Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu aonana na Waziri Mkuu wa India

Msingi wa ushirikiano imara na wenye manufaa wa Iran na India

Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran  leo alasiri (Jumatatu) ameonana na Narendra Damodardas Modi Waziri Mkuu wa India ambapo amaeashiria uhusiano mkongwe, wa muda mrefu na wa kihistoria  pamoja na mawasiliano ya kiutamaduni na kiuchumi ya watu wa mataifa haya mawili na kusema kuna nyanja nyingi mno za kuimarishwa uhusiano wa pande mbili hizi. Amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakaribisha kuimarishwa uhusiano na India ambayo ni moja ya nchi zenye uchumi unaoinukia na kuimarika duniani na kwamba Iran imeazimia vikamilifu kutekeleza mikataba ya pande mbili. Amesisitiza kuwa Iran kamwe haitaathirika na  siasa zozote zinazotaka kuvuruga jambo hilo. Ayatullah Khamanei ameashiria mustakbali mzuri wa uchumi wa India na vilevile vyanzo vya mafuta na gesi vya Iran ambavyo kwa ujumla vinaifanya kuwa nchi tajiri zaidi duniani na kusema: Mbali na mafuta na gesi, kama ulivyosema mwenyewe Chabahar ni moja ya nukta muhimu za mawasiliano kati ya nchi za Mashariki na Magharibi na Kaskazini na Kusini ambayo inaweza kuwa muundomsingi muhimu wa ushirikiano wa kina, wa muda mrefu na wenye manufaa. Huku akiashiria siasa sahihi za serikali ya India za kutojiunga na moja ya  miungano eti ya kupambana na ugaidi inayoongozwa na nchi za Magharibi na Marekani, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Mapambano ya kweli na halisi dhidi ya ugaidi yanaweza kuwa moja ya nyanja za ushirikiano wa Iran na India kwa sababu baadhi ya nchi za Magharibi hazina azma thabiti ya kupambana na ugaidi na zimekuwa na nafasi muhimu katika kubuni makundi ya kigaidi nchini Afghanistan na vilevile Iraq na Syria. Amesisitiza kwamba mapambano dhidi ya ugaidi ambayo kwa masikitiko makubwa yanahusishwa visivyo na Uislamu yanapasa kuachiwa Waislamu na nchi za Kiislamu. Amesema ni wazi kwamba nchi za Kiislamu ambazo zinapasa kujumuishwa kwenye mapambano hayo ni zile zisizofuata siasa za nchi za Marekani na Magharibi kwa sababu nchi hizo hazina nia thabiti ya kupambana na magaidi. Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeazimia vilivyo kupambana na ugaidi na kwamba itatumia suhula zake zote katika mapambano hayo. Huku akiashiria hatua ya taasisi na makundi ya kigaidi ya kutumia vibaya matatizo na nukta dhaifu za jamii za Kiislamu katika nchi mbalimbali kwa lengo la kuvutia wafuasi wao, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba nchi zinapasa kuwapokonya magaidi visingizio hivyo. Amesema ugaidi ni moja ya maradhi hatari ya kuambukiza na kuongeza kuwa kama ambavyo kila ugonjwa wa kuambukiza unaweza kuondolewa, mapambano dhidi ya ugaidi pia yanaweza kufanikiwa na maradhi hayo sugu kuondolewa kabisa.
Katika mazungumzo hayo ambayo pia yalihudhuriwa na Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Waziri Mkuu wa India aliashiria safari iliyofanywa na Kiongozi Muadhamu nchini India mwaka 1980 na kusema safari hiyo iliandaa uwanja wa kuimarishwa zaidi uhusiano wa pande mbili. Ameongeza kuwa katika safari hii mapatano mazuri na maamuzi makubwa yamechukuliwa ambapo amesema ana yakini kwamba yatafikia natija nzuri iwapo pande mbili zitakuwa na azma thabiti ya kuyatekeleza. Bwana Narendra Modi ameunga mkono matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusiana na hatari ya ugaidi a udharura wa kupambana nao vilivyo na kusema: Kwa bahati mbaya baadhi ya nchi zinaugawa ugadi katika makudi mawili ya ugaidi mzuri na mbaya na kutoa matamshi matupu yasiyotekelezwa kuhusiana na suala hilo. Huku akisema kuwa Uislamu ni dini ya upendo na mahaba ambayo haina uhusiano wowote na ugaidi, Waziri Mkuu wa India ameongeza kuwa miaka kadhaa iliyopita India ilitoa pendekezo la kufanyika mkutano wa kimataifa wa kupambana na ugaidi ukizishirikisha nchi za Kiislamu ambapo pendekezo hilo lilipingwa na baadhi ya nchi za Magharibi. Ameongeza kuwa nchi ambazo zina azma thabiti ya kupambana na ugaidi zinapasa kuungana na kushirikiana kwa karibu ili kufikia lengo hilo.

 

700 /