Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Hotuba ya Kiongozi katika hadhara ya watu wa Najaf Abad

Hotuba ya Kiongozi katika hadhara ya watu wa Najaf Abad
Bismillahir Rahmanir Rahim (1)
Hamdu zote zinamstahikia Mwenyezi Mungu Mola wa walimwengu na salamu na swala zimwendee Bwana wetu Muhammad na Aali zake watoharifu na laana ya Mwenyezi Mungu iwe juu ya maadui wao wote.
Nikakukaribisheni nyote ndugu na dada wapendwa wa Najaf Abad ambao kwa hakika na kwa kusema ukweli mmekuwa na mngali ni mfano wa wanaume na wanawake wa kimapinduzi, waumini na wa kujitolea katika vipindi vyote vya Mapinduzi. Na hasa familia tukufu za mashahidi na wanazuoni waheshimiwa pamoja na matabaka mbalimbali ya wapendwa. Mimi ninakisadikisha na kukiunga mkono kile ambacho kimesemwa Bwana Hasanati kuhusiana na Najaf Abad. Mimi pia kwa hakika ninashuhudia kwamba watu wa Najaf Abad wana sifa na mambo ambayo wanayashindia maeneo mengine mengi ya nchi. Katika kujitolea kwao na rekodi yao ya Mapinduzi katika kipindi ambacho mapambano na harakati za Kiislamu zilikuwa hazijulikani vyema. Najaf Abad ilikuwa ni sehemu ya kukuzwa na kuimarishwa kwa fikra za mapambano hayo. Mimi katika kipindi hicho – miaka ya kabla ya Mapinduzi – nilikuja na kuiona Najaf Abad kwa karibu. Nilishuhudia hamu kubwa ya watu, kudiriki kwao mambo, mahudhurio na kufahamu kwao masuala ya Mapinduzi; matabaka yote ya wananchi, na sio tabaka la vijana au wanafikra wa zama hizo tu. Mtu alipokuwa akizungumza na baadhi ya wanavijiji na watu wa kawaida (kuhusu) masuala ya Mapinduzi alikuwa akiona kwamba wana uelewa, wanafahamu na wanazingatia. Mwenyezi Mungu awarehemu wale wote waliofanya jitihada na juhudi za kuwazindua watu kwenye njia hii.
Baada ya Mapinduzi kupata ushindi, bado Najaf Abad ilikuwa katika safu za mbele. Wameashiria jeshi la Najaf. Shihidi Kadhimi (2) na mashahidi wengine wa jeshi hilo; makamanda hawa wakweli, wazingatia dini, waaminifu, wenye bidii na wachapa kazi. Nilienda na kukitembelea kikosi hiki katika eneo la operesheni kwenye medani yenyewe ya vita – zaidi ya mara moja – huko mtu aliweza pia kushuhudia alama za sifa hizi zilizo wazi. Mlisimama, mkapambana, mlikuwa wakweli na kujitolea, mlitoa mashahidi, majeruhi; malipo yenu yako kwa Mweyezi  Mungu. Jina lenu linang’ara kwenye loho ya dhahabu ya historia ya Mapinduzi. Mnapasa kudumisha njia hii; bado hatujafika tunakokwenda; tunapasa kuendelea mbele. Bado tuapasa kujitahidi. Bado tuna wajibu wa kufanya Jihadi, medani zimebadilika lakini bado Jihadi ni  ileile. Iwapo tutafanikiwa kukikabidhi amana hii kizazi kijacho tutakuwa tumetekeleza jukumu letu. Alhamdulillah vijana wenu wanafanya kazi, wanajitahidi, wako macho na nchi pia ni ya vijana. Tunatumai Inshallah, Mweyezi Mungu Mtukufu atakulindieni baraka za mashahidi, wazee na wanazuoni wenu wakubwa ambao mji huu umewakabidhi, iwe ni wale waliokuwa Najaf Abad, Esfahan, Mash’had au Qum. (Yaani) biasharanje ya elimu na mujahideen kutoka mji huu ulio na baraka nyingi, ili tupate kuona natija ya baraka hizi katika nchi nzima.
Hebu niashirie pia siku za maombolezo ya mpendwa wa Ahlul Beit, Fatima az-Zahra, Swadiqa at-Twahira (as) ambapo kwa mujibu wa riwaya ya siku 75, siku hizi ni siku za kuuawa shahidi mtukufu huyo. Huku akiwa na moyo uliojaa huzuni na kifua kilichojaa simanzi Amir al-Mumineen katika siku hizi aliagana na mpendwa wake na kumrejeshea Mtume Mtukufu amana hiyo yenye thamani kubwa. Licha ya kuwa moyo wake ulikuwa umejaa huzuni lakini jambo hilo halikumpunguzia hata kidogo irada na azma yake. Hili ni somo kwangu na kwenu nyinyi. Baadhi ya wakati moyo hujaa huzuni – kutokana na masuala kama haya katika maisha ya mwanadamu; yawe ni maisha ya mtu binafsi au ya kijamii – lakini azma na irada zinapasa kuwa imara. Hatua muhimu zinapaswa kuchukuliwa; kuna huzuni ambazo huvunja milima (lakini) haziwezi kumvunja mtu aliye na imani thabiti; njia inapasa kudumishwa.
Kutokana na kuwa tunakaribia uchaguzi na uchaguzi ambao ni muhimu sana, ningependa kuzungumzia hapa nukta kadhaa kuhusiana na suala hili.
Nukta ya kwanza ni umuhimu wa uchaguzi huu wenyewe. Hii haina maana kwamba twende kwenye sanduku la kupigia kura na kutumbukiza kwenye sandugu karatasi iliyo na jina la mtu au watu fulani. Suala ni hili kwamba uchaguzi katika nchi yetu una maana ya kuimarishwa utukufu wa kitaifa. Kupitia uchaguzi wananchi huweka vifua vyao mkabala na adui kama ngao na kumtunishia misuli. Huu ndio umuhimu wa uchaguzi. Wakati adui anapoona kwamba hata baada ya kupita miaka 37 na pamoja na kuwepo kwa mashinikizo haya yote, vikwazo hivi vya kidhalimu, propaganda hizi zote chafu na za ukorofi, hajafanikiwa kuwazuia wananchi kuubai mfumo (wa Kiislamu), hapo ndipo ukubwa wa Mapinduzi haya unapopata umuhimu machoni pake na taifa la Iran pamoja na Mapinduzi yake kupata utukufu; huu ndio uchaguzi. Uchaguzi una maana ya kulindwa izza ya kitaifa na kujitawala kwa taifa pamoja na mapambano ya taifa la Iran. Tazameni, hivi sasa Bwana Hassanati amezungumzia kujitolea na mapambano ya watu wa Najaf Abad; nyinyi mumehisi fahari nyoyoni mwenu na mimi pia. Wakati kundi fulani linapojitolea na mapambano, nguvu, azma na irada yake kudhihiri, kila mtazamani na msikilizaji hijifaharisha na suala hilo. Uchaguzi ni kuonyesha kujitolea kwa taifa ka Iran. Taifa la karibu watu milioni themanini hutangaza kuwepo kwake kwenye medani hii iliyojaa maadui, mabomu ya kutegwa ardhini, medani ya makabiliano na mapambano ya uovu na ukorofi kwa namna hii ya ushujaa na ujasiri; huu ndio uchaguzi. Tazameni jinsi ilivyokuwa na umuhimu! Kila mtu anayezingatia utukufu wa Iran ya Kiislamu, ni lazima ashiriki kwenye uchaguzi huu na bila shaka atashiriki. Inshallah mtaona, siku ya Ijumaa dunia itaona jinsi watu wa Iran watakavyokuwa wakielekea kwa hamu kubwa kutekeleza majukumu yao na kuthibitisha haki  - ambapo ni jukumu na pia haki -  kwa mtazamo wangu hii ndiyo nukta muhimu zaidi ambayo inapaswa kuzungumziwa kuhusiana na suala la uchaguzi na mimi nimekuwa nikilikariri na ninalikariri tena; huu ndio msingi wa uchaguzi.
Nukta ya pili ni kwamba sisi taifa la Iran kama ambavyo tunazingatia na kuujali uchaguzi huu kama zilivyokuwa chaguzi nyingine zote katika kipindi cha miaka 37 iliyopita, ndivyo maadui zetu pia wanavyozingatia na kuufuatilia kwa karibu. Kwa kutumia visingizio tofauti wanataka kuukosoa uchaguzi huu; kwa kutumia kila aina ya visingizo. Wakati fulani walijaribu kusema kuwa uchaguzi ni uongo; asilani hakuna uchaguzi unaofanyika nchini Iran. Ambapo tunaona kinyume chake uchaguzi ulifanyika mbele ya macho ya wote. Kampeni za uchaguzi katika miaka hiyo ya mwanzo zilikuwa hivihivi. Wakati mwingine walitumia propaganda za wazi na kuwataka wananchi wasiende kupiga kura. Hata katika kipindi fulani cha uchaguzi, zikiwa zimebaki siku mbili tatu hivi kabla ya kufanyika uchaguzi huo, rais wa Marekani alihutubia taifa la Iran kwa kusema, msiende kupiga kura! Lakini badala yake wananchi walifanya nini? Walifanya kinyume. Katika kipindi hicho walishiriki kwa wingi kwenye uchaguzi kuliko wakati mwingine wowote. Hii ilikuwa mbinu ambapo walitumia hila na propaganda tofauti kujaribu kuwazuia watu wasiende kupiga kura. Mbinu nyingine waliyotumia ni kujaribu kuwakinaisha watu kwamba kura yao haikuwa na faida yoyote; nyinyi mnaandika jina la Zeid lakini ni jina la Amru ndilo linalotokea. Walikuwa wakiyasema haya; mnakumbuka; huenda vijana wasiyakumbuke haya kwa kuwa hawakuwepo siku hizo. Lakini wengi wangali wanayakumbuka. Walikuwa wakibuni na kuyasema haya kama nara na kwa masikitiko baadhi ya watu walioghafilika ndani ya nchi walikuwa wakishirikiana nao kwa kuyakariri hayohayo kwa muda fulani. Hayo yote hayakuwafaa. Mbinu hizo hazikuwakatisha watu tamaa. Mbinu hizo hazikuweza kuathiri uelewa na kudiri watu umuhimu wa suala hilo. Hivi sasa wanajaribu kutumia njia nyinginezo. Ni wazi kuwa viongozi wa serikali ya Marekani sasa wametambua kupitia uzoefu kwamba wanapasa kunyamaza kimya kwa sababu kila wanapozungumza ndivyo watu hufanya kinyume na matakwa yao. Kwa hivyo mara hii wamenyamaza kimya. Viongozi wa Marekani wamenyamaza. Hawasemi lolote kwa kuhofia hueda maneno yao yakawafanya watu kufanya kinyume na wanavyotaka wao. Ama wale wanaofanya kazi kwa niaba ya uistikbari  na wameenda huko kulipwa na serikali za Marekani na Uingereza, wanajishughulisha; kwenye redio, vyombo tofauti vya upashaji habari, mitandao na intaneti na mfano wa haya. Wanashughulika usiku na mchana. Moja ya shughuli zao ni kutangaza kura ya maoni bandia na kufikia natija kwa msingi wa kura bandia hiyo kwa kudai kuwa watu hawana tena hamu na uchaguzi.
Mbinu nyingine ambayo wamejifunza hivi karibuni na kuitekeleza ni kubuni kambi mbili bandia, kambi mbili za uongo. Nukta hii ni muhimu sana. Ndugu na dada zangu wapendwa nitazungumzia kwa urefu kidogo nukta hii: Kambi mbili bandia.
Sawa, uchaguzi ni mashindano. Ni wazi kuwa kwenye mashindano kila mtu hufanya juhudi za kushinda. Kila mtu hujitahidi kuwa mbele. Kawaida ya mashindano ni harakati, msisimuko, kukimbia na mambo kama hayo. Uchaguzi ni mashindano; mtu mmoja huwa mbele na mwingine kubakia nyuma. Huu si uadui wala kuwepo kambi mbili. Kwenye redio, televisheni na vyombo vyao tofauti vya habari daima huzungumzia kugawanyika kwa taifa la Iran katika kambi mbili – yaani kambi mbili zinazohasimiana. Nam, katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuna aina fulani ya kambi mbili ambapo moja ni ya Mapinduzi ni nyingine ya uistikbari. Wale ambao ni masalio ya kipindi cha uistikbari na kila mtu anayewafuata na kushirikiana nao kifikra, nam, hawa wanachukia Mapinduzi. Kuna aina hii ya kambi mbili lakini wananchi waliowengi wa Iran ni wanamapinduzi wanaounga mkono Mfumo wa Kiislamu na wanampenda Imam na kumbukumbu zake.  (Hata) wale ambao hawakuwahi kumuona Imam hata mara moja na walizaliwa baada ya Imam kuaga dunia lakini wanavutiwa na maneno, sauti, nasaha na misingi ambayo iliasisiwa na Imam. Sehemu kubwa ya wananchi wa Iran wanavutiwa na mambo haya. Nam, kuna aina fulani ya ukambi mbili (baina) ya watu wanaompenda Imam na Mapinduzi na wale wasiokubali kabisa Mapinduzi na Mfumo. Ni wazi kuwa kambi mbili huwa hivi. Bila shaka, mimi niliwaambia hata wale ambao hawakubali Mfumo; Si mnaikubali Iran; (basi) njooni kwa ajili ya heshima ya Iran. Sasa baadhi yao husikia na wengine kupuuza.
Sasa wanazungumzia kuwepo kambi mbili katika uchaguzi huu, asili ya suala hilo liko huko. Suala hili mara nyingine hukaririwa hapa, lakini watu wanaoelewa propaganda za wageni husikiliza na kuelewa kuwa suala hili ni lao (wageni). Kambi mbili za bunge linalounga mkono serikali na linaloipinga kana kwamba nchini Iran kuna kundi moja linalopendelea bunge linalounga mkono serikali na jingie linalopendelea bunge lililo dhidi ya serikali. Hapana, taifa la Iran halitaki bunge linalopendelea serikali wala linaloipinga bali linataka bunge ambalo linafahamu vyema majukumu yake; linalotambua wadhifa wake kwa msingi wa katiba, linalowajibika, lenye kuzingatia dini, shujaa, lisilotishwa na Marekani, linalozingatia maendeleo halisi ya nchi, linalotambua kwamba maendeleo halisi ya nchi yanapatikana katika kuwalea kielimu vijana walio na vipawa wa nchi na taifa hili. Wanataka bunge kama hili ambalo litaelewa machungu ya watu na ya nchi na kufanya juhudi za kuyatibu na kuyatatua – huu dio utungaji sheria – watu wanataka bunge kama hili. Majlisi (bunge) ya serikali na isiyo ya serikali yaani nini! Hizi ni kambi mbili bandia. Mpigieni simu kila raia wa Iran na mumuulize, je, unataka bunge ambalo linafahamu machungu na matatizo ya nchi na wananchi na kufanya juhudi za kuyatatua au bunge linalomuunga mkono Zeid na Amru, halafu muone majibu yao yatakuwa yapi? Ni wazi kuwa wananchi watachagua chaguo la kwanza. Hili ni muhimu kwa wananchi; bunge linalozingatia dini, linalowajibika, shujaa lisilohadaika na hadaa ya adui, bunge linalotoa umuhimu kwa heshima na kujitawala kwa taifa na kutokanyaga izza ya taifa. Kutokanyaga kujitawala kwa taifa na; kusimama imara mbele ya tamaa na uchochezi wa uistikbari, mbele ya tamaa ya madola makubwa ambayo mikono yao imekatwa nchini Iran na yanafanya juhudi za kurejea na kudhibiti tena uendeshaji wa nchi hii. Bunge la aina hii. Tulizungumzia suala la uchumi unaotokana na vyanzo vya ndani ya nchi. Wananchi wanataka bunge ambalo litaainisha muda wa kujadili uchumi unaotokana na vyanzo vya ndani kwa maana yake halisi. Litengeneze njia na serikali kulazimika kuifuata njia hiyo. Haya ndiyo mambo wanayoyataka wananchi.
Nukta nyingine ni hii kwamba niliposema siku chache zilizopita kwamba kuweni macho dhidi ya ya wapenyaji, baadhi ya watu walikasirika bila ya sababu yoyote; hakuna haja ya kukasirika. Wamarekani walikuwa na njama ya kutekeleza baada ya mazungumzo ya nyuklia kwa ajili ya ndani ya Iran na eneo. Hili lilikuwa wazi kwetu na limebainika wazi. Walikuwa na njama dhidi ya Iran na bado wana njama hiyo. Walikuwa na njama dhidi ya eneo, bado wana njama hiyo na wanafanya juhudi. Wanajua ni nani aliyesimama imara mbele ya malengo yao maovu katika eneo; wanalijua hili na wanafahamu. Nam, wakati adui ana mpango kwa ajili ya ndani ya nchi, hufanya nini? Humtumia mpenyaji (kibaraka). Maana ya mpenyaji, haina maana kwamba bila shaka ameenda na kuchukua pesa na kisha kurejea na kupenya kwenye idara fulani na pia awe anafahamu anachokifanya; la hasha. Mara nyingine mpenyaji huwa ni mpenyaji asiyejijua! Imam (MA) alisema baadhi ya wakati maneno ya adui husikika kwa hatua kadhaa kupitia watu wanaoelewa mambo. Imam alikuwa macho na mwenye uzoefu. Adui anapotaka kusema au kutaka jambo, hutumia njia mbalimbali na kupitia hatua kadhaa ili maneno hayo yasemwe na mtu fulani anayeelewa mambo, mtu ambaye huenda hajachukua pesa au kutoa ahadi yoyote kwa adui huyo. Je, hatujayaona mambo haya? Je, kwani hatuna uzoefu nayo? Je, hatukuona katika Majlisi hiihii ya Ushauri ya Kiislamu mbunge akiutuhumu Mfumo kuwa unasema uongo! Alisema kwa muda wa miaka 10 au 13 sasa tunaidanganya dunia. Kwenye mimbari ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (bunge)! Katika mimbari hii ya umma. Sawa, huyu anazungumza maneno ya adui; adui alikuwa akitwambia, ‘nyinyi mnasema uongo!’ Sasa mmoja wetu anajitokeza na kusema Mfumo unasema uongo! Je, huyu si mpenyaji? Mara nyigine huwa hana habari na hafahamu. Tulikuwa na Majlisi ambayo wakati ambapo mazungumzo magumu ya nyuklia yalikuwa yamepamba moto na katika kipindi ambacho rais wetu mpendwa wa hivi sasa alikuwa ndiye mkuu wa timu ya mazungumzo hayo, na akifanya juhudi kubwa na kupitia usumbufu mwingi katika kuijadiliana na upande wa pili, kwa hakika alikuwa akifanya mapambano ili kufanikisha msimamo wa Iran, wabunge waliwasilisha mswada wa dharura bungeni kwa ajili ya kufanikisha msimamo wa adui! Wakati huo mkuu wa timu ya mazungumzo ambaye ni rais wetu hivi sasa, alilalamikia jambo hilo na kusema, sisi tunapambana huko na hapa hawa mabwana wanatayarisha mswada kwa mslahi ya adui. Nam, huu ni upenyaji. Haya ni nini? Kwani upenyaji una pembe na mkia, ambapo neno upenyaji linapotajwa baadhi ya watu hukasirika na kusema, Bwana! Umesema upenyaji, upenyaji? Nam tunapasa kuwa macho. Kwa hivyo adui anafikiria njia za kupenya; ni nani anayepasa kuwa macho? Wananchi wanapasa kuwa waangalifu  na pia viongozi, wanasiasa na shakhsia wa kisiasa, hawa ndio wanaopasa kuwa waangalifu zaidi. Wawe waangalifu wasije wakafanya kitu ambacho adui anakitaka. Wakati wanapoona kwamba adui anasema mambo ambayo yanalenga kuwagawanya watu, kwa mfano kukusifu, huyu anataka kuzua shaka. Ni wazi kuwa adui si rafiki yako. Unapoona kwamba adui anatumia mbinu hii dhihirisha chuki na kujitenga naye bila kusita, (na) mwambie sihitaji unisifu. Si unasema kuwa kwa maneno haya adui anataka mfarakano, basi usiruhusu shaka ienee kwenye fikra za watu. Tunapasa kuzingatia mambo haya. Tunayarejea maneno ya Imam. Imam alikuwa akisema kuwa adui anapokusifu, basi tilia shaka tabia na mwenendo wake na jirejee ili upate kufahamu ulikosea wapi hata adui akafurahishwa na jambo hilo na kuanza kukusifu. Hii ndiyo sera ya Mapinduzi. Tunapasa kuwa hivi, tunapasa kusonga mbele hivi na wala hatupasi kughafilika. Kuendesha nchi si jambo rahisi. Kuongoza taifa kubwa, tukufu na shupavu kama hili si jambo dogo; kwa hivyo tunapasa kuwa waangalifu. Tunapasa kusonga mbele tukiwa macho wazi na kukabiliana na adui kwa azma thabiti. Nukta hii niliyoizungumzia pia ni muhimu.
Nukta nyingine ni kwamba tusitumie fasihi ya kisiasana inayotumiwa na maadui. Mimi ninasisitiza suala hili kwa ndugu zangu wapendwa na waheshimiwa wanaohudumu katika nyadhifa mbalimbali za kisiasa, za serikali na zisizo za serikali na nyadhifa nyingine mfano wa hizi. Tusitumie fasihi ya maadui. Tokea siku ya kwanza maadui wa Mapinduzi ya Kiislamu walianza kutumia ibara za misimamo mikali na ya wastani wakidai, fulani ni mwenye misimamo mikali, fulani ni wa mrengo wa misimamo mikali na fulani ni wa mrengo wa misimamo ya wastani. Siku hiyo mtu aliyekuwa na misimamo mikali zaidi kuliko watu wengine kwa mtazamo wao, alikuwa ni Imam mpendwa;  na leo pia mtu aliye na misimamo mikali zaidi katika mtazamo wao ni huyu mtumishi dhalili (mimi). Misimamo ya wastani ni neno zuri, lakini Uislamu hausemi hivi (kama wanavyosema wao); tuyaelewe vyema maarifa ya Kiislamu. Uislamu unaunga mkono misimamo ya wastani na ya kati kwa kati: Na vivyo hivyo tumekufanyeni muwe umma wa wastani3, lakini nini maana ya wastani katika Uislamu? Je, neno hili liko mkabala na msimamo mkali? La hasha, bali wastani ni mkabala na upotovu: Kulia na kushoto ni njia za upotovu, na njia ya kati ndio njia ya sawa4. Hii ni Nahjul Balagha. Njia ya wastani yaani ni njia nyoofu. Iwapo njia ya sawa itapinda sana na kutochukua mkondo wa njia hiyo nyoofu - iwe ni upande huu au ule – basi hiyo haitakuwa tena njia ya wastani. Kwa hivyo mkabala na msimamo wa wastani sio msimamo mkali bali ni upotovu. Hawi mwenye msimamo wa wastani mtu aliyepotoka na kuacha njia ya sawa; lakini kwenye njia kunao wanaoenda kwa kasi na wengine kwenda taratibu. Kwenda haraka kwenye njia nyoofu si jambo baya; Kimbilieni maghufira ya Mola wenu5 endeni mbele. Leo wale ambao wanasema, wenye misimamo mikali, wakiwa nje ya nchi wana makusudio na maana maalumu wanayofuatilia. Marafiki na ndugu zetu walio ndani ya nchi wawe waangalifu wasije wakakariri yale yanayokusudiwa na watu hao. Wale wanaosema wenye misimamo mikali, makusudio yao ni wale watu waliosimama imara na kuwa na azma thabiti zaidi katika njia ya Mapinduzi. Wanawatuhumu Mahizbullah kuwa ni wenye misimamo mikali na kuwaita wanaosalimu amri mbele yao (maadui) kuwa ni wenye misimamo ya wastani. Katika fasihi ya kisiasa ya Marekani na Uingereza na mfano wao, maana ya misimamo mikali na ya wastani ni kwamba, walio na misimamo mikali ni wale wanaofungamana na Mapinduzi na wenye misimamo ya wastani ni wale wanaosalimu amri mbele ya matakwa yao. Sasa ni nani nayesalimu amri mbele yao? Kwa bahati nzuri wao wenyewe pia wanakiri na kusema kwamba nchini Iran hakuna watu walio na misimamo ya wastani; wote ni wenye misimamo mikali. Maneno haya ni sahihi. Katika taifa la Iran hakuna mtu anayeunga mkono kufungamana na watu hao (Wamagharibi). Mara nyingine, baadhi ya watu hughafilika, kuteleza na kufanya makosa, lakini kwa ujumla sehemu kubwa ya taifa la Iran inaunga mkono Mapinduzi, kuyafuata na kuyatetea kwa dhati. (Maadui) hawa huwaita watu hao kuwa ni wenye misiammo mikali. Ni kwa nini sisi tukariri maneno yao? Wanawaita Daesh pia kuwa ni wenye misimamo mikali; je, Daesh wana misimamo mikali? Daesh ni wapotovu, wamepotea na kuacha njia ya Uislamu, Qur’ani na njia nyoofu. Misimamo mikali haina maana hii. Watahadhari wasije wakakariri fasihi inayotumiwa na maadui kwa maana na malengo maalumu.
Nitazungumzia nukta nyingine ambayo itakuwa ya mwisho. Ndugu wapendwa, dada wapendwa, watoto wangu wapendwa, vijana! Kila mtakayemchagua mtakuwa mmejichagulia wenyewe. Chaguo lenu zuri litawarejea nyinyi wenyewe; iwapo mtafanya uchaguzi kwa kughafilika ni wazi kuwa ubaya na madhara yake yatakurejeeni nyinyi wenyewe. Hii ndiyo hali halisi ya mambo. Kwa kutilia maanani kwamba mnatekeleza jambo fulani kwa hiari na irada yenu wenyewe, jaribuni mtekeleze vyema jambo hilo. Iwapo mtatekeleza vyema jambo hili mtapata faida mbili: Ya kwanza ni kuwa Mwenyezi Mungu atakuridhieni kutokana na kuwa mmetekeleza vyema jukumu lenu na ya pili ni kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kufikiwa natija sahihi. Iwapo mtatekeleza jambo kwa tahadhari na uangalifu kuna uwezekano pia wa natija kutokuwa nzuri na ya kuridhisha lakini pamoja na hayo bado kuna yale malipo ya mwanzo. Wakati mnapotekeleza kazi kwa umakini na mwamko, Mweyezi Mungu huikubali kazi hiyo hata kama mtu atakuwa amefanya baadhi ya kasoro wakati wa kutekeleza kazi hiyo. Lakini kama utakuwa umefanya uzembe wakati wa kutekeleza kazi hiyo, Mwenyezi Mungu Mtukufu pia hataridhika na uwezekano wa kuwa sahihi kazi hiyo pia utapungua. Chagueni chaguo mnalotaka. Tambueni na kuchagua; tambueni. Jueni dini yao, uaminifu wao, mfungamano wao na Mapinduzi, ukakamavu wao kwenye njia ya Mapinduzi, azma na irada yao, ushujaa wao na kuhakikisha kwamba hawatishiki (na maadui). (Baada ya hapo) pigeni kura; iwe ni kwenye uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (bunge) au wa Baraza la Wanachuo Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi wa Mapinduzi, hakuna tofauti. Chaguzi mbili hizi zote ni muhimu, ambapo awali nilizungumzia umuhimu wa chaguzi mbili hizi. Hata kama hautakuwa unawafahamu (wagombea) usiseme mimi sitapiga kura kwa sababu siwafahamu, hapana, waendeeni wale mnaoamini kuwa wana habari za kutosha kuhusiana na dini, auminifu na mwamko wao. Waulizeni hao; hii ndiyo njia ya utatuzi wa suala hili. Kwa hivyo njia imebainika wazi, lengo liko wazi, wadhifa na jukumu liko wazi na kazi pia ni kubwa. Mtu anapotekeleza kazi kubwa ya Mwenyezi Mungu kwa njia sahihi, basi Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atakunusuruni6. Unapochukua hatua ya kumnusuru Mwenyezi Mungu bila shaka Mwenyezi Mungu Mtukufu naye atakunusuru. Katika hali hiyo, matokeo ya uchaguzi Inshaalah yatakuwa ni matokeo yatakayokuwa kwa manufaa ya nchi, yawe yatakavyokuwa. Jueni ya kwamba mimi nina imani thabiti kwamba licha ya juhudi zote zinazofanywa na adui – ambapo katika kipindi hiki cha miaka 37, adui daima amekuwa akifanya jitihada –za kutoa pigo dhidi ya Mapinduzi, lakini Mapinduzi na nchi daima imekuwa ikiendelea mbele kinyume na matakwa yao na licha ya kuchukizwa na jambo hilo. Jueni ya kwamba baada ya hapo pia Mwenyezi Mungu amekukadarieni ushindi wa mwisho nyinyi taifa la Iran na nchi hii, na Inshallah mtafikia natija na Mwenyezi Mungu kuwashinda maadui wenu. Kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, adui hataweza kutoa pigo lolote lile dhidi ya Mapinduzi na mfumo huu wa Kiislamu.
Tunamwomba Mwenyezi Mungu anyanyue nafasi ya mashahidi watukufu na ya Imam mpendwa ambao walitufungulia njia hii. Tunamwomba pia Mungu wa walimwengu alifanikishe taifa la Iran katika majukumu yake yote na hasa katika utekelezaji wa jukumu hili ambalo Inshallah litatekelezwa siku mbili zijazo.
Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.
(1)    Mwanzoni mwa hotuba hii, Hujjatul Islam Mustafa Hassanati ( Imam wa Ijumaa wa Najaf Abad) alitoa hotuba fupi.
(2)     Shahidi
(3)     Ahmad Kadhimi (kamanda wa jeshi la nchi kavu la Walinda Mapinduzi ya Kiislamu)
(4)     Surat al-Baqarah, sehemu ya aya ya 143
(5)     Nahjul Balagha, hotuba ya 16
(6)     Surat al-Hadid, sehemu ya aya ya 21
(7)     Surat Muhammad, sehemu ya aya ya 7

 

700 /