Tovuti ya Habari ya Ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullahil Udhmaa Sayyid Ali Khamenei

Hotuba ya Kiongozi Muadhamu katika Haram ya Imam Khomeini

Umapinduzi, njia pekee ya maendeleo na kufikiwa malengo

Akizungumza leo asubuhi (Ijumaa) mbele ya halaiki kubwa ya matabaka mbalimbali ya wananchi waliofika kuomboleza kwenye Haram ya Imam Khomeini (MA), Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mpainduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa hayati Imam Khomeini (MA) alikuwa mtu muumini, mswalihina na mwanamapinduzi. Huku akisisitiza juu ya umuhimu wa kudumishwa njia ya Imam mwanamapinduzi wa taifa kama njia pekee ya kufikia maendeleo na malengo ya wananchi na Mfumo wa Kiislamu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha vielezo (vipimo, viashiria, alama) vitano muhimu vya umapinduzi na kuongeza kuwa tunapasa kunufaika na uzoefu wa mazungumzo ya nyuklia yaani kuthibitisha kutoaminika Marekani, katika kudumisha njia ya maendeleo ya nchi. Akizugumza katika maadhimisho ya mwaka wa 27 wa kuaga dunia Imam Khomeini (MA), Ayatullah Khamenei amesema kuwa ibara ya ‘muumini mswalihina mwanamapinduzi’ ni sifa kamilifu aliyosifika nayo marehemu Imam na kuongeza kuwa Imam mpendwa alimwamini Mwenyezi Mungu, wananchi, lengo na njia ambayo ilimfikisha kwenye lengo hilo. Kuhusiana na sifa yake ya kuwa mswalihina, Ayatullah Khamenei amesema Imam Khomeini (MA) alikuwa mja mwema wa Mwenyezi Mungu, myenyekevu na aliyejishughulisha sana na dua. Akiashiria sifa ya tatu ya Imam Khomeini (MA), Ayatullah Khamenei amesema kuwa Imam alikuwa mwanamapinduzi na kuwa hiyo ndiyo iliyokuwa sababu kuu ya madola ya kibepari kuchukizwa naye. Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba madola yenye nguvu kubwa duniani yanatishwa sana na neno mapinduzi na umapinduzi wa taifa la Iran na kuongeza kuwa chanzo halisi cha mashinikizo haya yote ambayo yamekuwa yakitolewa dhidi ya taifa la Iran katika miaka hii yote kwa visingizio tofauti vikiwemo vya suala la nyuklia na haki za binadamu ni sifa hii ya taifa la Iran na Mfumo wa Kiislamu kuwa wa kimapinduzi. Kiongozi Muadhamu ameashiria kutoka Iran katika udhibiti wa madola yenye nguvu na kubadilika kuwa mfumo wa Kiislamu na hivyo kuvutia na kuyahamasisha mataifa mengine ya dunia, na kusema kwamba suala ni hili kuwa Imam wa Kimapinduzi aliweza kunusuru na kuiondoa nchi kwenye vinamasi (mikwamo),  vikiwemo vinamasi vya utegemezi, ufisadi wa kisisa, kimaadili, udhalilishaji wa kimataifa, kubaki nyuma kielimu, kiuchumi, kiufundi na udhibiti wa Marekani na Uingereza na hivyo kuleta mabadiliko makubwa katika muelekeo wa nchi na taifa zima la Iran. Huku akisisitiza kwamba Imam Mpendwa Khomeini (MA) aliweza kubadili reli ya nchi kuelekea malengo makubwa yaani utawala wa dini ya Mwenyezi Mungu nchini, Ayatullah Kahamenei amesema kuwa utawala wa dini ya Mwenyezi Mungu una maana ya kuthibiti uadilifu halisi wa kijamii, kuondolewa umasikini na ujinga, kuondolewa unyonge na madhara ya kijamii, kuanzishwa mjumuiko wa thamani za Kiislamu, kudhaminiwa usalama wa kimwili,kimaadili na kimaanawi, maendeleo ya kielimu nchini, utukufu na utambulisho wa kitaifa, kuimarishwa nguvu ya taifa katika ngazi za kimataifa na pia uwezo wa nchi. Huku akisisitiza kwamba hayati Imam (MA) kwa baraka za Mapinduzi ya Kiislamu aliweza kuilekeza nchi kwenye malengo haya, Kiongozi wa Mapindizi ya Kiislamu amesema kuwa hata kama kufikiwa malengo haya kunahitajia wakati na juhudi kubwa lakini yanaweza kufikiwa kwa sharti kwamba njia ya mapinduzi na umapinduzi ifuatwe. Ameashiria baadhi ya mambo yanayodhuru na kuhatarisha mwenendo wa harakati ya Mfumo wa Mapiduzi ya Kiislamu na kusema: ‘Baada ya kuaga dunia Imam Mpendwa (MA), kila sehemu tulipofanya mambo kimapinduzi tulipata maendeleo na katika kila kipindi tulichoacha kuzingatia na kughafilika na umapinduzi na harakati ya kijihadi, tulibaki nyuma na kushindwa.’ Ayatullha Khamenei ameyahutubu matabaka mbalimbali ya wananchi kwa kusema: ‘Inawezekana kutembea kimapinduzi kwenye njia hii ambapo katika hali hiyo maendeleo yamedhaminiwa na pia inawezekana kutembea kwenye njia hiyo kwa mbinu nyinginezo ambapo katika hali hiyo hatima huwa haijulikani vyema na hivyo taifa la Iran na Uislamu kupata pigo.’ Amesema Mapinduzi ya Kiislamu ni rasilimali bora na ya kipekee ya taifa na nchi na kusisitiza kwamba ili Mapinduzi yafikie natija, gharama kubwa zilitumika lakini kando na gharama hizo kuna manufaa mengi ambayo yamepatikana pia. Kiongozi Muadhamu ameashiria kuimarika zaidi Mapinduzi ya Kiislamu baada ya kupita miaka 37 na kuongeza kuwa hii leo hali ya taifa la Iran imebainika na kuboreka zaidi kuliko huko nyuma na sasa gharama zinaweza kuepukika zaidi. Amesisitiza kwamba Mapinduzi yalithibiti kwa azma, irada na imani ya wananchi na kubakia pamoja na kuimarika zaidi kutokana na nguvu hii hii ya wananchi. Amesema yameweza kusimama imara mbele ya vitisho vya kijeshi na vikwazo kutoyalemaza kwa njia yoyote ile bali yameendelea mbele na harakati zake kwa ushujaa na utukufu na kuwa yatadumisha harakati hii siku zijazo. Huku akiashiria kuwa umapinduzi hauhusiani tu na kipindi cha mapambano au zama za uhai wa Imam Khomeini (MA) Ayatullah Khamenei amesema: ‘Mapinduzi na umapinduzi ni wa zama zote na Mapinduzi ni mto ambao watu wote wanaotekeleza majukumu yao kwa msingi wa vielezo vya umapinduzi, wanasifika kuwa ni wanamapinduzi hata wale vijana ambao hawajawahi kumwona Imam (MA).’ Ayatullah Khamanei amezungumzia ile fikra inayoutaja umapinduzi kuwa sawa na upindukiaji mipaka na kuwagawa watu katika makundi mawili ya walio na misimamo mikali na wengine walio na misimamo ya wastani  na kusema mgao huu ambao unaletwa na wageni na maadui haupasi kuingizwa kwenye utamaduni wa kisiasa wa nchi. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kosa jingine linalofanywa kuhusiana na suala la uanamapinduzi na umapinduzi na kusema: ‘Matarajio ya kuwa watu wote wanaofuata njia ya vielezo (viashiria) na mielekeo ya Mapinduzi wanapasa kuwa ni wa kiwango kimoja cha umapinduzi ni kosa na la msingi ni kuwa inatosha kwa watu hao kuwa na vielezo vya umapinduzi.’ Ayatollah Khamanei ameongeza kuwa inawezekana kwa mtu mmoja kufanya vyema kuhusiana na maana  ya mapinduzi na utendaji wa kimapinduzi na mwingine kutofanya vyema wala kuzingatia sana masuala hayo lakini wote wawili ni wanamapinduzi na wala hatupasi kumtuhumu kila mtu nayefuata njia ya vilezo vya Mapinduzi lakini hafanyi vizuri sana kuwa si mwanaumapinduzi na aliye dhidi ya mapinduzi. Kiongozi Muadhamu kisha amebainisha viashiria vikuu vya umapinduzi ambapo amefafanua viashiria vikuu vitano kwa kusema: ‘Kufungamana na misingi na thamani kuu za Mapinduzi ya Kiislamu, daima kulenga malengo matukufu na kufanya juhudi kubwa za kuyafikia, kufungamana na kujitawala kwa pande zote kwa nchi, kutahadhari adui na kutomfuata na takwa ya kidini na kisiasa. Katika kubainisha kiashiria cha kwanza cha umapinduzi yaani kufungana na misingi na thamani za Mapinduzi Ayatullah Khamenei amesema: ‘Kuamini Uislamu halisi mkabala wa Uislamu wa Kimarekani ndiyo nukta kuu na muhimu zaidi ya kiashiria hicho.’ Amesema: ‘Uislamu wa Kimarekani una matawi mawili ya ‘Uislamu ulioganda’ na ‘Uislamu wa kisekulari’ ambapo uistikbari unayaunga mkono matawi hayo yote mawili.’
Ayatullah Khamanei amesema imani  thabiti ya kuwategemea wananchi ni msingi mwingine mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusisitiza kwamba katika Mfumo wa Kiislamu, maoni, matakwa, malengo na manufaa ya wananchi ni msingi na kwamba kuyaamini kikweli masuala hayo ni miongoni mwa mambo ya dharura ya umapinduzi. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema maendeleo, mabadiliko na ukamilifu ni thamani nyingine za msingi za Mapinduzi na kuongeza kuwa mwanamapinduzi pia anaiamini thamani hii na kila siku hufanya juhudi za kufikia mabadiliko na kuboresha hali ya mambo. Uteteaji wanyonge na matabaka ya watu dhaifu yakiwemo mataifa yanayonyongeshwa duniani ni thamani nyingine iliyozungumziwa na Kiongozi Muadhamu katika kubainisha kiashiria cha kwanza cha umapinduzi yaani kufungamana na misingi na thamani kuu za Mapinduzi ya Kiislamu. Amesema iwapo kufungamana huku na kama inavyosema Qur’ani Tukufu , ‘kusimama sawasawa’ kutakuwepo  basi harakati ya viongozi wa Mfumo wa Kiislamu katika tufani ya matukio pia itakuwa kwenye njia nyoofu na imara, la sivyo, watachukua hatua za kupindukia mipaka na kubadilisha misiammo yao mara kwa mara kwa msingi wa mielekeo ya matukio yanayowakabili. Katika kubainisha kiashiria cha pili cha umapinduzi yaani daima kulenga malengo matukufu na kufanya juhudi kubwa za kuyafikia, Ayatullah Khamanei amesema: ‘Hakuna hali yoyote ambayo inapasa kufanya malengo makubwa ya Mapinduzi na wananchi yaache kufuatiliwa, au kuridhia hali iliyopo.’ Amesema uzembe, uhafidhina na kukata tamaa ni mambo yanayokabiliana na kiashiria hiki na kusisitiza kwamba njia ya maendeleo haina mwisho na kuwa daima njia hii inapasa kufuatwa kwa kuzingatia umapinduzi. Kiashiria cha tatu cha umapinduzi ambacho ni cha kufungamana na kujitawala nchi ni suala jingine ambalo lilizungumziwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hadhara kubwa ya makumbusho ya mwaka wa 27 tokea aage dunia Imam Khomeini (MA), ambapo alichambua suala hilo katika pande tatu za kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi. Aliongeza kuwa maana halisi ya kujitawala kisiasa ni kutohadaika na mbinu tofauti zinazotumiwa na adui na kuchunga kujitawala kwa ndani, kieneo na kimataifa katika kila hali. Huku akiashiria mbinu na hila zinazotumiwa na maadui na hasa Marekani, Ayatullah Khamenei amesema kwamba wao daima hufuatilia malengo yao kwa kutumia vitisho. Mara nyingine hufuatilia malengo hayo kwa kutabasamu na hata kujipendekeza. Kiongozi Muadhamu ametoa mfano kwa kusema: ‘Kwa mfano, huandika barua na kusema njooni tutatue matatizo ya dunia kwa kushirikiana. Katika hali hii mtu naweza kushawishika kwamba, ni sawa twende tushirikiane na dola lenye nguvu kubwa zaidi duniani katika kutatua matatizo ya kimataifa huku tukiwa tumeghafilika na ukweli kwamba adui anafuatilia malengo mengine katika undani wa kadhia hii.’ Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: ‘Wito wa adui wa kushirikiana katika kutatua masuala ya kimataifa, yaani ni wito wa kushiriki katika mchezo na medani ambayo adui huyo tayari ameianisha kwa ajili ya kutatua masuala ambayo anayakusudia yeye.’  Katika kuthibitisha suala hilo ametolea mfano Syria na kusema: ‘Sababu ya sisi kutoshiriki katika muungano unaotajwa kuwa wa Kimarekani kuhusu suala la Syria na masuala mengine mfano wa hayo ni kwamba tulijua vyema kuwa wanataka kutumia nguvu na ushawishi wetu na wa nchi nyingine katika kufikia malengo wanayoyakusudia.’ Katika tahadhari muhimu, Kiongozi Muadhamu amesema kwamba mambo kama haya ambayo kidhahiri yanaonekana kutopingana na kujitawala kwa nchi kwa hakika ni kuwasaidia maadui na bila shaka ni dhidi ya kujitawala nchi. Katika kubainisha maana ya pili ya kiashiria cha kujitawala, Ayatullah Khamanei amesisitiza umuhimu wa kipekee wa kujitawala kiutamaduni na kuongeza kuwa umapinduzi una maana ya kuchaguliwa mtindo wa maisha wa Kiirani na Kiislamu na kujiepusha kabisa kuiga mitindo ya Magharibi na ya wageni. Kuhusiana na suala hilo amesema kuwa vyombo vipya katika mtandao wa intaneti ni vyombo vya uhandisi wa kupata habari na maelezo ya siri na udhibiti wa nchi za Magharibi wa utamaduni wa mataifa ya ulimwengu na kuongeza: ‘Vyombo (suhula) hivi bila shaka vinaweza kuwa na manufaa lakini udhibiti wa adui unapaswa kuondolewa kwenye vyombo hivyo, ili kuzuia kubadilishwa intaneti kuwa chombo cha kupenya na kuimarishwa utamaduni wa adui.’ Kujitawala kiuchumi kwa maana ya kutomezwa na mfumo wa kiuchumi wa jamii ya kimataifa ni nukta nyingine muhimu ambayo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliizungumzia katika kubainisha kiashiria cha tatu cha umapinduzi yaani kufungamana na kujitawala kwa pande zote kwa nchi.
Amesema: ‘Baada ya mazungumzo ya nyuklia Waarekani walisema: Muamala wa nyuklia na Iran unapasa kupelekea uchumi wa Iran kuunganishwa na jamii ya kimataifa. Maana ya maneno haya ni kuwa Iran inapasa kumezwa na njama pamoja na mfumo ambao umebuniwa na mabepari ambao kimsingi ni Wazayuni kwa lengo la kupora maslahi ya kifedha ya dunia.’ Ayatullah Khamenei amesema: ‘Kupitia vikwazo Wamarekani walikuwa wakifuatilia kulemaza (kusambaratisha) kabisa uchumi wa Iran. Hivi sasa ambapo mazungumzo yamefikia natija ya kiwango fulani, wanataka uchumi wa Iran umezwe na mfumo wa kimataifa ambao unadhibitiwa na Wamarekani.’ Kiongozi Muadhamu amesema njia pekee ya kuthibiti kujitawala kiuchumi ni kupitia uchumi ngangari na kuongeza kuwa kwa bahati nzuri kwa mujibu wa ripoti ambayo imewasilishwa na serikali, katika mwaka huu wa kaulimbiu ya ‘Uchumi Ngangari, Hatua na Vitendo’ kuna hatua ambazo zimechukuliwa ambapo iwapo zitaendelea kwa kasi hii hii, bila shaka wananchi wataona athari zake. Amesema uchumi ngangari unapaswa kupewa uzito mkubwa katika maamuzi yote makubwa yanayochukuliwa na kazi zote ikiwemo mikataba inayotiwa saini na nchi za kigeni.
Ayatullah Khamenei amewakosoa wale watu wanaodhani kwamba ustawi wa kiuchumi unatimia tu kupitia uwekezaji wa kigeni na kusema kuvutia uwekezaji wa nje ni jambo zuri na la lazima lakini muhimu kuliko jambo hilo ni kuhamasisha na kutumia uwezo wa ndani ya nchi na kwamba si kila jambo linapaswa kufungamanishwa na uwekezaji wa nje. Kwa mtazamo huohuo, ametahadharisha kuhusiana na suala la teknolojia ya kisasa na iliyostawi na kusema: Kama nchi za nje zitapeana teknolojia kama hiyo ni vizuri lakini hata kama hazitapeana, vijana ambao wameiwezesha Iran tukufu kuwa miongoni mwa nchi 10 bora duniani katika nyanja za nano, nyuklia na nyanja nyinginezo, iwapo mipango mizuri itawekwa bila shaka wataidhaminia teknolojia nyinginezo inazozihitajia.
Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi kisha amebainisha kiashiria cha nne cha umapinduzi yaani tahadhari katika kukabiliana na adui na kusema, kama ilivyo kwenye vita, kila hatua ya adui inapasa kufuatiliwa kwa karibu na kutathminiwa kwa makini. Amesema malengo yake yanapasa kufahamika vyema, tahadhari ya lazima kuchukuliwa na kiuasumu kutayarishwa kwa ajili ya kukabiliana na sumu tarajiwa ya vitendo vyake.
Ayatullah Khamanei amewakosoa watu wanaofumbia macho uadui wa wazi na wa kudumu wa Marekani na ambao wanadai kuwa kuzunguzia uadui wa Marekani ni njama, na kusema kuwa kukanusha kuwepo uadui mkubwa, wa kudumu na wa wazi wa Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu na taifa la Iran ni njama ambayo imepangwa kwa ajili ya kupunguza hisia za kuchukiwa shetani huyo mkubwa. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa uadui wa Marekani dhidi ya Mapinduzi ya Kiislamu ni wa dhati na kuendelea kusema: ‘Mfumo wa kibeberu kwa kutumia vita, kuunga mkono ugaidi, kukandamiza wapigania uhuru na kuwadhulumi wananchi madhlumu wa Palestina, umedhihirisha wazi tabia yake ya kawaida, na wala Mfumo wa Kiislamu hauwei kukaa kimya na kutoshughulishwa na ukandamizaji huo.’ Kiongozi wa Mapinduzi amesema kuwa msaada wa moja kwa moja wa Marekani kwa nchi ambayo inawahujumu wananchi wa Yemen ni kushiriki katika hujuma ya mabomu na mauaji ya watu wasio na hatia na kusisitiza kuwa kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu, haiwezekani kukaa kimya mbele ya jinai hizo. Katika kufupisha maneno yake kuhusu suala hilo, Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba kila mtu au mrengo anaohudumia Uislamu na kutekeleza majukumu yake kwa jina la Uislamu bila shaka utakuwa umefanya kosa kubwa na hatimaye kupata pigo kubwa iwapo utaamua kuiamini Marekani. Amesema, katika miaka hii hii ya hivi karibuni pia baadhi ya makundi ya Kiislamu katika eneo kwa kisingizio cha ‘akili ya kisiasa’ na ‘mbinu’ yalishirikiana na Marekani lakini hivi sasa yanapitia kichapo cha kumwamini shetani mkubwa. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Waengereza ni maadui wengine khabithi kabisa wa taifa la Iran na kuongeza: ‘Hakuna wakati wowote ambao Waengereza wamewahi kuacha ukhabithi wao dhidi ya taifa la Iran.’ Amesema ni kutokana na mwendelezo wa uadui huo ndipo katika kukaribia maadhimisho ya kukumbuka kifo cha Imam mpendwa na msafi, ndipo chombo cha propaganda cha serikali ya Uingereza kwa kushirikiana na Wamarekani kikabuni nyaraka bandia na kueneza propaganda dhidi ya hayati Imam wa taifa la Iran. Kiongozi Muadhamu amesema utawala haramu wa Israel ukishirikiana na Marekani na Uingereza ni adui mwingine wa taifa la Iran na kusisitiza kwamba tunapasa kuwa waangalifu sana mbele ya adui na kuchukua tahadhari kubwa tunapojadili mapendekezo yao yakiwemo ya kisiasa na kiuchumi.  Amesema, ikiwa tahadhari hii itachukuliwa bila shaka kutowafuata maadui pia kutafuata katika hatua ya baadaye, jambo ambalo ni ileile Jihadi kubwa.
Katika kubainisha kiashiria cha mwisho cha umapinduzi, yaani takwa ya kidini na kisiasa, Ayatullah Khamenei amesema kwamba takwa ya kidini ina maana ya kufanya juhudi na kuwa waangalifu kwa ajili ya kufikia malengo yote ambayo Uislamu umeyaainisha na kuitakia jamii. Amesema, katika uwanja huu hatupasi kutegemea tuu mahesabu ya kiakili kwa sababu ufuatiliaji wa malengo haya ni taklifu ya kidini na kwamba kila mtu anayeutenganisha Uislamu na masuala ya kijami ina kisiasa, basi hajaielewa  vyema dini tukufu ya Mwenyezi Mungu. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: ‘Iwapo takwa ya kidini itatimia takwa ya kisiasa pia itatimia na kumlinda mwanadamu kutokana na mtelezo wa kisiasa na kimajukumu.’ Sehemu ya mwisho ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu katika halaiki kubwa ya watu waliofika kwenye Haram ya hayati Imam Khomeini (MA) kwa ajili ya kujadidisha ahadi ya kufuata malengo yake ilihusiana na nasaha kadhaa muhimu ambapo ya kwanza ilihusu kuzingatiwa Imam akiwa mfano uliokamilika. Kuhusu jambo hilo Aatullah Khamanei amesema: ‘Katika ramani ya njia ambayo imebainishwa leo, Imam yuko katika kilele cha viashiria hivi vyote na anapaswa kuzingatiwa kama mfano kamilifi wa kuigwa. Amesema uzingatiaji na uchunguzi wa kina na wa kudumu wa mjumuiko wa fikra na wasia wake pamoja na kufarijika na maneno na misimamo yake ni njia ya kuchukuliwa hayati huyo mpendwa kuwa mfano bora. Amewausia watu wote na hasa vijana kuzingatia suala hilo. Nasaha ya pili ya Kiongozi Muadhamu ilihusiana na kutosahaulika kwa uzoefu uliopatikana kwenya mazungumzo ya nyuklia. Amesisitiza kwamba uzoefu huu unatufunza kwamba hata kama tutalegeza misimamo mbele ya Marekani lakini nchi hiyo haiko tayari kuachana na njama zake haribifu. Ayatullah Khamenei ameashiria mazungumzo ya 1+5 na hata mazungumzo ya pande mbili na nchi hiyo kuhusu suala la nyuklia na kusema: ‘Kwa juhudi za ndugu zetu wenye bidii, mazungumzo yalifikia nukta ya pamoja lakini pamoja na hayo bado Marekani hadi sasa inakwepa kutekeleza  majukumu na ahadi zake.’ Amesema wengi hata kabla ya kuanza mazungumzo hayo walikuwa wakijua tabia hiyo ya Marekani na kuitabiri lakini wengine hawakuwa wakiijua ambapo sasa wanapasa kuijua. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kwamba hata tukifaradhisha,jambo ambalo kwa hakika haliwezekani, kwamba leo hii tuketi na Marekani kwenye meza moja na kujadiliana nayo kuhusiana na masuala tofauti yakiwemo ya haki za binadamu, makombora, ugaidi, Lebanon, Palestina na kadhia nyingine yoyote, na kulegeza misingi na misimamo yetu, nchi hiyo kamwe haiwezi kulegeza misimamo yake na baada ya kutabasamu na kuzungumza bado kivitendo itaendelea kufuatilia malengo yake. Nasaha ya tatu ya Kiongozi Muadhamu ilihusiana na umoja wa serikali na wananchi. Amesema kila mtu katika vipindi tofauti huridhishwa au kutoridhishwa na serikali fulani ambalo ni jambo la kawaida  lakini akasisitiza kwamba umoja wa serikali na wananchi haupasi kuvurugwa kwa vyovyote vile. Ayatullah Khamenei amesema: ‘Hakuna tatizo katika kuikosoa serikali na kuitaka iwajibike na wala hilo halipingani na umoja lakini kama nilivyoziusia serikali zote, tahadhari inapasa kuchukuliwa ili kuzuia chuki na uadui na wote washirikiane na kushikamana katika kukabiliana na vitisho na uadui.’ Hhuku akisisitiza juu ya kuwepo umoja kati ya mihimili mitatu ya serikali, Kiongozi wa Mapinduzi amesema: ‘Umoja haupingani kwa vyovyote vile na utekelezaji wa majukumu ya kisheria ya mihimili hii lakini hisia za kibinafsi au kimirengo hazipasi kudhuru mshikamano na ushirikiano wa mihimili.’ Ayatullah Khamenei amesisitiza kwamba matamshi yanayoleta umirengo na kambi mbili na vilevile uhasama yanapasa kuepukwa ili adui aione Iran nzima kuwa kitu kimoja. Nasaha ya nne ya Kiongozi Muadhamu ilihusiana na kuyachukulia makabiliano na Marekani kuwa medani ya vita. Amesem: ‘Bila shaka Marekani iko kwenye kitivo cha medani hii, lakini pamoja na hayo medani hii huenea na kufika sehemu tofauti na hata mara nyingine ndani ya nchi, ambapo tunapasa kuwa waangalifu na kufuatilia viashiria vyote vya siri na vya dhahiri vya medani hiyo.’ Kuwa wazi na kukolea rangi mistari inayotutenganisha na maadui ni nasaha ya tano aliyoitoa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika maadhimisho ya mwaka wa 27 wa kukumbuka kifo cha Imam Khomeini (MA). Amesisitiza: ‘Baadhi ya makundi ya ndani ya nchi yameghafilika na udharura huu na kutolinda mistari ya mipaka na hivyo kudhoofisha na kufifisha vitenganishi hivi. Ama tunapasa kuwa waangalifu na kuchunga mistari hii inayotutenganisha na maadui wa Mapinduzi, Imam na taifa, isije ikafifia rangi.’ Na nasaha ya mwisho ya Aatullah Khamanei kwa taifa na viongozi ilikuwa: ‘Iaminini ahadi ya nusra ya Mwenyezi Mungu na kuweni na yakini kwamba mustakbali (ushindi wa mwisho) ni wa taifa na vijana wa Iran, na kwa masikitiko ya (wapende wasipende)  maadui.’
Kabla ya hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Hujjatul Islam wal Muslimeen Sayyid Hassan Khomeini, msimamizi wa Haram ya Imam Khomeini (MA) alitoa hotuba ambapo aliyataja Mapinduzi ya Kiislamu kuwa Mapinduzi yanayoungwa mkono na Mwenyezi Mungu pamoja na wananchi. Amesema kunufaika na mwongozo wa Mwenyezi Mungu, utukufu, mapenzi na huruma, umoja, nusra ya Mwenyezi Mungu na uungaji mkono wa wananchi ni baadhi ya sifa maalumu na zisizo na mfano wake za harakati kubwa na ya kihistoria ya Imam Khomeini na kwamba harakati na jitihada hizo kubwa zinaendelezwa kwa njia bora zaidi na mrithi anayefaa wa Imam (Ayatullah Khamenei) aliyechaguliwa kushika hatamu za uongozi baada ya kuaga dunia Imam Khomeini (MA).

 

700 /