Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu katika hadhara ya wanachama wa Umoja wa Jumuiya za Wanafunzi

Kupambana na vita laini kunahitajia malezi ya vijana wa kimapinduzi na wenye azma thabiti

Akizungumza leo asubuhi (Jumatano) na maelfu ya wanachama wa Umoja wa Jumuiya za Kiislamu za Wanafunzi kutoka kote nchini, Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiiskamu amesema kuwa moja ya medani muhimu za Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kukabiliana na kambi ya uistikbari ni suala la vijana na kusisitiza kuwa, kambi iliyo mkabala na Mfumo wa Kiislamu inataka kubadilisha utambulisho wa kidini na kimapinduzi wa vijana wa Kiirani na kuondoa miongoni mwao matumaini, uchangamfu na motisha. Amesema kuwa njia pekee ya kupambana na mkabiliano huo uliofichika na mgumu ni kuwalea vijana wanaoshikamana na dini, wa kimapinduzi, wasafi, wenye azma thabiti, walio na mwamko, waliojaa motisha, wenye matumaini, wenye fikra, shujaa na wa kujitolea kwa anwani ya makamanda wa vita laini.
Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu amewanasihi vijana kunufaika na fursa kubwa ya mwezi huu wa Rajab na hatimaye miezi ya Shaaban na Ramadhani na kuongeza kuwa: Miezi hii mitatu ni machipuo ya kimaanawi na vijana ambao wako kwenye umri wao wa machipuo wanaweza kunufaika na fursa hii yenye thamani kubwa kwa ajili ya kuimarisha pande zao za kimaanawi. Ayatullah Khamenei kisha ameashiria baadhi ya medani ambapo Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu unakabiliana na kambi ya uistikbari unaoongozwa na Marekani na Uzayuni na kuongeza: Kujitawala kwa nchi iwe ni katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni ni moja ya nyanja na medani hizo kwa sababu madola makubwa ya dunia hukabiliana na kila nchi ambayo inataka kusimama mbele ya ubeberu na upenyaji wa wageni kwa ajili ya kulinda kujitawala kwake. Amesema suala la maendeleo ni sehemu nyingine ambapo Mfumo wa Kiislamu unakabiliana na  uistikbari na kusema: Madola makubwa ya dunia husimama mbele ya kila nchi inayotaka kufikia maendeleo bila ya kuyategemea kwa sababu maendeleo kama hayo yanaweza kuchukuliwa kuwa mfano bora wa kufuatwa na nchi pamoja na mataifa mengine. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema moja ya sababu muhimu za madola ya kiistikbari kushirikiana kwa ajili ya kukabiliana na juhudi za Iran za kujipatia elimu na teknolojia ya nyuklia ni suala hilohilo na kusisitiza kuwa: Iwapo tutasalimu amri mbele ya madola hayo, bila shaka yatapinga pia maendeleo ya Iran katika nyanja za bioteknolojia, nano na taalumu nyingine nyeti. Hii ni kwa sababu wao wanapinga kila aina ya maendeleo ya kielimu, kiuchumi na kiustaarabu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ayatullah Khamenei amesema kuwepo imara Iran katika eneo la Asia Magharibi na duniani kwa ujumla, suala la Palestina, suala la mapambano na suala la mtindo wa maisha ya Kiirani ni nyanja nyingine ambazo mrengo wa uistikbari unahitilafiana na Mfumo wa Kiislamu na kuongeza: Iwapo mtindo wa maisha wa Kimagharibi utaenea katika nchi yoyote ile, bila shaka viongozi wake watakuwa ni wa kusalimu amri mbele ya siasa za uistikbari. Ameashiria suala la vijana kuwa nyanja nyingine muhimu ya hitilafu hizo na kusema: Kuna vita vikubwa laini vya chini kwa chini (nyuma ya pazia) kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa upande mmoja na Marekani na Wazayuni pamoja na wafuasi wao katika upande wa pili. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema vijana wanafunzi na wanachuo ni makamanda (viongozi) wa vita hivyo na kuongeza: Katika vita hivi laini tunaweza kutasawari maafisa wawili walio na utambulisho tofauti ambapo natija ya vita hivyo huainishwa kwa msingi wa utambulisho wa maafisa hao tofauti. Huku akisisitiza kuwa vita laini ni hatari zaidi kuliko vita vya zana za kawaida, Ayatullah Khamenei ameashiria baadhi ya maneno ya kipuuzi ya maadui na kusema: Baadhi ya wakati hututisha sisi kuwa watatushambulia kwa zana za kivita na mabomu ambapo maneno hayo ni ghalati kubwa. Hii ni kwa sababu hawawezi kudhubutu kufanya hivyo na hata mara nyingine wakitekeleza jambo kama hilo bila shaka watapata kichapo kikali.
Huku akiashiria kwamba vita laini bado vingali vinaendeshwa dhidi ya Mfumo wa Kiislamu na kwamba badala ya kujilinda tu tunapasa pia kushambulia adui Kiongozi Muadhamu amesema: Ikiwa tutakuwa na makamanda wanaozingatia dini, wa kimapinduzi, wenye azma thabiti, wenye mwamko, wanaofanya bidii, wenye fikra, shujaa na wa kujitolea kwenye kamandi na ngome tunaweza kukisia kupata natija (ushindi) kwenye vita hivi. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza: Ama iwapo tutakuwa kwenye vita hivi laini na makamanda wanaosalimu amri, wanaohadaika, wanaodanganyika na tabasamu ya adui, wasio na motisha, wasio na fikra, wasiojali hatima yao na ya wenzao na  wanaojishughulisha na matamanio kwenye kamandi na ngome hizi, matokeo ya vita yanafahamika wazi. Ayatullah Khamenei amesema: Kwa hivyo makamanda walio na utambulisho wa aina mbili tofauti wanaweza kuwa kwenye vita hivi laini; mmoja anayependelewa na kufadhilishwa na Jamhuri ya Kiislamu na mwingine anayependelewa na mrengo wa uistikbari, na kuwepo kwa makamanda wawili hawa tofauti kunaweza kubadilisha hatima ya vita.
Huku akisisitiza kwamba kutilia mkazo, dini, usafi, utakasaji nafsi za vijana  na kujiepusha kwao kushughulishwa na matamanio hakupaswi kutajwa kuwa ni taasubi na kuganda fikra, Ayatullah Khamenei amesema: Wamagharibi na hasa Wamarekani wanataka kuwafanya vijana wa Iran wawe ni watu wasiokuwa na imani, ushujaa, motisha, harakati, matumaini, wanaomdhania vizuri adui na walio na dhana mbaya kuhusu kamanda na hatima yao. Ama Mfumo wa Kiislamu unataka kulea vijana ambao ni kinyume na matakwa ya mrengo wa uistikbari. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameunasihi sana Umoja wa Jumuiya za Kiislamu za Wanafunzi na Wanachuo kufanya jitihada za kulea vijana walio na umbo na utambulisho wa kidini na kimapinduzi na kueneza moyo huo kwa vijana wote wa rika zao. Ameendelea kusema: Kama ambavyo sisi tuna mpango wa muda mrefu kuhusiana na harakati ya kielimu, kidini na kimapinduzi kwa ajili ya vijana wa taifa hili, adui pia ana mpango kama huo, na njia ya kukabiliana na mpango huo ni kuimarishwa kwa viwango na ubora wa vijana wanaoshikamana na Mapinduzi na dini na kuimarisha msimamo na uthabiti wao. Kiongozi Muadhamu kisha ameashiria majukumu ya viongozi kuhusiana na vijana na kusema kuwa Wizara ya Elimu na Malezi ina uongozi unaozingatia dini na kwamba fursa hiyo inapasa kutumiwa vyema na kuongeza: Mbali na shule kujishughulisha na masuala ya kuwafundisha wanafunzi masomo ya kawaida zinapasa pia kuweka mipango sahihi ya kuwashughulisha na masuala ya Mapinduzi ili kizazi cha vijana kiwe ni kizazi cha kimapinduzi. Amewashauri viongozi wa Wizara ya Elimu na Malezi wazipe fursa jumuiya za kimapinduzi  na kidini kama vile Umoja wa Jumuiya za Kiislamu za Wanafunzi na Basiji ya Elimu na kuongeza: Imesikika kwamba baadhi ya shule zinapinga shughuli za kimapinduzi ambapo Wizara ya Elimu na Malezi inapasa kukabiliana na suala hilo. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa mazingira ya vijana nchini ni mazingira ya kutia matumaini na kusisitiza: Licha ya kuwepo mambo tofauti yanayopotosha na mrengo mkubwa wa uadui, lakini bado nchini tuna vijana wapenda dini, Mapinduzi, wanaotawasali, kutembea kwa miguu Siku ya Arbaini (ya Imam Hussein (as)), wanaozingatia Qur’ani, kufanya itikafu na wanaosimama imara katika medani za Mapinduzi, ambapo tunapasa kumshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa hilo.
Ayatullah Khamenei amesema kuwa ni suala muhimu mno kuwa na vijana kama hawa nchini na huku akisisitiza kuwa licha ya kupita miaka 37, kambi ya uistikbari imeshindwa kuifuta Jamhuri ya Kiislamu ya Iran au kuzuia ustawi na nguvu zake katika eneo,  ameongeza kuwa: Pamoja na kuwepo vitisho vya kivitendo na propaganda chungu nzima, lakini leo hii Hizbullah ya Lebanon imeweza kudhihirisha uwepo na dhihirisho lake lililokomaa katika ulimwengu wa Kiislamu na wala kulaaniwa kwake kwenye karatasi isiyo na thamani yoyote na serikali fasidi, tegemezi na tupu hakuna umuhimu wowote. Huku akiashiria kushindwa kwa utawala wa Kizayuni na Hizbullah ya Lebanon katika vita vya siku 33 na kuulinganisha ushindi huo na kushindwa kwa majeshi yenye nguvu ya nchi tatu za Kiarabu na utawala huo, Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba: Hizbullah na vijana wake walioshikamana na dini wanang’ara kama jua na hivyo kuwa fahari kwa ulimwengu wa Kiislamu. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa dhati ya harakati zilizosimama juu ya msingi wa haki inazidi kuimarika na kustawi na kuongeza kuwa hata kama ukweli huenda ukakabiliwa na baadhi ya matatizo lakini hatimaye utashinda tu. Ayatullah Khamenei amesema kuwa sharti muhimu la ushindi wa ukweli ni kusimama imara makamanda wa vita laini dhidi ya matatizo na kusisitiza kwamba: Ukweli ni wa vijana na kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu siku itafika ambapo matatizo taratibu yatatoweka na vijana kusimama kwenye kilele.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam Walmuslimeen Haj Ali Akbari, Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu katika masuala ya Umoja wa Jumuiya za Kiislamu za Wanafunzi, alitoa ripoti kuhusiana na shughuli za umoja huo na kusema: Tumaini (lengo) letu leo ni kulea wanafunzi katika mizani ya Mapinduzi ya Kiislamu na ni kwa msingi huo ndipo malezi ya Kiislamu yanayofungamana na maarifa ya Imam Ali (as) yakachukuliwa kuwa kipimo cha mipango yote. Vilevile wanafunzi wawili wanachama wa Umoja wa Jumuiya za Kiislamu za Wanafunzi walitoa hotuba wakibainisha mitazamo na madukuduku yao kuhusiana na shughuli za wanafunzi, masuala ya vijana, masomo na malezi katika shule mbalimbali nchini.

 

700 /