Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Marekani na madola yanayodai kupambana na ugaidi hayasemi ukweli katika uwanja huo

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo jioni (Jumatatu) ameonana na Rais Nursultan Nazarbayev wa Kazakhstan ambapo amegusia udharura wa kuongezwa kiwango cha ushirikiano wa nchi mbili katika nyuga tofauti za kisiasa, kiuchumi, kimataifa na katika vita dhidi ya ugaidi.  Amesema kuwa: Baadhi ya madola hususan Marekani si wakweli katika madai yao ya kupambana na ugaidi, lakini nchi za Kiislamu zinaweza kupambana vilivyo na vitisho vyote vinavyoukabili ulimwengu wa Kiislamu kwa kuwa na ushirikiano wa kweli baina yao.
Ayatullah Khamenei ameitaja misaada ya Wamarekani kwa kundi la Daesh huko Iraq kuwa ni mfano wa wazi wa kutokuwa na ukweli miungano mbalimbali inayodai kupambana na ugaidi na kuongeza kuwa: Madola hayo yanafanya njama za kuhalalisha vitendo vyao hivyo vya kindumilakuwili kwa kuugawanya ugaidi katika aina mbili; ugaidi mzuri na ugaidi mbaya.
Kiongozi Muadhamu wa Maipinduzi ya Kiislamu Ayatullah Khamenei ameashiria uraia wa nchi za Ulaya wa watekelezaji wa mashambulizi ya kigaidi barani Ulaya na vilevile suala la kuwepo raia wengi wa nchi hizo katika makundi ya kigaidi huko Syria na Iraq na kusema kuwa, ukweli huo unathibitisha kwamba, Magharibi hususan na Marekani haina azma na nia ya kweli ya kupambana na ugaidi. 
Amesema dunia ya leo ni dunia isiyo na uthabiti na kuongeza kuwa: suala linalotia wasiwasi zaidi ni kwamba, kwa upande mmoja nchi za Kiislamu hii leo zinakabiliwa na hatari ya makundi ya kigaidi yanayohujumu Uislamu na Waislamu kwa kutumia jina la Uislamu, na katika upande mwingine madola makubwa ya Magharibi hayataki kuona nchi za Waislamu zikishikamana na kuwa pamoja.
Ayatullah Khamenei amelitaja suala la kupambana na hatari ya ugaidi na mienendo ya kindumakuwili ya madola ya kibeberu kuwa linahitajia ushirikiano wa nchi za Kiislamu chini ya msingi wa siasa za kimantiki na zinazokubalika na kuongeza kuwa: Sisi tunazitambua nchi zote za Waislamu kuwa ni ndugu zetu na kwamba misimamo ya Iran na Kazakhstan nayo ni ya aina moja katika masuala mengine ya kimataifa.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria pia ushirikiano wa Kazakhstan na Iran katika jumuiya za kimataifa na kusisitiza kuwa: Pamoja na mataifa haya mawili kuwa na dini, historia na utamaduni wa aina moja pamoja na fursa na nyuga nyingi za ushirikiano baina ya mataifa hayo mawili, lakini kiwango cha uhusiano wa kibiashara na kiuchumi wa nchi hizo mbili hakionekani kupanda na sisi tunakaribisha kuongezwa kiwango cha ushirikiano wa nchi hizi mbili katika masuala tofauti ya kisiasa, kiuchumi, kibiashara, usafiri na uchukuzi pamoja na ushirikiano katika masuala ya mfumo wa kisheria wa eneo la bahari ya pamoja.
Katika mazungumzo hayo ambayo yamehudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Nursultan Nazarbayev wa Kazakhstan amesema: "Iran ni jirani yetu mkubwa na mwenye nguvu, anayeaminika na anayefaa kutegemewa".  Ameongeza kuwa: Nchi hizi mbili zina fursa na nyuga nyingi za kustawisha uhusiano wao na sisi katika ziara yetu hii tumefikia makubaliano mazuri sana katika upande wa masuala ya kiuchumi na kibiashara na ni matumaini yetu kupitia mikataba hiyo kutakuwa na ongezeko zuri la ushirikiano baina ya nchi mbili.
Rais wa Kazakhstan ameongeza kuwa, ugaidi ni tishio kubwa na huku akigusia matukio ya kigaidi yanayotokea katika nchi za Magharibi na njama za Wamagharibi za kujaribu kuuhusisha Uislamu na vitendo hivyo vya kigaidi na kusema kuwa: Ugaidi na wimbi la wakimbizi kwa hakika ni vitu vinavyotokana na vitendo vya madola ya Magharibi kukabiliana na tawala halali katika eneo hili, kwani wakati serikali kuu inapokosa utulivu na kushindwa kudhibiti masuala ya nchi, nafasi yake huchukuliwa na ugaidi.
Rais Nazarbayev amezungumzia pia uwezo na nguvu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ushawishi wa kimaanawi alio nao Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika nchi za Kiislamu na kumwambia Ayatullah Khamenei kwamba: Mimi ninaafikiana kikamilifu na nadharia zako kuhusu umoja wa ulimwengu wa Kiislamu na tunapaswa tuuoneshe ulimwengu mzima kuwa Uislamu ni dini ya maendeleo, ya umoja na ni dini inayopiga vita kikamilifu vitendo vyote vya kigaidi. 

700 /