Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Ujumbe wa Kiongozi kwa bunge la kumi

Uchumi ngangari na utamaduni wa Kiislamu, vipaumbele vya haraka

Vilevile amewanasihi wabunge kutojishughulisha na masuala ya pembeni ya vyama na kutofadhilisha maslahi yao binafsi juu ya maslahi ya umma. Amewahutubu kwa kuwaambia kuwa jukumu lao la kimapinduzi na kisheria ni kulifanya bunge kuwa ngome imara ya kukabiliana na hila na matakwa ya ziada na ya kidhulma ya uistikbari na vilevile kulifanya bunge kuwa tegemeo la kung’ara la wananchi waumini na wa kimapinduzi. Ujumbe huo wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ambao umesomwa  leo (Jumamosi) asubuhi na Hujjatul Islam wal Muslimeen Muhammadi Gulpaigani, Mkuu wa Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika sherehe za ufunguzi wa bunge hilo la awamu ya kumi ni kama ifuatavyo:

Bismillahir Rahmanir Rahiim

Ninalipongeza taifa tukufu la Kiislamu la Iran na nyinyi (wabunge) mliochaguliwa na kukubali majukumu makubwa kwa mnasaba wa kuanza awamu ya kumi ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu katika mwezi mtukufu wa Shaban ambao ni mwezi wa umaanawi, unyenyekevu na idi za kimadhehebu. Ninawashukuru wananchi wote wapendwa ambao kupitia hamasa ya uchaguzi wameendeleza gurudumu lisilosimama la utungaji sheria na hivyo kuongeza kikuku kingine kwenye mnyororo huu muhimu. Haya yote yanatokana na taufiki ya Mwenyezi Mungu na yanayonyesha kuwa baraka na rehema zake ambazo zinatokana na uwezo wake mkubwa usiokuwa na kifani zimelisaidia taifa, nchi na mfumo wa Kiislamu. Moyo na ulimi wetu hauna uwezo wa kushukuru neema hizi zote. Kwa kushiriki kwa wingi katika uchaguzi muhimu wa bunge, taifa la Iran liliweza kukariri tena uaminifu na utiifu wake wa muda mrefu kwa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu na kwa lugha hiyo ya wazi kuweza kutoa jibu la moja kwa moja kwa maadui. Uaminifu wa thamani kubwa wa taifa bila shaka unawataka viongozi katika sekta mbalimbali kuwajibika na kushukuru neema. Dhima yetu sisi viogozi sasa imekuwa nzito zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Kiapo cha wabunge ambacho kitafanyika katika siku ya kwanza ya kazi ya wabunge ni kiapo cha kidini na cha kuwajibisha, masuala muhimu ambayo yanabainisha nyadhifa na majukumu ya uwakilishi bungeni. Nyinyi ndugu na dada waheshimiwa mnaweza kupitia hekima, busara, ikhlasi na auminifu kutekeleza jukumu hili katika kipindi cha shughuli zenu za kisheria ambazo kimsingi ni kutunga sheria na kusimamia  (utendaji wa vyombo na idara tofauti za serikali) na hivyo kufanikiwa mbele ya wananchi na Mwenyezi Mungu. Ni kwa kutumia suala hilo tu ndipo nafasi ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya ‘kuwa katika kilele cha kila jambo’ inaweza kulindwa.

Mazingira ya kidhoruba ya hivi sasa katika upeo wa kieneo na kimataifa na chokochoko za madola ya kibeberu na vibaraka wao zimeipelekea Iran ya Kiislamu kukabiliwa na hali tata zaidi kuliko ilivyokuwa huko nyuma. Kuiwezesha nchi kukabiliana na mazingira hayo kunahitajia azma thabiti na ubunifu wa kiutendaji kwa upande wa viongozi. Jukumu lenu la kimapinduzi na kisheria nyinyi wabunge waheshimiwa ni kulifanya bunge hilo kuwa ngome imara katika kukabiliana na hila na matakwa ya ziada na kidhulma ya uistikbari na nukta ya egemeo linalong’ara la wananchi waumini na wa kimapinduzi. Kufikia uchumi ngangari na masuala yote yanayofungamana nao na pia kufanya juhudi za dhati za kueneza na kuimarisha utamaduni wa Kiislamu ni vipaumbele viwili vinavyopasa kushughulikiwa kwa haraka kwa sasa. Kuna vipaumbele vingine muhimu katika sekta mbalimbali zinazohusiana na nguvu ya kitaifa na uimarishwaji wa usalama na kulindwa nchi, ambavyo vinadhamini uwepo wa audilifu wa kijamii, kujitawala na maendeleo ya nchi. Kuvielewa vipaumbele hivyo ni miongoni mwa majukumu ya wabunge na vinaweza kufikiwa na akili yao erevu. Ninawausia wabunge waheshimiwa watawakali kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu na Muweza na kuamini ahadi zake na kusimama imara kwenye njia yake nyoofu, na kukutahadharisheni dhidi ya kujishughulisha na masuala ya pembeni ya kimirengo na maslahi binafsi badala ya kushughulikia maslahi ya umma.

Ni wajibu wangu kuwashukuru wabunge wote waheshimiwa wa bunge la tisa na spika wake mwenye bidii kubwa na hadimu pamoja na baraza zima la usimamizi wa bunge hilo. Kama ninavyotoa shukrani zangu za dhati kwa wsimamizi na idara zote husika zilizoandaa uchaguzi wa bunge la kumi. Ninatoa heshima zangu na kumuenzi hayati Imam mpendwa, mashahidi na waliojitolea kwenye njia hii. Nasalimu na kumtukuza Walii Mtukufu wa Mweyezi Mungu (Imam Mahdi (AF)), roho zetu ziwe fidia kwake na ninamuomba Mwenyezi Mungu Mtukufu akupeni nyote taufiki.

Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Sayyid Ali Khamenei

 Khordad 8, 1395 (May 28, 2016)

700 /