Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hadhara ya wafanyakazi

Ayatullah Khamenei: Marekani inawaogopesha wawekezaji wa kigeni kuwekeza Iran

Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran leo asubuhi (Jumatano) katika kuwadia Siku ya Wafanyakazi Duniani, ambayo ni Mei Mosi amekutana na maelfu ya wafanyakazi na huku akiisifu jamii ya wafanyakazi nchini kutokana na uaminifu na uthabiti wao kwa Mapinduzi na Mfumo wa Kiislamu, amesisitiza juu ya kutatuliwa matatizo yao, kuimarishwa uzalishaji wa bidhaa za ndani ya nchi, udharura wa kupambana vilivyo na magendo ya bidhaa na kuzuiwa uagizaji kutoka nje wa bidhaa ambazo ni sawa na zile zinazozalishwa ndani ya nchi. Ameashiria kuendelea kwa uadui wa Marekani dhidi ya Iran na kusema: Wamarekani ni watu wasioweza kuaminika na kwamba kwa kuendelea kusisitiza juu ya kuiwekea vikwazo mbalimbali nchi hii wanafanya juhudi za kufanya Iran iogopwe kimataifa na hivyo kuweka vizuizi katika njia ya miamala ya kiuchumi ya Iran na nchi za kigeni. Kiongozi Muadhamu pia ameashiria duru ya pili ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran, yaani bunge hapo siku ya Ijumaa wiki hii na kuwataka wananchi wote waliotimiza masharti ya kupiga kura kushiriki kwa wingi kwenye uchaguzi huo. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameshukuru juhudi kubwa zinazofanywa na jamii ya wafanyakazi nchini na huku akidhihirisha mapenzi yake makubwa kwa jamii hiyo amesema kuwa kazi na jitihada kwenye jamii ni thamani. Amesema kila mtu anayefanya kazi kwenye jamii awe ni kiongozi, waziri, muhadhiri wa chuo kikuu, mwanachuo, mwanazuoni, mkurugenzi na wengineo kwa maana jumla, ni mfanyakazi (wa kazi za mkono) na kwa hakika anazalisha thamani. Ayatullah Kahamenei amesisitiza kwamba kwa mtazamo wa Uislamu kutofanya kazi, uzembe na kupoteza ovyo wakati ni kinyume na thamani na kuongeza kuwa watu wote wanaojishughulisha na kazi katika Nyanja tofauti mbali na kuimarisha viwango vya kazi wanapasa kutekeleza vyema kazi hizo na kujitoa wakfu kwa ajili ya kazi hizo.
Kiongozi Muadhamu ameongeza: Kila mtu nchini amekubali majukumu fulani kwa hivyo anapasa kutumia wakati na nguvu zake zote katika kuyatekeleza vyema na kwa njia sahihi. Huku akiashiria uaminifu na uthabiti wa jamii ya wafanyakazi nchini kwa Mapinduzi na Mfumo wa Kiislamu katika kipindi cha miaka 37 iliyopita, Kiongozi Muadhamu amesema licha ya kuwepo matatizo mengi ya kimaisha lakini wafanyakazi kamwe hawajahadaika na propaganda zilizo dhidi ya Mapinduzi wala kushawishika kusimama dhidi ya Mfumo wa Kiislamu, bali daima wamekuwa wakiutetea. Ameishukuru kwa dhati jamii ya wafanyakazi kwa kuwa waaminifu na wenye mwamko kuhusiana na masuala ya Mapinduzi na Mfumo wa Kiislamu na kuashiria suala la majukumu, mashirika ya kiuchumi na viongozi katika utekelezaji wa siasa za uchumi ngangari. Amesema ujumbe muhimu wa ‘Uchumi Ngangari, Hatua na Vitendo’ ni kwamba viongozi wanapasa kukiwekea kila kimoja kati ya vipengee vya siasa kuu za uchumi ngangari mipango maalumu na kuitekeleza vyema mipango hiyo. Kuhusiaa na nafasi pamoja na hisa ya wafanyakazi katika utekelezaji wa siasa za uchumi ngangari, Ayatullah Khamenei amesema kuwa jukumu muhimu la wafanyakazi katika sekta hiyo ni kutekeleza vyema, kwa viwango bora na kwa uimara unaohitajika. Huku akisisitiza juu ya umuhimu wa kuimarisha viwango vya kazi (uzalishaji), Ayatullha Khamenei amesema miongoni mwa masuala muhimu yanayoimarisha ubora wa kazi inayofanywa na wafanyakazi ni kuzingatiwa suala la kuboreshwa na kuimarishwa ujuzi wa wafanyakazi ambapo serikali ina majukumu maalumu katika uwanja huo. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema suala jingine ambalo linaboresha viwango vya kazi zinazofanywa na wafanyakazi za mikono ni kudhaminiwa usalama wa kazi zao (uwepo wa kazi hizo) na kuongeza kuwa kudhaminiwa kwa usalama wa kazi hizo ni jukumu la viongozi wa serikali na pia waajiri wengine. Ayatullah Khamenei amesema kufungwa kwa viwanda kunatokana na matatizo kama vile ya uhaba wa fedha na suhula au kuzeeka kwa mitambo, jambo ambalo amesema wenye makosa kuhusu suala hilo sio waajiri bali ni viongozi husika katika sekta ya viwanda na biashara, mabenki, viongozi katika sekta ya teknolojia na mashirika ya kielimu, ambapo wanapasa kutekeleza majukumu yao. Amesema, bila shaka katika baadhi ya sehemu tatizo hilo linatokana na utumizi mbaya wa mikopo na misaada ya kifedha unaofanywa na baadhi ya waajiri ambao badala ya kutumia fedha hizo katika uzalishaji huzitumia katika masuala ya ujenzi wa majumba na mijengo  ambapo katika uwanja huo vyombo vya mahakama, serikali na vyombo vya usalama vinapasa kufuatilia kwa karibu suala hilo. Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba hakuna mtu yoyote anayepinga uzalishaji wa utajiri lakini kwamba jambo hilo halipasi kufanyika kwa gharama ya kukanyagwa jamii ya wafanyakazi wa kazi za mikono na matabaka ya wanyonge. Ameendelea kusema kuwa kuungwa mkono bidhaa zinazozalishwa na wafanyakazi wa Kiirani, usalama wa mazingira ya kazi na kuongeza mishahara katika gharama za uzalishaji ni mambo mengine yanayochangia kuimarika kwa viwango vya kazi zinazofanywa na wafanyakazi wa kazi za mikono na kusisitiza kwamba ili kufanikisha masuala hayo yote, njia sahihi, uzoefu wa nchi nyingine na mipango sahihi inapasa kuwekwa ili kuimarisha motisha wa wafanyakazi na ubora wa kazi (bidhaa) zinazofanywa na wafanyakazi na vilevile kulinda maslahi ya waajiri. Katika kuendelea na hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amebainisha haki za waajiri na kusisitiza kwamba muajiri na mfanyakazi katika mantiki ya Kiislamu wanakamilishana na wala sio kuwa wapinzani na maadui.
Huku akiwashukuru waajiri ambao badala ya kuweka pesa zao sehemu tulivu na isiyo na wasiwasi kwenye benki wameamua kuziweka pesa hizo kwenye nyanja za uzalishaji na uandaaji wa nafasi za ajira, Ayatullah Khamenei ameongeza kuwa: Ushirikiano wa dhati kati ya wafanyakazi na waajiri, juhudi zinazofanywa na viongozi kwa ajili ya kuandaa mazingira yanayofaa kwa ajili ya uwekezaji katika sekta mbalimbali, kuandaliwa mazingira ya uuzaji nje bidhaa za Iran na kutetea maslahi ya wauzaji nje bidhaa hizo katika nchi za kigeni ni miongoni mwa haki za waajiri ambazo zinapaswa kuheshimiwa. Kuhusiana na suala hilo amewaambia viongozi na maafisa wa serikali: Usalama na ubora wa bidhaa zinazosafirishwa nje unapaswa kudhibitiwa kwa sababu mauzo ya nje ya bidhaa mbovu na zisizo na viwango vinavyokubalika yataiharibia jina Iran na hivyo kutoa pigo kwa mauzo yake ya nje. Ayatullha Khamenei amesisitiza sana juu ya thamani na umuhimu wa uzalishaji wa ndani ya nchi na kuongeza kuwa: Uzalishaji wa ndani unapasa kuchukuliwa kuwa jambo tukufu na uungaji mkono kwake kuwa taklifu ya lazima. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuingiza nchini bidhaa ambazo zina mfano wazo nchini ni marufuku kabisa na kuongeza kwamba baadhi ya maduka yanapiga marufuku uuzaji wa bidhaa zisizozalishwa nchini ambapo watu kama hao wanaojivunia na kuwa na ari na nchi yao wanapasa kupongezwa. Ameongeza kuwa bila shaka kuna baadhi ya maduka makubwa na mara nyingine yanayofungamana na serikali ambayo bidhaa zao zote ni za kigeni ambapo jambo hilo ovu, kivitendo hupelekea kukosa kazi wafanyakazi wa Kiirani na kuboreka kwa hali ya wafanyakazi wa kigeni. Huku akikosoa utamaduni wa kupenda na kununua bidhaa za nje na kujigamba kwa bidhaa zilizo na nembo za kigeni, Ayatullah Khamenei amesema licha ya kuwa sisi tuna miamala na dunia (nchi za nje) lakini uagizaji, uuzaji na matumiza ya bidhaa za nje katika hali ambayo sisi wenyewe tuna uzalishaji wa ndani wa bidhaa hizo yanapaswa kuchukuliwa na kutangazwa kuwa ni jambo lililo dhidi ya thamani. Amesema: Bila shaka sisi hatuungi mkono tabia za kupindukia mipaka kuhusiana na suala hili bali tunapasa kukabiliana nalo kwa hekima na busara. Kama mfano, Ayatullah Khamenei ameashiria uagizaji nchini wa magari ya Kimarekani na kusema: Wamarekani wenyewe hawana hamu ya kununua magari hayo kutokana na matumizi yake ya juu na makubwa. Sasa je, sisi hii leo, katika mazingira haya tuje tununue magari kutoka kwa kiwanda fulani cha Marekani ambacho kinakaribia kufilisika? Hili ni jambo la kushangaza sana. Ameongeza kuwa: Wakuu na viongozi waheshimiwa wanapasa kusimama imara mbele ya mashinikizo ya siri yanayotolewa katika nyanja hizi na wala wasiruhusu kabisa masuala kama haya kutekelezwa. Ayatullah Khamenei vilevile amekosoa vikali uagiza nchini wa baadhi ya bidhaa za kigeni zisizo za dharura ambazo zinagharimu mabilioni ya fedha na kuashiria tatizo kubwa la ulanguzi na magendo ya bidhaa nchini na kuongeza: Mimi nimewatahadharisha mara kwa mara viongozi wa serikali mbalimbali kuhusiana na suala hili nao wanasema kuwa wakipandisha bei ya bidhaa magendo ya bidhaa hizo itaongezeka, hoja ambayo haikubaliki. Amesema magendo ni balaa kubwa na sumu kwa uzalishaji wa ndani. Huku akikosoa vikali kutokuwepo mapambano ya kutosha dhidi ya suala hilo, Kiongozi Muadhamu amesisitiza kwamba walio na misimamo imara zaidi wanapaswa kupewa jukumu hilo na serikali kuimarisha vyombo husika kwa ajili ya kupambana vilivyo na magendo iliyoratibiwa. Ayatullah Khamenei amesema: Bila shaka kusudio la kupambana na magendo halina maana ya kupambana na watu dhaifu ambao wanaingiza nchini bidhaa ndogondogo katika baadhi ya sehemu, bali ni mapambano dhidi ya walanguzi na wafanyamagendo wakubwa ambao huingiza nchini makumi na mamia ya makontena ya bidhaa za magendo.
Hukua akiashiria suala jingine muhimu kuhusiana na kadhia ya uzalishaji wa ndani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Mara nyingine bidhaa inaweza kuzalishwa nchini, lakini waagizaji ambao hupata faida kubwa hutumia njia tofauti zikiwemo za kutoa hongo kubwa, vitisho na hata kufanya jinai ili kuzauia uzalishaji wake. Amesisitiza kwamba suala hilo ni muhimu na la usalama mkubwa ambapo haipasi kukabiliana nalo kwa njia za kawaida tu. Katika kuendelea na hotuba yake Ayatullah Khamenei ameashiria umuhimu wa kuchuinguzwa masuala yanayozuia uzalishaji wa ndani na kuwakosoa vikali watu wanaotumia kisingizio cha teknolojia ya zamani ya uzalishaji wa bidhaa za ndani ili kupata mwanya wa kuendelea kuingiza nchini biadhaa za kigeni. Amesema: Baadhi ya watu wanaotetea uagizaji wa bidhaa za nje kila mara wanaposhindwa kwa hoja husema kuwa teknolojia ya nje ni ya kisasa na kwamba ya ndani ni ya zamani na iliyozeeka. Basi kama ni hivyo, je ni kwa nini hamtatui tatizo hilo kwa kutumia vipawa na akili hii kubwa ya uvumbuzi wa Kiirani? Kiongozi Muadhamu ameuliza: Je, akili hii ya Kiirani ambayo inaweza kutengeneza kombora linalosafiri kwa zaidi ya masafa ya kilomita 2000 na kuweza kulenga shabaha kwa uwezekano wa kukosea kwa chini ya mita 10 tu, haiwezi kutatua matatizo ya kiteknolojia ya baadhi ya sekta ikiwemo ya utengenezaji magari? Basi ni kwa nini hamuwarejei vijana kama hawa katika kutatua matatizo? Ayatullah Khamanei ameongeza kuwa baadhi ya maendeleo ya nchi ni siri na hayawezi kutangazwa hadharani la sivyo watu wote wangeshangazwa na talanta na vipawa vya juu walivyonavyo vijana wa nchi hii. Katika kufupisha maneno yake katika uwanja huo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Mimi nina dhana nzuri kuhusiana na  jamii ya wafanyakazi, waajiri na viongozi wa serikali, lakini ukweli wa mambo ni kwamba kazi inakwenda kwa mwendo wa kinyonga katika baadhi ya sehemu na baadhi ya mambo na watu wanazuia juhudi kuzaa matunda yanayohitajika. Viongozi wafanye juhudi na kwa kutambua na kuondoa kasoro hizo, waongeze kasi ya nchi kufikia maendeleo. Amesisitiza kwamba Iran kufikia kilele cha juu cha ustaarabu wa Kiislamu sio shaari wala majigambo bali ni jambo linalothibitishwa na ukweli wa mambo, suhula, sifa na uwezo wa nchi ambapo iwapo hayo yatazingatiwa, bila shaka yataandaa uwanja wa kufikiwa lengo hilo. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Bila shaka bado adui anaendelea kufanya uadui na kuweka vizuizi ambapo maadui hao wanaogozwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. Ayatullah Khamenei ameongeza: Baadhi ya wakati Wamarekani hulalamika kwa mbali kwamba ni kwa nini nyinyi mna dhana mbaya kutuhusu? Ni sawa, tunayaona mambo ambayo husababisha dhana mbaya hiyo na wala hatuwezi kuyafumbia macho. Amesema miamala ya kibenki inatekelezwa taratibu sana na kwa usumbufu mkubwa na kwamba uingiliaji wa Marekani katika miamala hiyo ni mfano wa wazi wa mambo yanayosababisha dhana mbaya hiyo kwa Marekani na kuongeza: Sasa suala la uingiliaji huo wa Marekani katika miamala ya kibenki ni jambo linalozungumziwa pia na viongozi wa serikali lakini je, ni kwa nini benki kubwa za dunia haziko tayari kushirikiana na Iran? Kiongozi Muadhamu amesema: Sababu ya benki kubwa za dunia kutoshirikiana na Iran ni ‘uogopeshaji dhidi ya Iran’ uliofanywa na ambao unaendelea kufanywa na Wamarekani. Amesema: Nimekuwa nikisema mara nyingi kwamba Wamarekani sio watu wa kuaminika na sasa sababu ya kusema hivyo inaendelea kubainika wazi. Ayatullah Khamenei ameashiria kwamba wao huandika na kusema kwenye karatasi kwamba ‘benki ziamiliane na Iran’ lakini kivitendo kufanya kinyume ili kuifanya ‘Iran iogopwe’ na kuongeza: Wamarekani wanasema Iran ni nchi inayounga mkono ugaidi na huenda ikawekewa vikwazo kutokana na uungaji mkono huo kwa ugaidi. Amesisitiza: Je, maneno hayo hutoa ujumbe gani kwa benki na pande zinazotaka kushirikiana na Iran? Ujumbe wa maneno hayo ni kwamba msiamiliane na Iran na matokeo yake kivitendo ni kuwa benki na wawekezaji wa kigeni huingiwa na woga wa kushirikiana na Wairani.
Kiongozi wa Mapinduizi ya Kiislamu amesema: Bila shaka kuhusiana na suala la ugaidi, Wamarekani ni magaidi wabaya zaidi kuliko magaidi wengine wote na kwa mujibu wa takwimu zilizopo bado wanawaunga mkono magaidi wanaojulikana wazi. Ayatullah Khamenei ameashiria mbinu nyingine inayotumiwa na serikali ya Marekani kufanya Iran iogopwe duniani ili kivitendo kufanya benki na wawekezaji wa kigeni wasishirikiane na Iran na kusema: Wao wanadai kwamba sababu ya nchi za kigeni kutoshirikiana na Iran ni hali ya ndani ya nchi hii katika hali ambayo katika mazingira ya hivi sasa hakuna ya nchi yoyote iliyo na usalama mkubwa katika eneo kama Iran na hali ya ndani ya Iran ni bora zaidi kuliko hata ya Marekani yenyewe ambako kila siku watu kadhaa huuawa, na vilevile ni salama zaidi kuliko hata nchi za Ulaya. Hali ya ndani ya Iran kinyume na wanavyotaka maadui, ni nzuri sana. Kiongozi wa Mapinduzi amesema kuwa viongozi wa Marekani kuendelea kusisitiza kwamba mfumo wa vikwazo utaendelea kutekelezwa dhidi ya Iran ni mbinu nyingine inayotumiwa na viongozi hao kwa lengo la kuendeleza siasa zao za kuifanya Iran iogopwe na hivyo kuzuia wawekezaji wa kigeni kuwekeza nchini na kusema: Sisi tunakabiliana na uadui kama huyu na tunapasa kuzingatia hilo katika kila shughuli tunayotaka kuifanya. Ayatullah Khamenei ameashiria maendeleo makubwa ambayo yamefikiwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kipindi cha miaka 37 iliyopita licha ya kuwepo uadui wa Marekani na kusisitiza: Hata kama uadui huo utaendelea kwa miaka mingine mia moja bila shaka tutazidi kuendelea wapende wasipende. Ameongeza kuwa Marekani ni adui, tuiambie moja kwa moja au tusiiambie na tuseme kwa sauti kubwa au tusisema; uadui huo hautaisha.
Ayatullah Khamenei amewausia viongozi wa mihimili yote mitatu ya serikali, idara na taasisi za Mapinduzi na vilevile wananchi kutambua nguvu na uwezo wa nchi na kuongeza: Sisi kama alivyokuwa Amir al-Mu’mineen Ali (as) tumedhulumiwa lakini tuna nguvu na iwapo tutatumia vyema uwezo wetu na kwa njia bora zaidi, za kiutu na Kiislamu zaidi bila shaka tutavishinda vizuizi vyote. Amesisitiza kwamba njia yetu sio safi (isiyo na milima na mabonde/vizuizi) na wala si yenye mawe (iliyojaa vikwazo na vizuizi) na kwamba iwapo tutategemea uwezo wetu bila shaka tutafanikiwa na kufikia maendeleo zaidi. Katika sehemu ya mwisho ya hotuba yake, Kiongozi Muadhamu ameashiria kufanyika kwa duru ya pili ya uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (bunge) siku ya Ijumaa tarehe 29 Aprili katika baadhi ya miji na kusema: Umuhimu wa duru ya pili sio mdogo kuliko umuhimu wa duru ya kwanza na wote waliotimiza masharti ya kupiga kura washiriki kwenye uchaguzi huu. Ayatullah Khamenei ameongeza: Kushiriki kwenye uchaguzi ni muhimu sana kwa sababu kama hatutashiriki kwenye uchaguzi hamu, kupendelea na utambulisho huu hautadhihirishwa kwenye masanduku ya kupigia kura.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Waziri wa Ushirika, Kazi na Masuala ya Kijamii alitoa salamu za heri ya Siku ya Wafanyakazi na kuashiria matatizo yanayowakabili wafanyakazi na wale waliostaafu na kusema kwamba katika kipindi cha miaka miwili iliyopita na kwa baraka za mazingira ya maelewano na huruma yaliyotawala kati ya wafanyakazi na waajiri, pengo lililopo kati ya ughali wa maisha na mishahara limepungua. Huku akisisitiza juu ya udharura wa kuimarishwa biashara ndogondogo na za wastani kwa ajili ya kuondoa umasikini na kubuni nafasi za kazi nchini, Bwana Rabii amesema kwamba kuimarishwa bima na kupewa bima watu milioni 10 wasio na bima ya afya, kupambana na umasikini na ufisadi, kuboreshwa kwa hali ya watoto wanaofanya kazi, kuimarishwa kwa jumuiya za ushirika, kupelekwa kwa huduma za afya kwenye maeneo ya watu masikini, uwezeshaji kwa msingi wa kuimarishwa ufundi na ujuzi, kubuniwa mpango wa msaada kwa walemavu na kuwaandalia nafasi za kazi na makazi, kutolewa bima kwa wanawake wanaosimamia familia zao, kutatua matatizo ya kijamii, na kusisitiza juu ya kulindwa heshima ya wafanyakazi ni miongoni mwa mipango na shughuli muhimu zaidi ambazo zimetekelezwa na Wizara ya Ushirika, Kazi na Masuala ya Kijamii.

 

700 /