Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ujumbe wa kiongozi Muadhamu kwa duru ya tano ya Baraza la Khubregan

Jukumu la Khubregan ni kusimamia utambulisho wa Kiislamu na Kimapinduzi wa Mfumo

Kwa mnasaba wa kuanza duru ya tano ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi wa Mfumo wa Kiislamu, Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu  kupitia ujumbe,  ametoa mkono wa heri na pongezi kwa wanachama wa baraza hilo kutokana na kuaminiwa na kuchaguliwa na wananchi. Amesisitiza kwamba umuhimu wa baraza hilo tukufu unatokana na jukumu kubwa mbalo limebebeshwa baraza hilo, jukumu ambalo ni la kulinda kwa makini na kwa pande zote utambulisho wa Kiislamu na Kimapinduzi wa Mfumo wa Kiislamu unaotawala nchini na kuongoza idara ambazo zinafungamana na mfumo huu kuelekea malengo yake makuu na matukufu. Ujumbe huo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambao ulisomwa leo asubuhi kwenye kikao cha ufunguzi wa duru ya tano ya baraza hilo na Hujjatul Islam wal Muslimeen Muhammadi Gulpaygani, Mkuu wa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu ni kama ifuatavyo:
Bismillahir Rahmanir Raheem,
Kuanza kazi kwa duru ya tano ya Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi wa Mfumo wa Kiislamu katika siku hizi za kukumbuka kuzaliwa Hadhrat Waliyullah al-A’dham, roho zetu ziwe fidia kwake, ni sadfa yenye baraka ambayo inapasa kuchukuliwa kuwa ishara njema na kuongezeka imani juu ya msaada na uungaji mkono wa Mwenyezi Mungu pamoja na usimamizi na ridhaa ya Imam wa Zama (AF) katika nyoyo za waumini kuhusiana na ukweli wa ahadi za Mwenyezi Mungu.
Vilevile kusadifiana kwa duru hii na tarehe 3 Khordad (tarehe 23 Mei) ambayo ni nembo ya mapambano na kupeperushwa kwa bedera ya ukumbozi na nusra ya Mwenyezi Mungu kunapasa kuchukuliwa kuwa ni alama ya nguvu na somo kutokana na tukio hili la kushangaza. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu Mtukufu na Mwenye Hekima kwa moyo wetu wote, ambaye amewawezesha wananchi walio na imani, mashujaa na waaminifu kufanikisha muundo wa baraza hili na hivyo kuupa tena Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu fahari ya kuweza kupata beia na tangazo la utiifu kutoka kwa wananchi. Tunakupongezeni pia nyinyi wanachama ambao mmeweza kuaminika na kuchaguliwa na wananchi na tunamwomba Mwenyezi Mungu Mjuzi na Anayeona kila jambo akupeni taufiki ya kuhudumia vyema nchi na wananchi.
Umuhimu wa baraza hili tukufu unatokana na ukubwa wa majukumu waliyobebeshwa wanachama wake, majukumu ambayo kwa sentensi moja ni: Kulinda kwa makini na kwa pande zote utambulisho wa Kiislamu na kimapinduzi wa mfumo unaotawala nchini na kuziongoza idara zinazofungamana nao kuelekea malengo yake makuu na matukufu. Utekelezwaji wa jukumu hili zito unahitajia ustahiki ambao umetajwa kwenye katiba. Uainishwaji wa kuwepo na kudumishwa kwa ustahiki huu ni jukumu la baraza hili tukufu ambapo jambo hilo kwa upande wake huliletea baraza hilo majukumu makubwa. Kufahamu nafasi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika dunia ya leo, kuzingatia tukio la kuvutia la utawala wa demokrasia ya kidini kati ya mifumo mingine mingi ya utawala mbapo umaanawi na dini  au wananchi au yote mawili yamekuwa wahanga, kuzingatiwa nafasi isiyo na kifani ya imani na itikadi zinazotokana na maarifa ya Kiislamu katika uchaguzi wa wananchi, uzingatiaji wa athari ya takwa ya mtu binafsi na kisiasa ya Kiongozi katika kulinda imani ya wananchi na usalama, uthabiti na uimara wa Mfumo…. haya yote ni sehemu tu ya majukumu ya baraza hili tukufu ambalo linaundwa na mafuqaha wanaoungwa mkono na wananchi na walio na athari kubwa, na ambayo yanapasa kutekelezwa. Kila moja ya mambo yaliyotajwa linafungamana na majukumu ambayo utekelezwaji wake sahihi unaiongoza nchi na mfumo kuelekea kwenye kheri na uthabiti, na wakati huohuo kumuwezesha Kiongozi kutekeleza majukumu yake makubwa na yasiyo na mfano wake. Tunamwomba Mwenyezi Mungu Mtukufu atupe sisi na nyinyi waheshimiwa taufiki ya kutuwezesha kutembea kwenye njia hii yenye baraka ambayo ilikuwa njia ya Imam Mpendwa  na lengo lake kuu na muhimu.
Sayyid Ali Khamenei
Khordad 1, 1395 (Mei 24, 2016)

 

700 /