Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu:

Uhusiano wa Iran na Korea Kusini haupaswi kuathiriwa na hila za Marekani

Kiongozi Maudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei leo jioni (Jumatatu) ameonana na kufanya mazungumzo na Rais Park Geun-hye wa Korea Kusini hapa mjini Tehran. Katika mazungumzo hayo Ayatullah Khamenei akiashiria mtazamo chanya wa Jamhuri ya Kiislamu katika suala la kupanua ushirikiano baina yake na nchi za bara la Asia na kulitaja suala la kuwepo mawasiliano ya kudumu baina ya Iran na Korea Kusini kuwa ni jambo lenye manufaa sana kwa nchi zote mbili. Amesisitiza kuwa, maafikiano na mikataba inayowekwa baina ya nchi mbili inapaswa iwe kwa namna ambayo haitaweza kuathiriwa na mambo ya pembeni na vikwazo kwa sababu haifai kwa uhusiano wa nchi kama Korea Kusini na Iran kuathiriwa na matakwa ya Marekani.
Ayatullah Khamenei amesema, kuweko mabadilishano ya uzoefu katika nyuga mbalimbali za kielimu, kiteknolojia, kisiasa, kijamii na kiusalama kuna  manufaa kwa nchi zote hizi mbili na kuongeza kuwa: Sisi katika siasa zetu za kigeni, tunapendelea zaidi kuwa na ushirikiano na nchi za Asia kwa sababu tunashirikiana katika mambo mengi ya kiutamaduni na kihistoria na ni kwa sababu hiyo ndio maana tunaamini kuwa, kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kufikiwa maelewano, mwafaka na ushirikiano baina ya nchi za bara hili ikiwemo Korea Kusini ambayo ni moja kati ya nchi zilizoendelea barani Asia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amegusia matatizo makubwa ya kiusalama yaliyopo katika eneo la Mashariki ya Kati na duniani kwa ujumla na kusisitiza kwamba: Kama hakutakuwapo mapambano ya kweli dhidi ya hatari ya ugaidi na ukosefu wa usalama, basi itakuwa vigumu sana kukabiliana na hatari hiyo katika siku za usoni na hakuna nchi yoyote itakayobakia salama mbele ya hatari ya ugaidi.
Vilevile ameashiria jinsi Wamarekani wanavyougawa ugaidi katika makundi mawili ya ugaidi "mzuri" na ugaidi "mbaya" na kusema kuwa: Wamarekani wanajinadi kuwa wanapambana na ugaidi lakini kivitendo hawapambani kwa dhati na ugaidi wakati ambapo ugaidi wa namna yoyote ile ni hatari kwa usalama wa mataifa yote duniani na sababu yake ni kuwa, iwapo usalama na amani haitakuwepo, maendeleo yanayotakiwa nayo hayawezi kupatikana.
Ayatullah Khamenei vilevile amezungumzia ushirikiano na maafikiano baina ya nchi mbili za Iran na Korea Kusini na kugusia pia mambo yanayopasa kupewa kipaumbele katika ushirikiano wa pande hizo mbili.  Amesema: Kuna uwezekano mkubwa wa kuwepo ushirikiano wenye faida kubwa baina ya Iran na Korea Kusini lakini vipaumbele vyetu katika ushirikiano huo havimalizikii tu katika masuala ya biashara bali inabidi kutiwe saini mikataba inayohitajiwa na Iran katika miundombinu na uchumi kwa ujumla.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema pia kuwa, kutoathiriwa na mambo ya pembeni kwa maelewano na mikataba ya pande mbili ni miongoni mwa mambo ya msingi yanayopasa kupewa kipaumbele katika ushirikiano wa nchi mbili na kusisitiza kuwa: Si sahihi kuruhusu uhusiano wa Iran na Korea Kusini ufungamanishwe na vikwazo na ushawishi na hila za Marekani, bali inabidi uhusiano wa nchi hizi mbili uwe wa kuendelea, wa kudumu, usiotetereka, wa kiudugu na wa kupendana kikweli kweli.
Vilevile amegusia historia takriban ndefu - lakini yenye panda shuka na misukosuko mingi - ya uhusiano wa Iran na Korea Kusini na kusisitiza kuwa: Kwa bahati nzuri serikali iliyoko madarakani huko Korea Kusini hivi sasa ni serikali inayopenda maelewano na kwa upande wake, Iran ina uwezo mkubwa ikwia ni pamoja na nguvu kazi mahiri ya vijana wenye vipaji na wasomi, suala ambalo linatoa fursa ya kuwepo ushirikiano wa kudumu, mpana na usioyumba baina ya nchi mbili.
Katika mazungumzo hayo yaliyohudhuriwa pia na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Rais Park Geun-hye wa Korea Kusini amesema kuwa ziara yake ya kutembelea Tehran ni fursa yenye thamani kubwa kwa ajili ya kustawisha uhusiano wa pande mbili na kuzidisha kiwango cha kuaminiana. Ameongeza kuwa: Sisi hata katika kipindi cha kuwekewa vikwazo Iran tulijitahidi kuendelea kuwepo nchini Iran kadiri tulivyoweza.
Rais wa Korea Kusini amesema, Iran ni nchi yenye fursa nyingi yenye nguvu kazi muhimu, madhubuti na yenye taathira kama ambavyo pia ni nchi iliyopo kwenye eneo la kijiografia lenye umuhimu wa kipekee. Amesema: Ni matumaini yetu kuwa uhusiano wa nchi hizi mbili hususan katika sekta ya uchumi ya ustawi, utaimarika zaidi.
Rais Park Geun-hye wa Korea Kusini amegusia pia mitazamo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu ustawi wa kiuchumi wa Iran na vilevile sisitizo lake la mara kwa mara la kutiliwa mkazo ustawi wa kielimu, kiuchumi na kiviwanda kwa kutegemea nguvu na suhula za ndani ya nchi na kusema: Nina yakini kwamba sisitizo lako juu ya ustawi na juu ya kuboreshwa uchumi wa Iran litailetea nchi hii mustakbali mzuri sana, na sisi pia tuko tayari kuzidisha ushirikiano wetu katika nyuga tofauti kama vile mazingira, sayansi na teknolojia pamoja na masuala ya kiuchumi. 

700 /