinachotumika wakati wa sherehe za Nairuzi za mwaka mpya wa Kiirani wa Hijria Shamsia) na wanafanya udanganyifu wa kitoto kutoa ujumbe wa baraka na fanaka za Nairuzi ili kujionesha hawana uadui na taifa letu kama njia ya kuwapumbaza vijana wetu. 
Vilevile amesema: Sababu ya kuweko miamala hiyo ya kindumilakuwili ni kwamba viongozi wa Marekani hadi leo hii wameshindwa kulielewa taifa lililo macho la Iran na wanashindwa kujua kuwa taifa hili erevu linazitambua vyema njama za siri za maadui.
Baada ya hapo Ayatullah Khamenei amesema kuwa: Sisi hatuna tatizo na wananchi wa Marekani kama ambavyo hatuna tatizo pia na wananchi wa mataifa mengine yote, bali tunachofanya sisi ni kupambana na siasa za kiuadui za nchi hiyo. Baada ya hapo amebainisha mambo mbalimbali ambayo iwapo yatazingatiwa, basi yataonesha njia sahihi ya kupitia harakati ya maendeleo ya kiuchumi ya Iran.
Rasilimali na uzoefu mkubwa na wa kila aina wa kiasili na wa kibinadamu kwa ajili ya maendeleo makubwa mno ya kujizalisha yenyewe, fursa mbalimbali za kimataifa, nguvu zenye taathira katika eneo na katika baadhi ya mambo kwenye uga wa kimataifa pia, ni jambo la kwanza lililoashriwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika upande huo.
Vilevile ameutaja uadui wa wazi wa Marekani kwa taifa la Iran na kwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kuwa ni suala jingine ambalo linadhihirisha wazi uadui wa Marekani kwa taifa na kwamba vitisho vya mara kwa mara vya Wamarekani, njama zao zisizosita za kujaribu kuzuia kufaidika Iran na matunda ya makubaliano ya nyuklia yanayojulikana kwa jina la JCPOA ni mifano ya wazi ya kuthibitisha uhakika huo.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa, katika wakati huu ambapo imebakia miezi michache tu hadi kufanyika uchaguzi wa rais nchini Marekani, wagombea wa uchaguzi kila mmoja anashindana na mwenzake katika kuisema vibaya Iran kama ambavyo hakuna dhamana yoyote kuwa, serikali ijayo huko Marekani itaheshimu hata hizi ahadi chache walizozitoa kupitia JCPOA, na pamoja na hayo utaona kuna baadhi ya watu nchini wanakereka na kuudhika kila mtu anapozungumzia uadui wa Marekani dhidi ya taifa letu.
Jambo la tatu lililogusiwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika uwanja huo ni kutokuwa na kikomo mbinu za uadui wa Marekani dhidi ya taifa la Iran.
Amekumbusha kwa kusema: Wamarekani wanatumia mbinu tatu kuu na zenye taathira katika kuendeshea uadui wao dhidi ya Iran: propaganda, kujipenyeza na vikwazo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo zaidi suala la vikwazo kwa kusema: Uhakika wa mambo ni kuwa, adui anahisi kuwa vikwazo vinasaidia katika kutoa pigo kwa Iran, tab'an miamala na mienendo yetu nayo imechangia na kum nguvu ya adui ya kuwa na hisia kama hizo.
Ayatullah Khamenei ameendelea kusema: Kuna wakati fulani baadhi ya watu hapa ndani ya nchi walikuwa wanayakuza sana madhara na matatizo yatokanayo na vikwazo kama ambavyo katika kipindi fulani pia zimekuzwa kupindukia athari za kuondolewa vikwazo hivyo, wakati ambapo hadi hivi sasa hakuna lolote lililotokea kwenye uwanja huo na kama hali itaendelea hivi hivi, basi hakuna lolote la maana litakalotokea katika siku za usoni.
Baada ya kutoa uthibitisho kuhusu sehemu hasa inayolengwa na adui katika kadhia ya vikwazo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameuliza swali moja la kimsingi akisema: Sasa njia sahihi ya kukabiliana na wenzo huu wa mashinikizo na uadui ni ipi? 
Amejibu swali hilo kwa kuashiria tena njia mbili za uongo ambazo Wamarekani wanazionesha kujibu swali hilo yaani ama kusalimu amri mbele ya mabeberu au kukubali kuwa katika vikwazo na mashinikizo na kuongeza kuwa: Kuna njia mbili za kweli na zisizo za uongo katika uwanja huu nazo ni kwamba ama tukae tu na kuvumilia matatizo yanayosababishwa na vikwazo bila ya kuchukua hatua yoyote, au tusimame kidete juu ya uchumi ngangari ili tuweze kuyashinda matatizo hayo.
Baada ya hapo, Ayatullah Khamenei amejikita katika kuelezea maana ya nara na kaulimbiu ya mwaka huu wa Kiirani wa 1395 Hijria Shamsia yaani kaumlimbiu ya "Uchumi Ngangari, Hatua na Vitendo" na kusema: Baadhi ya kazi muhimu zimefanywa na serikali kama vile kuunda kamati kuu ya kusimamia na kuendeleza uchumi ngangari na kumepatikana matunda mazuri kama vile kuingia katika mkondo chanya masuala ya biashara na kupunguza uagiziaji wa bidhaa kutoka nje lakini kuna wajibu wa kufanyika kazi nyingine za kimsingi katika uga huo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea na hotuba yake kwa kusisitizia udharura wa kujulikana wazi na kuchorwa muongozo maalumu wa kufanikisha uchumi huo na pia ametoa mapendekezo kumi ya kimsingi kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kivitendo kwa ajilli ya kufanikisha uchumi wa kimuqawama.
Kuhusu pendekezo lake la kwanza amesema kuwa ni kuchunguza na kugundua pamoja na kujikita katika kazi na michakato yenye faida, ya kiuchumi, ili kwa njia hiyo kuweze kupatikana njia nyingine nyingi za kutia nguvu na kustawisha uchumi nchini.
Kuhuisha na kuufanya amilifu uzalishaji wa bidhaa za ndani ya nchi, ni pendekezo la pili la kimsingi la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa viongozi nchini Iran kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kividendo za kufanikisha mchakato wa uchumi usioyumba wa kimuqawama. 
Ameongeza kuwa: Baadhi ya ripoti zinaonesha kuwa, asilimia 60 ya suhula za uzalishaji wa ndani ya nchi ima hazitumiki kabisa au zinatumika chini ya kiwango cha uwezo wake. Hivyo Serikali inaweza kufufua uzalishaji wa ndani kwa kusikiliza maoni mbalimbali yakiwemo ya wataalamu na wanauchumi welewa wa mambo na wakosoaji.
Kujiepusha kikamilifu na kununua bidhaa za nje ambazo zinadhoofisha nguvu za uzalishaji wa ndani pamoja na kuhakikisha kunakuwa na usimamiaji makini wa fedha na vyanzo vya kifedha ambavyo vinaingia nchini Iran kutokea nje ya nchi ni mapendekezo mengine mawili muhimu yaliyotolewa na Ayatullah Khamenei kwa maafisa na viongozi watendaji nchini.
Ameongeza kusema kuwa: Hadi leo hii fedha za Iran hazijafika nchini kutokana na uafiriti wa Wamarekani na kutokana na baadhi ya mambo mengine, lakini pamoja na hayo inabidi kuwa macho na kuhakikisha kuwa vyanzo hivyo vya fedha havitumiki kwa fujo na israfu au kununuliwa vitu visivyo vya lazima.
Pendekezo la tano la Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kivitendo na viongozi nchini ni kuhakikisha kuwa elimu ya kimsingi inakuwa sehemu muhimu ya uchumi usioyumba. 
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Vipaji vya Kiirani ambavyo vina uwezo wa kutengeneza kombora lenye uwezo wa kupiga shabaha iliyoko umbali wa kilomita elfu mbili kwa kukosea mita chache tu kwenye nukta hasa iliyokusudiwa, bila ya shaka yoyote vinaweza kutumiwa katika sekta nyinginezo muhimu kama vile za mafuta na gesi na uzalishaji wa injini za magari, ndege na treni; kuleta ubunifu wa aina yake hivyo Serikali inapaswa kuandaa mazingira mazuri ya kufanyika mambo hayo.
Kustafidi vizuri na sekta ambazo huko nyuma zilitengenezewa uwekezaji mkubwa kama vile sekta za petrokemikali na ujenzi wa vinu mbali mbali na vilevile kuhakikisha kwamba sharti la miamala yote ya kigeni liwe ni kuhamishia teknolojia ya miamala hiyo ndani ya Iran, ni mapendekezo ya sita na saba yaliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya maendeleo na uimarishaji wa uchumi nchini.
Vilevile amelaumu makelele ya kisiasa na kimagazeti yanayotolewa kuhusiana na "ufisadi" na kuongeza kuwa: Pendekezo langu la nane kuhusiana na hatua na vitendo vya kufanikisha uchumi ngangari ni kupambana vilivyo na kwa nguvu zote na ufisadi hususan vitendo kama vya magendo ambavyo vinatoa pigo kubwa kwa uchumi wa nchi.
Kuongeza kiwango cha kustafidi vizuri na nishati suala ambalo katika baadhi ya mwahala linaweza kupelekea kuokolewa mamia ya mabilioni ya fedha na vile vile kuvipa mazingatio maalumu na kuvisaidia viwanda vidogo vidogo na vya daraja ya kati kwa ajili ya kuzalisha nafasi za kazi na kuleta harakati ya kiuchumi, ni mapendekezo ya mwisho kati ya mapendekezo kumi yaliyotolewa na Ayatullah Khamenei kwa viongozi na maafisa watendaji nchini kwa ajili ya kufanikisha nara na kaulimbiu ya mwaka huu wa Kiirani yaani shaari ya "Uchumi Ngangari, Hatua na Vitendo."
Ameongeza kusema kuwa: Kuna na kazi nyingine ambazo zinaweza kufanyika katika uwanja huo, lakini kama mambo haya kumi yatafanyiwa kazi, basi kutashuhudiwa harakati kubwa ya kimapinduzi na ya kimaendeleo ambayo itauwekea kinga nzuri uchumi wa Iran na kupunguza kikamilifu athari mbaya za vikwazo na mashinikizo ya kiuchumi ya maadui.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa: Iwapo harakati hii ya kimantiki na kimapinduzi itatekelezwa ipasavyo, basi hakutakuwa na mtu tena atakayetetereshwa na vikwazo na hakutakuwa na haja tena ya kuachana au kulegeza kambi katika misingi, usuli, matukufu na mistari myekundu kwa hofu ya vikwazo na mashinikizo ya Marekani.
Ayatullah Khamenei Khamenei amegusia pia udharura wa kuweko msaada wa wananchi, wataalamu wa kisiasa na kiuchumi kwa Serikali sambamba na kuweko ushirikiano, uratibu na fikra za pamoja baina ya mihimili mitatu mikuu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama) na kuongeza kuwa: Ni matumaini yetu - chini ya kivuli cha hatua na vitendo kwa ajili ya kufanikisha uchumi ngangari- serikali itaweza, ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, kufufua maelfu ya viwanda na karakana na za uzalishaji bidhaa na za kilimo; na wananchi watahisi na kushuhudia kwa macho yao uhuishaji huo, na hatimaye watazidi kupata imani na utulivu moyoni. 
Vilevile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la kutekeleza mambo kivitendo na kimapinduzi kuwa ni jambo lilioloandaa mazingira ya kupatikana mafanikio ya kila namna katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita nchini Iran. Aidha amesisitizia tena udharura wa kuenziwa na kupewa heshima kubwa nguvukazi za kimapinduzi na za watu walioshikamana vizuri na mafundisho ya dini na kuongeza kuwa: Matunda yaliyoletwa na wasomi na wanasayansi wa nyuklia wa Iran waliouawa shahidi, mafanikio ya shahid Tehrani katika suala la makombora, mafanikio ya Kazemi katika fani ya seli shina na shahid Avini na marehemu Salahshour katika masuala ya utamaduni ni mambo ambayo yanaonesha ni namna gani moyo na fikra ya kimapinduzi inavyoweza kutatua matatizo mengi na kuleta mafanikio makubwa. 
Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, masuala ya kiutamaduni yana umuhimu mkubwa na kuongeza kwamba: Kwa mara nyingine ninawasisitizia viongozi nchini kuzisaidia na kuziunga mkono majimui za wananchi zinazojitolea zenyewe katika kona mbali mbali za nchi kufanya kazi za kiutamaduni.
Ameongeza kuwa: Majimui hizo zinapaswa kuongezeka na kunawiri siku baada ya siku na kwa upande wa taasisi za kiutamaduni pia, badala ya kuwakumbatia watu ambao hawaukubali Uislamu, wala Mapinduzi ya Kiislamu na wala matukufu ya mapinduzi hayo, ziwaunge mkono watu wenye imani thabiti za Kiislamu na wenye fikra za kimapinduzi na za kushikamana vilivyo na dini.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aidha amewalenga katika hotuba yake hiyo vijana wa Iran akiwaambia: Nchi na mustakbali wa leo na kesho ni wenu vijana, na iwapo mtaingia katika medani kwa kujipamba kwa imani thabiti na kujiamini na kufanya harakati kwa kuwa na silaha kama hizo, basi kuweni na yakini kuwa Marekani na anayemzidi Mmarekani hawezi kufanya ghalati wala upuuzi wowote.
Vilevile amegusia msiba wa kufariki dunia aalimu mpigana jihadi, mwanaharakati na mtumishi wa Haram tukufu ya Imam Ridha AS na ambaye alikuwa akifanya kazi zake kwa ikhlasi, marehemu Ayatullah Vaiz Tabasi na kusema kuwa, kumpoteza mwanachuoni huyo mkubwa mwanaharakati na mwanamapinduzi, ni pigo kubwa sana.
 

700 /