Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Kutetea Palestina ni nembo ya kutetea Uislamu, utawala wa Kizayuni umepatwa na kiwewe zaidi

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei alasiri ya leo (Jumapili) amekutana na kufanya mazungumzo na Katibu Mkuu wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina, Bwana Ramadhan Abdullah Shallah na ujumbe unaoandamana naye. Ayatullah Khamenei ametoa uchanganuzi kamili kuhusu hali ya sasa ya Mashariki ya Kati na kusema kuwa, hali hii ni jitihada za kambi ya Magharibi inayoongozwa na Marekani kwa ajili ya kulidhibiti eneo hili kupitia njia ya vita kubwa na pana dhidi ya kambi ya Uislamu. Amesisitiza kuwa, vita kubwa inayoendelea sasa katika eneo hili ni mwendelezo wa vita vilivyoanza miaka 37 iliyopita dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na katika mpambano huo suala la Palestina ni suala la asili na kuu, na Jamhuri ya Kiislamu kama ambavyo tangu hapo mwanzoni ililitambua suala la kuitetea Palestina kuwa ni wadhifa wake, katika siku zijazo pia itaendelea kutekeleza wadhifa huo.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, msimamo wa Jamhuri ya Kiislamu katika kadhia ya Palestina si msimamo wa muda na kipindi maalumu bali tangu mwanzoni mwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kipindi cha mpambano, suala la kutetea Palestina na ulazima wa kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Israel limekuwa likikaririwa katika misimamo ya Imam Khomeini (Mwenyezi Mungu amrehemu), na baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu jambo hilo limekuwa miongoni mwa ajenda kuu za Iran; kwa msingi huo suala la kutetea thamani na malengo ya Palestina limo katika dhati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 
Ayatullah Khamenei amesema kuwa, Mapinduzi ya Kiislamu yalipata ushindi katika kipindi ambacho Wamarekani walikuwa katika kilele cha nguvu katika kanda hii na kidhahiri mambo yote yalikuwa yakiendela kwa maslahi ya Marekani; hata hivyo Mapinduzi ya Kiislamu yalitoa msukumo na roho mpya katika mwili wa jamii ya Kiislamu na kubadilisha kikamilifu hali ya Mashariki ya Kati. 
Amegusia mashinikizo mbalimbali na makubwa ya kisiasa, kipropaganda, kiuchumi na hata ya kijeshi kwa ajili ya kuyapigisha magoti Mapinduzi ya Kiislamu au kuyalazimisha kuacha misimamo yake na kusema: Kinachoendelea kwa sasa katika Mashariki ya Kati ni mwendelezo wa hujuma ya Marekani dhidi ya utawala wa Kiislamu hapa nchini. 
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, lengo kuu la vita kubwa ya sasa ya kambi ya Magharibi inayoongozwa na Marekani dhidi ya kambi ya Uislamu ni kutaka kulidhibiti eneo la Mashariki ya Kati. Ameongeza kuwa: Hali ya eneo hilo inapaswa kuchunguzwa na kuchambuliwa katika fremu hiyo na masuala ya Syria, Iraq, Lebanon na Hizbullah ni sehemu ya mpambano huo mkubwa. 
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, katika hali kama hii kuitetea Palestina ni nembo ya kuutetea Uislamu. Ameongeza kuwa: Kambi ya ubeberu inafanya jitihada kubwa kuarifisha mpambano huo mkubwa kuwa ni vita baina ya Shia na Suni. 
Ameashiria kwamba huko Syria hakuna serikali ya Kishia na kusema: Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaitetea serikali ya Syria kwa sababu watu wanaopigana na Syria kwa hakika ni wapinzani wa asili ya Uislamu na wanahudumia maslahi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel. 
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema, madai ya kuwepo mapigano baina ya Shia na Suni ni njama ya kikoloni na Kimarekani. Amesisitiza kuwa, suala muhimu zaidi katika kipindi cha sasa katika eneo la Mashariki ya Kati ni kutambua vyema kambi mbili kuu za mapigano hayo makubwa na kutambua nafasi yetu sahihi, kwa sababu iwapo hatutajua vyema mpaka unaotenganisha baina ya kambi hizo mbili yumkini tukapigana na kambi ya Uislamu bila ya kujua.
Ayatullah Khamenei amesisitiza kuwa, kwa mtazamo huo mpana kuhusu masuala ya kanda hii, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaitambua Marekani kuwa ni adui mkuu na utawala wa Kizayuni wa Israel uko nyuma yake. Ameongeza kuwa, Iran daima inakutambua kutetea na kuunga mkono kadhia ya Palestina kuwa ni wadhifa na jukumu lake na itaendelea kutekeleza wadhifa huo.
Ameashiria vikwazo vikubwa na visivyo na kifani vya Marekani na waitifaki wake dhidi ya Mfumo wa Kiislamu wa Iran katika miaka ya hivi karibuni na kusema: Lengo kuu la vikwazo hivyo ni kuiondoa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika njia na mwelekeo wake lakini hawakuweza kufikia malengo yao na hawatayafikia katika siku zijazo. 
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: "Tunaamini kwamba katika mpambano huo mkubwa tutapata ushindi na hadi sasa tumekuwa tukiibuka washindi, kwa sababu maadui wamekuwa wakifanya mikakati ya kuiangamiza Jamhuri ya Kiislamu lakini si tu kwamba utawala wa Kiislamu umeendelea kuwepo, bali siku baada ya siku umepiga hatua kubwa za maendeleo katika nyanja mbalimbali na umeimaika zaidi. 
Ayatullah Khamenei pia ameashiria matamshi yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina kuhusu baadhi ya njama zinazofanywa kwa ajili ya kuzidisha mashinikizo dhidi ya harakati ya Hizbullah ya Lebanon na kusema: Hizbullah ni imara zaidi kiasi kwamba haiwezi kutetereshwa na hatua kama hizo na leo hii wahka na woga wa utawala wa Kizayuni wa Israel mbele ya Hizbullah ni mkubwa zaidi kuliko huko nyuma. 
Ameashiria kanuni ya Mwenyezi Mungu ya kushinda kambi ya haki na kusema: Ushindi huo unakuja japokuwa utaandamana na panda shuka na misukosuko, na hapana shaka kwamba ahadi ya Mwenyezi Mungu kwa wanaoinusuru dini yake, itatimia.
Mwanzoni mwa mkutano huo Katibu Mkuu wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina Dakta Ramadhan Abdullah Shallah ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa misaada na misimamo yake katika kadhia ya Palestina na ametoa ripoti kuhusu hali ya sasa ya eneo la Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi mwa Mto Jordan. Amesema kuwa wananchi wa Gaza wanaendelea kusimama imara licha ya mzingiro wa Wazayuni na hali ngumu, na huko katika Ukingo wa Magharibi wimbi la Intifadha limeshika kasi kwa hima na azma ya kizazi kipya cha vijana wa Palestina licha ya ukandamizaji mkubwa na wa pande zote wa utawala wa Kizayuni. 
Amesema kuwa harakati za mapambano huko Palestina zimejiandaa vya kutosha na kwa uwezo wa kutahayarisha. Ameashiria hali ya sasa ya Mashariki ya Kati na kusema: Wamarekani na nchi vibaraka wao wanafanya mikakakti ya kudhihirisha sura isiyo sahihi kuhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kuwafanya walimwengu wasahau jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel na kueneza uvumi wa kuwepo vita baina ya Shia na Suni; kwa msingi huo mashinikizo dhidi ya Hizbullah yameongezeka lakini Jihad Islami ya Palestina inatambua vyema hali ya sasa na inasisitiza udharura wa kuungwa mkono Hizbullah na mapambano mkabala wa Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.             

700 /