Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Kiongozi Muadhamu akutana na baraza la Khubregan

Kiongozi aonya dhidi ya upenyaji wa adui

Ayatullahi Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, leo asubuhi (Alkhamisi) ameonana na mkuu pamoja na wajumbe waliochaguliwa na wananchi wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Mfumo wa Kiislamu na kusema kuwa baraza hilo kwa hakika ni tukio adhimu. Huku akibainisha utambulisho na njia ya kimapinduzi ya baraza hilo, Kiongozi Muadhamu amesisitiza kwamba njia pekee ya kudumu na kuendelea Mfumo na kuthibiti malengo ya Mapinduzi ni nguvu halisi ya nchi na Jihadi kubwa kwa maana ya kutomfuata adui. Amesmhukuru Mwenyezi Mmungu kwa kufanyika uchaguzi mzuri, ushiriki mkubwa wa wananchi kwenye uchaguzi na hatimaye kuweza kuchaguliwa kwa baraza hilo lenye athari na linaloheshimiwa na kuongeza kwamba Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Mfumo wa Kiislamu nchini ni baraka kubwa ya Mwenyezi Mungu ambapo hata tukifumbia machao majukumu yake kwenye katiba ya nchi, ni dhihirisho kubwa na lenye athari. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema nafsi ya kubuniwa kwa baraza hilo, linalochaguliwa na kuaminiwa na wananchi na linaloundwa na wanazuoni, wananadharia wa kidini na maulama, ni jambo lililo na umuhimu mkubwa na kuongeza: ‘Baraza hili muhimu na tukufu lina uwezo mkubwa wa kufanikisha mabadilishano ya kifikra, uratibu na shughuli zenye taathira.’ Ayatullah Khamenei ameashiria mawasiliano ya maulamaa na wanazuoni wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu (Khubregan) na matabaka tofauti ya wananchi katika pembe zote za nchi na taathira yao kubwa kwa fikra za waliowengi na kusema kuwa baraza hilo halipasi kukaa bila harakati zozote hadi wakati wa kutekelezwa majukumu yake yaliyoainishwa kwenye katiba. Amesema fikra ya pamoja kuhusu masuala tofauti, uzingatiaji wa masuala maalumu, utangazaji wa misimamo na matakwa, na kuainisha aina ya mijadala na matakwa ya umma ni miongoni mwa mambo yanayoweza kushughulikiwa na baraza la Khubregan na kusema: ‘Iwapo lengo hilo litafikiwa bila shaka mihimili tofauti na viongozi pamoja na maafisa waandamizi serikalini pia bila shaka watawajibika kufanya juhudi za kudhamini masuala hayo.’ Huku akisisitiza kwamba njia na malengo ya Baraza la Khubregan yanapasa kuwa ni yale yale ya Mapinduzi, Kiongozi wa Mapinduzi ameongeza kuwa Utawala wa Uislamu. Uhuru, kujitawala, uadilifu wa Kijamii, maisha bora ya umma, kuondolewa umasikini na ujahili, kusimama imara dhidi ya mafuriko haribifu ya ufisadi wa kiakhlaki, kiuchumi, kijamii na kisiasa yanayojiri katika nchi za Magharibi pamoja na kukabiliana na ubeberu na mrengo wa uistikbari ni miongoni mwa malengo muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu ya taifa la Iran. Amesema ubeberu ni dhati na kawaida ya uistikbari na kuongeza kuwa katika dhati yake, mrengo wa uistikbari unataka kueneza ubeberu katika mataifa yote na kwamba kila nchi na taifa lisilosimama imara mbele ya suala hilo hutumbukia kwenye mitego ya uistikabari huo. Ayatullah Khamenei amesema bila shaka Uislamu ndiyo dini inayoweza kutokomeza dhulma na kuongeza kuwa ni wazi kwamba Uislamu unaoweza kumudu na kusimama imara mbele ya wenye kiburi duniani na kuuangamiza mrengo wa ubeberu, unapasa kuwa mfumo imara wa utawala ulio na nguvu za kijeshi, kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na vyombo vya habari. Amesema kulinda mapinduzi ni kugumu zaidi kuliko kufanya mapinduzi yenyewe. Amebainisha jinsi ya kukabiliana kwa njia sahihi na  mrengo wa kidhalimu wa kimataifa na kuongeza: ‘Mwanzo, maadui wa taifa la Iran walitumia hujuma ngumu (zana za kivita na mbinu za dhahiri katika hujuma yao) dhidi ya taifa hili. Vita vya kulazimishwa vya miaka minane, uasi wa mwanzoni mwa Mapinduzi, uungaji mkono kwa makundi ya kigaidi, hujuma dhidi ya majukwaa ya mafuta ya Iran na kutunguliwa ndege ya abiria ni mifano ya hujuma hiyo ambayo ilishindwa kutokana na msaada na uwezo wa Mwenyezi Mungu, uongozi shupavu wa Imam Khomeini na subira pamoja na mapambano ya taifa. Kiongozi Muadhamu amesema shambulio laini ni hatua nyingine ya hujuma isiyo na kikomo ya waonevu wa kimataifa na kuongeza kwamba vikwazo vya kudumu, mashambulio yasiyokoma ya kisiasa, propaganda za kuvutia na kuvuruga mpangilio (ushawishi) wa Jamhuri ya Kiislamu katika nchi nyingine ni mbinu zinazotumika katika hatua ya pili ya hujuma ya maadui dhidi Iran, hujuma ambayo kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu na ukakamavu wa taifa na viongozi imeshindwa kufikia natija inayofuatiliwa na maadui hao. Ayatullah Khamenei amesema kuwa sehemu ya tatu ya hujuma ya maadui yaani upenyeji ni hatari sana na kwamba ni muendelezo wa vita laini na kusisitiza kwamba uistikbari unafuatilia malengo kadhaa makuu katika stratijia yake ya upenyaji ambayo ni kuwa na ushawishi katika vituo vya kubuni na kuchukua maamuzi, kubadilisha imani za watu, na kubadilisha mahesabu na misimamo ya viongozi.
Amesema kushambuliwa misingi na taasisi za Mapinduzi likiwemo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah), Baraza la Kulinda Katiba, vijana wa kihizbullah na wanazuoni wa kimapinduzi ni miongoni mwa mbinu zinazotumiwa na maadui wa kigeni na kusisitiza kwamba lengo kuu la maadui katika hatua hii ya vita laini ni kuandaa uwanja wa kuufanya Mfumo wa Kiislamu kuwa mtupu  kwa kuzipokonya nguvu taasisi zake za ndani. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema iwapo lengo hilo litathibiti na Jamhuri ya Kiislamu kupokonywa taasisi zake za nguvu, basi kuifuta au kubadilisha kabisa muelekeo wake haitakuwa kazi ngumu. ‘Ni kutokana na ukweli huu ndipo tukasema kuwa usisitizaji juu ya kutomfuata adui na kusimama imara mbele ya matakwa yake ni Jahadi kubwa.’ Amesema Kiongozi Muadhamu. Baada ya kubainisha muelekeo wa kimapinduzi wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Mfumo wa Kiislamu, Ayatullah Khamenei amesema kuwa ubunifu unaofanyika kwenye misingi ya kidini wa wasomi walio na uwezo wa kutoa maamuzi na fatwa na kuponya majeraha yanayosababishwa na adui ikiwa ni pamoja na mifarakano ya kimadhehebu na kikabila, hitilafu za mirengo na kubuni kambi mbili bandia nchini ni majukumu mengine ya baraza la Khubregan. Amewahutubu wajumbe waliochaguliwa na wananchi wa baraza la tano la Khubregan kwa kusema: ‘Kuwa bila harakati ni jambo lisilofaa. Daima mnapasa kuzingatia vilivyo msingi wa mabadiliko na maendeleo kwa ajili ya kufikiwa malengo ya Uislamu na Mapinduzi.’ Sehemu ya mwisho ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu ilitumika kubainisha na kufafanua majukumu makuu ya viongozi wa mfumo wa Kiislamu katika zama hizi. Amesema nchi kuwa na nguvu za kweli ndiyo njia pekee ya kuendelea kuwepo, kudhaminiwa maendeleo na kufikiwa malengo ya Mapinduzi na taifa na kuongeza kuwa katika njia hii viongozi wote na idara za serikali zina majukumu ambayo zinapasa kuyatekeleza vizuri. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kwamba nchi kuwa na nguvu kunaiwezesha kupata fursa hata kutoka kwa nchi zenye nguvu kubwa duniani la sivyo hata serikali dhaifu na zilizodhalilika zaidi duniani zitaanza kuiandama Iran.
Huku akibainisha mfano mmoja wa kupata fursa kutoka kwa adui katika kivuli cha nchi kuwa na nguvu, Ayatullah Khamenei amesema: ‘Ndugu zetu wapendwa wanasema tuliweza kupata fursa kwenye mazungumzo ya nyuklia na pande za mkabala wetu kukubali kuwepo kwa sekta ya nyuklia ya Iran. Bila shaka suala hili lilifikiwa baada ya kudhihiri nguvu ya Iran yaani ya kuweza kurutubisha urani kwa kiwango cha asilimia 20. Hii ni kwa sababu wote wanajua kwamba katika urutubishaji urani, kufikia kiwango cha asilimia 20 ndiko kugumu zaidi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema uzalishaji wa mashinepewa (centrifuge) 19,000 za kizazi cha kwanza, kutumika kwa mashinepewa 10,000, kutengenezwa kwa kizazi cha kwanza, cha pili, cha tatu na cha nne cha mashinepewa na kiwanda cha kuzalisha maji mazito ni mifano mingine ya nguvu ya nyuklia ya Iran. Ameongeza: ‘Adui ambaye wakati mmoja hakuwa tayari kukubali hata mashinepewa moja kuwa nchini Iran, hatimaye alilazimika kukubali jambo hilo baada ya kukabiliwa na nguvu ya nyuklia ya nchi. Kwa hakika Wamarekani hawakutoa fursa hii bali ni sisi ndio tuliochukua haki yetu kwenye mwanga wa nguvu zetu.’ Kiongozi wa Mapinduzi amesema: ‘Inshallah kwa kufikia natija uchumi ngangari na kupata nguvu uchumi wa nchi, adui pia atadiriki kutokuwa na athari silaha ya vikwazo. Ayatullah Khamenei amesema kutaka na kufuatilia uthibiti wa taasisi za nguvu za ndani kwa viongozi na idara mbalimbali ni miongoni mwa nyadhifa za baraza la Khubregan na kuongeza: ‘Baraza hili adhimu pia linaweza kuwa na taathira katika mwenendo huu.’
Ayatullah Khamenei vilevile amesema kuwa takwa, ushujaa, mwamko, kuwa muwazi inapobidi, kutoogopa lawama za wengine na kuelewa pamoja na kutambua vyema ngome na hila za adui ni vipimo halisi vya kuwa mtu wa kimapinduzi.  Amesema: ‘Baadhi ya wakati adui hufanya mambo ambayo kidhihiri huonekana kuwa chanya kwa lengo maalumu, na mambo hayo kupokelewa vizuri nchini Iran lakini kama tutadiriki vyema lengo lake halisi, kamwe hatuwezi kuhadaika.’ Nasaha za mwisho za Kiongozi Muadhamu kwa wajumbe waliochaguliwa na wananchi wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu zilikuwa ni kuamini nafsi ya ndani na kutahadhari maafa (kushindwa) ya kiroho. Amesema: ‘Tahadharini uoga na kushindwa kwa ndani ya nafsi zenu. Hii ni kwa sababu hilo likitimia basi katika medani ya matendo pia mtashindwa.’
Mwanzoni mwa hotuba yake, Kiongozi Muadhamu aliwakaribisha wanachama wapya wa baraza la Khubregan na hasa mamujtahidi vijana na wachangamfu. Pia aliwaenzi wanachama wa baraza hilo walioaga dunia na hasa marehemu Ayatullah Waidh Tabasi.
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Jannati, Mkuu wa Baraza la Wanazuoni Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Mfumo wa Kiislamu alimshukuru Kiongozi Muadhamu kwa ujumbe wake wa kushajiisha alioutoa kwa mnasaba wa kuanza kazi baraza hilo na kusema kuwa ujumbe huo ulituliza  mazingira ya baraza hilo na kuyafanya kuwa na nidhamu maalumu. Huku akiashiria nafasi maalumu ya baraza hilo, Ayatullah Jannati amesema baraza hilo linaheshimika katika fikra za waliowegi. Sambamba na kuashiria kuwa tunapasa kutekeleza vyema majukumu yetu kwa lengo la kumridhisha Mwenyezi Mungu na pia watu, mkuu huyo wa Khubregan amesema kuwa baraza hilo litazingatia sifa ya mapinduzi katika pande zote za shughuli zake. Katika kikao hicho Ayatullah Hashimi Shahrudi, makamu wa pili wa mkuu wa baraza la Khubregan ametoa ripoti akiashiria kikao cha kwanza cha baraza hilo na kusema kwamba, udharura wa watu kuwa wa kimapinduzi kuwaza kimapinduzi na kutenda kimapinduzi, sisitizo la vyombo vyote kufanya juhudi za kutekeleza miongozo ya Kiongozi wa Mapinduzi na udharura wa watu  wote na hasa viongozi kujiepusha kutoa matamshi yanayozua mfarakano katika jamii ni baadhi ya masuala muhimu yaliyojadiliwa na wanachama katika kikao hicho. Ayatullah Shahrudi ameongeza kwamba wanachama wa Khubreagan walitoa madukuduku na matakwa yao kuhusiana na changamoto mbalimbali muhimu zinazoikabili nchi ikiwa ni pamoja na mapungufu ya kiutamaduni, matatizo ya kimaisha na kiuchumi, ajira kwa vijana, mdororo, magendo, kutothibiti uchumi ngangari, kutotekelezwa mfumo wa benki za Kiislamu, kudhihiri kwa fikra potofu na za kupindukia mipaka, madhara ya mitadao ya intaneti na matatizo ya mikoa ya mpakani.

 

700 /