Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu katika hadhara ya washiriki wa mashindano ya Qur’ani

Marekani ni taghuti na shetani mkubwa

Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapiduzi ya Kiislamu ya Iran leo Jumatano amewakaribisha washiriki wa duru ya 33 ya mashindano ya kimataifa ya Qurani Tukufu yaliyomalizika ramsi hapa mjini Tehran hapo jana Jumanne. Amesema imani kwa Mwenyezi Mungu na kumkufuru taghuti ni msingi wa asili na wa kweli wa nguvu, na huku akisisitiza kwamba Marekani ni taghuti na shetani mkubwa ameongeza kuwa leo wadhifa na jukumu muhimu zaidi la maulama, wanafikra na wasomi ni  kufafanua mambo na kufanya jihadi ya mwamko katika kukabiliana na hila za mataghuti na kuutaka Umma wa Kiislamu pia usihadaike na hila hizo wala kutishwa na vitisho vyao. Huku akiwashukuru waandaaji na wasimamizi wa mashindano haya ya Qur’ani, Kiongozi Muadhamu amesema kuwa Qur’ni ni muhimili wa umoja kati ya Umma wa Kiislamu na kuongeza kuwa katika hali ambayo siasa za uistikbari zimesimama kwenye msingi wa kuleta hitilafu na mivutano kati ya Waislamu, Umma wa Kiislamu unapasa kushikamana na neema hiyo kubwa ya Mwenyezi Mungu katika kufuata njia ya umoja na mshikamano. Ayatullah Khamanei amesema kuwa moja ya baraka za vikao vya Qur’ani ni kufarijika matabaka mbalimbali ya watu na hasa tabaka la vijana na  kuongeza: Umma wa Kiislamu hii leo unahitajia mafudisho, fikra na maarifa ya Qur’ani kuliko wakati mwingine wowote kwa sababu hali halisi ya maisha ya Waislamu iko mbali sana na Qur’ani. Huku akiashiria juhudi kubwa zinazofanywa na madola ya kitaghuti kwa ajili ya kutoa pigo dhidi ya Uislamu na Umma wa Kiislamu, Ayatullah Khamenei amesema: Wao wanafahamu vyema kuwa iwapo Waislamu watapata nguvu na sauti yao kusikika na kuwa kubwa, bila shaka hawataweza tena kuyadhulumu mataifa na suala la Palestina kwa maana ya kughusubiwa taifa la Kiislamu litaondoka na kusahaulika kabisa.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema siri ya kuvunjwa njama hizo ni kushikamana kikamilifu na Qur’ani Tukufu na kupata misingi halisi ya nguvu. Ameongeza kuwa nguvu halisi inapatikana katika imani, kusimama imara na kukufuru taghuti. Huku akielezea masikitiko yake kuhusiana na hatua ya baadhi ya nchi ya kushikamana na taghuti badala ya Mwenyezi Mungu, Ayatullah Khemeni amesisitiza kwamba nchi ambazo zinatekeleza siasa za Marekani katika eneo kwa hakika zinafanya hiana dhidi ya Umma wa Kiislamu na kuandaa uwanja wa Marekani kupenya zaidi katika eneo. Amesema, imani na uthabiti wa taifa la Iran na mapambano yake katika kukabilian ana matakwa ya ziada ya Marekani ndicho chanzo halisi cha nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusisitiza kwamba sababu ya madola makubwa kuliogopa taifa la Iran na kutekelezwa njama tofauti dhidi ya taifa hili ni nguvu yake iliyosimama juu ya msingi wa Uislamu na kwamba bila shaka adui anauogopa Uislamu wenye nguvu na ulio shujaa. Huku akisisitiza kwamba misimamo na utendaji wenye nia nzuri wa Iran ndicho chanzo cha kuwa na athari na ushawishi wa nchi hii miongoni mwa Waislamu na sababu nyingine ya nguvu na uwezo mkubwa wa Mfumo wa Kiislamu, Ayatullah Khamenei amesema kuwa si ahadi za mataghuti zimeweza kulihadaa taifa la Iran wala vitisho vyao kulifanya liogope. Ayatullah Khamanei amesema kuwa moja ya mahitaji muhimu ya ulimwengu wa Kiislamu ni kutohadaika na ahadi za madola makubwa na pia kutoogopa vitisho vyao. Ameongeza kuwa hii leo wadhifa na jukumu muhimu zaidi la watu wote kwenye Umma wa Kiislamu na hasa maulamaa, wanafikra na wasomi wa nchi za Kiislamu ni mapambano kwa ajili ya kuleta mwamko na jihadi ya ufafanuzi wa mambo kuhusiana na uhalisi wa mambo katika ulimwengu wa Kiislamu. Amesema kudhihiri kwa makundi ya kigaidi na kitakfiri katika eneo na kuzua vita na hitilafu miongoni mwa Waislamu kwa niaba ya maadui ni nitija ya upotovu na kutokuwa na mwamko na kusema: Vikao vya Qur’ani vinapasa kutumika kwa ajili ya kuleta mwamko na watu wanaoshiriki kwenye vikao hivi kutoka nchi mbalimbali wanapasa kuongoza na kuleta utambuzi wa mambo katika nchi zao. Huku akisisitiza kuwa msaada na nusra ya Mwenyezi Mungu inatokana na harakati ya mataifa ya Kiislamu ambayo nayo (harakati hiyo) inatokana na jihadi ya mwamko. Kiongozi Muadhamu amesema kuwa hakuna shaka  kwamba hatimaye mrengo wa kufri utalazimika kusalimu amri mbele ya mrengo wa Uislamu wa mapambano na wa jihadi.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Mudhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam wal Muslimeen Muhammadi, Mwakilishi wa Kiongozi Muadhamu ambaye pia ni Mkuu wa Taasisi ya Wakfu na Masuala ya Kheri, amesema kuwa kaulimbiu ya duru hii ya 33 ya mashindano ya kimataifa ya Qur’ani Tukufu ilikuwa ni ‘Kitabu Kimoja, Taifa Moja’ ambapo washiriki 130 kutoka nchi 70 za dunia wameshiriki katika vitengo vya hifdhi na kiraa ya kitabu hicho kitakatifu. Huku akiwaenzi mashahidi wa maafa ya Mina na hasa mashihidi wa Qur’ani Tukufu Hujjatul Islam wal Muslimeen Muhammadi amesema kuwa mahudhurio ya kwanza ya wasomaji Qur’ani wasio na uwezo wa kuona kutoka nchi tofauti katika mashindano hayo, kuenziwa kwa familia za mashahidi wa Qur’ani na mashahidi wa kulindwa Haram ya Bibi Zeinab (as) huko Damscus Syria, kuwasilishwa kwa makala na utafiti wa Qur’ani pamoja na kufanyika maonyesho na vikao vya Qur’ani ni miongoni mwa shughuli zilizotekelezwa katika duru hii ya 33 ya mashindano ya kimataifa ya Qur’ani Tukufu.

 

700 /