Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Hotuba ya Kiongozi Muadhamu katika hadhara ya walimu kutoka pembe zote za nchi

Kizazi kijacho kilelewe kwenye misingi ya utambulisho huru na utukufu wa kidini

Leo asubuhi (Jumatatu) Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amezungumza mbele ya hadhara ya maelfu ya walimu na walimu wapya kutoka pembe zote za nchi ambapo amewashukuru kutokana na juhudi kubwa zinazofanywa na jamii ya walimu nchini. Amesema malezi ya kizazi kijacho kwenye misingi ya utambulisho huru na mtukufu ulio na viwango bora na wenye athari muhimu kwenye jamii ni jukumu halisi na lenye umuhimu mkubwa la Wizara ya Elimu na Malezi pamoja na jamii ya walimu nchini. Amesisitiza kwamba iwapo jamii itakuwa na sifa hizi, bila shaka hapo ndipo uchumi ngangari na usiotegemea mafuta, ulio na utamaduni huru, marekebisho ya matumizi ya bidhaa na moyo wa mapambano mkabala wa tamaa na matakwa ya ziada ya Marekani yanapopata maana. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa kazi ya ualimu ni kazi ngumu sana na kuongeza kuwa kazi inayofanywa kwa ikhlasi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ni ya kudumu na inayoleta wongofu na kwamba bila shaka kuna mazingira ya kazi yenye ikhlasi kwenye kazi ya ualimu. Ayatullah Khamenei amesema harakati na athari za Shahid Ayatullah Mutahhari ni mfano unaong’ara wa kazi yenye ikhlasi na baraka na kuongeza kuwa natija ya ikhlasi ya alimu huyo aliyefahamu vyema zama zake na mahitaji ya watu ni kubakia kwa athari zake muhimu kwa kadiri kwamba hata baada ya kupita makumi ya miaka tokea kuuawa kwake shahidi huyo lakini bado wanafikra wananufaika kwa njia bora zaidi na athari (vitabu/maandishi) zake. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Bila shaka ikhlasi na kukinai kwa jamii ya walimu hakupasi kupelekea viongozi waghafilike na masuala ya kimaada na kimaisha ya jamii hiyo inayofanya bidii kubwa, na kama ambavyo tumesema mara kadhaa na bado tunasema, kila fedha na bajeti inayotumika katika masuala ya elimu na malezi kwa hakika ni uwekezaji. Kiongozi Muadhamu kisha amezungumzia maudhui muhimu ya hotuba yake na kusema: Maudhui kuu ni hii kwamba je, Wizara ya Elimu na Malezi inataka kulea kizazi cha baadaye kilicho na sifa gani, na je, nchi inahitajia kizazi cha aina gani katika kuendeleza njia yake? Kabla ya kubainisha sifa zinazihitajika kwa ajili ya kulea kizazi cha baadaye, Ayatullah Khamenei ameashiria nukta moja muhimu na kusema: Sisi kwa ajili ya kulea kizazi cha baadaye hatuko kwenye mazingira na medani tupu isiyo na washindani bali tunakabiliana na mshindani  na adui ambaye anajulikana kwa jina la ‘mfumo wa ubeberu wa kimataifa.’ Amesema Huenda baadhi ya watu wakashangaa na kuuliza, kuna uhusiano gani kati ya elimu na malezi na mfumo wa ubeberu wa kimataifa? Hii ni katika hali ambayo mfumo wa ubeberu una mipango madhubuti kwa ajili ya kizazi cha vijana wa mataifa mbalimbali na hasa wa Iran. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Marekani, mabepari wa Kizayuni na baadhi ya madola ya kiistikbari ndio dhihirisho la mfumo wa ubeberu wa kimataifa na kusisitiza: Mfumo wa ubeberu unataka vizazi vijavyo vya mataifa viwe na fikra, utamaduni, mitazamo na mapendeleo kama yake kuhusiana na masuala ya kimataifa na mwishowe kuwafanya wasomi, wanasiasa na watu walio na athari katika jamii wafikirie na kufanya kama unavyotaka mfumo huo.
Kwa kuzingatia mpango huo mkongwe wa kiutamaduni wa ukoloni, Ayatullah Khamenei amesema: Wanafikra wa Magharibi wamesema mara kwa mara kwamba badala ya kuanzisha vita vya kuzikoloni nchi kama ilivyofanyika katika karne ya kumi na tisa, njia bora na yenye gharama ndogo zaidi ni kupenyeza fikra na utamaduni wetu kwenye kizazi cha vijana wa nchi hizo na kuwalea wasomi na wanafikra ambao watakuwa wakiuhudumia mfumo wa ubeberu kama askari watiifu kwa mfumo huo. Amesema baadhi ya serikali za Kiarabu za eneo ni mfano wa wazi unaotokana na mpango huo wa uistikbari na kuongeza: Serikali hizo hivi sasa zinafanya yaleyale mambo yanayotakiwa na Marekani na hata kulipia gharama zote za mipango hiyo ya Marekani na bila kupata fursa wala malipo yoyote isipokuwa kulindiwa usalama na Marekani na kuzizuia zisianguke. Huku akisisitiza kwamba mshindani wetu ana mpango kama huu kwa ajili ya kizazi kijacho cha nchi yetu Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza juu ya kuimarishwa na kuenezwa fikra, utamaduni na lugha za kizalendo na kitaifa kwa kuongeza: Kwa bahati mbaya katika baadhi ya sehemu badala ya kuimarishwa lugha ya Kifarsi lugha ya Kiingereza ndiyo inayoenezwa kwa kadiri kwamba sasa lugha hiyo inafundishwa kwenye shule za chekechea. Ayatullah Khamemeni amesema kwamba, suala hilo halina maana ya kupinga lugha za kigeni bali mjadala halisi ni kwamba utamaduni wa kigeni unaenezwa miongoni mwa watoto na vijana nchini. Huku akisisitiza kwamba nchi nyingine zina mipango ya kukabiliana na kuenezwa lugha na utamaduni wa kigeni katika nchi hizo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Kwa masikitiko makubwa hakuna mpango maalumu wa kukabiliana na susala hilo nchini kwetu na uwanja umewachwa wazi kwa ajili ya kuenezwa utamaduni wa kigeni. Kiongozi Muadhamu ameashiria aina mbalimbali za vikwazo na matatizo yanayoanzishwa kwa makusudi ili kuzuia kuenezwa kwa lugha ya Kifarsi katika baadhi ya nchi za Magharibi na kusema: Katika hali ambayo wao hawaruhusu kufundishwa kwa lugha ya Kifarsi, sisi hapa tunaruhusu kuenezwa kwa lugha na utamaduni wao. Je, suala hili kwa kweli ni la kimantiki? Ayatullah Khamenei amesema: Matamshi haya hayana maana ya kusimamishwa mafunzo ya lugha ya Kiingereza katika shule humu nchini, lakini suala muhimu ni kwamba tufahamu tunakabiliana na mshindani gani na ana mipango gani madhubuti kwa ajili ya kukiathiri kizazi kijacho cha nchi. Kisha amebainisha vipimo na sifa zinazohitajika kwa ajili ya kulea kizazi cha baadaye nchini na kusema: Kipimo muhimu zaidi kinachopasa kuzingatiwa katika malezi ya wanafunzi, ni kubuniwa kwa utambulisho huru,wenye utukufu na wa kidini kwa ajili ya kizazi cha baadaye. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza: Tunapasa kuwalea vijana kwa namna ambayo itawawezesha kufuatilia siasa, uchumi na utamaduni huru na kuona kila aina ya utegemezi katika masuala hayo kuwa ni jambo linalochukiza. Amesema nchi iko kwenye hatari ya kudhurika kuhusiana na suala hilo na kuongeza: Hamu ya kupindukia ya kutumia ibara za kigeni ni aina moja ya madhara hayo ambayo tumeyarithi kutoka zama za Taghuti (Shah). Amesema moja ya njia muhimu za kufikia uchumi ngangari ni kupatikana kwa utambulisho huru miongoni mwa vijana na kuongeza kuwa madamu moyo wa kujitegemea, kuwa ngangari na kusimama imara hautakuwepo, hata kama viongozi wataandaa mamia ya vikao kwa ajili ya kuhamasisha watu kuhusiana na suala la uchumi ngangari, suala hilo mwishowe halitakuwa na natija kamili wala sahihi. Kiongozi Muadhamu amesema uchumi ngangari, usiotegemea mafuta na utamaduni huru hupata maana pale utambulisho huru unapokuwa kwenye jamii.
Ayatullah Kahamenei amesema sifa bora na za kipekee pamoja na fikra zinazoibua harakati na mwamko katika wanafunzi ni jukumu jingine zito la walimu na Wizara ya Elimu na Malezi na kuongeza: Imani, uimarishaji fikra, ushiriki na ushirikiano wa kijamii na marekebisho ya matumizi ya bidhaa ni miongoni mwa sifa na vipimo hivyo muhimu ambavyo vinapaswa kuimarishwa katika kizazi kijacho. Akiashiria matatizo yaliyopo kuhusiana na matumizi ya bidhaa nchini Kiongozi Muadhamu amebainisha baadhi ya mifano na kusema: Matumizi ya bidhaa za kigeni na magendo ya bidhaa za anasa yanayogharimu makumi na mamia ya mabilioni ya fedha ni mfano wa matumizi mabaya ya bidhaa yaliyopo nchini jambo ambalo linapasa kurekebishwa na moja ya miundombinu ya kulirekebisha ni kurekebisha utamaduni miongoni mwa kizazi cha vijana. Kiongozi Muadhamu amesema kuvumilia wapinzani ni sifa nyingine kati ya sifa muhimu kwa ajili ya kizazi cha baadaye na kuongeza: Kumvumilia mpinzani ni jambo ambalo halijaimarishwa kwenye jamii kwa sababu mtu anapokejeliwa kidogo tu basi humpiga ngumi kifuani mtu aliyemkejeli (bila kusita). Hii ina maana ya kutowavumilia wapinzani.
Ayatullah Khamenei amesema tabia njema, ucha Mungu na kutokubali ubwenyenye ni miongoni mwa sifa nyingine za lazima katika malezi ya wanafunzi na kusisitiza kwamba kuimarishwa kwa sifa hizi katika kizazi kijacho na kukiwekea utamaduni unaofaa ni miongoni mwa majukumu makubwa ya walimu na Wizara ya Elimu na Malezi. Huku akisisitiza kwamba Wizara ya Elimu na Malezi haiwezi kutekeleza wadhifa huo mtakatifu peke yake, ameashiria nafasi ya sekta na idara tofauti katika utekelezaji wa jukumu hilo na kusema: Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia masuala ya Elimu na Malezi ni miongoni mwa sekta zilizo na athari kubwa na jukumu zito katika uwanja huo na zinapasa kuchukua hatua muhimu, zenye lengo maalumu, erevu na salama katika mtazamo wa itikadi, kisiasa na kimaadili katika njia hiyo na bila shaka kila aina ya uzembe katika uwanja huo ni pigo kwa masomo na malezi ya kizazi kijacho.
Kiongozi MUadhamu amesema Taasisi ya Idhaa na Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB ni moja ya idara zilizo na majukumu muhimu katika suala zima la kuweka mikakati ya viwango bora vya kizazi cha baadaye na kuimarisha utamaduni katika uwanja huo. Amekosoa utendaji wa Taasisi ya Idhaa na Televisheni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema: Mwaka uliopita pia suala la kuwepo udharura wa Taasisi ya Idhaa na Televisheni IRIB kuweka mipango madhubuti na sahihi kwa ajili ya kizazi cha vijana lilizungumziwa lakini kwa masikitiko hakuna kilichofanyika. Amesema: Taasisi ya Idhaa na Televisheni inapasa kuwa na agenda maalumu ya mafunzo kwa kunufaika na wanafikra na wataalamu.  Ayatullah Khamenei  ameashiria barua ya mmoja wa wanafunzi waliokutana naye wiki iliyopota, ambaye alilalamikia kutokuwepo kwa vipindi vinavyofaa na vyenye taathira kwenye Taasisi ya Idhaa na Televisheni kwa vijana wa shule za sekondari na kusema: Chombo hiki cha kitaifa cha upashaji habari kinapasa kutumia njia za usanii na utaalamu kuandaa vipindi vya kuwakinaisha vijana kifikra, kiroho, kidini na kielimu, na vipindi vilivyopo hivi sasa katika baadhi ya kanali havikidhi mahitaji katika uwanja huu kwa vyovyote vile. Amesema Wizara ya Mawasiliano pia ni idara nyingine inayopasa kuwajibika kuhusu suala la malezi ya kizazi cha vijana ambapo huku akiashiria kuenea kwa mawasiliano ya mtandao wa intaneti na kuenea kwa kasi kubwa kwa mawasiliano hayo kila siku na kuendelea kufungamana vijana na mawasiliano hayo ya mtanao Ayatullah Khamenei amesema: Hakuna mtu anayepinga matumizi ya intaneti lakini jambo la msingi ni kuwa katika uwanja kama huu ambao baadhi ya wakati una mtelezo, uwanja wa matumizi sahihi ya mtandao unapasa kuandaliwa na  sio kuwachwa ovyo bila ya kuwepo udhibiti wa aina fulani. Huku akilalamikia Wizara ya Mawasiliano na Baraza Kuu la Mtandao wa Intaneti Ayatullah Khamenei amesema hakuna mtu aliye na nia ya kufunga mtandao wa intaneti nchini kwa sababu hilo si jambo la kimantiki lakini akahoji ni kwa nini sisi tumewacha wazi mtandao wa intaneti katika hali ambayo nchi nyinginezo zimeuwekea vidhibiti kwa ajili ya kulinda utamaduni wao? Amesema kazi nyingine ya lazima inayopasa kufanywa kuhusu suala la elimu na malezi ni kuweka moyo wa uchangamfu na ujana kwenye jamii ya walimu na hivyo kuukarabati mfumo wa elimu nchini. Kiongozi Muadhamu amaeashiria kuzeeka kwa mfumo wa elimu nchini na kusema: Mfumo wa elimu wa hivi sasa umechukuliwa kutoka kwenye mfumo wa masomo wa Ulaya na umeendelea kubaki hivyohivyo na kuzeeka bila kuguswa ni kana kwamba ni vitu vya maonyesho ya kale. Hii ni katika hali ambayo mfumo huo unapaswa kukarabatiwa na kufanywa kuwa mpya.
Ayatulla Khamenei amesema ni makosa makubwa kuufanyia marekebisho mfumo wa elimu na kuufanya kuwa wa kisasa kwa kuiga mitindo ya Magharibi na kuongeza: Bila shaka ni vizuri kunufaika na uzoefu lakini wanafikra na wataalamu (wa ndani ya nchi ) wanapasa kubuni na kutekeleza mfumo wa kisasa wa elimu na malezi. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema uzingatiaji wa umuhimu wa vituo vya ufundi katika kuimarisha na kunyanyua viwango vya taaluma na ujuzi wa kizazi cha vijana ni mojawapo ya vipaumbele vya mfumo wa elimu na malezi na kuongeza: Kwa mujibu wa ripoti kuna aina 12,000 za kazi nchini lakini je, kuna ulazima wa wanafunzi wote ambao wana vipawa na talanta mbalimbali kufuata njia moja tu ya masomo? Kiongozi Muadhamu amesisitiza: Vipawa vya wanafunzi vinapaswa kutambuliwa na kulelewa ili viwe chanzo cha uvumbuzi wa kazi na ufundi mbalimbali. Kukosolewa kwa matumizi ya baadhi ya majina na nembo zilizokuwa zikitumika katika zama za Taghuti kama vile Pishahangan (dalili/ishara) ni suala jingine lililozungumziwa na Kiongozi Muadhamu katika hotuba yake kwa viongozi wa masuala ya elimu na malezi. Amesema: Katika mfumo wa elimu na malezi na kwa kuwepo kwa jumuiya kama vile Basij ya Masomo na Umoja wa Jumuiya za Kiislamu za Wanafunzi, ibara na lafudhi za zamani ambazo zina maana maalumu hazipasi kutumika. Katika kuendelea na hotuba yake, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameazungumzia shule za serikali na zisizo za serikali na kusema, katika katiba suala la elimu na malezi limewekwa chini ya usimamizi wa serikali lakini hii haina maana ya serikali kubeba mabegani mzigo na majukumu yote yanayohusiana na elimu na malezi. Amesema, pamoja na hayo serikali inapasa kuwa mstari wa mbele kuhusiana na suala zima la elimu na malezi na kwa msingi huo kubadilishwa kila mara kwa shule zinazosimamiwa na serikali na kufanywa kuwa za kibinafsi mbapo baadhi yazo hutoza karo kubwa, si dharura kuwa ni jambo sahihi na la sawa. Kiongozi Muadhamiu amesisitiza: Viwango na ubora wa shule za serikali unapaswa kuinuliwa kiasi cha kuzifanya familia ziwe na hamu kubwa ya kuwapeleka watoto wao kwenye shule hizo. Ayatullah Khamenei ameashiria usalama wa kifikra na wa kivitendo wa Waziri wa Elimu na Malezi na kusisitiza juu ya udharura wa kunufaika na fursa hiyo katika utekelezaji wa majukumu mazito katika wizara hiyo na kuongeza: Chuo Kikuu cha Walimu ni moja ya vituo muhimu sana ambapo nguvu na uwekezaji unapaswa kuwekwa humo kadiri ya uwezo kwa ajili ya kunyanyua viwango na ubora wake. Katika kukalisha hutoba yake, Kiongozi Muadhamu amesisitiza juu ya umuhimu wa kujengwa na kuimarishwa nguvu ya nchi na vilevile nafasi muhimu ya walimu katika njia hiyo na kusema kuwa elimu ndilo jambo muhimu katika upatikanaji wa nguvu hiyo na kuongeza: Nguvu haipatikani tu kwa kutumia silaha bali elimu, imani, shakhsia ya kitaifa, mapambano na utambulisho wa kimapinduzi ni masuala yanayoleta nguvu. Ameendelea kusema: Wakati adui anapoona nguvu zako, bila shaka atalazimika kurudi nyuma. Lakini tunaposita, kulegea, kukataa au kuogopa kuonyesha misimamo yetu thabiti na nguzo za nguvu yetu mbele ya adui bila shaka adui huyo atakuwa na kiburi na ukaidi.
Ameahiria mswada ambao umewasilishwa kwenye Congress ya Marekani dhidi ya manuva ya kijeshi ya majini ya Iran na kusema: Hii leo adui anatamka maneno ambayo ni makubwa kuliko kinywa chake, na kwa mfano anapanga kwamba Iran asiweze kufanya manuva ya kijeshi katika Ghuba ya Uajemi, katika hali ambayo maneno haya ni ghalati ya ziada (ya kipumbavu na yasiyo na thamani).
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema taifa kubwa na lenye mwamko la Iran lina uwezo wa kujibu matakwa haya ya ziada na kuongeza: Ghuba ya Uajemi ni nyumba na mahali pa mahudhurio ya Wairani na fukwe za Ghuba ya Uajemi na nyingine nyingi za Bahari ya Oman ni za taifa hili shupavu. Kwa msingi huohuo tunapasa kuwepo, kufanya manuva na kudhihirisha nguvu zetu katika eneo hili. Ni Wamarekani ndio wanapasa kusema ni kwa nini wametoka upande ule wa dunia na kuja hapa kufanya kufanya manuva. Kiongozi Muadhamu amesema, hivi ndivyo madola yenye matakwa ya ziada yanavyopaswa kukabiliwa. Amesema kudumu na kuendelea kuongezeka nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kila siku ni ishara tosha ya kushindwa adui na kuongeza: Qur’ani imetufundisha kwamba tunapasa kujitayarisha kwa namna ambayo itamfanya adui daima awe na woga na hofu. Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Bwana Ali Asghar Fani Waziri wa Elimu na Malezi alitoa heshima na kuwakumbuka Mashahidi Mutahhari, Rajai na Bohanar na pia kutoa salamu za heri kwa Wiki ya Walimu na kusisitiza kwamba Wizara ya Elimu na Malezi inajitahidi kuweka msingi mzuri wa kutekelezwa kivitendo uchumi ngangari kupitia mikakati ya utamaduni. Bwana Fani amebainisha kwamba kwa kutilia maanani kwamba mipango ya kistratijia ya elimu na malezi katika kipindi cha Mpango wa Sita wa Ustawi wa Uchumi itasimama juu ya msingi wa utekelezwaji wa Waraka wa Mabadiliko, kubuniwa kwa ramani ya njia kwa ajili ya kuleta mabadiliko katika mfumo wa masomo, kubainishwa taaluma mpya, kuboreshwa hali ya walimu, kubuniwa mipango ya kistratijia kwa ajili ya wafanyakazi wa Wizara ya Elimu na Malezi, Vyuo Vikuu na Kituo cha Mafunzo ya Walimu cha Sahidi Rajai, kuimarishwa ushiriki wa umma na kuboreshwa vituo vya utafiti vya wanafunzi ni miongoni mwa shughuli muhimu zaidi ambazo zilitekelezwa na wizara yake mwaka uliopita.

 

700 /