Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei:

Ninaunga mkono hatua yoyote yenye maslahi kwa taifa

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, leo adhuhuri (Jumatano) na katika muendelezo wa vikao vya sikukuu ya Nairuzi ameonana na kuhutubia majimui ya viongozi wa serikali, wajumbe wa Kamati Kuu ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) viongozi wa ngazi za juu wa chombo cha Mahakama na viongozi wa taasisi na asasi nyingine nchini. Amewashukuru viongozi hao hususan viongozi wa serikali kwa juhudi na kazi kubwa inayofanywa na serikali katika utekelezaji wa siasa za uchumi ngangari, amelitaja suala la kudumisha upendo na maelewano pamoja na umoja na mshikamano baina ya viongozi nchini kuwa ni jambo muhimu sana katika ufanikishaji wa siasa hizo. Ameongeza kuwa kituo kikuu cha kuendeshea uchumi ngangari inabidi kisimamiwe na serikali hususan Makamu wa Kwanza wa Rais mwenyewe na sambamba na kuvutia ushirikiano na msaada wa vyombo na taasisi nyingine zote, kituo hicho kikuu kinapaswa kifuatilie kwa kina harakati na kazi za sekta tofauti na kusaidia sekta ya uzalishaji wa bidhaa za ndani pamoja na kuandaa mazingira ya kuchukuliwa hatua kubwa na za pande zote kwa ajili ya kufanikisha uchukuaji hatua na utekelezaji wa kivitendo wa siasa za uchumi ngangari.
Amesema, nafasi ya kusimamia kituo kikuu cha uchumi ngangari ni muhimu mno katika suala zima la kuchunguza na kufuatilia kwa kina kazi za taasisi na vyombo mbali mbali na kuongeza kuwa: Katika ufuatiliaji huo wa kina, inabidi taasisi zote zinazofanya kazi katika kalibu na fremu ya siasa za uchumi wa kimuqawama zitiwe nguvu, na zile taasisi ambazo zinapuuza na hazishughulishwi na siasa hizo, inabidi ziingizwe kwenye mkondo wa kufanikisha siasa hizo na wakati huo huo vizuiwe vitendo vya taasisi na vyombo ambavyo vinakwenda kinyume na uchumi wa kimuqawama.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, hatua na vitendo katika uchumi wa kimuqawama inabidi viwe kwa namna ambayo itakapofika mwishoni mwa mwaka huu (wa Kiirani wa 1395 Hijria Shamsia), kuweze kutolewa ripoti ya kina na ya kivitendo kuhusiana na kazi zilizofanyika katika nyuga tofauti za ufanikishaji wa uchumi huo. 
Ameongeza kuwa: Majimui ya taasisi za utekelezaji na utendaji nchini Iran, zinao uwezo wa kufanikisha siasa za uchumi ngngari na Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) nayo ina wajibu wa kuisaidia serikali katika suala hilo.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Tunachotaka sisi si kupandisha juu matarajio na matumaini yetu kwa serikali na tunatambua matatizo na changamoto mbalimbali zilizopo, lakini kunaweza kufanyika mambo makubwa kupitia njia ya kubana matumizi katika baadhi ya sekta kwa ajili ya kujaza mapungufu na nakisi zilizoko katika sekta nyinginezo.
Amesema, majimui ya viongozi nchini ni ya watu muhimu sana katika jamii ambao wana uzoefu na wana msukumo mkubwa wa kazi na fikra nzuri na ni wachapaji kazi. Ameongeza kuwa: Kituo kikuu cha kuendeshea siasa za uchumi ngangari ni kituo cha kifikra na pia cha amali na vitendo na kinapaswa kutumia vizuri uwezo wa viongozi nchini na pia kistafidi vilivyo na uwezo na suhula zilizopo katika asasi na vyombo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuchukua maamuzi sahihi na kutekeleza kivitendo maamuzi hayo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, kazi ya kuendesha nchi, jukumu ambalo ni la serikali hususan mheshimiwa Rais mwenyewe ni kazi nzito sana na kuongeza kuwa: Kutokana na mheshimiwa Rais kuzongwa na kazi na majukumu mengi, badala yake Makamu wa Kwanza wa Rais ambayo ana nafasi ya juu serikalini anaweza kutoa mchango maalumu na wa kipekee katika kuongoza kituo kikuu cha uchumi ngangari. 
Ayatullah a Khamenei amesisitiza kwamba: Mimi nitaunga mkono vilivyo hatua yoyote ile ya Serikali, ya Bunge na ya Chombo cha Mahakama ambayo kwa hakika inalenga kuwahudumia wananchi na kutatua matatizo yao; lakini kwa sharti kwamba ihisike kuwa kazi inayofanyika ni ya lazima na ina manufaa kweli kwa taifa. 
Amesisitiza kuwa: Utekelezaji wa siasa za uchumi ngangari, inabidi utegemee kikamilifu uwezo na suhula zote zilizopo nchini na ambazo si kidogo.
Vilevile Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa Marekani ni nembo ya tabia mbaya na ahadi zisizo na mwamana na kuongeza kuwa: Wamarekani hawaaminiki hata kidogo, na ukiwaweka pembeni Wamarekani, kuna baadhi ya nchi za Magharibi ambazo nazo ni vivyo hivyo haziaminiki, hivyo tunapaswa kutegemea uwezo wetu wenyewe. Aidha amesema: Misimamo na hatua zinazochukuliwa na viongozi wa Marekani nazo zinathibitisha uhakika huo.
Ayatullah Khamenei amesema kwa kusisitiza kuwa, iwapo tutaingia kiikhlasi na kiukweli katika medani ya ufanikishaji wa siasa za uchumi huo, basi bila ya shaka yoyote Mwenyezi Mungu atatusaidia na atakuwa pamoja nasi. Ameongeza kuwa: Katika njia ya maisha ya mtu binafsi na ya jamii nzima kiujuma, siku zote kuna misukosuko na panda shuka nyingi, lakini lililo muhimu ni kuwa, watu wote na katika mazingira yoyote wawayo, wanapaswa kuhakikisha kuwa hawaisahau na wala hawatoki nje ya njia ya asili.
Amesema, ni jambo la lazima kulipa umuhimu na uzito wa hali ya juu suala la kuisaidia na kuiunga mkono sekta ya uzalishaji wa ndani na kuongeza kuwa: Lazima uzalishaji uzingatiwe vilivyo na upewe kipaumbele maalumu katika sekta zake zote mbili, sekta ya viwanda na sekta ya kilimo.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja suala la maelewano, mapenzi na mshikamno baina ya viongozi kuwa ni mambo yanayoandaa uwanja wa kufanikiwa uchumi ngangari na kusisitiza kuwa: Hakuna jambo lolote litakaloweza kufanyika bila ya kuweko ushirikiano baina ya viongozi wote.
Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran siku zote imekuwa na bahati nzuri ya kuwa na umoja wa kitaifa, lakini pambizoni mwa umoja huo wa kitaifa, inabidi yaweko pia mapenzi na mshikamano baina ya viongozi na kwamba umoja na mshikamano huo haukinzani hata kidogo na suala la kuweko watu wenye mitazamo na fikra tofauti katika jamii.
Aidha amesema, mkutano huo wa leo ni dhihirisho la wazi la mapenzi na maelewano, ukuruba na kushibana viongozi nchini na kuhimiza kuwa: Inabidi viongozi nchini na licha ya kuwa na fikra na mitazamo tofauti washikamane vilivyo katika ufanikishaji wa malengo makuu ya Mapinduzi ya Kiislamu.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa: Leo hii humu nchini kuna hisia kuwa viongozi wa mihimili mitatu mikuu ya dola (Serikali, Bunge na Mahakama) pamoja na viongozi wakuu wa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu wana fikra na mtazamo mmoja kuhusu wajibu wa kufanikisha malengo makuu ya Mapinduzi ya Kiislamu licha ya kuwa na fikra tofauti na kutofautiana juu ya njia za kufanikisha malengo hayo.
Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei ametoa shukrani zake nyingi kwa watu wa familia za viongozi nchini hususan wake wa viongozi hao kutokana na subira na uvumilivu wao mkubwa na kuongeza kuwa: Sehemu kubwa sana ya jitihada na kazi muhimu na kubwa zinazofanywa na viongozi zinafanikishwa kwa subira na uvumilivu wa wake zao ingawa juhudi hizo za wake wa viongozi mara nyingi huwa hazionekani.
Katika mkutano huo, Bw. Jahangiri, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemshukuru Kiongozi Muadhamu kwa miongozo na nasaha zake za busara na uungaji mkono wake kwa Serikali na kusema: Serikali imeandaa ratiba kuu ya kutekeleza kivitendo siasa za uchumi wa kimuqawama na kwamba siasa hizo ni sawa na cheti cha dawa za kuponya matatizo ya kiuchumi nchini.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa: Serikali ina imani na inaziamini kikamilifu siasa za uchumi wa kimuqawama na kwamba inakubaliana na siasa hizo kisheria, kikanuni na kiutaalamu.
Bw. Jahangiri amegusia pia vipaumbele vilivyoainishwa kwa ajili ya uchumi wa Iran katika mwaka huu wa 1395 Hijria Shamsia katika vikao viwili vya hivi katibuni vya kituo kikuu cha uchumi wa kimuqawama na kuongeza kuwa: Usiku uliopita kulifanyika kikao kirefu baina ya Serikali na mashirika makubwa ya kiuchumi nchini na kwamba Serikali ina nia ya kweli ya kutia nguvu uzalishaji wa bidhaa za ndani ya nchi, kustawisha usafirishaji nje bidhaa na kusahilisha ufanyaji kazi, pamoja na kuihusisha vilivyo sekta binafsi katika ufanikishaji wa mambo hayo. 
Amesema, ni jambo la lazima kwa serikali kusaidiwa na mihimili na taasisi nyingine nchini hususan Shirika la Sauti na Televisheni la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB katika ufanikishaji wa siasa za uchumi wa kimuqawama na kuongeza kuwa: Ninakuhakikishieni kwamba Serikali haitazembea hata kidogo kutumia uwezo wake wote wa kielimu, kiuzoefu, uendeshaji mambo na kila uwezo ilio nao kwa ajili ya kufanikisha siasa za uchumi usioyumba wa kimuqawama.
Kabla ya mkutano huo, viongozi waliohudhuria mkutano huo wamesalishwa sala za Adhuhuri na Laasiri na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei.

700 /