Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ayatullah Khamenei katika mazungimzo yake na Rais wa Afrika Kusini:

Kuna udharura wa kukabiliana na vizuizi vya madola ya kibeberu dhidi ya nchi zinazojitawala

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo jioni (Jumapili) amemkaribisha na kuzungumza na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ambako amesisitizia udharura wa kuzidishwa ushirikiano wa aina zote katika nyuga za kiuchumi na kisiasa. Amesema kuwa, ushirikiano wa nchi huru na zinazojitawala unapaswa kuimarishwa kadiri inavyowezekana na nchi hizo inabidi zizidi kukurubiana licha ya baadhi ya madola ya kibeberu kufanya njama za kukwamisha jambo hilo.
Ayatullah Khamenei ameashiria jinsi Tehran ilivyokata uhusiano wake mara moja na utawala wa ubaguzi wa rangi wa Makaburu wa Afrika Kusini mara baada ya kupata ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kusema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikata uhusiano wake na utawala wa Kizayuni wa Israel na utawala wa ubaguzi wa rangi wa Afrika Kusini takriban kwa wakati mmoja.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekumbushia nafasi muhimu ya hayati Nelson Mandela wa Afrika Kusini katika kuanguka utawala wa ubaguzi wa rangi nchini humo na historia yake nzuri, ya kiudugu na kimapenzi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza kuwa, utawala huo dhalimu na uliokuwa dhidi ya ubinadamu ulianguka kwa mapambano ya Nelson Mandela na wananchi wa Afrika Kusini, na kwamba kwa kazi yake hiyo, kwa hakika Mandela alitia uhai mpya katika mapambano ya bara zima la Afrika.
Amesema, mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu Afrika Kusini ni mtazamo mzuri na kubainisha kuwa, uhusiano wa Iran na Afrika Kusini ni mzuri sana. Ameongeza kuwa, ushirikiano wa nchi hizo mbili katika jamii za kimataifa pia unasaidia sana. Pamoja na hayo amesema, bado uwezo wa nchi hizi mbili haujatumiwa ipasavyo kwa ajili ya kukuza mabadilishano ya kiuchumi na kibiashara baina ya pande mbili.
Ayatullah Khamenei ameutaja ushirikiano wa Iran na Afrika Kusini katika Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) kuwa unaonekana kwa uwazi sana na kusisitiza kuwa: Ushirikiano huo uba faida kwa nchi zote wanachama wa NAM.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza pia kuwa, manufaa ya nchi huru yamo ndani ya kuimarisha ushirikiano baina ya nchi hizo katika nyuga mbalimbali na kuna udharura wa kusimama imara kukabiliana na vizuizi vyote vinavyowekwa na baadhi ya madola ya kibeberu ili kukwamisha ushirikiano huo.
Kwa upande wake Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa uungaji mkono wake kwa wananchi wa nchi yake wakati wa mapambano na ubaguzi wa rangi na kusema kuwa, wananchi wa Afrika Kusini kamwe hawawezi kusahau uungaji mkono huo wa taifa la Iran kwao.
Rais wa Afrika Kusini aidha ameunga mkono matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema kuwa, baadhi ya madola ya kibeberu yanatumia visingizio visivyokubalika kujaribu kuzuia ushirikiano na kuimarika uhusiano baina ya nchi zinazojitawala lakini nchi hizo zinaweza kutatua matatizo mengi kwa kuungana na kuwa na kauli moja katika masuala ya kimataifa.

700 /