Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amwambia Waziri Mkuu wa Italia:

Matunda ya mazungumzo hayahisiki katika safari za viongozi wa Ulaya nchini Iran

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi Ayatullah Ali Khamenei leo jioni (Jumanne) ameonana na kufanya mazungumzo na Bw. Matteo Renzi, Waziri Mkuu wa Italia hapa mjini Tehran. Amegusia historia ya uhusiano mzuri baina ya nchi mbili za Iran na Italia tangu huko nyuma na namna nchi hizo mbili zinavyokaribisha kuongezwa wigo wa ushirikiano huo na kusema kuwa, tatizo na udhaifu wa safari za mara kwa mara za hivi karibuni za viongozi wa Ulaya nchini Iran ni kule kushindwa kuonekana matunda ya kivitendo na ya waziwazi ya mazungumzo na safari hizo. Amesisitiza kuwa: "Mtazamo wetu katika ushirikiano wetu na Italia na serikali yako ni mtazamo tofauti na huo, bali ni mtazamo chanya na mzuri na ni matumaini yetu ziara yako hii nayo itazidi kutilia nguvu mtazamo wetu huo."
Ayatullah Khamenei ameutaja mwenendo wa Italia katika kipindi cha vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran kwamba ulikuwa wa kimantiki zaidi ikilinganishwa na nchi nyingine za Magharibi na kuongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha juhudi za kustawisha uhusiano wake na Italia katika nyuga mbalimbali hususan katika upande wa ushirikiano wa kiuchumi.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, jambo muhimu katika safari na kufanya mazungumzo na nchi za nje ni kuhakikisha makubaliano yanayofikiwa yanatekelezwa kivitendo. Amekukumbusha kuwa: Baadhi ya tawala na mashirika ya Ulaya yanatembelea Iran na kufanya mazungumzo lakini matunda ya mazungumzo hayo hayajaonekana hadi leo hii!
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: Baadhi ya madola na mashirika hayo yanawabebesha Wamarekani lawama za jambo hilo, lakini tunapoangalia historia na vitendo vya huko nyuma vya nchi na mashirika hayo tutaona kuwa madai hayo hayakubaliki, kama ambavyo pia hadi hivi sasa nchi hizo zimeshindwa kutekeleza ahadi zao katika mazungumzo ya nyuklia na badala yake zinachukua hatua na kutoa matamshi yasiyokubalika kwa nia ya kuzitisha nchi nyingine ziogope kushirikiana na Iran.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia pia ziara ya kwanza kabisa ya barani Ulaya ya Rais Hassan Rouhani huko nchini Italia na kusema kuwa, hiyo inathibitisha kwamba mtazamo wa Iran kwa Italia ni mtazamo chanya na mzuri. Ameongeza kusema kuwa: "Hatuna mtazamo huo chanya kuhusu baadhi ya nchi za Ulaya kwani nchi hizo jicho lao lote limeelekezwa kwa Marekani zikisubiri amri tu ili ziitekeleze".
Vilevile amesema, suala la kupambana na ugaidi ni uwanja mwingine wa ushirikiano wa nchi mbili za Iran na Italia na kuongeza kuwa: Kuna baadhi ya nchi za Ulaya kwa muda zilikuwa zinayasaidia na kuyaunga mkono makundi katili na hatari ya kigaidi na matokeo yake ni kuwa leo hii wimbi hatari na la kila upande la ugaidi limefika hadi barani Ulaya.
Ayatullah Khamenei ameitaja misaada ya fedha na silaha ya Marekani kwa makundi ya kigaidi kuwa ni katika vizuizi vikubwa vinavyokwamisha vita dhidi ya ugaidi na kuongeza kuwa: Kuna habari zenye ushahidi na za uhakika kabisa zinazoonesha kuwa Marekani inalipa misaada ya aina mbalimbali kundi la Daesh na makundi mingine ya kigaidi na hata hivi sasa ambapo wameunda muungano wa kupambana na Daesh, baadhi ya taasisi za Marekani zinaendelea kulisaidia kundi la Daesh kwa sura nyingine.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameunga mkono matamshi ya Waziri Mkuu wa Italia kuhusiana na udharura wa kupambana na ugaidi kwa njia za kiutamaduni sambamba na kupambana nao kwa njia za kijeshi na kifedha na kuongeza kuwa: Taasisi kubwa za kipropaganda duniani ambazo ziko chini ya ubeberu wa wanasiasa wa Magharibi zinatumia kisingizio cha vitendo vya baadhi ya watu waovu na magaidi ili kueneza chuki dhidi ya Uislamu na kufanya njama za kisiasa zilizo nyuma ya pazia, suala ambalo linakwamisha jitihada za kupambana na ugaidi kwa njia za kiutamaduni.
Katika mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Waziri Mkuu wa Italia Bw. Matteo Renzi amesema kuwa: "Katika mazungumzo yetu ya leo na viongozi mbalimbali wa Iran kwa mara nyingine tumeweza kujadili masuala muhimu hususan masuala ya kiuchumi na inabidi baadhi ya masuala ya kiuchumi na kifedha yarekebishwe ili upatikane ufanisi unaotakiwa wa mazungumzo hayo".
Bw. Renzi ameongeza kuwa: Msimamo wa Italia umesimama kikamilifu juu ya msingi wa kuheshimu makubaliano yanayofikiwa na ni kwa sababu hiyo ndio maana tunaamini kuwa, vikwazo dhidi ya Iran inabidi viondolewe kama yanavyosema makubaliano ya nyuklia na sisi hatuna wasiwasi bali tumeamua kikweli kweli kutekeleza vilivyo ahadi tuliyotoa.
Waziri Mkuu wa Italia ameendelea na matamshi yake kwa kugusia namna vitendo vya kigaidi vilivyoenea hadi barani Ulaya na kusema kuwa, njia bora ya kuweza kukabiliana na vitendo hivyo ni kung'oa mizizi ya kijeshi ya magenge ya kigaidi na kukata kikamilifu vyanzo vyao vya kifedha ambavyo ni pamoja na kuuza mafuta na athari za kale za kihistoria na kuongeza kuwa: Suala la kung'oa mizizi ya kundi la kigaidi la Daesh ni katika vipaumbele vyetu hivi sasa na tunafurahi kuona kuwa tuna misimamo ya pamoja na Iran katika suala hilo.
Aidha ameelezea masikitiko yake kwa kuona kuwa sura ya Uislamu inaharibiwa kwa kisingizio cha ugaidi na kuongeza kwamba: Leo hii wakati magaidi wanapofanya vitendo vyao kigaidi barani Ulaya baadhi ya viongozi (wa nchi za Magharibi) badala ya kuwalaani magaidi wenyewe, wanaulaani Uislamu kiasi kwamba mgombea katika uchaguzi wa Rais wa Marekani anathubutu kusimama juu ya jukwaa la kampeni zake na kudai kuwa mkosa katika suala la ugaidi ni Uislamu!
Bw. Renzi aidha amesema, suala la kiutamaduni ni sehemu nyingine muhimu katika mapambano na ugaidi na kuongeza kuwa: Tunapaswa tuoneshe kuwa, dini zote zinapigania amani, mazungumzo na kuishi pamoja kwa salama na wamani wanadamu wote na amemwambia Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei kwamba: Nguvu, uwezo na mchango wako ukiwa ni Kiongozi Mkuu katika ulimwengu wa Kiislamu ni muhimu mno katika kueneza fikra na mtazamo huo.
 
 

 

700 /